miércoles, 16 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA MATAWI MWAKA-C

JUMAPILI YA MATAWI MWAKA-C
Somo I: Isa 50:4-7
Somo II: Flp 2:6-11
Zab: 22:7-8, 16-17a, 18-19, 22-23, (K) 22:1
Injili: Lk 22:14; 23:56 au Somo fupi Lk 23:1-49
Nukuu:
“Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatokea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate,” Isa 50:5-6

“naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8

Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti,” Mt 26:14-16

“Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa,” Mk 14:10-11.

Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye!” Lk 22:21-22 

Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura,” Lk 23:34

Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati,” Lk 23:44-45 

Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu,” Lk 23:46
TAFAKARI: “Yesu Kristo Mfalme  Mtaabika na Masikini ili mimi na wewe tuwe warithi na matajiri, mwili na roho.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha jumapili ya Matawa ya mwaka “C” wa Kanisa, ingawa tofauti ipo tu kwenye somo la Injili kwa mwaka “A”, “B” na “C”. Somo la Injili ambalo hubeba simulizi la mateso, kufa, na kufufuka kwake Kristo, kwa Mwaka “A” tunasoma Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo, mwaka “B” Mwinjili Marko, na Mwaka “C” Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka.

Jumapili hii ya Matawi kama tulivyoona, sehamu ya kwanza tunaona Bwana wetu Yesu Kristo anavyoingia Mjini Yerusalemu kwa shangwe na vifijo, huku alaiki ya watu wakiimba Hosana Mwana wa Daudi. Yesu anaingia Kifalme na kupokelewa kifalme.

Mashangilio haya na maandamano tuliyokwisha yafanya yana maana kuu tatu: Kwanza, tunamuungama Kristo kwa tendo hili la umati wa watu. Pili, tunatambua njia yake ni njia yetu katika maisha yetu yote. Njia hii ni njia ya mateso ambayo ndio mlango wa Utukufu na Ufufuko. Hivyo nasi tutafufuka naye tukimwamini na kumfuata mpaka mwisho. Yesu anatuhaidi katika hili kwamba, mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 24:13, Mk 13.13. Na tatu, tunakubali njia hii na tunamwahidi Kristo kumfuata. Hivyo katika juma hili Mama Kanisa linatuzamisha katika mateso, kufa na kufufuka kwake Kristo.

Sehemu ya pili tunaona anavyotaabika na kuhujumiwa na kusalitiwa na zile nderemo na vifijo alivyopewa awali. Furaha na shangwe inageuka kuwa mateso, na kifo.

Mpendwa katika Kristo, leo tumtazame Bwana wetu “Yesu Kristo aliye Mtaabika na Maskini ili mimi na wewe tuwe warithi na matarijiri, mwili na roho.” Mungu aliyeupenda ulimwengu na viumbe vyake hasa mwanadamu, anamtoa mwanaye mpenzi kuteseka, na kuufia ulimwengu ili mimi na wewe tuwe warithi wa kweli, matajiri wa kweli, mwili na roho. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9

Kazi na njia ya kufika hatma hii si rahisi kutokana na hali na uharibifu wa mwanandamu anayetakiwa kukombolewa. Nabii Isaya anatabiri dhihaka hii ya huyu atakayebeba jukumu hili na kusema, “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatokea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate,” Isa 50:5-6

Yesu Kristo yupo tayari kuteseka, na kufa kwa ajili yangu na wewe. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Lakini binadamu haachi kuwa kigeugeu. Tunapenda utukufu pasipo mateso. Tunapenda maisha mazuri pasipo kufanya kazi. Tunapenda kuwa wafalme bila kutumikia. Tunapenda kuwa na mali bila kujishughulisha. Hii tamaa ya kupenda kusiko kuwajibika ni mwinamio wa dhambi na mwelekeo wa dhambi. Leo Bwana wetu Yesu Kristo anakubali kuteseka na kufa ili tuwe hayo tunayotamani katika kweli na ukamilifu.

Tunakuwa warithi na matajiri wa kweli, tunapoachilia haya ya ulimwengu  kwa kujisalimisha kila siku mikononi mwa Mungu. Kristo anatufanya warithi na matajiri mwili na roho kwa kujisalimisha mikononi mwa Mungu bila kusita na kuwa na mashaka kwa unyenyekevu mkubwa. “Naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8. Ndugu yangu kujisalimisha kwa kujinyenyekesha kwa kila mmoja wetu kupitia wito ulioitiwa na Mungu, (Ndoa, maisha ya wakfu, na ukleri) ndiyo njia pekee ya kuurithi utajiri anautoa leo Yesu Kristo kwa njia ya mateso na kifo chake.

 Tokeo la kujinyenyekesha ni kukuzwa na kuhesabiwa haki, siyo kwa mkono wa mwanadamu, bali Mungu mwenyewe. Mtoza ushuru anahesabiwa haki kwa kujisalimisha kwa kujinyenyekeza. “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni; bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule (Mfarisayo); kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:13-14.

Ndugu yangu, yapo mambo mengi sana tunayoweza kujifunza katika njili ya leo, ila napenda tujikite sana katika usaliti wetu, unaotokana na dhambi. Tamaa kubwa ya mwanadamu ni ile ya kupenda kuwa kitu kingine zaidi na kujikataa kuwa kile alicho. Yesu Kristo anasalitiwa na wale wanaomjua vizuri na kuonja upendo wake. Leo tuseme hivi; wanaomsaliti Bwana wetu Yesu Kristo, ni wafuasi wake, yaani mimi na wewe tulio batizwa. Yuda Iskariote, mfuasi wake wa karibu, na mshika kasma, ndiye anayemsaliti Kristo. Huku ni kukosa shukrani, fadhila na moyo wa upendo kwa yule anayekutegemeza kila siku na kwa kila kitu. Ni sawa na kukata tawi la mtu ulilolikalia. Habari hiyo ilikuwa hivi, kadiri ya Mwinjili Mathayo; Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti,” Mt 26:14-16. Yesu anawindwa na yule anayemfahamu vizuri.

 Naye Mwinjili Marko anaongelea usaliti huo hivi; “Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa,” Mk 14:10-11. Na habari hiyo pia ilikuwa hivi, kadiri ya Mwinjili Luka, Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye!” Lk 22:21-22. Ndugu yangu, ni mara ngapi unamsaliti Kristo kadiri ya wito wako? Kumsaliti huku Kristo ni pale tunaposhindwa kuishi ahadi za wito na ubatizo wetu. Kila mmoja wetu ajitazame na kujipima uaminifu wake katika wito wake.

Mzee Amani katika ndoa yake alifanikiwa kuwapata mtoto mmoja tu wa kiume ambaye alijulikana kwa jina la Upendo. Upendo alikuwa ndiye kila kitu kwa Mzee Amani. Upendo alikuwa karibu sana na watu, alipendwa na kila mtu kwani pamoja na utajiri alikuwa nao baba yake kamwe hakujigamba nao. Tendo hili lilimpa sana faraja baba yake, na hivyo hakuona shida kuwaandalia wageni wa Mtoto wake Upendo kila anapokuwa na marafiki zake nyumbani.

Pamoja na Upendo kuwa na marafiki wengi, Sikujua Mafikiri alikuwa rafiki yake wa karibu sana, kiasi kwamba wengi walidhani ni ndugu yake. Ukaribu huu wa Upendo na Sikujua Mafikiri, ulimfanya Mzee Amani amchukulie Sikujua kama mwanaye pia. Basi Mzee Amani alimshauri mwanaye Upendo kama inawezekana Sikujua aishi pia nyumbani kwake.

Upendo alifurahi sana kusikia jambo hilo la faraja kutoka kwa Baba yake. Hivyo Sikujua aliamia nyumbani kwa Mzee Amani na kushiriki kila kitu cha nyumba ile bila utofauti wowote. Basi siku moja Mzee Amani alikuwa akiongelea  mali alizokuwa nazo na hata miradi aliyokuwa akiifanya. Na mwisho ya maongezi haya, Mzee Amani alisema hayo yote ni kwa ajili ya familia yake kwa sasa, akimaanisha wote, Upendo na Sikujua.

Kusikia vile, Sikujua aliingiwa na wivu na tamaa, na kuanza kufikiri ingekuwa vyema kama yeye angeyapata hayo yote. Basi baada ya miezi kama sita hivi, Sikujua aliamua kuchukuwa sumu na kuwekea Upendo kwenye chai. Upendo alifariki, na kilio kile kilisikika kila kona ya kijiji, kwani alipendwa na kufahamika na kila mtu wa kijiji kile.

Baada ya msiba na matanga kumalizika, ikiwa zishapita wiki kama tatu hivi, Sikujua aliugua sana rohoni mwake kwa kitendo alichokifanya. Hivyo aliomba kuongea na Mzee Amani. Mzee Amani alimruhusu. “Baba sidhani kama unanielewa na kuelewa nitakayo kuambia jioni ya leo. Ukweli ni kwamba, baada ya kuongelea kuhusu mali zako na miradi yako niliingiliwa na tamaa na kuona ingekuwa vizuri kama mimi ningekuwa mrithi wa mali zote. Hivyo tamaa hii ilinichukua na kuamua kumuua mwanao Mpendwa na rafiki yangu Upendo. Nilifanya jambo hilo kwa kumwekea sumu. Hivyo nakuomba sana msamaha kwa tendo hilo, na ninajuta sana,” Sikujua alilisema neno lile kwa majuto makubwa. “Mwanangu kuwa na Amani moyoni mwako. Ni jana tu, nimetoka mahakamani kubadili mrithi wa mirathi ya mali zangu zote. Mwanzoni kabla la mwangu kufariki, nilizigawa nusu kwa nusu, yaani wewe na yeye. Na sasa mali zote ni zako, nawe ndiwe mwana wangu Mpendwa. Nimefarijika sana na kuwa na  furaha tena kwa majuto yako, na kukubali kuwa mwanangu. Hii hapa nakala ya mirathi yako,” Mzee Amani aliyasema hayo kwa upole na upendo mkubwa huku akamkabidhi hati ile ya mirathi.

Ndugu yangu, huu ndio upendo wa Mungu Baba kwetu sisi wanadamu. Mwanaye Yesu Kristo na Mfalme, kwenye milki zote, anakuwa masikini kwa mateso na kifo chake msalabani, ili wewe na mimi wadhambi tuwe warithi na matajiri mwili na roho. Kibarua chetu ni kimoja tu; kuupigania ukamilifu kwa kufanya toba na majuto ya kweli ya dhambi zetu, na kuishi katika hali ya neema. Ukamilifu ndiyo cheo cha kila mbatizwa, na huu ndiyo wito wa utakatifu tunaoitiwa kila siku. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48

Tumsifu Yesu Kristo!

Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye!” Lk 22:21-22

Ee Yesu Kristo, kwa kifo chako cha aibu cha msalaba nijalie neema ya kuona umasikini wako uliopeleka mimi leo kuwa mrithi na tajiri, mwili na roho. Amina


No hay comentarios:

Publicar un comentario