sábado, 13 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 1 YA KWARESMA-C

JUMAPILI YA 1 YA KWARESMA YA MWAKA-C

Somo I: Kumb 26:4-10
Zab: 91:1-2, 10-15
Somo II. Rum 10:8-13
Injili: Lk 4:1-13
Nukuu:
Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito,” Kumb 26:6

Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu,” Kumb 26:7

Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali,” Kumb 26:8-9

Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee Bwana. Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako,” Kumb 26:10

Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9

Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:10

Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika,” Rum 10:11 

Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13

Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate,” Lk 4:3

Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu,” Lk 4:4

Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo,” Lk 4:6

Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako,” Lk 4:7

Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake,” Lk 4:8 

Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake wakulinde; na ya kwamba,mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe,” Lk 4:9-11

Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako,” Lk 4:12 

Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda,” Lk 4:13 

TAFAKARI: “Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kwanza ya Kwaresma mwaka “C.” Masomo yetu yote matatu yanatualika tusimame katika Imani ya kweli, na hasa katika matendo. Pili, yatupasa kuwa imara hata baada ya kuyashinda majaribu katika vita hivi vya Imani, kwa sababu yule mwovu shetani kushindwa kwake siyo mwisho wake wa kutujaribu. Basi Yesu alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda,” Lk 4:13.

Ni kwa namna hiyo kwamba Imani kwa Waisraeli haikuwa ni kitu cha kufikirika au kuwazika kwa mbali, bali matendo halisi. Pale walipogundua yote yamefanyika kwa mkono wa Mungu hawakuacha kuonyesha kwa matendo Imani yao. Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu,” Kumb 26:7. Kilio cha wana wa Israeli ni juu ya mateso waliyoyapata huko Misri. Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito,” Kumb 26:6. Kwa tendo hili na mkono huu wa Mungu kuwaondoa katika mateso yao, na hasa kuwapatia ardhi kwao hakikuwa kitu cha kawaidasi kitu hata kidogo. Ni zaidi ya miaka mia nne walikuwa utumwani. Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali,” Kumb 26:8-9.

Maisha ya Kiyahudi yalionekana kutiliwa mkazo kwenye mambo makuu matatu; moja, umuhimu wa Hekalu Takatifu kama sehemu pekee ya kuabudu na kumtokea Mungu shukrani zao na sadaka za kuteketezwa. Pili, Maandiko Matakatifu, yaani Torati. Na mwisho milki ikiwa ni ardhi pamoja na uongozi madhubuti uliowekwa na Mungu mwenyewe. Hivyo kile walichokipata kutoka ardhi walikitoa kwa Mungu wakitambua ni kwa namna gani alivyowatendea. Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee Bwana. Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako,” Kumb 26:10. Imani na matendo halisi vilikwenda pamoja. “Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili. Kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko. Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” Ybs 35: 7-9. Jambo hili litakupa wajibu wako mbele ya Mungu. Na utawajibika kumrudishia Mungu kilicho chake. Mara nyingi tunamrudishia Mungu mabaki ya kazi za mikono yetu. Elewa vitu vyote ni mali yake MUNGU.

Wapendwa wana wa Mungu, Biblia Takatifu siyo kitabu cha katekesi wala tafiti ya kiteolojia, bali ni historia ya wokovu yenye kuonyesha mwingiliano wa matendo ya wokovu ya Mungu kwa watu wake. Uhusiano wa Mungu na watu wake haukuwa wa kufikirika, bali wa kuchangamana na matendo makuu ya Mungu. Uhusiano huu wa Imani na Muumba wetu unaoendana na matendo yetu, Mtume Paulo anauzungumzia katika ukiri wa Neno la Mungu, na Bwana, yaani Yesu Kristo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9. Kulikiri jina Yesu ni kutambua mambo makuu manne katika ibada yenye kumpendeza Mungu, yaani kuabudu kuliko sahihi, halisi, kutafakari, na matendo. Kama haya mambo manne hayapo na hayafanyiki katika kuabudu kwetu, basi huo sio ukiri bali ni ibada ya ‘kupayukapayuka.’ Na katika kulifanya jambo hili la ukiri lililo sahihi, halisi, la tafakari, na matendo, “hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13. Kuliita jina hili la Bwana siyo kwa kupayuka, wala kusukumwa kwa hisia zetu.

Hakika Yesu angezifuata hisia zake, hasingeweza kuyashinda majaribu kule jangwani. Yesu hakuziruhusu hisia zake zimtawale kwa sababu alimruhusu Roho wa Mungu ayatawale maisha yake. Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Ni Roho huyu aliyeyasukuma yote aliyoyafanya na hasa pale alipotangaza rasmi mapambano ya kweli na haki katika lile lililo ovu na kumkomboa mwanadamu. Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,” Lk 4:18. Na ni Roho huyu huyu aliyemwezesha kuyaona yote kwa mwelekeo wa Mungu Baba. Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:2.

Huyu ndiye Roho aliyemwezesha kuyashinda yale majaribu jangwa juu ya Sifa, Mamlaka, Utajiri, na Umaarufu, [Lk 4:4, 6, 8, 9-11]. Baada ya ushindi huu wa Yesu, Ibilisi alimwacha kwa muda. Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda,” Lk 4:13. Unaposhinda majaribu katika maisha yako usije ukajisahu na kubweteka kana kwamba vita hiyo ishafikia ukomo. Yakupasa kuwa macho muda wote kama asemavyo Mtume Petro, Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5:8.

