KUFUFUKA KWA BWANA WETU YESU KRISTO
USIKU MTAKATIFU
VIJILIA YA PASAKA
Somo I: Mwa 1:1-2:2
Somo
II: Mwa 22:1-18
Somo III: Kut 14:15-15:1
Somo IV: Rum
6:3-11
Zab: 118:1-2, 16-17, 22-23
Injili: Lk
24:1-12
Nukuu:
“Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura
yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi
yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26
“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu
alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba,” Mwa 1:27
“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke,
mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na
kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa 1:28
“Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye,
Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu
ya mlima mmojawapo nitakaokuambia,” Mwa 22:2
“Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee
neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao,
mwanao wa pekee,” Mwa 22:12
“Katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha
nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na
uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na
katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti
yangu,” Mwa 22:17-18
“Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao
wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake
lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake,” Kut 14:17
“Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu
wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na
mpanda farasi amewatupa baharini,” Kut 15:1
“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika
mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa
Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4
“Maana kwa kule kufa
kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia
Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi
jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu,” Rum
6:10-11
“Magdalene, na Mariamu
yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana
alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia,” Mt
28:1b-2
“Na
sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi
wakatetemeka, wakawa kama wafu,” Mt 24:3-4
“Malaika
akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa
mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni,
mpatazame mahali alipolazwa,” Mt 28:5-6
“Na
tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu,
wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende
Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt 28:9-10
“Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti,
aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka,” Mk 16:6
“Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro,
ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7
“Ikawa
walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama
karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia,
Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?” Lk 24:4-5
“Hayupo
hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, akisema, Imempasa Mwana wa
Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya
tatu,” Lk 24:6-7
“Nao
ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake
wengine waliokuwa pamoja nao; hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo. Maneno yao
yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki,” Lk 24:10-12a
“Lakini Petro aliondoka
akaenda mbio hata kaburini, akainama akachungulia ndani, akaviona vile vitambaa
vya sanda tu; akaenda zake akiyastaajabia yaliyotukia,” Lk 24:12b
TAFAKARI: “Mnamtafuta
Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa, amefufuka; yupo nasi kila siku katika maisha
yetu, na tunakutana naye Galilaya.”
Wapendwa
wana wa Mungu, Usiku huu Mtakatifu, Mama Kanisa popote duniani anafanya sikukuu
kubwa sana, ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ufufuko wa Bwana wetu Yesu
Kristo ni ushindi dhidi dhambi na Kifo. Ufufuko wa Yesu Kristo ni hitimisho la
malengo ya Mungu kumkomboa mwanadamu, na ni hakikisho la umilele, na maisha
mapya ndani ya Kristo, na katika Kristo kuelekea umilele. Hivyo Usiku huu
Mtakatifu tunasoma habari hii Njema ya wokovu wetu kama ilivyoandikwa na
Wainjili ‘fanana’ watatu, ikiwa kila mwaka
kulingana na mwaka wa Kanisa tuliopo. Kwa namna hiyo, usiku huu tukiwa
mwaka “C” wa Kanisa tunasikia simulizi hili kuu kama lilivyosimuliwa na
Mwinjili Luka 24:1-12. Kwa mwaka “B” wa Kanisa tulisikia kutoka Mwinjili Marko
16:1-8, na kwa mwaka “A” wa Kanisa tulisikia simulizi hili kuu kutika Mwinjili
Mathayo 28:1-10.
Wapendwa
wana wa Mungu, masomo yote ya agano la Kale tuliyoyasikia usiku huu Mtakatifu,
yanatupatia historia nzima ya wokovu wetu. Kwa maana hiyo, uwepo wetu hapa
duniani si wa bahati mbaya, wala wewe kuwa katika ulimwengu huu si kwa bahati
mbaya. Ulimwengu umeumwa kwa Upendo wa Mungu kwa upande mmoja, na kwa upande
mwingine ulimwengu huu kama ulivyo umemlenga mwanadamu na kwa lengo la kumweka
huru.
Msingi
wa haya yote, na sababu yake, tunauona kwenye kitabu cha mwanzo. Wakati
ulipotimia na kufaa, Mungu aliumba ulimwengu kwa neno, na ukawa kama ulivyo. Ni
siku ya sita alipoona inafaa na kumpendeza akamwumba mwanadamu kwa sura na
mfano wake. “Mungu akasema, Na
tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na
ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa
kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26. Kwa vile ulimwengu ulimlenga mwanadamu, ni
binadamu huyu tu, anayepewa mamlaka ya kuvitawala vile alivyoviumba Mungu.
Utawala huu siyo wa kujifanyia tunavyotaka, ila kuvimiliki katika maana ya
kuvitunza ili viongezeka na kudumu. Tunapewa wajibu huu mkubwa kabisa ambao
hata malaika hawakupewa.
Binadamu huyu kwa upendo wa Mungu, ameumbwa katika usawa.
Hakuna mtumwa na mtwana, au bwana na mjakazi. Wote tumeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu tukiwa na mastahili sawa kati ya mwanaume na mwanamke. “Mungu akaumba
mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba,” Mwa 1:27. Mastahili haya yanaendana na wajibu wetu, kila mmoja
kadiri ya jinsia yake. Kwa upande mwingine, haikumaanisha kwamba jinsia moja
kuitawala nyingine kwa vigezo vya utamaduni wetu, mila zetu, makabila yetu,
wala utaifa wetu. Mbele za Muumba wetu sote tu sawa.
Na ni kwa sababu hii, kunakuwa na uwezekano wa kuzaa na
kuongezeka kadiri ya mpango wa Mungu. Ni kwa sababu hii binadamu anabarikiwa,
anawezeshwa na anashirikishwa uumbaji wa pamoja akishirikishwa na Mungu.
Binadamu anakua “Co-creator of God.” “Mungu
akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na
kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe
chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa 1:28. Ndugu yangu, pamoja na uhuru
tuliopewa, Mungu hakutupa mamlaka ya kubadili mpango wake ndani yetu.
Leo
kutokana na ufahamu wa binadamu kuongezeka katika kuyafahamu yanayomzunguka,
amefikia hatua ya kumkosoa Mungu, na kufanya kinyume cha kile alichokinuia. Leo
wapo baadhi yetu wangependa na wanapigania kwa nguvu zao zote kujigeuza jinsia
zao na kuwa vingine. Hili ni kosa ndugu yangu. Kuwa kile alichokufanya; yaani
sura na mfano wake. Tuelewe kwamba ufahamu wa binadamu wote na wenye
kustaajabiwa, ni ujinga wa Mungu. Yatupasa kufuata mapenzi na matakwa ya Mungu.
Hivyo, “Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima;
Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu,” Mit 9:10
Kuishi
Imani hii na mwelekeo wa Mpango wa Mungu, utapimwa kila wakati. Mungu utupima
imani yetu juu yake. Katika safari nzima ya mwokovu wetu, tumeona watu
mbalimbali wakipimwa imani zao. Ibrahimu ni mfano nzuri ya Imani na Utii kwa
Mungu. Mungu anamjaribu Ibrahimu, “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee,
umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya
kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia,” Mwa 22:2. Kwa utii
Ibrahimu anafuata maagizo ya Mungu, licha ya kuwa na mtoto huyo tu mpendwa, na
tena mtoto wa uzee wake.
Baada ya kufanya maandalizi hayo na kuchukua kisu ili amtoa
sadaka mtoto wake, Mungu ananena na Ibrahimu, “Akasema, Usimnyoshee kijana
mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu,
iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,” Mwa 22:12. Mwitikio huu ya Imani
na Utii unampatia baraka Ibrahimu. “Katika
kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za
mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui
zao; na katika uzao wako mataifa
yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:17-18.
Mungu Muumba wetu ni Mungu mwenye wivu katika maana ya viumbe vyote twapaswa
kumrudia na kufanya kadiri ya matakwa yake, ingawa twaweza kukataa. Ila
tukitaka baraka na neema yatupasa kuyafanya yote kadiri ya matakwa yake.
Mipango ya Mungu ndani yetu ucheleweshwa na wakati mwingine
kusubirishwa pale tunapoenda kinyume na mipango yake. Jambo hili linajitokeza
katika kitabu cha kutoka. Licha ya wana wa Israeli kukaa utumwani Misri kwa
miaka mia nne na ushee, Mungu bado anampango na taifa lake teule. Ilipofikia
wakati wake, Mungu anamtoa mmoja katikati yao, yaani Musa kuendeleza makusudi
ya Mungu. Jambo hili halikuwa rahisi kwa Waisraeli kuendelea na mpango wa Mungu
baada ya miaka yote hiyo. Ndugu yangu, wapo waliozaliwa Misri na kufia huko
huko Misri. Wengine walikuwa na mababu waliozaliwa Misri na kufanya maneno ya
Musa kwa maelekezo ya Mungu, kutosadikika na kueleweka. Ilikuwa vigumu kuyaacha
maisha yale na kwende kule Mungu alipowaandalia.
Hivyo Mungu anaamua kuifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu ili
Waisraeli watambue ujumbe wake na kuondoka. Misri hapakuwa hitimisho la Mungu.
Mungu anamwambia Musa, “Nami,
tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia,
nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na
kwa wapanda farasi wake,” Kut 14:17. Mungu hutumia mazingira na hali zetu za
kila siku ili tuujue ujumbe wake. Je, unapopatwa na mazingira kama hayo unaweza
kuzisoma alama za nyakati? Au, kila mara unapenda kupingana na kupigana na
Mungu?
Wana wa Israeli walipotambua mpango wa Mungu, na kutii,
Mungu anatenda jambo kubwa juu yao. “Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia
Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka
sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini,” Kut 15:1. Hakuna
lisilowezekana kwa Mungu tunapoishi kadiri ya mpango na malengo yake kwetu.
Ni kwa upendo huo aliokuwa nao Mungu ndani mwetu wakati
ulipotimia alituma mwanaye mpenzi kuikamilisha nia na makusudi yake. “Hata
ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na
mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi
awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa
wana,” Gal 4:4-5. Kwa vile vyote viliumbwa kupitia Yesu
Kristo, ni kwa namna hiyo Mungu alipenda kupitia kwake vyote vikombolewe. “Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati
ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6. Kazi hiyo Kristo ameifanya na mwisho wa siku
ilimgharimu maisha yake kwa ajili yako na yangu. Na kwa tendo hili leo dunia
nzima inashuhudia wokovu huu.
Ndugu yangu, leo ni ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Je,
unastaajabu? “Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka;
hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka,” Mk 16:6. Wapendwa, kuna shuhuda
mbali mbali za uthibitisho wa ufufuka wa Kristo. Zipo zile shuhuda ya mbali na
karibu. Shududa za mbali ni pamoja na unabii uliotabiriwa juu ya Yesu Kristo,
ikiwa ni pamoja na makusudi yake hapa duniani, na lengo lake mahususi. Pia
Kristo mwenyewe amekuwa akilisimulia jambo hili la uteswa, kufa na kufufuka,
(Mt 17:22, Mk 9:31, Lk 9:22, na Yoh 2:19)
Hatuna sababu yoyote ya kustaajabu mpango huu wa Mungu.
Shuhuda za karibu, ni pamoja na Kaburi kuwa wazi. Huu ni ushuhuda kwamba Kristo
hayupo na amefufuka. Uimara wa imani katika kumuhubiri Kristo, pamoja na ukuaji
wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo na hadi sasa Kanisa lake ulimwenguni pote, ni
uthibitisho kwamba Kristo kafufuka na anaishi ndani mwetu hasa kwa wale
waliomridhia. Je, sasa tunakutana na
Kristo Mfufuka wapi?
Wapendwa
katika Kristo, leo tunakutana na Kristo Mfufuka tunapoishi kwa uaminifu wito
wetu, kila mmoja kadiri ya mpango wa Mungu. Hapo ndipo Galilaya yako. “Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi
wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama
alivyowaambia,” Mk 16:7. Mimi kama mtawa na
padre, na wewe kama mlei, sote kwa nafasi ya upendeleo tunakutana naye kila
siku ya maisha yetu tunapoishi kwa uaminifu wito wetu. Hii ndiyo Galilaya ambapo
twaweza kumwona. “Kisha Yesu akawaambia, Msiogope;
enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt
28:10
Wapo wengi miongoni kwetu, twaingiwa na
kishawishi cha kutafuta maisha mbadala baada ya kukiri. Kubabaika huku ni kupoteza
muda ili hali wakati na masaa hayatusubiri. Kengele itakapolia, hatutakuwa na
sababu ya kujitetea. Tunapotazama masimulizi mbalimbali ya maandiko matakatifu
na hasa Injili, utagundua kwamba yote yanalenga katika nia moja. Kufahamu
makusudi ya Mungu, na mwisho wa safari kutokupata nafasi ya kujitetea kokote
kule wakati wa kutoa hesabu ya maisha yako hapa duniani.
Leo usiku huu kupitia Injili hizi “fanana,”
ufufuko wa Kristo umeturahisishia kujua sintofahamu yetu pale tunapojaribu
kupoteza muda kwa kujiulizauliza kama nipo njia sahihi. “Hayupo hapa, amefufuka.
Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, akisema, Imempasa Mwana wa
Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya
tatu,” Lk 24:6-7. Ujumbe huu wa malaika kwa bahati mbaya haupokelewi vizuri na
Mitume wale wa Yesu. “Nao ni Mariamu
Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine
waliokuwa pamoja nao; hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo. Maneno yao
yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki,” Lk 24:10-12a. Ni wazi
kutokupokeleka kwa habari hii njema na wanafunzi wa Yesu kunatufundisha uovu
uliopo kwenye mila na desturi zetu juu ya mitazamo ya kijinsia.
Wapendwa wana wa Mungu,
kadiri ya mila na desturi za kiyahudi, ushahidi kutoka kwa mwanamke haukaminika
kabisa. Lakini kadiri ya tendo hili la ufufuko tofauti zetu zilikwisha ondolewa
kwa kifo chake Yesu pale msalabani, na hasa alipoitoa roho yake ikiendana na
ishara ya kupasuka kwa pazia la hekeluni. “Naye
Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu
likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba
ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka
makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea
wengi,” Mt 27:50-53. Ishara hii ni mwanzo mpya ndani na katika Kristo Yesu kwa
kila mmoja wetu. Ni kwa mantiki hii, leo Kanisa linamtambua Maria Magdalene
kama ‘Mtume wa Mitume,’Apostola Apostolorum. Leo
Yesu anatuelekeza tutakapokutana naye. Na inanipasa kumwona Kristo Mfufuko kwa
ye yote yule ninaye kutana naye. Hapo ulipo kadiri ya wito wako ndipo kwa
kukutana naye. Ndugu yangu, jambo la msingi kupita yote ni kuboresha hali yako
hapo ulipo.
Kuboresha hali hiyo ni pamoja na kujihoji
nafsi kama unaishi kadiri ya huo wito ulioitiwa. Ukipata jibu la swali hili,
hakika utakuwa njia moja na yule
aliyekuita, Yesu Kristo akiwa dereva wa yote utakayofanya. Ni Kristo tu kwa
kufufuka kwake na kuyashinda mauti anayejua usalama wa njia tusafiriyo kuelekea
umilele. “Maana kwa kule kufa kwake, aliifia
dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni
kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu,” Rum 6:10-11.
Ndugu yangu ni nani kama Kristo katika maisha yako?
Wapendwa, tunapoifia
dhambi pamoja na Kristo, kwa njia ya ubatizo, ni mwanzo wa maisha mapya pamoja
naye. Hakuna utukufu pasipo msalaba. Na kufa kwetu huku kila siku na Kristo
dhidi ya dhambi ndiko kunakotuweka salama kuelekea umilele. “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia
ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa
njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,”
Rum 6:4. Je, mateso na mahangaiko yangu ya kila siku nayachukulia kama sababu
ya utakaso wangu?
Lucia, mmoja wa viongozi wa kikundi cha Wanalegio Maria,
hakuwahi hata mara moja kuishi zaidi ya mwezi mmoja bila kuugua au kuuguza mara
baada ya ndoa yake. Lucia akiwa na umri wa
miaka 38, na miaka 15 ya ndoa yake, aligundulika kuwa na kansa ya
kizazi. Jambo hili lilimtia majaribuni sana na wakati mwingine kukatishwa tamaa
kwa kuona kwamba Mungu, na hasa kupita Mama Bikira Maria kutokuyasikia maombi
yake.
Mara zote aliombea familia yake afya, ikiwa pamoja na yeye,
lakini mambo hayakuwa hivyo. Wengi waliomwomba awaombee kwa nia mbalimbali,
walirudi na kumshukuru kufanikiwa kwa maombi yao. Kwa upande wake hakuweza
kuelewa nini sababu ya hali ile. Mara zote alijisemea moyoni hivi, “Ni kifa na
kubahatika kumwona Yesu, nitamwuliza swali hili, ‘kwa nini mara zote hukutaka
kunisikia shida zangu na badala yake uliwasikia wengine kupitia mimi?’
Lucia akiwa na umri wa miaka 45, alifariki kwa ugonjwa wa
kansa ya kizazi. Mungu hakuacha kutimiza ile nia yake ya kumwuliza Yesu swali
lake. Mara alipomwona Yesu alijawa na huzuni na kumwuliza. ‘kwa nini mara zote
hukutaka kunisikia shida zangu na badala yake uliwasikia wengine kupitia mimi?’
Yesu akamjibu, “Lucia, kuwa na furaha na amani moyoni mwako. Nimekuwa nawe muda
wote wa maisha yako na sasa yale yote uliyokumbana nayo ndiyo hayo
yaliyokufanya Mungu akuhesabie haki na kuwa mahali hapa. Isitoshe napenda
nikuonyeshe safari yako yote uliyoisha ukiwa duniani. Mimi ndiye Bwana.”
Mara wakatoka na kuanza kutembea na mara Yesu akasimama na
kumwuliza Lucia. “Je, unaona nini mbele yako? Bwana naona nyayo za watu wawili
wakielekea njia moja,” Lucia alijibu wa upole. “Basi upande wa kulia nilikuwa
mimi, na upende wa kushoto ulikuwa wewe. Wakati ukiwa katika shida ndogondogo
nilikuwa upande huo wa kulia nikikusaidia, na ilikuwa sehemu ya utakaso wako na
utakatifu wako,” Yesu alimwelezea huku akimwonyesha kwa mkono.
“Mbona hapa naona nyayo za mtu mmoja?” Lucia alicharuka kwa
kumwuliza Yesu. “Hizi ni nyayo zangu. Nyakati hizi ni zile ambazo ulikuwa mauti
uti. Ilibidi nikubebe. Pia nyakati hizi ni zile watu walipokuomba uwaombee na
hasa kupitia nia zao kwa mama yangu
Bikira Maria. Kwa vile ulikuwa umechoka ilinipasa nikubebe ili uzitamke nia
hizo. Na kwa sababu hiyo, jina langu limesikika sana juu yao, na mama yangu
kuheshimiwa kwa uaminifu wake kwa kuyaleta maombi yote kwangu. Mimi ndiye Bwana
wa wazima na wafu.” Yesu alimjibu Lucia akiwa ameshika bega lake la kulia.
Ndugu yangu, Kila teso tupatalo hasa tunapoishi na Kristo
Mfufuka lina maana sana juu ya maisha yetu. Yote hayo tuyapatayo yanalenga
katika umilele. Pili, hapo ulipo sasa kadiri ya wito wako ndipo Galilaya yako
na kutakapo kupatia cheo chako, yaani UTAKATIFU WAKO. Hakuna sehemu nyingine
utakayoweza kukutana na Yesu. Je, waamini hilo?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kisha Yesu akawaambia, Msiogope;
enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt
28:10
Ee
Yesu Mfufuka, kwa tendo hili kuu la wokovu wetu, asante sana kwa kuyafumbua
yote ya umilele ndani ya wito na maisha yangu. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario