ALHAMISI
WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo:
Yer 7:23-28
Zab:
95:1-2, 6-7, 8-9
Injili:
Lk 11:14-23
Nukuu:
“Taifa hili ndilo
lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu
umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao,” Yer 7:28
“Lakini, ikiwa mimi
natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk
11:20
TAFAKARI:
“Huwezi
shindi vita na Mungu. Ushindi ni kuishi kwa ajili yake na katika yeye tu, yaani,
kujisalimisha kwake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tutafakari kwa undani juu ya neno hili, “Huwezi shindi vita na Mungu.
Ushindi ni kuishi kwa ajili yake na katika yeye tu, yaani, kujisalimisha kwake.”
Wengi wetu kwa kufahamu au kutokufahamu, tunaishi kwa kupingana na Mungu. Mfumo
huo kimaisha hautaweza kuleta mafanikio yo yote hata kama tukiweka bidii zetu
zote, yaani, nguvu, akili, na moyo katika mpango huo. Tendo hilo kiimani ni
kuwekeza pasipo na usalama. Huu ndio wito wa masomo yetu yote ya leo.
Somo la kwanza
linatueleza hasara ya kutosikiliza sauti ya Mungu kupitia watumishi wake
manabii. Waisraeli wanasahau kwamba hakuna kushinda bila uwepo wa Mungu.
Kinyume chake wanakosa baraka na msaada wa Mungu kwa kila wafanyacho. Hii ni
laana ya wazi kabisa. Mungu anasema kupitia kinywa cha Nabii Yeremia, “Taifa
hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho;
uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao,” Yer 7:28
Ndugu yangu, unapokosa
uaminifu mbele ya Mungu, hakuna mafanikio yo yote uwezayo kupata kwa sababu
huamini nguvu ya Mungu na msaada wa wake. Huku ni kujihesabia haki mbele ya
Mungu pasipo mastahili. Uaminifu mbele ya Mungu hujengwa kwa kujisalimisha
kwako. Kujisalimisha mbele ya Mungu ni tendo zima la KUABUDU.
Tendo hili la kujisalimisha kwa maana nyingine ni
kujiweka kwa ajili ya Mungu tu. Ni kujiweka wakfu kwa ajili yake, Kumfanya Yesu
Bwana wako, Kuchukuwa msalaba wako, Kuifisha nafsi, na Kujitoa kwa Roho
Mtakatifu. Ni kitu ambacho kibinadamu ni vigumu kufanya kwa sababu hakuna anayetaka
kupoteza kwa ajili ya kupoteza, hasa kwa ulimwengu wetu huu wa ushindani. Tupo
kwenye ulimwengu wa kushinda tu, na mashindano muda wote. Lakini Yesu anatupa
angalizo na kusema, “Kwa kuwa itamfaidia
mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi
yake?” Mk 8:36-37. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, njia
sahihi ya maisha yako ni kujisalimisha katika mikono salama ya Mungu.
Nini
maana ya kujisalimisha?
Kujisalimisha kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu
kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu hana hiari, au kuwa na
udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo. Inaweza kumaanisha
kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili kubadilisha
yanahitajika kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu waliojisalimisha
kwake kupiga vita kwa jina lake. Kujisalimisha sio kwa uoga au mazulia. Mungu
asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe kama mitambo
(robots) ili kumtumikia. Kujisalimisha siyo kukomesha utu wako. Badala ya
kukomesha utu wako, kujisalimisha hukutia nguvu. C. S Lewis alisema, “kadiri
tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi wenyewe, kwa sababu
yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu wote tofauti ambao mimi
na wewe tulikusudiwa kuwa… Ni pale ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi
yangu kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu halisi.”
Kujisalimisha kunadhihirika vyema katika KUTII. Unasema
‘ndivyo, Bwana’ kwa chochote anachokueleza. Kusema “hapana, Bwana” ni kutamka
vinyume. Hatuwezi kumwita Yesu Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada
ya usiku kucha bila kupata samaki, Simioni alionyesha kujisalimisha pale Yesu
alipomwambia kujaribu tena” “Bwana tumefanya kazi kwa bidii usiku wote na
hatujakamata samaki yeyote. Lakini kwa sababu umesema, nitatia nyavu majini,” Lk.5:5.
Watu waliojisalimisha hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na
maana.
Jambo lingine katika kujisalimisha ni IMANI. Ibrahimu
alifuata maelekezo ya Mungu bila kujua alikokuwa akienda. Hana alisubiri wakati
wa Mungu bila kujua ni lini. Mariamu alitarajia muujiza bila kufahamu
utatendekaje. Yusufu aliamini lengo la Mungu bila kujua kwa nini mazingira
yalikuwa hivyo. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa amejisalimisha kwa Mungu alipomtegemea.
Utafahamu umejisalimisha kwa Mungu unapomtegemea Mungu
akutengenezee mambo yako badala ya kujaribu kuwafanyia hila wengine, ukapitisha
jambo lako, na mwisho ukatawala mazingira hayo. Unamwachia Mungu afanye,
Huhitaji wakati wote kuwa, “mwangalizi.” Mzaburi anasema, “Jisalimishe nafsi
yako kwa Bwana, na umsubiri kwa uvumilivu.”
Zab. 37:7a. Baada ya kujaribu sana, umwamini zaidi. Pia unafahamu kwamba
unajisalimisha unapokuwa huchukizwi na lawama na kukimbilia kujitetea. Mioyo
iliyojisalimisha huonyesha mahusiano mazuri na wengine. Huwatupilii mbali
wengine, hudai haki zako, na hutumikii nafsi yako kama umejisalimisha.
Eneo gumu sana kwa watu wengi kujisalimisha ni PESA zao.
Wengi wamefikiri, “Nataka kuishi kwa ajili ya Mungu lakini pia nataka kupata
pesa nyingi ili niishi kwa raha baadaye nipumzike.” Kupumzika siyo lengo la
maisha ya kujisalimisha, kwa sababu huku ni kushindana na Mungu kwa sababu ya
kuweka mkazo kwanza kwa maisha yako. Yesu anasema, “Huwezi kutumikia Mungu na
pesa,” Mt. 6:24 na kwamba “popote hazina yako ilipo ndipo na moyo wako upo,”
Mt. 6:21. Yesu anatupa angalizo la shamba la mtu yule mmoja tajiri lililo kuwa
limezaa sana. Mtu huyu alipanga kujibohofisha; kupumzika, kula, kunywa na
kufurahi. Naye Yesu anasema, “Lakini Mungu
akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu
ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo
alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21.
Wapendwa wana wa Mungu, kielelezo kikubwa cha
kujisalimisha ni Yesu. Usiku ule kabla ya mateso Yesu alijisalimisha kwa mpango
wa Mungu. Alisali, “Baba kila kitu kinawezekana kwako. Tafadhali niondolee
kikombe hiki cha mateso. Lakini nataka mapenzi yako, siyo yangu,” Mk.14:36
Yesu hakuomba, “Baba, kama unaweza kuniondolea
maumivu haya, tafadhali fanya hivyo.” Alikuwa tayari amethibitisha kuwa Mungu
ana uwezo wa kufanya lolote! Badala yake aliomba, “Mungu, kama inapendeza kwako kuniondolea mateso haya, tafadhali
fanya hivyo. Lakini kama yanatimiza kusudi lako, ndivyo ninavyotaka
pia.
Kujisalimisha halisi husema, “Baba, kama tatizo hili,
maumivu, ugonjwa, au hali yoyote inahitajika kutimiza lengo lako na utukufu
kwako katika maisha yangu au ya mwingine, tafadhali usiliondoe.” Kiwango hiki
cha ukomavu hakiji kwa urahisi. Kwa upande wa Yesu, aliugua sana kuhusu mpango
wa Mungu kiasi cha kutoa jasho la damu. Kwa upande wetu, ni vita kali dhidi ya
asili yetu ya ubinafsi.
Kujisalimisha ndiyo njia bora ya kuishi:
Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama
sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa,
chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tamaa mbaya, au ubinafsi. Ulibuniwa
kumwabudu Mungu-na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine
(sanamu) ili uvipe maisha yako. Unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako,
lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, “kama
hutajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko.” Kujisalimisha si
njia bora ya kuishi; ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha
kukufanikisha.
Njia nyingine zote
hukuongoza kwenye kukukatisha tamaa, na kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King
James huita kujisalimisha “huduma yenu yenye maana.” Rum 12:1. Tafsiri nyingine
inasema, “njia yenye maana zaidi ya kumtumikia.” Rum 12:1 Kusalimisha maisha
yako si hisia za kipumbavu lakini ni tendo la akili na busara ambalo unaweza
kulifanya kwa ajili ya maisha yako. Ndiyo maana Paulo alisema, “Ni lengo letu
kwamba tumpendeze yeye,” 2Kor 5:9. Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo
unasema NDIYO kwa Mungu.
Wakati mwingine huchukua miaka, lakini hatimaye unagundua
kwamba kizuizi kikubwa kwa Baraka za Mungu maishani mwako sio watu wengine, ni
wewe mwenyewe, yaani, matakwa yako binafsi, kiburi cha hali ya juu, na
matarajio yako. Huwezi kutimiza lengo la Mungu kwa maisha yako huku ukikazania malengo yako binafsi.
Kama Mungu ataenda kufanya kazi ya kina ndani yako,
itaanza hivyo. Kwa hiyo mpe yote Mungu: kushindwa kwako hapo nyuma, matatizo
yako ya sasa, matarajio yako ya mbele, hofu zako, ndoto, udhaifu, tabia,
maumivu, na madhara yoyote uliyo nayo. Mweke Yesu katika kiti cha dereva wa
maisha yako na uondoe mikono yako toka kwenye usukani. Usiogope; hakuna
chochote katika uongozi wake kinaweza kupoteza dira. Chini ya uongozi wa Kristo
kunaweza kudumu chochote. Utakuwa kama Paulo, “Niko tayari kwa lolote na kuwa
sawa na chochote kwa njia ya yeye anayetia nguvu ndani yangu, yaani,
ninajitosheleza katika utoshelvu wa Kristo.”Flp 4:13
Kujisalimisha kwa Paulo kulitokea katika njia ya Dameski
alipoangushwa chini na mwanga mkali uliompofusha. Kwa watu wengine, Mungu
anapata mwitikio wao bila kutumia njia ya ajabu sana. Pamoja na hayo,
kujisalimisha siyo tukio la wakati mmoja tu. Paulo anasema, “Nakufa kila siku.”
I Kor 15:3 Kuna wakati wa kujisalimisha, na kuna tendo la kujisalimisha, ambalo
ni la muda-hadi-muda na maisha yote. Tatizo la sadaka iliyo hai ni kwamba inaweza kutambaa na kutoa madhabahuni, hivyo
unaweza kutakiwa kujisalimisha hata mara hamsini kwa siku. Ni lazima ufanye
jambo hili kuwa tabia yako ya kila siku. Yesu anasema,” kama watu wanapenda
kunifuata ni lazima waache mambo wanayoyapenda. Lazima wawe tayari kuacha
maisha yao kila siku na kunifuata,” Lk 9:23
Ngoja nikuonye: unapoamua kuishi maisha ya kujisalimisha
kikamilifu, uamuzi huo utapimwa. Wakati mwingine itamaanisha kufanya mambo
yasiyostahili, ya gharama, au yanayoonekana hayawezekani. Mara nyingi
itamaanisha kufanya kinyume cha unavyojisikia kufanya.
Lakini tukijipima nguvu
zetu na Mungu, kamwe vita hii hatuwezi kushinda. Ni kupiga ngumu kwenye upepo
au ukuta. Ni kujaza maji kwenye gunia la katani, kamwe halitajaa. Tujisalimishe
kwake, kwa kuwa, “Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza,
wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia,” Kumb 4:31. Katika historia ya
wokovu wetu, mara zote binadamu ameshindwa kwa kosa la kutojisalimisha kwa
Mungu.
Injili yetu ya leo
inafafanua kwa undani zaidi namna ya kujisalimisha, na hasa kujisalimisha kwa
ufalme wa Mungu. Ndugu yangu, katika miaka ile mitatu ya mwisho ya Bwana watu
Yesu Krisito, alisisitiza mambo makuu matatu; kwanza, kufanya toba ya kweli kwa
kuwa ufalme wa Mungu u karibu (Mk 1:15), Pili, kuwachagua na kuwaandaa wafuasi
wake kwa kazi hii ya kuhubiri habari njema (Mk 1:16-20, Mt 28:19-20), na tatu,
kulitakasa Hekalu (kama jengo na nyumba ya sala, na mwili ambao ni hekalu la
Roho Mtakatifu; Yoh 2:14-21, 1Kor 6:19)
Injili ya leo Yesu
Kristo analifanya jambo hilo la tatu; kulitakasa Hekalu-Mwili ambalo ni makazi
ya Roho Mtakatifu. “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu
aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa
kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” 1Kor 6:19-20.
Ndugu yangu, kwa vile
tusivyojisalimisha kwa Mungu, hujisalimisha kwa vitu au watu. Watu waliokuwepo
katika uponyaji wa bubu aliyekuwa na pepo bubu, wanamuhukumu Yesu kuwa anayafanya
hayo kwa nguvu za Beelzebuli. Mara nyingi huwa tunawahukumu watu kwa namna
tunavyofikiri na kutenda. Kwa vile wao huamini juu ya nguvu hizo za Beelzebuli,
wanafikiri na Yesu Kristo anayafanya hayo kwa nguvu hizo. La hasha! Yesu
anawaambia, “Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa
Mungu umekwisha kuwajilia,” Lk 11:20. Yesu anayafanya hayo kwa mkono wa Mungu.
Ndugu yangu, leo wapo
watu ambao hawaamini nguvu ya Mungu, na uwepo wa Kristo katika maisha yao. Watu
wa mtindo huu, wapatwapo na majaribu kidogo tu, hukimbilia kupata ishara nje ya
Kristo. Kristo kwetu anatosha. Hatuitaji ishara zaidi yake. Mateso, kifo na
ufufuko wake ni Ushindi mkubwa wetu na Ishara ya kutosha kabisa. Ndugu yangu,
kiguru na njia kila siku kwa waganga utaacha lini? Kama wewe ni Mkristo na
waamini uwepo wa Kristo katika maisha yako, mganga wa kienyeji ana nafasi gani
kwako? Kwa nini wajisalimisha kwa mwanadamu na wakati mwingine kwa shetani?
Ndugu yangu, elewa
jambo hili, “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu,
Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana,” Yer 17:5
Tumsifu Yesu Kristo!
“Taifa hili ndilo lisilosikiliza
sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea,
umekatiliwa mbali na vinywa vyao,” Yer 7:28
Ee Yesu Kristo, hakuna usalama na
hata ushindi nisipojisalimisha kwako. Nisaidie mara zote kuelewa kuwa Wewe ndiye Njia, Uzima, na Ukweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario