JUMAPILI
YA 5 YA KWARESMA YA MWAKA-C
Somo
I: Isa 43:16-21
Zab:
126:1-2, 2-3, 4-5, 6
Somo
II: Flp 3:8-14
Injili:
Yoh 8:1-11
Nukuu:
“Bwana
asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji
yenye nguvu; atoaye gari na
farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa
mfano wa utambi,” Isa 43:16-17
“Tazama,
nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia
hata jangwani, na mito ya maji nyikani,” Isa 43:19
“Si kwamba
nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili
nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu,” Flp
3:12
“Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole
chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi
miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe,” Yoh 8:6b-7
“Nao
waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia
tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke
amesimama katikati,” Yoh 8:9
TAFAKARI: “Tazama,
nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia
hata jangwani, na mito ya maji nyikani,” Isa 43:19
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo
Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tano ya Kwaresma ya Mwaka “C” wa Kanisa.
Masomo yetu yote matatu leo yanatuelekeza kwenye kweli ya ‘Mungu wetu aliye hai.’ Mungu wetu
huyu ni Upendo, Haki, Kweli, Huruma, Msamaha na Asiyechoka kwa ajili ya viumbe
vyake. Kwa mantiki hii ya Mungu wetu aliye hai, hakuna sababu ya sisi viumbe
vyake kukata tamaa na kukosa matumaini. Mambo yote tunayokutana nayo katika
maisha tuyaone katika mtazamo wa Mungu wetu huyu aliye hai. Ni katika mtazamo
huo wa Kimungu yote hupata maana yake halisi. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu
wetu aliye hai.
Nabii Isaya katika somo la kwanza
anaifunua kweli ya Mungu wetu aliye hai. Nabii Isaya anaamsha tumaini jipya kwa
wana wa Israeli waliokwisha anza kulipoteza tumaini hilo. Bwana asema, “Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je!
Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani,” Isa
43:19. Huyu ni Mungu aliye hai na
asiyeshindwa kutenda lolote kwa wale wote aliowaridhia na walio mridhia. Tatizo
kubwa tulilokuwa nalo wengi ni kukosa subira pale mambo yanapokwenda kombo.
Katika hali hii ya sintofahamu Yesu anatukumbusha na kusema, “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina
langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22.
Mateso na mahangaiko yako yasiwe ukuta wa kutokuona mbele na kukosa tumaini
tena. Kristo aliyeyashinda mateso kwa ajili yako na yangu, awe faraja yetu siku
zote. “Kwa kuwa kama vile
mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya
Kristo,” 2Kor 1:5
Wapendwa wana wa Mungu,
ahadi atuhaidiazo Mungu ikiwa ni pamoja na mawazo yake kwetu ni amani na yana
umilele ndani yake. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana,
ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za
mwisho,” Yer 29:11. Tumaini katika Mungu ni tumaini hai na yenye mwanga halisi
kwa kule tunapokwenda, tusipopajua au kufunuliwa wazi kwetu. Mungu anataka
tufahamu ukweli huu: “Wanyama wa kondeni
wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito
nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu
wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu,” Isa 43:20-21. Wewe
unayekata tamaa na kukosa mwelekeo wa maisha, elewa kuwa u mteule wa Mungu,
umebeba sura na mfano wa Mungu, na u sifa halisi ya Mungu. Hii ndiyo huruma ya
Mungu kwetu isiyokifani.
Tumaini
hili la Mungu kwa watu wake na warithi wake limejifunua wazi kwa Mwanaye Mpenzi
Yesu Kristo. Huyu ndiye Imanueli, “yaani, Mungu pamoja nasi,” Mt 1:23b. Mungu
huyu pamoja nasi, yaani, Yesu Kristo, anajidhihirisha katika Injili ya leo kuwa
ni Mungu wa haki, kweli, huruma na Upendo juu ya mwanamke aliyefumaniwa katika
uzinzi. Kwa kosa alilofumaniwa mwanamke huyu tulitegemea mbele ya mashtaka yake
angekuwepo na aliyeshiriki naye tendo lile. Lakini hilo halionekani. Huu ni
uonevu wa kimazingira, kitaratibu na kisheria kwa tuhuma alizobebeshwa mwanamke
huyu. Hata hivyo, lengo la Waandishi na Mafarisayo halikuwa tu kumweka mwanamke
yule hatiani, bali na Yesu pia katika uamuzi atakao utoa kuhusu shauri lile.
Kwa kuwa shauri hili hatma yake ni mauti, yaani muhusika kupigwa mawe hadi
kufa, Yesu anazisoma dhamiri zao na kuwaambia, “Yeye asiye na
dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe,” Yoh 8:7. Matokeo ya
mtihani huu na zoezi hili la dhamiri ni kwamba, “Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka
mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake,
na yule mwanamke amesimama katikati,” Yoh 8:9. Mungu aliye hai anazifufua
dhamiri za Waandishi na Mafarisayo zilizokuwa zimekufa. Swali linabaki kwako na
kwangu, Je, hukumu tuzitoazo kila siku twazitoa katika dhamiri iliyo hai? Na
kama dhamiri ni hai, Je, hukumu hiyo imejikita katika misingi ya kweli, na
haki, huruma na upendo?
Wapendwa katika Kristo,
huruma na upendo lazima vitawale kabla na hata baada ya hukumu yoyote ile
uitowayo wewe uliye na hofu ya Mungu. Ukweli huu tunauona kwa Kristo Yesu baada
ya kubaki na mshtakiwa, yaani mwanamke yule aliyefumaniwa kwa uzinzi. Mambo
yalikuwa hivi; “Yesu akajiinua asimwone mtu
ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je!
Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda
zako; wala usitende dhambi tena,” Yoh 8:10-11. Ndugu yangu, tazama huruma na
upendo wa Mungu ulivyo mkubwa kwetu! Maneno “enenda zako; wala usitende dhambi
tena,” kwa namna nyingine yana maanisha hivi: “na sasa uanze upya ndani na
katika Kristo Yesu kwa sababu, “Mimi ndimi
njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,”” Yoh 14:6.
Amina!
Wapendwa
wana wa Mungu, kielelezo cha Mungu wetu aliye hai ni Kristo mwenyewe kama Mtume
Paulo anavyotuwasa katika somo letu la pili. Kristo kwa Mkristo ndiyo kila kitu
kwake. “Naam,
zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na
kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara
ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo,” Flp 3:8. Ukimpata
Kristo na kuishi ndani na katika yeye umeyapata yote yaliyofunuliwa kwake
yamuhusuyo Mungu Baba Mwenyezi. Na hayo ndiyo ule uzima wa milele.
Ukiwa ndani na katika
Kristo atakayeonekana katika maisha yako si wewe na ubinafsi wako, bali Kristo
mwenyewe. Kama binadamu sintakuwa na chochote cha kujivunia zaidi ya Kristo
mwenyewe. “Tena nionekane katika yeye,
nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa
imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani,” Flp 3:9.
Mateso na mahangaiko ya Mkristo anayeishi ndani na katika Kristo hupata maana
halisi. Huwezi kumjua Kristo kwa kupiga
kisogo. Namjua Kristo kwa kuishi ndani na pamoja naye, na kwa kufikiri na
kutenda kama yeye. Hivyo, naihitaji neema “ili
nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake,
nikifananishwa na kufa kwake; ili
nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu,” Flp 3:10-11.
Hatua hii ya kukua
kiroho ndani na katika Kristo, hutuondolea kiburi na majivuno yote
yanayotukwamisha kuuona uzuri wa Kristo ndani yetu. Huku ndiko kupungua ili
Kristo aongezeka kila siku ya maisha yetu. “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa
mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili
yake nimeshikwa na Kristo Yesu,” Flp 3:12. Pasipo kujishusha hatuwezi kufika
pale alipo Kristo. Kaa yangu kila siku iniweke karibu na Kristo na kamwe
nisichoke kuutafuta uso wake. Mtume Paulo anasema, “Ndugu,
sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu;
nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele,” Flp 3:13.
Tuliyokwisha yafikia kimaisha leo na sasa hayana umuhimu mkubwa sana
tukilinganisha na yale ambayo yapo mbele yetu kuliko na uzima wa milele. Hivyo
mara zote nikaze “mwendo, niifikilie mede
ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu,” Flp 3:14. Na mwito mkuu
wa Mungu katika Kristo Yesu ni huu, ‘kuwa
wakamilifu, kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu, Mt 5:48.’
Ndugu
yangu, ni kama wiki tatu zilizopita katika Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria
kulitokea wizi wa tairi la akiba ya gari ya Paroko. Kwa jumapili mbili
mfululizo yalitolewa matangazo yakisisitiza aliyechukua tairi hilo arudishe.
Matangazo hayo yaliambatana na novena ya
siku 21 kusali kwa nia ya kurejeshwa kwa tairi hilo la akiba la gari ya Baba
Paroko.
Basi
jumapili ya tatu baada ya tukio hilo kutoke, zilisikia kelele barabarani mara
baada ya misa la pili parokiani hapo. Waamini wengi walikimbilia barabarani
kujua kulikoni. Na tazama alikuwa Baba mmoja wa umri wa kutosha akiwa amebeba
mahindi matatu mabichi akiwa anapata kichapo cha nguvu na kulia kama mtoto.
“Jamani nihurumieni ni kwa sababu ya njaa tu nimefanya haya yote,” Baba yule
alisikika akisema maneno hayo kwa uchungu.
Kundi
lile lililotoka Parokia sauti zilisikika zikisema, “huyu atakuwa ni kibaka yule
yule aliyeiba tairi la akiba la Baba Paroko. Dawa ya vibaka kama hawa ni
kuwachoma moto. Na tutafute galoni ya kuchukulia petroli hapo sheli.” Mara hara
hara watu wawili kutoka kundi lile walijitolea kwenda kufuata mafuta ya Petroli
baada ya kupitishwa kwa mchango wa haraka wa fedha za kununulia Petroli ile.
“Jamani
msiniue. Nina familia, mke wa watoto ndugu zangu,” Baba yule aliyasema maneno
yale kwa msisitizo. Hata hivyo hakuna aliyemsikia. Umati wote kila mtu alikuwa
na chochote mkononi kwa kuumaliza uhai wa yule Baba. Mara vijana wale wawili kutoka
sheli waliwasili na Petroli yao. Baba yule alimwagiwa Petroli ile na kutiwa
kiberiti. Moto ulivyopamba vya kutosha, kila mmoja alisambaa kivyake. Waliokuwa
wametoka misa ile ya pili na kushiriki uuaji ule walienda majumbani mwao, na
waliokuwa wakienda misa ya tatu walifanya hivyo katika utoshelevu wao kwa tendo
lile. Na baada ya saa moja hivi baadaye Baba yule alifariki kwa mateso makubwa
sana.
Ndugu
yangu, simulizi hili linasema chochote juu ya Ukristo wako?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yeye asiye na dhambi miongoni
mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe,” Yoh 8:7
Ee Yesu, nijalie utu wema, huruma
na upendo wa kweli kwa wema na waovu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario