miércoles, 2 de marzo de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 3 YA KWARESMA

IJUMAA WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo: Hos 14:2-10
Zab: 81:6c-8a, 8bc-9 10-11ab, 14, 17
Injili: Mk 12:28-34
Nukuu:
“Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo, kwa maana hasira yangu imemwacha,” Hos 14:4

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Mk 12:30-32

TAFAKARI: “Kumpenda Mungu, Nafsi, na Jirani”

Wapenda wana wa Taifa la Mungu, kadiri ya masomo ya leo na tufakari kwa pamoja, “kumpenda Mungu, Nafsi, na Jirani.” Wapendwa neno upendo si geni katika masikio yetu. Ni neno linalotumika sana, na kwa mizania hiyo ni neno linaloongoza kwa kuchakachuliwa sana na kupoteza ule umaana wake. Neno hili upendo limebeba maana tofauti kwa kila kundi au rika la watu, hasa katika jamii yetu ya leo. Kwa watoto neno upendo huwa na maana na tafsiri nzuri pale tu wazazi wao wanapoishi na kuonyesha upendo huo wao kwa wao, na kwa familia. Wazazi wakiishi hovyo basi na watoto huwa na mwono mbaya wa upendo.

 Neno upendo kwa vijana walio wengi linatafsiri ya usaliti. Waliosalitiwa kwa upendo hukosa kuamini uhalisia wa upendo, na hivyo hubaki katika hofu na majuto muda wote. Humfanya kijani kuishi katika hatia. Hatia hii huondoa umaana wa maisha na makusudi halisi ya uumbaji wake. Maisha na uzuri wake hukosa mwelekeo wa Kimungu, na kubaki katika hali ya kutofahumu muda wote. Ni vigumu kuamini tena kama kuna upendo wa kweli. Mara nyingi kijana huyu anapoyajenga mahusiano na kijana mwenzake baada ya usaliti wa kwanza, swala la kwanza na la msingi kujua huwa hivi, “tafadhili sipendi kuumizwa tena, kama upo ‘serious’ na utakacho niwe mimi na wewe.”

Kwa walio na umri wa kati-wazazi walio wengi, neno upendo linatafsiri ya “yawezekana,” katika hali ya sintofaumu bado. Wengi katika kundi hili bado wanatafuta upendo wa kweli na kuishi katika mahangaiko yasiyo na kikomo. Wazazi walio wengi, upendo haupo tena, na hivyo huamisha mapendo yao kwa watoto kama wamebahatika kuwa nao. Ndoa yao ina uhai kwa sababu ya watoto. Nyumbani wazazi hawa huishi kama wapangaji. Wote wawili yaani baba na mama wanaishi katika mfumo wa “kukubaliana kwa kutokubaliana,” yaani ilimradi liende tu.

Kwa kundi la wazee, upendo hutegemea historia nzima ya ujana wao, na uzazi wao ulivyokuwa. Kama waliishi vizuri hatua hizo, basi uzee wao hujaa matumaini makubwa na furaha. Kama waliishi hovyo, basi uzee wao huwa na mateso makubwa sana. Hutamani wakati kwingine kufa mapema. Kila kitu kwao huwa kibaya. Kila siku kwao huishi kwa kulalamika na kutoa laana.

Ndugu yangu, hata wewe unayesoma tafakari hii, unayo mengi ya kusema kuhusu upendo na hasa ukiyatazama maisha yako unayoishi sasa, uliyaishi na mtazamo wako wa baadaye. Upendo wa Binadamu yeyote anayemjua Mungu na asiye mjua Mungu, huegemea katika mambo matatu; kwa mwenye imani na uwepo wa Mungu, basi atampenda Mungu; Nafsi yake; na jirani yake. Asiyeona uwepo wa Mungu, basi badala ya Mungu atapenda kitu fulani ua nguvu fulani, nafsi yake, na jirani yake.

Somo la kwanza, msisitizo upo katika kumpenda Mungu. Tunampenda Mungu kwa sababu ya kile tulicho, kwamba tumeumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27, na hivyo ipo nguvu ndani yetu inayotuvuta kwake, ingawa twaweza kumsaliti, na kufuata njia zetu kutoka na uhuru aliotuachia. Twampenda Mungu pia kwa sababu Yeye ni UPENDO, MSAMAHA, na yote MEMA upatikana kwake. Ukamilifu wote upo kwake. Yeye ni yote katika yote. Naye Mungu anasema, “Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao, nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo, kwa maana hasira yangu imemwacha,” Hos 14:4.

Ndugu yangu, Mungu ni mwema na hutuwazia mema muda wote. Tunapoasi na kumsaliti, huadhibiwa kadiri ya makosa yetu. Ila tunapojirudi na kukiri wema wake, Yeye husamehe yote na kuanza mpya nasi. “Kwa maana Bwana asema hivi, Kama nilivyoleta mabaya makuu haya yote juu ya watu hawa, vivyo hivyo nitaleta juu yao mema yote niliyowaahidia,” Yer 32:41. Tunachotakiwa kufanya nyakati zote ni kutenda mema na kutafuta mema kwa watu wote. “Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana, Mungu wa majeshi, watawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu,” Amo 5:15.