Kila mmoja wetu anajangwa lake ambalo ukitaka uzima wa milele utaupata na ukitaka ya hapa duniani utayapata pia. Ila ni vigumu sana kuyapata ya milele kama utabobea kwa haya ya leo na kesho, yaani ya hapa duniani. Ukiyachuchumilia ya umilele, kuna uhakika wa kuyapata yote ya duniani kwa amani na furaha. Basi utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa,” Lk 12:31. Maisha yangu kama Mtawa na Padre ni yanipasa kuyaisha kwa uaminifu huku nikiyashinda majaribu yangu ya kila siku kwa nguvu ya sala na uwezo wa Roho Mtakatifu. Nawe ule mlei na kadiri ya wito wako, ni vyema ukajua yakupasayo kuishi na hasa uaminifu kwa kile ulichoitiwa. Kipindi hiki cha kwaresma tunapata nafasi ya kuzama ndani ya nyoyo zetu kwa lengo la kujitakasa na kumrudia Mungu katika kumwabudu kuliko sahihi, halisi, tafakari, na kwa matendo hai. Ibilisi utuacha tu kwa muda ila hajaghairi nia yake ya kutudondosha. Basi tukeshe tukiomba na kushikamana na Kristo aliyeyashinda majaribu yake jangwani.

Daudi Kibobo alidumu zaidi ya miaka mitatu akimwomba Mungu ampatie kwa namna yoyote ile mtaji wa kufanya biashara, kutokana na vibarua vigumu alivyokuwa anafanya kila siku. Siku mmoja mvua zilinyesha siku nzima. Hivyo hapakuwa na kibarua cha kufanya. Ilipofika jioni ya saa kumi na moja hivi huku kukiwa bado na manyunyu ya mvua, aliwaza aende shambani angalau alime matuta matatu ya viazi vitamu.

Akiwa njiani kuelekea shambani mwake, alikuta gari dogo limekwama barabarani. Alifaka pale na kumkuta Bwana mmoja akiwa hajui cha kufanya. Kwa kujua tatizo lile, Daudi Kibobo alilivamia pori na kukata fito za kutosha. Alizitandaza kwa ujuzi kwenye lile tope na kumwamuru mwenye gari awashe gari na kuondoka. Kweli gari ile ndogo ilitoka kwenye tope. Yule Bwana alimwita Kibobo na kumwambia, ndugu asante sana kwa msaada wako. Ningependa kukufahamu zaidi. Kibobo akamwambia jina lake na yule Bwana akajitambulisha kama Yonathani Nyare. Nyare alimtaka Kibobo akutane naye kesho ofisini kwake. Mapema asubuhi Kibobo aliwasili na kwa bahati nzuri alikutana na Bwana Nyare. “Hii ndiyo asante yangu,” Nyare alimkabidhi bahasha na ndani yake kulikuwa na milioni moja. Kabla Kibobo hajasema neno, Nyare alimwambia, “Bwana Daudi Kibobo, jana ungekuwa mtu mbaya ungeweza kuwa tajiri mkubwa leo. Kwenye gari yangu nilikuwa na milioni mia tatu. Nasema tena, asante sana.” Kibobo hakuamini macho yake. Alitoa shukrani zake na aliondoka.

Njiani Kibobo alipanga mipango yake vizuri kuhusu biashara atakayoifanya na kufikia muhafaka wa kufanya biashara ya kuuza mazao na hasa mahindi. Vile vile aliweka ahadi kwa Mungu kwamba kila atakapouza mazao yake, atamtolea Mungu asilimia kumi ya faida ile.

Kibobo alianza kazi ile mara moja. Mauzo ya kwanza alipata faida milioni moja, na kwa asilimia kumi alitoa laki moja kama shukrani kwa Mungu. Mzigo wa pili alipata faida laki tisa, na kwa asilimia kumi alimtolea Mungu shukrani ya elfu tisini. Alifanya zoezi hili kwa mwaka mzima na mambo yalikuwa vizuri sana. Akiwa mwaka wa pili wa biashara yake, mara moja alipata faida ya milioni 100, na kwa asilimia kumi ilimpasa amtolee Mungu milioni kumi. Akiwa analiwaza hilo ofisini mwake, akaja Bwana mmoja akiwa na lengo la kuuza gari yake ya mzigo aina ya  Fuso Mpya kwa milioni 10, kwani alikuwa  tatizo kubwa sana katika familia yake.

Basi, kwa uzuri wa gari lile la mizigo na hitaji alilokuwa nalo Kibobo alilinunua kwa fedha ile ambayo alishaitenga kwa kutoa shukrani kwa Mungu akiahidi kwamba mwezi ujao atamtolea Mungu milioni kumi na tano. Akiwa amejiridhisha na dhamiri yake, Kibobo aliondoka na dereva wake kufuata mzigo wa mahindi. Akiwa njiani wakati wa kurudi na akiwa na mzigo wa mahindi, gari ile ilipinduka na kuharibika kabisa, naye akavunjika mguu. Pesa aliyokuwa ameweka kwenye mfuko, kwa ajili ya kununulia mchele yote ilipotea. Ni jana tu alitoka Benki kutoa pesa yote na kubakiza milioni moja.

Kibobo alibaki na milioni yake moja aliyoanza nayo miaka mitano iliyopita. Leo milioni hiyo haitoshi hata kwa kumgharamia matibabu yake. Ndugu yangu, tuwe waaminifu kwa ahadi zetu tutoazo kwa Mungu, na tubaki kwenye imani ya kweli hata pale tunapopata majaribu.

Tumsifu Yesu Kristo!  


Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda,” Lk 4:13 

No hay comentarios:

Publicar un comentario