JUMAMOSI WIKI YA 4 YA MWAKA-C
Somo:
1Fal 3:4-13
Zab:
119:9-14
Injili:
Mk 6:30-34
Nukuu:
“Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa
ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa
juu ya madhabahu ile,” 1Fal 3:4
“Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya
usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe,” 1Fal 3:5
“Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu
wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu
wako walio wengi?” 1Fal 3:9
“Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala
hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala
hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama
ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako
hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe,” 1Fal
3:11-12
“Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata
hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote,” 1Fal 3:13
“Na mitume
wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na
mambo yote waliyoyafundisha,” Mk 6:30
“Akawaambia, Njoni
ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa
sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula,”
Mk 6:31
“Naye aliposhuka
mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo
wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi,” Mk 6:34
TAFAKARI: “Omba
utakalo nikupe.”
Wapendwa wana wa Mungu, haki huenda wa
wajibu. Kumbe utimizapo wajibu wako vyema una haki ya kupata kadiri ya wajibu
uliutimiza. Jambo la ajabu wapo kati yetu wengi hupenda kutendewa haki ilhali
ni wachengaji wazuri sana katika kutimiza wajibu wao. Mfalme Sulemani anatimiza
wajibu wake mbele ya Mungu. “Basi mfalme akaenda
Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu za kuteketezwa juu
ya madhabahu ile,” 1Fal 3:4. Kwa kutimiza
wajibu huu, Mfalme Sulemani anahesabiwa haki mbele ya Mungu. “Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika
ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe,” 1Fal 3:5. Mungu
hufurahishwa sana pale unapotimiza wajibu wako vyema na kwa uaminifu kadiri ya
nafasi na wito wako.
Wajibu huu muhimu hautegemea uziri wa kile ufanyacho au aina
ya kazi ufanyayo, bali ubora katika kufanya na ukamilifu wake. Mtakatifu
Theresa wa Yesu, anasema kila mmoja wetu aweza kuwa mtakatifu hasa kwa matendo
yale madogo madogo tuyafanyapo kwa ukamilifu wake na uaminifu. Kwa tendo hili
la kumtolea Mungu sadaka ya kuteketezwa, Mfalme Sulemani anahesabiwa haki mbele
ya Mungu na kupata fursa ya kuomba atakalo. Jambo la kujifunza hapa kutoka kwa
Mfalme Sulemani ni kwamba pamoja na fursa hiyo, Mfalme anaomba kitu ambacho
kitaweza kumfanya atumike vizuri zaidi na kumpendeza Mungu. Mfalme anaukwepa
ubinafsi wake na kujali zaidi wale aliokabidhiwa kuwaongoza. Naye Sulemani
anaomba hivi, “nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na
kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako
walio wengi?” 1Fal 3:9. Mfalme Sulemani
anaomba hekima. Jambo hili pia linamfurahisha Mungu.
Wapendwa
wana wa Mungu, sala ya utakatifu kwanza kabisa ni kuwa na imani ya kwamba kile
uombacho ushakipata bila kuwa na shaka yoyote juu Mungu. Pili, sala ya
utakatifu ni sala ile isiyobeba ubinafsi wako. Ni sala au maombi yanayojali
wengine na kwa nafasi ya pekee wale ambao wapo chini yako au unao wajibika kwao
moja kwa moja. Ombi la Mfalme Sulemani linathibitisha sala ya utakatifu. Mungu
hufurahishwa sana na sala au maombi ya namna hii. “Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili,
wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako;
wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama
ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako
hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe,” 1Fal
3:11-12. Ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, yachunguze maombi
yako na sala zako mbele ya Mungu.
Mtume Yakobo anatupa angalizo juu ya sala na maombi yetu na
kusema, “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili
mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Kumbe sala ya utakatifu ni kuepuka pia tamaa
zako kwa kile uombacho. Ndugu yangu, Mungu anayafahamu mahitaji yako yote na
atakupatia kadiri ya mahitaji hayo. Kumbe unapoishinda nafsi yako katika
ubinafsi wake kwa maombi na sala zako, Mungu hukupatia hata yale ambayo
hukuyaomba kwa sababu anajua unayahitaji katika kweli na haki. Mfalme Sulemani
anapewa uhakika huo na Mungu. “Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata
hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote,” 1Fal 3:13. Mungu anayajua mahitaji yako yote. Jambo la
muhimu ni hili, ‘timiza wajibu wako kwa uaminifu.’
Wanafunzi
wa Yesu wanatimiza wajibu wao kwa uaminifu na wanatoa taarifu ya kile
walichokifanya mbele ya Yesu. “Na mitume
wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na
mambo yote waliyoyafundisha,” Mk 6:30. Tendo hili la uaminifu kwa yale
waliyoyafanya mitume linamfurahisha Yesu, naye anawaonea huruma. “Akawaambia,
Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike
kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo
nafasi ya kula,” Mk 6:31. Ni furaha iliyoje tunapohesabiwa haki kwa yale
tuyafanyayo kwa uaminifu na yule mwenye Mamlaka na Haki? Ni furaha ya kweli
kweli!
Ndugu yangu, kile ufanyacho kwa uaminifu na kuwajibika kuliko
tukuka hubarikiwa na wale uliwahudumia hubarikiwa pia. Na ndivyo ilivyokuwa kwa
wanafunzi wale wa Yesu. “Naye
(Yesu) aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu
walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi,” Mk
6:34. Hivyo ni vyema kuuthamini wajibu wako na kufanya kwa uaminifu wote. Leo
kama tungewajibika kwa asilimia 50 tu kila mmoja wetu kwa nafasi yake na wito
wake, ulimwengu huu, na kwa namna ya pekee nchi yetu ingekuwa mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Basi nikusihi ndugu yangu anza kuwajibika hapo ulipo katika
uaminifu wote. Acha mazoea katika utendaji wako wa kila siku.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ili
mwenende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie
katika ufalme wake na utukufu wake,” 1The 2:12
No hay comentarios:
Publicar un comentario