JUMATANO
WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo:
Yer 18:18-20
Zab:
31:5-6 14, 15-16
Injili:
Mt 20:17-28
Nukuu:
“Niangalie, Ee Bwana,
ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema?
Maana wameichimbia nafsi yangu shimo,” Yer 18:19-20a
“Lakini haitakuwa hivyo
kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na
mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana
wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya
wengi,” Mt 20:26-28
TAFAKARI:
Tenda mema nyakati zote; KUTUMIKA ndiyo sababu ya UKRISTO wetu, na UTAMBULISHO
wetu mbele ya Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
tumshukuru Mungu kwa zawadi ya kila mmoja wetu, kwa maisha na wito anaouishi.
Leo niwakaribishe tena kwa namna ya pekee tutafakari kiini cha maisha yetu kama
wafuasi wa Kristo, yaani, “Tenda mema nyakati zote; KUTUMIKA ndiyo sababu ya
UKRISTO wetu, na UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu.” Wapendwa tulio wengi katika
hili huwa tunakosa mwelekeo na kuanza kujilinganisha kimaisha. Wapo leo walio
kwenye maisha ya Ndoa wangependa kuishi kama watawa na Makleri; na wapo pia
walio watawa na Makleri wangependa leo kuishi kama wana Ndoa. Haya ni matamanio
ya kawaida ya mwanadamu aliye kamilika.
Ndugu yangu, hakuna
wito ulio bora zaidi ya mwingine mbele ya Uso wa Mungu. Kila mmoja wetu ni
uzuri wa Mungu, na Mungu anataka iwe hivyo kwa kumpendeza. Umoja wetu katika
utofauti ndio uzuri wa Mungu. Sote mbele ya Mungu tunamizania iliyo sawa. Na
cheo chetu sote ni kimoja tu, nacho ni UTAKATIFU wetu. Ni ukweli usiotia shaka
kwamba, kila mmoja wetu katika maisha na wito anaoishi, atapimwa kwa maswali
haya mawili mbele ya Mungu;
Swali
la kwanza: Umefanya nini kuhusu Mwangu Yesu Kristo, kwa
kuutoa uhai wake kwa ukombozi wako, na kadiri ya wito wako?
Swali
la pili: Je, umefanya nini na vipaji nilivyokupa?
Tusipokuwa tayari
kuyafanyia kazi maswali haya mawili tungali hai hapa duniani; tuwe tayari kulia
na kusaga meno, na tusio na meno hakika tutasaga fizi. Usicheke! Ndugu yangu
katika hili, haijalishi hapa duniani ulikuwa nani, una umaarufu gani, cheo
gani, nafasi gani, na jina gani. Sote tunaitwa kuwa watakatifu kama Baba yetu
alivyo mtakatifu, Mt 5:48. Tukiwa tu waaminifu kwa kuyaishi hayo maswali
mawili, tutahuzunishwa na kukatishwa tamaa kama Nabii Yeremia alivyofanyiwa.
Nabii Yeremia kwa uchungu na unyonge, anamlilia Mungu kwa kusema, “Niangalie,
Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya
mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo,” Yer 18:19-20a.
Ndugu yangu, wapo
wanaotenda mema kila wakati lakini mwisho wa siku ni kuambulia masengenyo na
lawama. Tunapoona jambo hilo, tusikate tamaa kabisa. Hiyo ni alama ya kwamba
kazi uifanyao yampendeza Mungu na si mwanadamu. Hakuna mti wa mwiba upigwao kwa
mawe. Ni mti ule tu ulio na matunda, tena yalikomaa na kuwiva ndiyo
hushambuliwao kwa mawe. Katika hili Yesu anatuambia wazi, “Heri ninyi
watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili
yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa
maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Ndugu
yangu, wana heri tu wale wafanyiwayo hayo kwa jina la Yesu.
Tunapata neema na heri tunapoteseka
kwa ajili ya Yesu, na si vinginevyo. Kuteseka kwa ajili ya Yesu ni kuishi,
kutenda, kufikiri, na kupenda kama Yesu. Ni katika maana ya Ufalme wa Yesu
tunaweza kujifunza namna ya kutenda, kufikiri, kuishi, na kupenda. Kristo Yesu,
ni Mfalme wa Amani, Haki, Utii, Unyenyekevu, na Upendo. Kristo huyafanya haya
yote si kwa kutazamwa na watu, au kujipatia sifa binafsi, bali kwa KUTUMIKA, na
kuueneza Ufalme wa Baba yake. Hii ndiyo sababu ya Ukristo wetu.
Nabii Yeremia,
anahuzunishwa na mapigo anayoyapata kutoka kwa wale aliowapigania kwa jina la
Mungu. Mema yote aliyowatendea hawayaoni na badala yake wanakubali kuwa vipofu.
Yeremia, anasema, “Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa
ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate,” Yer 18:20b.
Ndugu yangu, wakutulipa
mema tunapoteseka kwa ajili ya Mungu na Mwanaye Yesu Kristo, na kwa kujua
sababu ya mateso hayo, si mwanadamu. Ukweli ni kwamba, “wasio haki watapotea,
nao wamchukiao Bwana watatoweka, kama uzuri wa mashamba, kama moshi watatoweka,”
Zab 37:20. Tuwe tayari kutumika muda na nyakati zote. Tuwe tayari kusema na
kuimba, “Bwana ni jabalí langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu,
mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome
yangu. Na wokovu wa wenye haki una
Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu,” Zab 18:2; 37:39.
Injili yetu ya leo
inalizungumzia kwa mapana swala hili la kutumika kwa ajili ya ufalme wa Mungu,
na ndiyo sababu ya Ukristo wetu, na utambulisho wetu mbele ya Mungu. Utambulisho
wetu mbele ya Mungu hautokani na sababu ya kukaa kushoto kwake au kulia kwake.
Jambo la msingi ni kuyaishi yale maswali mawili ya Msingi. Tukiwa waaminifu
katika hayo, Yesu anasema, “kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa
kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu,” Mt
20:23b. Waliowekewa tayari kwa maanisha wale walioyafanya mapenzi ya Mungu kwa
uaminifu. Swala hili halipo mwishoni mwa maisha yetu kama kupokea tunzo fulani,
bali kila siku ya maisha yetu twaishi tunzo hiyo, au kupokonywa tunzo hiyo.
Kila siku ya maisha yetu tupo darasani,
na mtihani wetu ni UPENDO. Upendo ndiyo mizania ya kila kitu tufanyacho.
Ndugu yangu
tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu, si
maisha ninayoishi, mfano; Maisha ya ndoa, Utawa, na Ukleri, au cho chote kile
ninachoishi kadiri ya wito wa Mungu, bali utambulisho wetu ni kwa namna
tunavyotumika kwa kuyatoa maisha yetu bila kujibakiza kwa upendo wake Mungu kwa
kile tulichoitiwa, na kama alivyofanya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Utambulisho
huu kwa maana nyingine ni UTAKATIFU tunaojichotea kwa maisha tunayoyaishi hapa
duniani kila mmoja kadiri ya wito wake. UTAMBULISHO huu ndiyo tunzo na
UTAKATIFU wetu mbele ya Mungu.
Ndugu yangu, kwa Mungu
hatuendi na “CV” zetu, kama tulivyozoea kusikua historia fupi ya Marehemu. Huko
Mbinguni hakuna kazi tena zaidi ya kuishi umelele tulioandaliwa, au kuteseka
katika umilele tuliojiandalia kwa kuishi ndivyo sivyo. Vyeti vyako, na historia
yako kitaaluma ikuwezeshe kuupata utakatifu huo kwa kutumika vyema. Kielelezo
chetu kama wafuasi wa Kristo, ni Kristo Yesu Mwenyewe.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na mtu ye yote anayetaka kuwa wa
kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt 20:27-28
Ee Yesu, nipe ufahamu wa kuelewa
vyema sababu ya yale yote unayonikirimia katika maisha na wito ninaoishi, nami
nitumike vyema kwa ajili ya wengine. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario