JUMATANO WIKI YA 4 YA MWAKA-C
Somo:
2Sam 24:2, 9-17
Zab:
32:1-2, 5-7
Injili:
Mk 6:1-6
Nukuu:
“Naye
Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee
Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu
kabisa,” 2 Sam 10b
“Na
Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake
Daudi, kusema, Nenda, ukanene na
Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja,
nikutendee hilo,” 2Sam 24:11-12
“Basi
Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie
katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku
wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa,
ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma,” 2 Sam 24:13
“Naye
Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke
katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika
mkono wa wanadamu,” 2Sam 24:14
“Basi
Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa
watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu.” 2Sam 24:15
“Huyu
si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na
Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake,” Mk 6:3
“Yesu
akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa
jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4
TAFAKARI:
“Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake,
na nyumbani mwake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Yesu anatukumbusha wajibu muhimu sana, yaani, tuviheshimu na kuvienzi
vilivyo vyetu. Pamoja na hayo yote, hukumu yetu iwe ya kweli na haki. Waswahili
wanasema, “masikini mnyongeni, ila haki yake mpeni.” Ni wazi watu wa nyumbani
mwake waliyastaajabia yale aliyoyatenda Yesu lakini hawakuutafakari Umungu
wake, bali waliutazama zaidi ubinadamu wake tena katika mwono wa historia yake.
Nao wanashangaa na kusema, “Huyu si yule
seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni?
Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake,” Mk 6:3. Hivyo leo ni wito
kwetu kwamba tusimdharau mtu kwa vile tunaifahamu historia yake na asili yake,
bali tumtazama katika upya wake.
Ni jambo la kushangaza
leo kuona katika jamii yetu Tanzania baadhi yetu kuwaweka watu fulani, au
makabila fulani, na hata ukanda fulani wa nchi walipotoka kama watu wasio na
maana na kutokuwa na jema lolote. Bila shaka ubaguzi huu unakusudi lake
kimkakati. Hata hivyo mikakati yote miovu ni chukizo kwa Mungu. Kuhusu hatari
hii, Yesu anasema, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe,
na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4. Kutokuheshimka na kupokeleka
kwetu hakutoki nje ya jamii tunayoishi. Mchawi ni sisi wenyewe. Dhambi hii ya
kubaguana kunakotokana na familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na elimu zetu
ni mbaya na yakuogopwa sana. Machafuko mengi ya kijamii na hata kufikia hatua
ya mauaji ya kimbari huanza na chokochoko hizi. Hakuna binadamu aliye na
thamani zaidi ya binadamu mwingine. Wewe ni nani na una ubora gani zaidi hata
umdharau mwenzako kutokana na familia yake, ukoo wake, au kabila lake? Tuelewe
kwamba mengine yote hapa duniani ni MBWEMBWE TU!
Tukubali wakati
mwingine tunafanya vibaya sana hata kama jambo hilo linatumika kama utani.
Utani upo kwa watani, na siyo kwa kila anayejisikia kufanya hivyo. Tuwahesimu
watu na utu wao. Tofauti zao ndio uzuri wa Mungu. Hatukuumbwa ili wote tufanane
kwa kila kitu. Ikiwa hivyo basi sisi si watu tena bali mitambo-“robots.”
Tujifunze unyenyekevu pale tulipokosea kama alivyofanya Daudi kwa kosa la
kuwahesabu watu na kutaka kujua idadi yao kinyume na atakavyo Mungu. “Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya
niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi
wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa,” 2 Sam 10b. Ni Daudi huyu huyu anaye
omba kwa unyeyekevu na kujuta dhambi zake anapogundua ndivyo sivyo uhusiano
wake na Mungu. “Ee Mungu, uniumbie moyo
safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala Roho yako
Mtakatifu usiniondolee,” Zab 51:10-11. Tumuombe huyu Roho Mtakatifu akaye nasi
ili tuweze kuyaona matakatifu kwa wale wote tunaoishi nao na wanaotuzunguka.
Yote
yasiyoongozwa na Roho wa Bwana yanamadhara sana katika maisha yetu. Mungu
hatosita kutufundisha kwa njia nyingine ili tumrudie. Kwa kosa alilofanya Daudi
anapewa mapendekezo matatu kuizuia hasira ya Mungu. “Basi
Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie
katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku
wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa,
ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma,” 2 Sam 24:13. Hapa pia tunaona unyenyekevu wa
Daudi anapoipokea adhabu hii. Daudi anapokea adhabu kwa moyo wa kushukuru. “Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika
mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake
ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu,” 2Sam 24:14. Mungu hubaki
kuwa Rehema, na Mungu wa Rehema kwetu. Pamoja na Bwana kuwaletea tauni na kufa
watu elfu sabini, “Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu
ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye
kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako,” 2Sam 24:16a.
Mungu wetu hughairi adhabu yake tunapojinyenyekesha kwake kwa kufanya toba ya
kweli na majuto ya dhambi.
Tumsifu
Yesu Kristo
“Mtu
kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana,” Mit
20:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario