JUMATANO
WIKI YA 1 YA KWARESMA
Somo:
Yon 3:1-10
Zab:
51:3-5, 12-13, 18-19
Injili:
Lk 11:29-32
Nukuu:
“Yona
akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya
siku arobaini Ninawi utaangamizwa,” Yoh 3:4
“Basi
watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za
magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo,” Yoh 3:5
“Habari
ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua
vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu,” Yoh 3:6
“Naye
akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na
wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya
ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia,
mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila
mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake,” Yoh 3:7-8
"Mungu akaona
matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile
baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende." Yon 3:10
“Maana,
kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa
Adamu kwa kizazi hiki,” Lk 11:30
"Watu wa Ninawi
watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na
hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko
Yona." Lk 11:32
TAFAKARI:
“Toba ya kweli na Msamaha wa dhambi kupitia Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, napenda leo tutafakari pamoja kuhusu "toba ya kweli na msamaha
wa dhambi kupitia Yesu Kristo." Tendo la toba huturudisha katika uhalisia
wetu kama viumbe na wanadamu. Toba utufikirisha na kutuongoza kwa undani kuhusu
mianguko yetu iliyotokana na kutokuupokea ubinadamu wetu na kutaka kuwa sawa na
Mungu. Somo la kwanza, Yona anawaelekeza
watu wa Ninawi kufanya toba ya kweli. Toba hii inasura ifuatayo; kwanza
kumfanya binadamu arudi kwenye hali yake na uhalisi wake. Hapa wote yaani
wakubwa, watoto na watawala akiwemo mfalme wanafanya toba ya kweli. “Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza
kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo,”
Yoh 3:5
Wanyama pia
hawakuachwa. Wanashirikishwa kufanya toba hiyo. “Naye
akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na
wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya
ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia,
mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila
mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake,” Yoh 3:7-8. Wazo kuu hapa ni kwamba, toba ya
kweli ni kurudi kwenye hali yako na uhalisi wako. Hii ndiyo maana halisi ya
kufanya toba ya kweli. Ni kushuka na kujishusha bila kujali nafasi, umaarufu,
cheo, utajiri, na hata uwezo uliokuwa nao. "Kiburi cha mtu kitamshusha;
Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa." Mit 29:23
Mwenye kiburi na
majivuno kamwe hawezi kufanya toba ya kweli. Bila toba ya kweli hakuna msamaha
wa dhambi. Utimilifu wa kazi ya Yesu na mwendelezo wake kupitia Mitume na
Kanisa leo ni kuhubiri habari njema ya wokovu, kufanya toba ya kweli na msamaha
wa dhambi. Hili ni agizo alilolitoa Yesu
kwa wanafunzi wake huko Emau mara baada ya ufufuko wake. Yesu akawaambia,
"ndivyo iliyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na
kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la
dhambi, kuanzia tangu Yerusalemu." Lk 25:46-47. Kanisa kwa kupitia
Sakramenti ya kitubio, Yesu anafanya ondoleo hilo la dhambi kwa kupitia
watumishi wake, yaani Mapadre na Maaskofu kwa Sakramenti yao ya Daraja
Takatifu. “Naye akiisha kusema hayo,
akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi,
wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Hii ni huruma ya Mungu kwetu kwa kupitia Kanisa
lake Takatifu.
Somo letu la injili,
yapo mambo mawili mazito ya kutafakari. Pamoja na Yesu kukemea uhitaji wao wa
ishara, Yesu anajitabanaisha kuwa yeye ndiye Ishara halisi ya Toba na msamaha
wa dhambi. Yeye ni Mungu aliyemwilishwa. Yeye ndiye njia, ukweli na uzima, (Yoh
14:6).
Ndugu yangu, wewe na
mimi kama wafuasi wa Kristo, na ndivyo tulivyo Wakristo, ni ndoto na ni jambo
lisilowezekana kwenda mbinguni bila kupitia kwa Yesu Kristo. Je, tunataka
ishara gani tena zaidi ya Yesu? Katika hili Yesu anachukua nafasi mbili kwa
wakati mmoja. Kwanza ni ishara kama kielelezo cha uhai kamili na umilele. Pili, Yesu ni mfanya ishara ambazo kwayo
zaonyesha Umungu wake. Kwa nini basi ndugu yangu ukiwa na maangaiko kidogo tu
unakimbilia kwa waganga wa kienyeji kupata ishara?
Ndugu yangu, kama
umepoteza ufunguo wa maisha yako mwendee Yesu. "Jesus is the master key." Damu yake haikumwagika
bure pale msalabani. "The blood of
Jesus is the master key." Ufunguo huu huwezi kuupata kwa mganga yeyote wa
kienyeji na hata chuo kikuu chochote mashuhuri duniani. Ufunguo huu hupatika
kwake Kristo Yesu tu, na kwa wale wenye unyofu wa moyo. "Afadhali maskini
aendaye katika unyofu wake, kuliko mpotofu wa njia ingawa ni tajiri." Mit
28:6. Wanyofu wa moyo ni wale wenye udongo mzuri na wenye kuzaa matunda kwa
kuvumilia. "Mbegu zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na
wema wa mioyo yao husikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa
kuvumilia." Lk 8:15
Tumsifu
Yesu Kristo!
"Watu
wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu
kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa
kuliko Yona." Lk 11:32
No hay comentarios:
Publicar un comentario