IJUMAA
WIKI YA 5 YA KWARESMA
Somo:
Yer 20:10-13
Zab:
18:2-3a, 3bc-4, 5-6, 7
Injili:
Yoh 10:31-42
Nukuu:
“Lakini Bwana yu pamoja
nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha, kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala
hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona
aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe
wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu
yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu,” Yer 20:11
“Kama sizitendi kazi za
Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi,
ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami
ni ndani ya Baba,” Yoh 10:37-38
TAFAKARI:
“Uovu wa mtu hufunika mema yote, Mungu mtetezi wa mwenye haki.”
Wapendwa wana wa Mungu,
“uovu wa mtu hufunika mema yote ya mtu mwenye haki, ila Mungu hubaki kuwa
mtetezi wa mwenye haki.” Chuki iliyojaa wivu kwa mtu humfanya kuwa kipofu na
hivyo kutokuona mazuri kwa wenzeke. Hali hii inajitokeza kwa Yeremia na Yesu
Kristo. Mtu mwenye haki anafanyiwa hila za kila namna ilimradi hasiweze
kufanikisha jambo alifanyalo.
Yeremia anafanyiwa
njama na kukatishwa tamaa kutokana na msimamo wake juu ya imani yake na Mungu.
Mtu kwenye haki anaposimama katika lililojema, Mungu huwa muhimili wake.
Kupingwa vita kwa kutenda mema ni vita ya kiroho. Hapa yakupasa kusimama katika
kweli na kamwe usitie shaka kwa hicho unachokisimamia. Mungu hatokuacha. Mungu
atakupigania daima.
Nabii Yeremia anajikuta
katika wakati mgumu, hasa pale anapoona hakuna hata mmoja anayemuunga mkono
licha ya ujumbe wa Mungu anaoutoa. Yeremia anafahamu kuwa anachofanya si chake
bali ni ujumbe wa Mungu. Yeremia hatii shaka juu ya Mungu. Na hivi anasema,
“Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha, kwa hiyo hao
wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu
hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.
Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo,
nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu,”
Yer 20:11
Mara zote
tunapomtegemea Mungu, hatuachi katika sintofahamu zetu. Hali aliyokuwa nayo
Yeremia kwa watesi wake, ndiyo hiyo hiyo Yesu anayopambana nayo na Wayahudi.
Wayahudi hawaoni mema ayafanyayo Yesu, na hivyo njia pekee ya kuondoka naye ni
kuutoa uhai wake. Makuhani na Mafarisayo wanapatwa na hofu kwa vile Yesu
anakubalika kwa mafundisho yake na hasa ukweli anaoufundisha kuhusu ufalme wa
Mungu.
Hofu za kisiasa,
kimaslahi na kimadaraka zinawafanya Makuhani na Mafarisayo kumwangamiza Yesu
Kristo mapema. Yesu Kristo anapewa shutuma ya kukufuru kwa kujiita yeye ni
mwana wa Mungu. Lakini jambo la ajabu ni Wayahudi kuwa na mioyo migumu na
kutotambua ukweli, nguvu na uwezo aliokuwa nao Yesu. Kutambua kwamba
anachofanya si kwa mapenzi yake ila ya Mungu, Yesu anawasihi kwa kusema, “Kama
sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa
hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu
ndani yangu, nami ni ndani ya Baba,” Yoh 10:37-38
Ndugu yangu, kutambua
mema kutoka kwa wenzetu ni kutambua uzuri na Utukufu wa Mungu ambao ujifunua na
kujionyesha kwa viumbe vyake alivyoviumba kwa namna ya ajabu. Hii ni njia
mojawapo muhimu ya kukua na kukomaa kiroho. Kutotambua ukweli huu, hutupofusha
na kupelekea kufanya dhambi ya mauti. Ndugu yangu, unapokosa uimara katika
kuona mema kutoka kwa mwenzako inakuwia vigumu kuwa na mizania sawa katika
kutoa hukumu ya kweli. Badala yake utaruhusu na kusukumwa sana na hisia na
vionjo vyako. Hata kama hatumpendi mtu kwa kile alicho, basi tuona uzuri wake
kwa yale ayafanyao.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kama sizitendi kazi za Baba yangu,
msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi;
mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba,”
Yoh 10:37-38
Ee Mungu, nijalie mara zote kuona
na kutambua wema na uzuri ulio kwa mwenzangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario