JUMAMOSI
WIKI YA KWANZA YA KWARESMA
20/2/2016
Somo:
Kumb 26:16-19
Zab:
119:1-2, 4-5, 7-8
Injili:
Mt 5:43-48
Nukuu:
“Umemwungama Bwana leo,
kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika
amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake,”
Kumb 26:17
“Lakini mimi nawaambia:
Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu
aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua
wenye haki na wasio haki,” Mt 5:44-45
“Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
TAFAKARI:
“Kuishi ahadi zetu za ubatizo: Kuwapenda Maadui zetu na kuwa wapatanishi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tuyatafakari makuu ya Mungu kwa “kuishi ahadi zetu za ubatizo; kuwapenda
maadui zetu na kuwa wapatanishi.” Somo letu la wana wa Israeli
wanamuungama Mungu kwa kuzishika amri zake. “Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye
Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na
maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake,” Kumb 26:17. Nasi
leo kama wafuasi wake Kristo somo hili latukumbusha ahadi za ubatizo wetu.
Ubatizo wetu ni kumwungama Kristo kwa fumbo la mateso, kifo na ufufuko
wake. Fumbo hili linatufanya kuzaliwa upya kwa Roho Mtakatifu. Kuzaliwa huku ni
kule Yesu anapomtaka Nikodemo azaliwe upya. “Yesu akamwambia, Amin, Amin,
nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu,”
Yoh 3:3.
Kuishi ahadi zetu za
ubatizo ni kutembea katika njia za Bwana wetu Yesu Kristo. Tu wakristo kwa
sababu tu wafuasi wa Kristo. Na kama tu wafuasi wa Kristo, yatupasa kutembea
katika njia zake. Tomaso alitaka kujua njia impasayo kuifuata kama mfuasi wa
Kristo. “Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?
Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia ya mimi,” Yoh 14:5-6.
Mpendwa njia yetu
wabatizwa na wafuasi wa Kristo ni Yesu mwenyewe. Na njia aliyochagua ni njia ya
Msalaba. Hatuwezi kuukwepa Msalaba kama tu wafuasi wa Kristo. Msalaba ni
utukufu wetu na ushindi wetu. Ukweli wake ni yale anayotufundisha, nayo ni
habari njema ya Wokovu. Habari hii ya wokovu ni uhai na umilele ambao yeye
mwenyewe anasema, “ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama,
upo, huku, au, kule kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,”
Lk 17:20b-21. Mfano mzuri ni pale ufanyapo mtihani. Mwanalimu anapokupa
mtihani, 100% unayo wewe mwenyewe. Yakupasa kumwonyesha mwalimu asilimia hiyo
100. Maana yake kufaulu kwa mtihani kupo kwako na ni juu yako.
Uzima katika Kristo
tunaupata tunaposhiriki masakramenti yake, na hasa sakramenti ya Ekaristi
Takatifu tukiwa na mioyo safi. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima;
yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,”
Yoh 6:35.
Tunaishi ahadi zetu za
ubatizo kwa kuzishika amri zake na kufuata maagizo yake. Ni kuwa na hofu ya
Mungu ndani mwetu. Na amri iliyo kuu ni ya upendo. “Amri mpya nawapa, Mpendane.
Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34.
Amri hii ya upendo na nyinginezo zatupasa kuzishika si kinadharia tu bali kwa
matendo yetu na yenye kumpendeza Mungu. Huku ni kudhihirisha tunampenda Yesu
Kristo na yule aliye mpeleka. “Yeye aliye na mri zangu, na kuzishika, yeye
ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na
kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Tendo hili la kuzishika amri za
Mungu ni kukaa katika pendo la Mungu. Huku ni kumuishi Kristo aliyekaa katika
pendo la Mungu kwa kushika amri zake. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika
pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika
pendo lake,” Yoh 15:10.