Ndugu yangu, leo katika Taifa letu tumefikia hatua mbaya sana. Leo kuutoa uhai wa mtu na kuufanyia mzaha mwili wa mtu ni jambo la kawaida na la kufikika. Jamii yetu leo ishaanza kuzoe hali hii. Ndugu zetu kwenye ulemavu wa ngozi-Maalbino, hawaishi tena kwa amani na matumaini. Viongozi wetu na wana harakati wanaosema na kukemea maovu wanauwawa na hata kupoteza baadhi ya viungo vyao kutoka na utawala dhalimu tulionao.

Je, Mungu anasema nini kuhusu jambo hili? Tusidhani kuwa Mungu hayaoni mambo haya. Mungu anasema, “ninyi mnaoyachukia mema, na kuyapenda mabaya; ninyi mnaowachuna watu ngozi yao, na nyama mifupani mwao. Naam, mnakula nyama ya watu wangu, na kuwachuna ngozi zao, na kuivunja mifupa yao; naam, kuwakata vipande vipande kama kwa kutiwa chunguni, na kama nyama sufuriani. Ndipo watakapomwomba Bwana, asiwaitikie; naam, atawaficha uso wake wakati huo, kwa kadiri walivyotenda mabaya kwa matendo yao,” Amo 3:2-4. Kwa matendo haya, tunajichumia laana kila siku kama Taifa.

Ndugu yangu, Injili yetu ya leo, inaliweka jambo hilo katika matendo; kumpenda Mungu, nafsi, na Jirani. Mizania ya kumpenda Mungu na jirani ni upendo ulionao wewe na hali uliyonayo kwa kujipokea kama ulivyo. Ni vigumu kumpenda Mungu na Jirani, kama wewe mwenyewe hujipendi, hujipokei, na hujithamini. Katika jambo hili,  Bwana wetu Yesu Kristo anasema, “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake,” Lk 6:45. Wapendwa, binadamu ye yote yule hutoa kwa wengine kile alichonacho. Huwezi kutoa usicho nacho. Hukumu yetu siku ya mwisho imejikita katika kutenda mema. Fanya ufanyacho leo katika maisha yako, lakini usisahau kutenda mema. Kutenda mema ikiwa ndiyo dira ya maisha yako kila siku, kamwe hutowaza kutenda mabaya.

Tendo hili la wema hutuinua hasa pale tunapolifanya hata kwa wabaya wetu. Tunainuliwa na kuwa wana wa aliye juu. Hiki ndicho cheo chetu chenye thamani kubwa kuliko vyote tunavyoweza kufikiri. Cheo hiki ni utakatifu wako. Katika jambo hili, Yesu anasema, “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu,” Lk 6:35. Tendo hili licha ya kutufanya wana wa Aliye juu, linatupa uhakika na mastahili ya Mungu kwa  uzima wa milele. Kwetu kama binadamu ni changamoto kubwa sana. Ukitenda mema utasemwa vibaya, na usipotenda mema utasemwa pia vibaya. Kilichobaki ni kutenda mema na kutotazama macho ya watu na maoni yao ikiwa jambo hilo linakibali mbele ya Mungu, kwani, “wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele,” Rum 2:7. Je, jambo hili maana yake nini?

Ndugu yangu, utendapo mema fanya hivyo pasipo ubaguzi. Usifanye kwa vile huyu ni ndugu yangu au kwa vile ninamfahamu. Fanya mema kwa vile wema ni sifa ya Mungu. Nitende sifa ya Mungu na kwa ajili ya Mungu. Kwa mantiki hii, “msilipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote,” Rum 12:17. Kati ya vitu ambavyo Mungu hutujibu mara moja tutendapo ni swala hili la wema. Na hapa ndipo tunaposema kwamba Mungu ni “mwema kila wakati.”  Utendapo jambo jema, Mungu hukujibu kabla ya kuzimia roho yako. Mpendwa, “tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu,” na tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho,” 2Kor 8:21, Gal 6:9. Tenda wema ndugu yangu na uende zako, wala usingoje shukrani.

Hii ndiyo sababu kubwa ya maneno ya Yesu katika injili ya leo, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Mk 12:30-32. Ndugu yangu, elewa kwamba, unaweza kutoa kitu bila kupenda hasa pale mtu huyo anaposisitiza kitu hicho, na ukasukumwa kutoa ili uachane na karaha ya kusumbuliwa. Ila huwezi kupenda bila kutoa. Kwa maana hiyo, upendo wetu kwa Mungu na Jirani unaonekana na kutulazimu kwa upendo kujitoa na kutoa. Tunatoa kwa Mungu na Jirani; nafsi zetu, muda wetu, maarifa yetu pamoja na vipaji vyetu, na mali tulizonazo. Anayeyaishi haya na kuyatenda kesha mwona Mungu.

Ndugu yangu, “mpenzi, usiuige ubaya, bali uige wema. Yeye atendaye mema ni wa Mungu, bali yeye atendaye mabaya hakumwona Mungu,” 3Yoh 1:11.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini ninyi, Ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema,” 2Kor 3:13


Ee Yesu Mwema, uliufia ulimwengu kwa sababu ya kunipenda kuliko vitu vyote. Nami nijalie neema hiyo ya kupenda kama ulivyonipenda. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario