IJUMAA WIKI YA 4 YA MWAKA-C
Somo:
YbS 47:2-13
Zab:
18:31, 47, 50-51
Injili:
Mk 6:14-29
Nukuu:
“Naye Bwana
akamwondolea dhambi zake, akaiinua pembe yake hata milele; akampa agano la
ufalme, na kiti kitakatifu cha enzi katika Israeli,” YbS 47:11
“Na kwa ajili yake
akainuliwa mwanawe, mtu wa ufahamu aliyekaa salama. Sulemani alimiliki katika
siku za kufanikiwa, naye Mungu akampa raha kumzunguka pande zote, ili alijengee
jina lake nyumba, na kumwekea tayari patakatifu pa milele,” YbS 47:12-13
“Maana Herode
alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na
alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa
furaha,” Mk 6:20
“Akamwapia, Lo lote
utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu,” Mk 6:23
“Basi akatoka,
akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji,” Mk
6:24
“Mara akaingia kwa
haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe
kichwa cha Yohana Mbatizaji,” Mk 6:25
“Mfalme akafanya
huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi
karamuni, hakutaka kumkatalia,” Mk 6:26
“Mara mfalme akatuma
askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle
gerezani,” Mk 6:27
“akakileta kichwa
chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye,” Mk
6:28
“Wanafunzi wake
waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini,” Mk
6:29
TAFAKARI:
“Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya
ufalme wangu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
sifa na kutaka umaarufu umewaponza wengi. Ni jambo la busara kujua uwezo na
mipaka yako hasa pale unapotakiwa kutoa maamuzi kwa nafasi uliyo nayo. Ni mara
ngapi kwenye vikao mbalimbali vya maandalizi ya matukio mbalimbali kama vile;
harusi, jenzi mbalimbali, unatoa ahadi ambazo kwa kiasi fulani zipo nje ya
uwezo wako. Waswahili wanasema hivi, “mbuzi hula umbali wa kamba yake.” Leo
tunaona katika Injili tukio la ajabu sana. Mfalme Herode anajiweka kitanzi
mwenyewe kwa kutaka sifa na umaarufu.
Ikiwa ni siku ya
kuzaliwa kwake, Herodi anatoa ahadi kwa Binti yake ambaye aliufurahisha ukumbi
kwa kucheza vizuri. Wakati mwingine yakupasa kuwa na hakiba ya maneno hata kama
hali ya kusema chochote inakuruhusu. Naye Herode akamwapia binti yake, “Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme
wangu,” Mk 6:23. Maneno haya yalikuwa mazito sana kwa binti huyu. Hivyo kwa
hali ile alihitaji ushauri wa haraka. “Basi
akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana
Mbatizaji,” Mk 6:24. Na hii ndiyo
iliyokuwa nafasi ya Herodia ya kumwangamiza Yohane Mbatizaji ambaye alionekana
kero na kiwingu kwa mahusiano yake na Herode. Tuelewe kwamba Herodia alikuwa
mke wa Filipo ndugu yake Herode. Yohane Mbatizaji alikemea uovu huu kwa nguvu
zake zote kwa Herode kumuoa mke wa ndugu yake. Na sasa Yohane Mbatizaji anakuwa
mbuzi wa kafara.
Wapendwa
wana wa Mungu, wapo wengi katika jamii yetu wanakutwa na umauti kama Yohane
Mbatizaji kwa vile tu wanasimamia kweli na wapo tayari kwa ajili ya kweli.
Maisha ya Yohane Mbatizaji hayana ndoa lolote katika jamii. Ukweli huu hata
Mfalme Herode anaufahamu. “Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki,
mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa
akimsikiliza kwa furaha,” Mk 6:20. Yule binti ya Herode bila kufahamu
kilichokuwa nyuma ya pazia anapeleka ujumbe kadiri alivyoambiwa na Mama yake.
Binti huyu pia anapenda kwa nafasi hii na umati huu wa watu wengi kumfurahisha
Mama yake. Nani kama mama jamani? “Mara akaingia kwa
haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, “nataka unipe sasa hivi katika kombe
kichwa cha Yohana Mbatizaji,” Mk 6:25.
Habari
hii inamuhuzunisha sana Mfalme Herode, ila kwa vile iliipenda sifa na umaarufu anashindwa
kuizuia nafsi yake iliyoegemea mwili kwa sasa. “Mfalme akafanya
huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi
karamuni, hakutaka kumkatalia,” Mk 6:26. Hapa
ndipo tunapoona matumizi mabaya ya madaraka tuliyonayo na kulevywa nayo kwa
ajili ya kujenga majina yetu na kusahau haki na unyenyekevu kama viongozi.
Uongozi ni dhamana. Uongozi ni kuwajibika kuliko haki na usawa. Uongozi ni
mizania ya haki kwa wote. Mfalme Herode anaisikiliza nafsi yake ambayo kwa sasa
inasukumwa na mwili. “Basi
matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui,
ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Maamuzi yoyote uyafanyayo katika
hali hii hayana baraka ndani yake. Hivyo, “Mara
mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata
kichwa mle gerezani,” Mk 6:27
Kifo cha
ukatili dhidi ya Yohane Mbatizaji mtu mwenye haki kinakuwa furaha ya muda mfupi
kwa Herodia. Naye yule askari mwaminifu
“akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye
yule kijana akampa mamaye,” Mk 6:28. Hata leo watumishi wetu waaminifu, askari
polisi na jeshi, huwa wanapewa maagizo na viongozi wetu wenye kutaka sifa na
kuyajenga majina yao kwa kumwaga damu za wenye haki kwa kile kisemwacho kama
maagizo kutoka juu. Ni mara ngapi tunashuhudia vitendo vya aibu na uvunjifu wa
haki za binadamu kwa “maagizo kutoka juu.” Ndugu yangu, aliye juu ni Mungu tu.
Wengine wote wanaojiona wapo juu ni kutaka kuchukua nafasi ya Mungu, ambayo
hata ibilisi alipenda kufanya hivyo na mwisho wa siku alilaaniwa milele. Je,
nawe wapenda laana hiyo?
Ndugu
yangu, ni vyema ukajua uongozi ni dhamana na mwisho wa siku itakupasa kutoa
hesabu yake. Basi pale tunapokosea kutokana na ubinadamu wetu, tuwe wepesi wa
kujirudi na kujirekebisa. Mfano mzuri wa kujirudi na kujirekebisha ni Mfalme
Daudi. “Naye
Bwana akamwondolea dhambi zake, akaiinua pembe yake hata milele; akampa agano
la ufalme, na kiti kitakatifu cha enzi katika Israeli,” YbS 47:11. Leo viongozi
wetu walio wengi wamefikia hali ya kuhalalisha maovu yao kwa kile wanachojiita
‘wazalendo na wenye mawazo mapana kwa manufaa ya nchi’ ilhali ni kwa manufaa
yao binafsi na familia zao na vyama vya
siasa wanavyoviwakilisha, ambavyo vinaonekana kushika hatamu ya umilele.
Wapendwa wana wa Mungu,
bila kujinyenyekeza kuliko kweli na haki kutoka mioyoni mwetu pale tunapopewa
dhamana na umma, hata yale mazuri tunayoyafanya hayana thamani yoyote mbele ya
Mungu. Mfalme Daudi kwa unyenyekevu wake na kujua nafasi aliyokuwa nayo kama
kiongozi wa kutenda haki kwa wote bila kujali maslahi binafsi na marafiki zake,
Ufalme wake unabarikiwa hata kwa mrithi wake. Hivyo, “na kwa ajili yake
akainuliwa mwanawe, mtu wa ufahamu aliyekaa salama. Sulemani alimiliki katika
siku za kufanikiwa, naye Mungu akampa raha kumzunguka pande zote, ili alijengee
jina lake nyumba, na kumwekea tayari patakatifu pa milele,” YbS 47:12-13. Jambo
la kushangaza leo ni hili; kwa asilimia kubwa viongozi tulionao katika jamii
yetu leo ni watoto au familia za viongozi waliokuwapo hapo awali katika
uongozi. Kwa jicho la kawaida kabisa waweza kuona mtoto huyu siyo njia yake,
bali ni mazoea ya kufaidika na mfumo ambao hauna uwajibikaji. Uongozi umekuwa
kama ajira ya kawaida na wala siyo huduma katika maana ya kutumika. Yesu
anatuambia, “na mtu ye yote anayetaka kuwa
wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa
nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt 20:27-28. Ni wazi kwa mfumo huu wa
kutokuwajibika na kutumika ndio unao tugharimu sana katika Taifa letu leo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kalibu ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa
kwa sifa zake,” Mit 27:21
No hay comentarios:
Publicar un comentario