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, somo la Injili latualika pia kutafakari juu ya upendo wetu na maadui
zetu, ambao tunda lake ni upatanishi. Si jambo rahisi kibinadamu kumpenda adui
yako, hasa pale tunapoyakumbuka mabaya aliyotutendea. Ila tusipo enda zaidi ya
kuwapenda wale tu ambao wanatupenda, ukristo na ufuasi wetu bado haujakomaa, na
imani yetu bado changa. “Lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni
wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye
huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,”
Mt 5:44-45. Huku ndiko kwenda zaidi ya yale yaonekanayo kwa mtazamo wa
kibinadamu ambayo kwayo hutupatia haki ya leo na sasa, na kukosa neema ya
huruma ya Mungu. Hivyo kwa kuyapata hayo tu huyafanya Maisha yetu ya kiroho
kuwa na ulakini.
Tunakuwa wana wa Mungu
tu kwa kuwapenda maadui zetu na kuwaombea. Kwa dhambi zetu tulikuwa maadui na
Mungu. Ila kwa kupitia mwanaye Yesu Kristo kwa mateso, kifo na ufufuko wake
tumepatanishwa na Mungu. Kristo ni kielelezo cha UPANANISHO HAI NA WA KWELI.
Nasi kwa kumfuata Kristo tunafanya kazi hiyo ya upatanisho kwa kuwaombea watesi
wetu kwa Mungu awabadili mienendo yao mibaya. “Maana
mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao
hawafanyi yayo hayo? Tena
mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa,
je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:46-47.
Wapendwa inasikitisha sana kuona miongoni mwetu kadiri ya wito na utume wetu,
tumekuwa wakristo wazuri sana wa jumapili, twakiri kuwa askari imara wa Kristo,
na ifikapo jumatatu tunatoroka kambini na kufanya kinyume kabisa na utambulisho
wetu kwa kutowapenda na kutokuwa tayari kuwasamehe watesi wetu. Kwa kweli haya
ni zaidi ya maigizo.
Ndugu yangu,
hatuwaombei mabaya maadui zetu. Tukumbuke nao
wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27. Mungu tu ndiye anayeweza
kuwabadili kwa sababu ndani yao ipo chapa yake-sura na mfano wake. Kwa upendo
alio nao Mungu wetu kwa wema na waovu, hata kaa kimya aache chapa yake ipotee
bure. Kwa msaada wa sala zetu, Mungu yupo tayari kuwabadili kwa tendo hili la
sala na majuto. Tunakuwa pia wana wa Mungu kwa kuwa wapatanishi. “Heri
wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9.
Upatanisho ni tendo la
ibada na ukombozi. Misa Takatifu kama ibada ya neno na Ekaristi Takatifu ni
tendo la upatanisho. Tunapatanishwa nafsi zetu, wenzetu (wema na waovu), na
Mungu. Huku ndiko kumwilishwa kwa neno (Mwana wa Mungu), kuwa mwili. Ni tendo
la upendo mkubwa wa Mungu Baba kwetu wanadamu. Ni ufupisho wa historia yote ya
wokovu wetu.
Hivyo basi, kama mfuasi
mwaminifu na mwenye hofu ya Mungu, wewe na mimi yatupasa kufurahi na
kushangilia pale tunaposhutumiwa kwa ajili ya haki, tunapoudhiwa na kunenewa
kila neno baya kwa uongo kwa ajili ya Kristo. Hii ndiyo maana halisi na mapaswa
ya kuwa mkristo wa kweli na mfuasi wa Kristo. Yesu anasema, “heri ninyi watakapowashutumu
na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini,
na kushangilia, kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana ndivyo
walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12.
Ndugu yangu, hii ndiyo
changamoto ya kweli ya ishi yetu kama wakristo. Kuishi huku kunakuhitaji
kuziishi ahadi zako za ubatizo kuwapenda maadui zako, na kuwa wakili wa
Kristo, yaani mpatanishi. Ahadi hizi za ubatizo ndicho alichokifanya Yesu
Kristo katika safari nzima ya wokovu wetu. Je, upo tayari kuvivaa viatu vya
Yesu?
Tumsifu Yesu Kristu!
“Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
Ee Yesu, uliye Njia, Ukweli, na
Uzima, kamwe usituache katika fumbo hili la wokovu wetu, yaani kuziishi ahadi zetu
za ubatizo na kuwa mawakili wako, yaani Wapatanishi. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario