JUMANNE
YA WIKI KUU
Somo:
Isa 49:1-6
Zab:
71:1-2, 3-4a, 5ab-6ab, 15, 17
Injili:
Yoh 13:21-33, 36-38
Nukuu:
“Wewe u mtumishi wangu,
Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3
“Ni neno dogo sana wewe
kuwa mtumishi wangu ili kuiinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli
waliohifadhiwa. Zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu
wangu hata miisho ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia,”
Isa 49:6
“Amini, amin,
nawaambieni: Mmoja wenu atanisaliti,” Yoh 13:21
“Ndiye mtu yule
nitakayemtowelea tonge na kumpa.” Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda,
mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu
akamwambia, “Uyatendayo yatende upesi,” Yoh 13:26-27
“Amin, amin, nakuambia:
Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.” Yoh 13:38
TAFAKARI:
“Saa ya kutukuzwa Bwana wetu Yesu Kristo
inakaribia; hofu na mfadhaiko wa kusalitiwa vikirindima.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni wazi tunakaribia saa ile muhumu sana katika safari ya wokovu wetu. Kuelewa
siri ya muda na hali aliyokuwa nayo Yesu Kristo, yatupasa kuzama ndani ya
tafakari hii kuhusu, “saa ya kutukuzwa Bwana wetu Yesu Kristo inakaribia; hofu
na mfadhaiko wa kusalitiwa vikirindima.” Yesu Kristo akiwa na asili ya Kimungu
na Kibinadamu, kama mwanadamu yupo katika wakati mgumu sana na mfadhaiko wa
moyo ambao hakuna aliyeweza kushiriki naye katika mahangaiko haya.
Ni ukweli usiotia shaka
kwamba, hata wanafunzi wake, hawakuwa na wazo kama yatakayotokea baadaye pale
msalabani yanaweza kuwa hivyo kwa mtu waliyemjua hasa kwa nje, juu ya uwezo
wake, miujiza na nguvu ya ajabu. Kutokuamini huku kunajionyesha baada ya
ufufuko wa Yesu Kristo kwa wale wanafunzi waliokuwa wakienda katika kijiji cha
Emau. Kutokana na sintofahamu waliyokuwa nayo, Kristo Mfufuka anataka kujua
kulikoni. Mmoja wao Kleopa, anamjibu Yesu bila kujua kama ndiye Bwana, na
kusema, “Je! Wewe peke yako u mgeni
katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi? Akawauliza, Mambo
gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo
katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa
makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha,” Lk
24:18-20. Ndugu yangu, ni kwa mtazamo huu waliokuwa nao wanafunzi kwamba kifo
hakiwezi kumpata Kristo. Hivyo mahangaiko aliyonayo Yesu sasa na wakati huu,
hakuna aliweza kuyashiriki, na mbaya zaidi hata wale aliokuwa nao karibu.
Ni simanzi kubwa na zito kuona mateso ndani
yako, lakini wanaokuzunguka wazo hilo halipo kwao. Kwa mfadhaiko Yesu anasema,
“Amini, amin, nawaambieni: Mmoja wenu atanisaliti,” Yoh 13:21. Ndugu yangu,
hata katika hali hii, Yuda anapewa nafasi ya kujirudi na kuacha mpango wake. Yesu Kristo katika hali hii, hakutaka jambo hili liwe
siri. Baada ya kuulizwa nani huyo ambaye anataka kumsaliti, Yesu analiweka wazi
jambo hili na kusema, “Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa.”
Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya
hilo tonge Shetani alimwingia. Basi Yesu akamwambia, “Uyatendayo yatende
upesi,” Yoh 13:26-27. Ndugu yangu, ni mara ngapi tunasutwa na dhamiri zetu
katika kufanya jambo ovu na bado tunaendelea na mpango wetu huo mwovu?
Pamoja na hali hii, Yesu lazima atimize yale yote
yaliyosemwa juu yake na Manabii. Yesu Kristo Mtumishi wa Mungu, anatukukuzwa
katika saa hii kupitia mateso na kifo cha msalaba, na kwa namna hiyo naye Mungu
anatukuzwa. Nabii Isaya analitabiri hili kwa kusema, “Wewe u mtumishi wangu,
Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa,” Isa 49:3. Yesu Kristo anatimiza ahadi
ya Mungu na kwa kupitia kifo chake wote tunapata wokovu naye anakuwa nuru ya Mataifa yote. “Ni neno dogo sana wewe
kuwa mtumishi wangu ili kuiinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli
waliohifadhiwa. Zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu
wangu hata miisho ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia,”
Isa 49:6.
Yesu Kristo anapokaribia kutukuzwa na kumtukuza Mungu,
hakosi kukumbana na usaliti ambao tumeuona kwa Yuda Iskariote, na sasa kwa
upande wa Petro. Petro naye hayupo nyuma kutoa ahadi hewa kwa Yesu. Petro
anamdanganya Kristo kwa kusema yupo tayari kuyatoa maisha yake kwa ajili ya
kuzuia kifo cha Yesu. Yesu kwa mara nyingine anatoa angalizo
kwa Petro kujirudi kabla ya saa ile. Yesu anamwambia Petro, “Amin, amin,
nakuambia: Jimbi hatawika hata wewe utakapokuwa umenikana mara tatu.” Yoh
13:38. Ndugu yangu, katika safari hii ya kuelekea kilele cha wokovu wetu, Yesu
hachoki kufundisha na kututaka kujirudi katika ahadi zetu zisizotekelezeka na
hali yetu ya dhambi kwa ujumla. Petro kama mimi na wewe, tunapewa nafasi ya
kufanya tafakari ya kina juu ya ahadi zetu katika maisha na wito wetu, na
kutathimini yale tuyasemayo kama kweli yanaendana na matendo yetu. TAFAKARI NA
CHUKUA HATUA!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Amini, amin, nawaambieni: Mmoja
wenu atanisaliti,” Yoh 13:21
Ee Yesu, nishirikishe mahangaiko
yako katika SAA hii ninapoutazama Msalaba wako Mtakatifu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario