domingo, 13 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 5 YA KWARESMA

JUMANNE WIKI YA 5 YA KWARESMA

Somo: Hes 21:4-9
Zab: 102:2-3, 16-18, 19-21
Injili: Yoh 8:21-30

Nukuu:
“Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu,” Hes 21:5

“Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti; hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi,” Hes 21:9

“Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu,” Yoh 8:23-24

“Mtakapokuwa mmemwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo,” Yoh 8:28-29

TAFAKARI: “Uovu wa Mwanadamu na ghadabu ya Mungu, toba ya kweli na Msamaha wa dhambi kupitia kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo Msalabani.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo na tutafakari neno hili, “Uovu wa Mwanadamu na ghadabu ya Mungu, toba ya kweli na Msamaha wa dhambi kupitia kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo Msalabani.” Huu ndio ukweli tunaouona katika somo letu la leo na injili.

Kwa uovu na hasa dhambi ya manung’uniko ya Wayahudi kule jangwani, Mungu anaghadabika, na hivyo anatuma nyoka za moto na watu wanang’atwa na kufa kwa idadi kubwa. “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, “ Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu,” Hes 21:5

Ni jambo la kawaida na la hulka ya mwanadamu kulaumu na kusahau yote ya nyuma mazuri anapopatwa na shida, na wakati mwingine kukosa shukrani. Ni wazi pia katika maisha yetu huwa rahisi kukumbuka siku za shida kuliko siku zile ambazo mambo yalituendea vyema. Manung’uniko ya Wayahudi yanafuta mema yote Mungu aliyo watendea na hasa kuwatoa utumwani Misri. Manung’uniko yao yanakuwa chukizo kwa Mungu. Wayahudi wanakosa uvumilivu na moyo wa shukrani.
Ndugu yangu, “Moyo usio na shukrani ukausha mema yote.” Tendo lako la shukrani kwa Mungu ni kutambua mema aliyokutendea na anayokutendea bila mastahili yako. Tendo hili la shukrani hubadilika na kuwa ombi tena kwa kile alichokukirimia kwa upendo wake.

Mungu kamwe hachelewi kurudisha ukarimu wake kwetu mara tunapotambua ukengefu wetu, na kumrudia kwa toba. Wayahudi wanatambua kosa lao na wanaomba huruma ya Mungu kupitia Musa Mtumishi wa Mungu. Mungu anampa Musa maelekezo ya  kufanya toba hiyo. Maagizo hayo ya Mungu kwa Musa ni kama ifuatavyo, “Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti; hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi,” Hes 21:8-9. Mimi na wewe kila mmoja akiitazama historia yake tunaweza kugundua ni maeneo gani tulikosa moyo wa shukrani na kudongoka katika dhambi ya manung’uniko. Hivyo ni wakati muhafaka wa kupokea huruma hii ya Mungu kwa kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi.

Injili ya leo imebeba taswira hiyo hiyo kama tulivyoona katika somo letu la leo. Wayahudi hawasadiki ayafundishayo Yesu Kristo. Kristo licha ya kuyasema yote wazi wazi na kuwapa chimbuko la yale ayasemayo, bado wayahudi wanakuwa na shingo ngumu kuyasadiki. Kwa kosa hili la kutokuamini kwao, Yesu anawaambia watakufa kwa dhambi zao. “Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu,” Yoh 8:23-24.

Hali ya ubinadamu wetu ni hali ya chini katika maana halisi ya anguko letu katika dhambi. Hali hii ya ubinadamu wetu, inaitaji msaada na neema ya Mungu kufikia ukamilifu. Mwenye uwezo wa kuyakamilisha haya ndani mwetu na kuujenga tena uhusiano wetu uliobomoka kwa sababu ya dhambi ni Kristo ambaye ni mpatanishi kati yetu na Mungu. Kwa mantiki hii, tusipoyasikia na kuyasadiki ayasemayo Kristo, hatutaweza kuokolewa katika dhambi zetu. Ni kwa kupitia Yesu Kristo kwamba, “mtu huyu Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na Msamaha wa dhambi,” Mate 5:31. Kwa tendo hili, Yesu Kristo ni zaidi ya Musa kwa sababu, “Mungu alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:13-15.

Ndugu yangu, hakuna njia nyingine kwetu kama Wakristo na wenye kufuata mafundisho yake Kristo, kupata wokovu na msamaha wa dhambi bila Yesu Kristo. Tendo hili Yesu kalikamilisha pale Msalabani alipoinuliwa kwa sababu ya dhambi zetu. Na hivi Yesu anasema, “Mtakapokuwa mmemwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo,” Yoh 8:28-29. Kama iliyokuwa nyakati za Musa walivyopata uponyaji kwa kupitia nyoka ya shaba kule jangwani, msamaha wa dhambi zetu, na wokovu unapatikana kwa kupitia mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.

Ndugu yangu tendo hili linawezekana tu kwetu tunapokuwa tayari kufanya toba ya kweli na kumrudia Mungu. Kristo muda wote yupo katika kiti chake cha hukumu yaani msalabani akiwa ameifungua mikono yake na kutuambia, “ona imefanya haya yote  kwa sababu ya upendo wangu kwako, njoo nami nakupokea kama ulivyo.” Je, mpendwa katika Kristo, washiriki mara kwa mara upendo wa Mungu katika Sakramenti yake ya upatanisho?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mtakapokuwa mmemwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo,” Yoh 8:28


Asante Yesu kwa kunipenda na kunipokea kama nilivyo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario