JUMATATU
YA OKTAVA YA PASAKA
Somo:
Mdo 2:14, 22-32
Zab:
16:1-2a, 5, 7-8, 9-10, 11
Injili:
Mt 28:8-15
Nukuu:
“Yesu
huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,”
Mdo 2:32
“Kisha Yesu akawaambia,
Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko
watakakoniona,” Mt 28:10
“Wakakusanyika pamoja
na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi
wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala,” Mt 28:12-13
TAFAKARI:
“Kuishi imani ya kweli”
Wapendwa wana wa Mungu,
tukiwa katika oktava ya pasaka, yaani siku nane za Pasaka, kwa leo tutafakari
neno hili, “kuishi imani ya kweli.” Moja ya kweli kwamba Kristo amefufuka na yu
hai, ni ujasiri wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo kuishi kwa matendo na
kumuhubiri Kristo mfufuka bila shaka na wasiwasi wowote. Jumuiya hii ya kwanza
wapo tayari kwa lolote limuhusuyo Kristo Mfufuka. “Yesu
huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,”
Mdo 2:32. Ushupavu huu ni kutokana na kuguswa na kuishi uhasilia wa Ufufuko wa
Kristo. Hapana shaka kwamba Kristo amefufuka na yu hai katika maisha yetu na
hali zetu kila siku.
Uthibitisho huu wa imani huondoa hofu yote kwani tegemeo
kubwa lishajionyesha katika maisha ya kila siku. Kufufuka kwa Bwana wetu Yesu
Kristo, Yesu analiweka jambo hili wazi kwa wale waliomfia na kumtumainia, “Kisha
Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya,
ndiko watakakoniona,” Mt 28:10.
Ndugu yangu, galilaya
yako ni pale unapoishi maisha ya kila siku. Kama mtu wa ndoa, uaminifu wako
katika Sakramenti hiyo ni makutano ya Kristo mfufuka na ndiyo Galilaya yako.
Kama wewe ni mtawa kama mimi, maisha haya ndiyo ninapokutana na Kristo mfufuka
pale ninapoisha nadhiri zangu kwa uaminifu kadiri ya mwongozo wa mwanzilishi
wetu na mtazamo wa Kanisa. Nje ya hapo ni kupoteza muda tu. Ni katika hali hii
naweza kukutana na Yesu Mfufuka. Hakuna mbadala wake. Ndugu yangu tuheshimu na
kuzijali ndoa na maagano yetu na nadhiri zetu katika maisha. Mateso na
mahangaiko katika wito wako ni ishara ya wazi kwamba unachokitaka na kukitafuta
kina gharama, thamani, na baraka mbele ya uso
wa Mungu. Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kinatufundisha
kwamba hakuna UTUKUFU PASIPO MSALABA.
Ukweli huu kuhusu
ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo walijaribu kuupotosha lakini hawakuweza.
“Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi
wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala,” Mt 28:12-13. Ndugu
yangu, huwezi kuzuiya upepe kwa mikono yako. Nguvu na kweli ya Mungu hii juu ya
maarifa yetu yote. Hivyo usipo jikabidhi kwa Kristo utajikabidhi kwa shetani.
Uchaguzi huu upo chini ya uwezo wako. Njia sahihi na ya kweli ni kujisalimisha
mikoni mwa Kristo ambaye ameyashinda yote.
Ndugu yangu, hakuna maisha
ya usalama kama hujikabidhi kila siku mikoni mwa KRISTO. Huyu ndiye ajuaye
yaliyo kabla na mwisho wa nyakati zetu. Kujikabidhi mikoni mwake kunaitaji
utayari wetu tu. Utayari huu ni kufanya mapenzi yake kila siku ya maisha yetu.
Ukaribu wetu na Kristo ni kuyafanya mapenzi ya Baba yake aliye Mbinguni. “Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba
yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu,” Mt
12:50.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yesu huyo Mungu
alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,” Mdo
2:32
Ee Yesu Mwema, niongoze katika
kuyafanya mapenzi yako na Baba aliye Mbinguni. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario