jueves, 18 de febrero de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 1 YA KWARESMA

IJUMAA WIKI YA KWANZA YA KWARESMA
19/2/2016
Somo: Eze 18:21-28
Zab: 130:1-2, 3-4, 5-7a, 7bc-8
Injili: Mt 5:20-26
Nukuu:
Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa,” Eze 18:21 

Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa,” Eze 18:26 

"Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai," Eze 18:27

Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa,” Eze  18:28

Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 5:20 

"Basi mimi nawaambia, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehenam ya moto," Mt 5:22.

Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23-24

TAFAKARI: “Tunaponywa na kuwa hai kwa kusamehe na kusamehewa.”

Wapendwa wana wa Mungu, karibuni tutafakari pamoja "uponyaji na uhai tuupatao kwa kusamehe na kusamehewa." Hili ndilo wazo kuu la Masomo yetu ya leo. Naomba tusafiri pamoja katika tafakari hii. Usiwe na haraka ya kumaliza kusoma. Usipopaelewa rudia tena kwa utulivu. Sasa tuanze safari yetu.

Ndugu yangu, swali la kujiuliza ni hili; Je, uponyaji na uhai huo tunaupataje? Kwa upande wa uhai, somo la kwanza limeeleza vizuri sana. Uhasili wa Mungu ni UHAI. Uhai ni zawadi kwetu na ni mali ya Mungu. Kama ni mali yake, Mungu hasingependa uhai huo ufifishwe kwa jambo lolote lile au kukatizwa kwa vyovyote vile.

Uhai tuliopewa na Mungu tuna uharibu na hata kuufifisha na kuua na kuutokomeza kabisa kwa dhambi na uovu. Njia moja na ya pekee kuupata na kuustawisha uhai huo ni kughairi njia mbovu na kumrudia mwenye uhai huo ambaye ndiye Mungu mwenyewe. Mungu anasema, "Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana Mungu; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?" Eze 18:23.

Ndugu yangu, wachagua kuishi au kufa? Wapo watu ambao leo tunaishi nao, sala yao kubwa kila siku ni kumuomba Mungu awape uhai ili waendelea kujiboofusha kwa maisha ya anasa na starehe. Pia wapo watu wengi leo wanaishi maisha ya taabu na mateso makubwa. Kauli mbiu yao ni "aheri ya jana kuliko leo." Je, Mungu halioni hilo? Je, Mungu mwenye kuhodhi uhai huu kwa nini yupo mbali na wanaoteseka?

Ndugu yangu, ni ukweli usiotia shaka kwamba sisi na vyote tulivyonavyo na kile tulicho ni mali ya Mungu. Swali ni kwamba, "Je! Tupate mema mikononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa mikono yake" Ayu 2:10b. Wapo wengi wanaokubwa na majaribu kama Ayubu. Ila kabla Mungu hajakujaribu na kuipima imani yako anajua kabisa jaribu hilo utalishinda na hasa pale utakapomwelekea Yeye tu. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13.  Mungu hawezi kuliumba jiwe kubwa akashindwa kulibeba. Huyo siye Mungu muumba mbingu na dunia. Huyo siye Mungu mweza wa yote. Hicho kitakuwa ni kitu kingine kabisa na ovyo kutokea!

Kwa upande mwingine Yesu anatupa angalisho kwa wale tunajiboofusha kwa anasa na starehe, na anasema, "Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?" Lk 9:25.

Ndugu yangu, uponyaji na uhai unapatikana kwa Mungu na kupitia mwanawe mpenzi Yesu Kristo tu. Kwa kuwa, "Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho." Yoh 6:44

Ndugu yangu, hasa ninayesafiri nawe kwenye tafakari hii, jeuri yako ya kutokughairi njia zako mbovu na ovu  zinatoka wapi? Bila Yesu utatoboa kweli mbingu? Yatupasa kutafakari sana juu ya maisha yetu na yenye kumpendeza Mungu. Majaribu yapo kila kona. Uhai huu tumekopeshwa tu kwa muda. Na hapa duniani tulipo ni mahali tu pa maandalizi ya maisha ya umilele. Kila mmoja wetu ajihesabie kwamba kengele ifuatayo kupigwa ni zamu yake. Je, umejiandaa? Au unapoteza muda kwa kuwaangalia wenzako na kuhesabu waliokufa, unaowazika na walikuwa mautiuti? Je, waona jambo hilo kwako haliwezi kutokea? Au lipo mbali? Ukweli ni kwamba nami pia nipo miongoni mwao. Ukweli huu hautoshi nisipozighairi njia zangu ovu na kuukumbatia uhai.

Wapendwa katika Kristo, Injili yetu ya leo yatufafanulia uponyaji kwa njia ya kusamehe na kusamehewa. Yesu katika hili anatoa angalizo kubwa na kusema, "haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni," Mt 5:20. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki kuwa ni watu wema, na ndiyo kipimo cha kweli. Ndugu yangu, Mungu pekee ndiye hutuhesabia haki, tena si kwa matakwa yetu, bali kwa matakwa yake kwa sababu  Yeye tu ndiye HAKI. Sisi binadamu tunashiriki tu ukamilifu wa Mungu kwa kuwezeshwa naye. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki na kuwa miungu watu. Huu ni upofu uliopitiliza. Kuwajua vizuri Mafarisayo na Waandishi nakualika usome sura yote ya 23 ya mwinjili Mathayo. Ni kwa sababu hiyo Yesu anatoa angalizo kwanza kama kweli tunataka uponyaji lazima kusamehe, kama hatua mahususi na kusamehewa ikiwa ndilo tokeo la tendo mahususi.

Kusamehe ni amri kama kweli na sisi tunataka kusamehewa. Sala ya ‘Baba yetu’ imeliweka jambo hili wazi kama sharti la upatanisho na Mungu. Cha ajabu sala hii tunaisali wengine kila siku na kila mara kwa siku, ila bado kusamehe ni shiiida! Je, utaponywaje kama tatizo lako ni kuvunjika mguu, ila "P.O.P" umefunga shingoni? Mbona kila siku unatibu ugonjwa usioumwa kwa dawa tofauti? Kwa nini inakuwiya vigumu kusamehe na kupatana na ndugu yako? Je, wewe ni mkamilifu sana? Unatofauti gani na mafarisayo na waandishi wanachukuwa nafasi ya Mungu kwa kujihesabia haki?

Agizo la Yesu ni kwamba, "patana na ndugu yako uwapo naye njiani," Mt 5:25. Maana yake ni nini? Ndugu yangu, maana yake yakupasa upatane na ndugu yako angali hai, na mungali mnaishi, ukiwa na ufahamu wa kutosha. Msivute muda pasipo sababu. Kengele ikishagongwa hakuna tena pa kujitetea. Maapizo na laana hazikusaidii chochote. Unazidi jizibia riziki zako bure kutoka kwa mwenyezi Mungu. Unaposamehe unajiponya na kumponya mwenzako pia. "Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi," Yoh 13:35.

Wapendwa wana wa Mungu, ibada na sadaka zetu kwa Mungu huwa safi na za kumpendeza Mungu pale tunapokuwa na amani ya kweli na ndugu zetu. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23-24. Amani hii ni pale unapokuwa tayari kupatana na kusamehe bila kipimo.

Tumsifu Yesu Kristo!

"Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai," Eze 18:27


Ee Yesu, nijalie Neema ya kughairi yasiyokupendeza. Nipe Neema ya kusamehe hata pale itakaponibidi kufanya sadaka kubwa. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario