JUMATATU
WIKI YA 5 YA KWARESMA
Somo:
Dan 13:1-9, 15-17, 19-30, 33-62,
Somo
fupi: Dan 13:41c-62
Zab:
23:1-3a, 3b-4, 5, 6
Injili:
Yoh 8:1-11
Au
Yoh 8:12-20
Nukuu:
“Ewe mzao wa Kaanani,
wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo
ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu
binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako,” Dan 13:56-57
“Mara hiyo makusanyiko
yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio,” Dan
13:60
“Yeye asiye na dhambi
miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Yoh 8:7
“Wala mimi sikukuhumu.
Enenda zako; wala usitende dhambi tena.” Yoh 8: 11b
“Basi
Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye
hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima,” Yoh 8:12
“Ninyi
mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu,” Yoh 8:15
“Nami
nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi
na yeye aliyenipeleka,” Yoh 8:16
TAFAKARI:
“Mungu mtetezi wa wanyonge, haki na hukumu vina Bwana Mungu wetu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo tutafakari neno hili, “Mungu mtetezi wa wanyonge, haki na hukumu
vina Bwana Mungu wetu.” Wanyonge mara zote huishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu.
Kujisalimisha kwao katika unyonge ndiyo njia pekee iliyobaki. Haki na mastahili
ya mtu ni moja ya uasili wake. Binadamu kwa hulka yake na nafasi yake kijamii
huvuka mipaka na kuvitwalia haki na
mastahili haya kwa nguvu. Kunapokuwa na hali hii, mtetezi wa huyu mnyonge ni Mungu
tu, ambaye kwa asili ndiye aliyevifanya hivyo vyote ndani ya mwanadamu.
Somo letu la leo pamoja
na injili, yanatufikirisha ni nini hasili ya haki na hukumu kwa lililo haki na
kweli. Binadamu kwa hulka yake ya kujipendelea yeye zaidi, hupora haki ya binadamu
mwenzake kwa tamaa zake. Mtume Yakobo anasema, “Lakini kila mmoja hujaribiwa na
tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha
kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti,” Yak
1:14-15. Wazee ambao kutokana na mang’amuzi yao katika maisha walitegemewa sana
kuwa watu wenye hekina, na hivyo kusimamia kweli na haki. Lakini kwa bahati
mbaya wanaheshimu tamaa zao za mwili na kudondoka katika uovu.
Kutokana na tatizo hilo
katika jamii, Susana anakuwa mmoja ya wale ambao hukandamizwa na kuporwa haki
zao. Susana katika hali hii, kimbilio lake na usalama wake unabaki kuwa ni
Mungu anayeona yote kwa hali na nyakati zote. Susana anajisalimisha kwa Mungu
katika unyonge wake kwa kusema, “Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika,
wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na,
tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya kamwe mambo kama hayo, ambayo watu
hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.” Dan 13:42-43. Ni katika kujiachia huku
Susana kwa Mungu aliye hai, Mungu anasikia kilio chake na kutoa utetezi
wake na
kumsimamisha kijana Danieli ambaye anatenda kweli na haki ya Mungu.
Danieli anakuwa mfano
bora na wakuigwa katika jamii kwa kuona uovu ule na kusimama kutetea kweli.
Danieli anawaonya hata wale waliokuwa na kauli nzito katika jamii, yaani wazee
ambao kwa kuwashwa na tamaa zao wanashindwa kutenda haki na kusimamia kweli.
Danieli katika jamii yetu leo anasimama badala ya wasomi hasa waliobobea katika
fani ya sheria, ila kwa kuwaka tamaa zao na uroho wa mali wanashindwa kusimamia
haki na kweli kwa wote na hasa wanyonge. Danieli anasimama katika nuru ya
kweli, na ndani yake umo uzima. “Yesu
anasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima,” Yoh 8:12
Ni katika nuru na uzima
huu Danieli anayasema maneno mazito kwa watesi wa Susana bila kupepesa macho,
“Ewe mzao wa Kaanani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa
imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa
hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako,”
Dan 13:56-57. Mmoja kati yetu anaposimama katika kweli, na kutenda haki, Mungu
huonekana katika tendo hilo kupitia mtu huyo. “Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza
sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio,” Dan 13:60. Ndugu
yangu, usiache kutenda mema na kusimama katika kweli. Kutokufanya hivyo ni
kumsaliti Mungu aliye kweli, haki, huruma, upendo na hukumu zake zina Yeye
daima.
Tukio la Susana linatuonyesha
ni kwa namna gani watu wengi na hasa wafungwa wanavyoweza jikuta katika hali ya
ufungwa pasipo haki na ukweli, na wakati mwingine hata kupoteza maisha na mali
zao. Wezi wakubwa na wahujumu wa kubwa wa uchumi wa nchi tunawaona tu mtaani
wakifurahia maisha. Jambo hili si kwamba Mungu haoni, ila lina muda na wakati
wake. Mungu kwa kutumia watu wake ipo siku atamsimamisha mmoja wetu kama
Danieli na yote yatakuwa sawa.
Injili yetu ya leo
inasema jambo hilo hilo juu ya kutokuwa na haki sawa kwa wote, ambapo mizani ya
hukumu huegemea upande mmoja. Injili inatupa angalizo pia pale tunapotaka
kupingana na Mungu na hata kumjaribu. Yesu anapoletewa mbele yake Mwanamke
mzinifu, watu hawa, ambao wakiwemo na Wazee, wanataka kumtia hatiani. Yesu
Kristo anatambua uovu wao na kuzikumbusha dhamiri zako zilizokufa. Yesu
anafufua ndani ya waovu hawa neema na uelewa wa amri ya mapendo. Upendo ambao
wameufifisha kwa kutenda maovu, Yesu Kristo anaufufua kwa kuwafanya watende
mema. Kipimo cha kutenda mema ni wao wenyewe kwa kujiweka katika hali ya
wanyonge na wale ambao haki zao zinafinyangwa. Zoezi hili la dhamiri Yesu
analifanya baada ya kutafakari na kujua uovu wao, na kusema “Yeye asiye na
dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Yoh 8:7. Kwa maneno
haya siyo kwamba Yesu anatutaka tusitoe haki kwa njia ya sheria na kuhukumu iliyokweli. La hasha! bali
tunapolifanya jambo hili, tujipime kwanza kama na sisi tunayo mastahili hayo
mbele ya Mungu. Vile vile, Yesu anatukumbusha kwamba, uhai ni zawadi ya Mungu
kwetu, na ni mali yake. Hukumu yoyote ile kabla na baada itanguliwe na huruma na upendo wa kweli.
Ndugu yangu, huruma na
msamaha wa kweli, ni dawa na njia mwafaka wa kumrekebisha aliyetenda kosa. Mara
nyingi watu wengi hawabadiliki tabia zao kwa sababu hatujawahi wasamehe wala
kuwaonea huruma. Unapomsamehe mtu kwa kosa ambalo anajua wazi si rahisi
kusamehewa, msamaha huo huwa dawa ya ugonjwa wake wa muda mrefu. Yesu Kristo
anatumia njia hii kwa mwanamke huyu mzinifu, na kusema, “Wala mimi sikukuhumu.
Enenda zako; wala usitende dhambi tena.” Yoh 8: 11b. Furaha aliyoipata mwanamke
huyu ni kubwa sana. Inawezekana katika maisha yake, hakuwahi kupata msamaha
kama huu. Hapa pia tunajifunza kwamba, “Mungu mtetezi wa wanyonge, haki na
hukumu vina Bwana Mungu wetu.” Ndugu yangu, kwa nini unakosa huruma na msamaha
wa kweli hasa katika hali kama ya huyu mwanamke aliyokuwa nayo?
Tumsifu Yesu Kristo.
“Nami
nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi
na yeye aliyenipeleka,” Yoh 8:16
Ee Bwana, unifanye
chombo cha amani yake, Mt. Franscisco wa Assis.
No hay comentarios:
Publicar un comentario