JUMANNE
WIKI YA 4 YA KWARESMA
Somo:
Eze 47:1-9, 12
Zab:
46:2-3, 5-6, 8-9
Injili:
Yoh 5:1-3a, 5-16
Nukuu:
“Tena itakuwa, kila
kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyom kitaishi;
kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko, maana
maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi popote utakapofikilia mto huo,”
Eze 47:9
“Akawajibu, “Yeye
aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, ‘Jitwike, uende,’” Yoh 5:11
TAFAKARI:
“Uzima na uponyaji upo ndani na katika Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, “uzima na uponyaji upo ndani na katika Yesu Kristo.” Maono ya Nabii
Ezekieli juu ya mto wa uponyaji ambao chanzo chake ni patakatifu, unatupa
maandalizi ya Mungu katika uponyaji ambao umekamilika ndani na katika Yesu Kristo.
Ndani ya maji hayo kutakuwa na uzima na kila kiumbe kitapata uhai. “Na karibu
na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa
chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe;
utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali
patakatifu. Na matunda yake yatakuwa ni chakula, na majani yake yatakuwa ni
dawa,” Eze 47:12
Ndugu yangu, neema na
baraka kadiri ya maono ya Nabii Ezekieli kulingana na mto huu zipo ndani ya Kristo, na Kikanisa
zinajidhihirisha katika masakaramenti yake. Katika injili ya leo, uzima na
uponyaji wajidhihirisha katika Kristo. Ndani ya Kristo tunapata uhai na uzima
tele. Ndani ya Kristo tunapata neema na baraka. Ndani ya Kristo tunatambua
njia, kweli, na uzima kuelekea umilele.
Katika uponyaji huu,
Yesu anamuuliza huyu asiyejiweza, “Wataka kuwa mzima?” Yoh 5:6. Ingawa jibu la
huyu asiyejiweza haliendani na swali (“Bwana, mimi sina mtu wa kunitia
birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu wingine hushuka
mbele yangu,” Yoh 5:7), Yesu anajua mateso na mahangaiko yetu, na hivyo
analitenda jambo kuu kwa ndugu huyu.
Yawezekana kutokana na
mahangaiko na mateso tuliyonayo, iwe ni ugonjwa au kitu kingine, yameshatufanya
tupoteze ufahamu na mwelekea wa matumaini. Lakini tukumbuke kwamba katika hali
hiyo Yesu anatuuliza kama twataka kuwa wazima. Yesu anaturudishia hadhi yetu na
utu wetu kuufanya upya na kutufanya tuanze maisha mapya. Angalisho kubwa katika
maisha haya mapya, ni kutokutenda dhambi. “Angalia, umekuwa mzima; usitende
dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi,” Yoh 5:14.
Ndugu yangu, tunaishi
katika neema na baraka zake Mungu tunapokuwa katika hali ya usafi kiroho na
kimwili, yaani hali ya kutokutenda dhambi. Kwa kipindi hiki cha kwaresma
tunapotafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni kipindi
pia cha kujitakasa kwa sala, na kuziungama dhambi zetu. Ndugu yangu, “tukisema
kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi
zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi,
twamfanya Yeye kuwa mwongo wala nena lake halimo mwetu,” I Yoh 1:8-10
Tumsifu Yesu Kristo!
“Maana
kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru,” Zab 36:9
Ee Yesu, ndani yako na katika wewe
upo uzima na uponyaji. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario