lunes, 8 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 5 YA MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 5 YA MWAKA-C
9/2/2016
Somo: 1Fal 8:22-23, 27-30
Zab: 84:3-5, 10-11
Injili: Mk 7:1-13
Nukuu:
Akasema Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote,” 1Fal 8:23

Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa,” 1Fal 8:29 

Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe,” 1Fal 8:30 

Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba,” Mk 7:3-4

Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:6-8 

Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo,” Mk 7:11-13 

TAFAKARI:Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.”

Wapendwa wana Mungu, kwa namna tunavyoishi leo wewe na mimi ni matokea ya mila na tamaduni fulani. Hivyo binadamu kajengeka kitabia kutokana na historia yake. Mila, tamaduni, na desturi za mahali hubeba pia falsafa yake, ikiwa ni pamoja na namna ya kuyaona mambo katika uhasili wake na ukweli wake. Hata hivyo mionekano hiyo wakati mwingine hubeba dhana potofu pale inapokuwa na mwelekeo wa kuhalalisha kila kitu bila kujali uhalisia wa kifu husika na kweli yake.

Uwepo wa Mungu ni dhahiri kwetu kwa njia ya UFUNUO wake. Hivyo kadiri ya historia ya wokovu wetu, Mungu ndiye aliyechukua nafasi ya kwanza kujifunua kwa mwanadamu, hii ikiwa ni pamoja na uumbaji wa ulimwengu huu tunaoishi leo pamoja na vitu vilivyomo, Mwa 1:1-31. Mwanadamu anachukua nafasi ya pekee katika uumbaji huu, yaani, kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27. Ikiwa uwepo wa Mungu ni dhahiri kwa njia ya ufunuo, mwitikio wa mwanadamu kwa ufunuo huu wa Mungu ndiyo njia ya kumfahamu Mungu na uwepo wake. Haya yote yanawezekana kwa neema za Mungu na Roho Mtakatifu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu,” 2Pet 1:21. Hivyo kwa hasili mwanadamu anashahuku hii ya kumtafuta na kumjua Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo Yesu anawakemea Mafarisayo na baadhi ya Waandishi kutokana na unafiki wao juu ya kweli ilivyo kadiri ya uwepo wa Mungu na ufunuo wake kwa mwanadamu. Wanafunzi wa Yesu wanakuwa gumzo kwa vile tu hawakufuata desturi za wazee na mapokeo yake. “Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi?” Mk 7:5. Mapokeo na desturi hizi za Kiyahudi zilibumbwa sana kutoka torati na kwa kiasi kikubwa walifuata TALMUD, ambayo ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Talmud hii ni tafsiri ya Torati ambayo iliubeba ubinadamu na kuacha maagizo ya Mungu kama yaliyokuwa katika Torati. Mapokea ya wazee ni pamoja na haya: Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba,” Mk 7:3-4. Yesu analikemea jambo hili kwa lengo la kuwarudisha kwenye kweli kwa kuwaambia, “Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:6-8. Hii ndiyo sababu ya maneno haya ya Yesu, Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie,” Mt 5:17-18.

Kwa kuwaonyesha kigeugeu chao katika sheria ya Mungu, yaani torati, Yesu anaawambia, Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo,” Mk 7:11-13. Hakika kile wakisemacho sicho wakiishicho! Hawa ndio wale Yesu aliowasema kuwa ni viongozi vipofu. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,” Mt 23:24. Alisemalo Yesu leo analisema kwetu pia na jamii yetu ya Tanzania. Si ajabu leo kuona mwizi wa kuku kafungwa gerezani wakati huo huo wezi wa mabilioni ya fedha za umma ‘wakila bata,’ mtaani kama ulivyo msema wa jamii yetu leo. DOUBLE STANDARD! Hili Yesu hapendi!

Wapendwa wana wa Mungu, hatuwezi kubeza uwepo wa Mungu katika maisha yetu. Leo wapo watu huko Kenya wanaotaka kujisajili kama jumuiya isiyotambua uwepo wa Mungu. Je, unaweza kuwaza kile ambacho hakipo? Ukweli ni kwamba kadiri unavyokataa uwepo wa Mungu, ndivyo hivyo hivyo unavyo ukubali. Kumbe ni vyema kuukiri uwepo wake hata kama huelewi sawasawa. Ni kwa njia hiyo ya kuukubali uwepo wa Mungu, na Mungu hujifua kwako taratibu. Mfalme Sulemani ni mfano mzuri na wakuigwa kama kiongozi kwenye hofu ya Mungu. Akasema Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote,” 1Fal 8:23. Bila hofu ya Mungu katika utendaji wetu, ni rahisi sana kufanya kazi ya shetani.

Wapendwa wana wa Mungu, utampata na kumfikia Mungu kadiri unavyomtafuta. Naye Mfalme Sulemani anasema, Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa,” 1Fal 8:29. Ndugu yangu, maisha yako yanasukumwa na nini? Maisha bila Mungu, ni sawa na boti baharini bila usukani. Safari ya mtindo huo ni majanga tu huko uendapo. Kumbe yatupasa kukiri uwepo wa Mungu na kuomba hivi kama alivyofanya Mfalme Sulemani, Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe,” 1Fal 8:30. Amina!

Tumsifu Yesu Kristo!

Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1


No hay comentarios:

Publicar un comentario