martes, 15 de marzo de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 5 YA KWARESMA

ALHAMISI WIKI YA 5 YA KWAREMA
Somo: Mwa 17:3-9
Zab: 105:4-5, 6-7, 8-9
Injili: 8:51-59
Nukuu:
“Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako,” Mwa 17:9

“Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele,” Yoh 8:51 

TAFAKARI: “Neno la Mungu ni Uzima wetu; Imani ndiyo msingi wa yote”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, “neno la Mungu ni Uzima wetu; Imani ndiyo msingi wa yote.” Kwa kuamini kwake Ibramu mambo mawili yanamtokea. Kwanza, jina lake lina badilika na kuwa Ibrahimu, yaani Baba wa mataifa mengi. Pili, Mungu anafanya naye agano la Milele. “Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako,” Mwa 17:9

 Agano hili, Mungu anahiari mwenyewe kuwa Mungu wake Ibrahimu, na kumilikisha mambo yote kwa ajili ya kizazi chake Ibrahimu na kizazi kijacho. Urithi huu na heshima hii kwa Ibrahimu imetokana na kuamini kwake kusiko na mashaka.

Katika injili ya leo tunaona mdahalo wa Yesu na Wayahudi, ambao unapelekea Wayahudi kutaka kumpiga mawe Yesu. Mzozo unazuka pale Yesu anapowashauri kulishika neno lake na kutokuona umauti. “Amin, amin, nawaambia: Mtu akishika neno langu, hataona mauti milele.” Yoh 8:5. Kulishika neno la Yesu ni kuamini asemacho na kumwamini yeye. Neno kwa maana nyingine ni yeye mwenyewe ambaye kwa kupitia neno Yeye alifanyika mwili, Yoh 1:14.

Ndugu yangu, unamwamini Yesu? Yesu Kristo ana nafasi gani katika maisha yako? Tulio wengi Yesu wetu ni Yesu wa historia. Ni yule tunayemtazama kwa mbali na tena tukiwa na shida na tunafanya hivyo tukiwa na mashaka makubwa kama ataweza kufanya kitu hasa kwa kile kinachotusibu. Tunapokuwa hatuna nafasi ya Yesu ndani ya Mioyo yetu, basi ni wazi nafasi hiyo kuna kitu badala yake. Kwa Wayahudi nafasi ya Yesu haikuwepo na badala yake kulikuwa na nafasi ya Ibrahimu ambaye pia hawakumjua. “Yesu akawaambia, “Amin, amin, nawaambia: Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.” Basi wakaokota mawe ili wampupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.” Yoh 8:58-59

Tumsifu Yesu Kristo!

“Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele,” Yoh 8:51

Karibu moyoni mwangu Yesu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario