JUMATANO
YA WIKI KUU
Somo:
Isa 50:4-9a
Zab:
69:8-10, 21-22, 31, 33-34
Injili:
Mt 26:14-25
Nukuu:
“Naliwatolea wapigao mgongo
wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na
kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia, kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa
sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya,”
Isa 50:6-7
“Ni nini mtakachonipa,
nami nitamsaliti kwenu?” Mt 26:15a
“Wakampimia vipande
thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti,”
Mt 26:15b-16
“Mwana wa Adamu aenda
zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa
Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa,” Mt 26:24
TAFAKARI:
“Ujasiri na utayari wa Yesu kubeba aibu yetu itokanayo na dhambi; hakika ni
laana kubwa kumtenda kwenye haki.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tutafakari ujasiri na utayari wa Yesu Kristo kubeba aibu yetu itokanayo na
dhambi; hakika ni laana kubwa kwa kumtenda kwenye haki.” Kadiri tunavyoijongea
ile saa ambayo Bwana wetu Yesu Kristo anayatoa maisha yake kwa faida yangu na
yako, ndivyo tunavyouona ujasiri wake, na utayari wake katika kuyakabili mateso
na kifo hiki cha msalaba.
Nabii Isaya anatoa
wasifu wa mtu kwenye haki ambaye yupo tayari kuufia ulimwengu ili utakaswe na
kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Unabii huu unamlenga Yesu Kristo.
“Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha
uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia, kwa
sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume,
nami najua ya kuwa sitaona haya,” Isa 50:6-7. Tendo hili la ujasiri na utayari,
msingi wake siyo kujionyesha kwa ulimwengu kwamba anaweza, bali ni tendo
linaloonyesha unyenyekevu na kujishusha chini kabisa kusiko kwa kawaida.
Sifa na ukuu, si
lieleleza cha kujitoa sadaka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa sababu vyote
vilivyopo vimeumbwa kupitia yeye. “Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,”
Yoh 1:2-3. Yaliyopo katika ulimwengu huu kwa yenyewe hayawezi kusadifu
majitoleo na sadaka ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Tendo hili la
unyenyekevu msingi wake ni upendo. Mt. Augustino anasema ukipenda kweli
utafanya yote. Mungu kupitia mwanaye Mpenzi anatupenda upeo, na kwa maana hiyo
yupo tayari kufanya yote.
Pamoja na upendo huu wa
Mungu Baba kwetu, inatuwiya vigumu sisi wanadamu kutambua thamani yake, na
hivyo tupo tayari kuusaliti na hata kuushusha chini kabisa na kuufanya kama
bidhaa isiyo na mwenyewe. Hili linaonekana hasa tunapoona Yuda Iskariote
akifanya mnada kwa kumwuza Mkombozi wetu. Yuda Iskariote anataka kujua
atakachopata kwa kumsaliti Yesu kwa Wayahudi. Yuda Iskariote anawaauliza, “Ni
nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu?” Mt 26:15a. Wapendwa hakuna kitu
chochote ambacho tunaweza kubadilisha chenye dhamani ya uhai na utu wa mtu.
Hakuna popote hapa duniani ambapo unaweza kununua uhai na utu wa mtu.
Uhai na utu wako na
wangu, ni zawadi kwetu, na ni mali ya Mungu. Itakuwaje kuuza uhai utu wa yule
atoaye uhai? Yesu Kristo ni Uzima wetu. “Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna
uzima milele. Mimi ndimi chakula cha uzima.” Yoh 6:47-48. Uhai wa Yesu
unathaminishwa kwa vipande thelathini vya fedha. “Wakampimia vipande thelathini
vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti,” Mt
26:15b-16.
Uhusiano wa Yesu Kristo
na wanafunzi wake haukuwa ule wa mtumwa na mtwana, kiasi kwamba mtumwa
angeshawishika kumpindua na hata kumfanyia hila mtwana wake. Yesu Kristo
anasema wazi uhusiano wake na upendo wake kwa
wanafunzi wake; “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa
uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda
niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake;
lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu
nimewaarifu,” Yoh 15:13-15. Kwa mantiki hii, Yuda Iskariote hakuwa na sababu yo
yote ya kumsaliti Yesu Kristo. Hakuna jambo lolote baya Yesu Kristo
alilolificha juu ya wanafunzi wake.
Ndugu yangu, tunapoishi
maisha na kweli aliotufundisha Kristo, sisi tu rafiki zake Kristo. Tunapoishi
maisha ya usaliti katika kweli ya Kristo, hatuna mastahili hata kidogo kuwa
rafaki yake Kristo. Dhambi hii katika usaliti ndani na katika Kristo ni nzito
sana. Majuto yake ni sawa na kutokuwepo katika ulimwengu huu. Yesu anatoa
angalizo hili kwako na mwangu pia, kwa kusema, “Mwana wa Adamu aenda zake, kama
alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu!
Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa,” Mt 26:24. Je, leo Kristo
asalitiwi?
Ndugu yangu, Kristo
mara nyingi amejifananisha kwa maskini, hasa maskini wa roho na anasema hivi,
“heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3. Maskini
wa roho ni kwa yeyote yule mwenye uhitaji wa Mungu, mwenye nafasi ya Mungu
ndani yake, na yeyote yule ambaye mwenye hofu ya Mungu ndani yake na kuyafanya
yote ndani na katika Kristo. Maskini hawa tupo nao muda wote hadi mwisho wa
nyakati. “Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami
sikuzote,” Yoh 12:8. Leo maskini hawa ndio wahanga wa kudhulumiwa haki zao.
Ndiyo wanaotumika kama barabara na madaraja ya kuvukia matajiri, wafanya
biasha, na wanasiasa. Mwisho wa siku, maskini
hawa hawana mtetezi wala mahali pa kutolea kilio chao hasa kwenye
utawala ulio kithiri kwa rushwa na udhalimu kama Tanzania yetu leo.
Yesu Kristo katika
Taifa letu hili kupitia maskini hawa, anateseka sana na tunamsulubisha sana.
Hata wale ambao tuliowategemea kuwa sauti ya wasio na sauti-maskini, wamekuwa
mstari wa mbele kuwahujumu maskini ili kulinda nafasi zao na familia zao. Kundi
hili la uovu lielewe vizuri maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo kwamba ‘ingekuwa
heri kwao kama wasingezaliwa.’ Kama wapo hai na wanafanya vitendo hivi vya ukandamizani wajue fika hukumu ya Mungu
haikwepeki hata kidogo.
Hawa ndiyo wale
wanasiasa ambao wanamwuza Yesu kwa vipande thalamini vya pesa na kuusaliti umma
wa walio wengi. Dhambi hii ndugu yangu, hata ukiama chama kimoja cha siasa na
kuamia kingine kwa usaliti wako kamwe hutopata amani ndani mwako. Mwisho wa
siku ni kuchukua maamuzi ya Yuda Iskariote ya kujinyonga. Hawa ndio wale ambao
wanafupisha maisha ya mabinti wadogo kwa kuwauza kwa “sahani ya chips, nusu
kuku, na soda ya Pepsi.” Hakika afadhali wasingelizaliwa! Laana hii
haitawaacha. Hawa ni wale ambao kwa kudanganywa na ulafi wao wa madaraka na
mali wapo tayari kuwauwa walemavu wa ngozi “Albinos” kufikia haja zao. Hakika
afadhali wasingelizaliwa! Wanaendeleza soko la kumnadi na kumwuza Yesu Kristo.
Ndugu yangu, yawezekana
umezoea kuzinyonga haki za wanyonge kwa njia mbalimbali, elewa leo usomapo
tafakari hii, ni mwaliko wa kuacha kumtesa na kumdhalilisha Kristo. Tenda haki
hata pale pasipo na msukumo wa kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo utakuwa mtetezi
wake Yesu Kristo, naye atakutetea mbele za Baba yake aliye mbinguni. “Basi,
kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye
mbinguni,” Mt 10:32. Kuwatetena wanyonge na kuwatendea haki, ni kumkiri Mungu
mbele za watu. Je, ni mara ngapi nimeshindwa kufanya hivyo kutokana na wito
wangu, nafasi yangu, cheo changu, na uwezo wangu?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwana wa Adamu aenda zake, kama
alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu!
Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa,” Mt 26:24
Ee Yesu, niongoze katika njia ya
haki na kweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario