domingo, 6 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 4 YA KWARESMA

JUMATATU YA 4 YA KWARESMA

Somo: Isa 65:17-21
Zab: 30:2, 4, 5-6, 11-12a, 13b
Injili: Yoh 4:43-54
Nukuu:
“Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni,” Isa 65:17

“Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?””, Yoh 4:44,48.

TAFAKARI: “Mara zote Mungu huanza upya na watu wake; Kristo Yesu ndiye ufunuo halisi wa utimilifu huo wa Mungu”

Wapendwa wana wa Mungu, “Mara zote Mungu huanza upya na watu wake; Kristo Yesu ndiye ufunuo halisi wa utimilifu huo wa Mungu.” Nabii Isaya katika somo letu la leo anaelezea furaha hiyo ya Mungu kuanza upya na watu wake baada ya kuyaona mateso yao. “Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni,” Isa 65:17. Mwanzo huu mpya ni pamoja na kuwapa watu wake maisha marefu, ila watenda dhambi watalaaniwa ingawa watafaidi kwa kuwa na umri mrefu. Kwa namna nyingine, mafanikio yetu pasipo Mungu si kidhibitisho cha kufaulu kwetu. Amani ya kweli upatikana pale tunapomuhusisha Mungu yote tufanyayo.

Utimilifu huu wa kazi ya Mungu ya kuanza upya na watu wake inajidhihisha ndani ya mwanaye, yaani Yesu Kristo. Ishara za Yesu Kristo zadhihirisha utimilifu wa ahadi ya Mungu kuanza mpya na watu wake. Jambo hili liliwekwa wazi siku ya kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo. “Alipokuwa katika kusema, wingi jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika like wingu, ikasema, Huyu ni Mwangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5. Je, waamini maneno hayo?

Ndugu yangu, kufanikiwa kwetu kiimani, ikiwa ni kuanza yote upya kuelekea maisha ya umilele, mpango huu unawezekana tu kwa njia ya Yesu na ndani ya Yesu. Kinachoongoza safari hii ya kiimani ni Msimamo wa Imani tuliyonayo juu ya Yesu. Tunapokuwa na imani thabiti, yote hudhihirishwa ndani yetu. Tunapokuwa na imani Mungu hufanya mambo makubwa na kujidhihirisha kwetu. “Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya  haradali mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu,” Mt 17:20.

Kwa njia ya Imani hii,  leo tunaona uponyaji wa mtoto wa diwani. Kwa kuiona imani hii, Yesu anamwambia, “Enenda; mwanao yu hai.” Yoh 4:50. Ila tunapewa angalizo na changamoto katika swala la Imani. Tusiamini tu kwa sababa ya kuziona Ishara. Imani ya kweli haiitaji Ishara. Ila tunapoamini kweli, Mungu ujidhihirisha ndani ya kile tunachoamini. Kwa jambo hili Yesu anasema, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?” Yoh 4:48. Ishara si kigezo cha Imani. “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1.

Ndugu yangu, tusisahau kwamba, “kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri,” Ebr 11:3. Na ni kwa njia hii ya imani yote yawezekana katika Yesu Kristo Kristo, ambaye yeye twapaswa kumwamini na kumsikiliza kila wakati.

Kwa nini basi ndugu yangu kila siku unahama makanisa na vikundi vya kitume tutafuta ishara?

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa imani yote yanawezekana ndani ya Yes una kwa nñjia ya Yesu. Amina.

…Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki,” Lk 11:29-30

No hay comentarios:

Publicar un comentario