jueves, 24 de marzo de 2016

TAFAKARI: IJUMAA KUU

IJUMAA KUU
Somo I: Isa 52:13-53:12
Zab: 30:2, 6, 12-17,25
Somo II: Ebr 4:14-16, 5:7-9
Injili: Yoh 18:1-19, 42
Nukuu:
Alidharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.” Isa 53:3

“Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake,” Isa 53:7

“Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” Ebr 4:15

“Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, “Ni nani mnayemtafuta?” Yoh 18:4

“Yesu akawaambia, “Ni mimi.” Yoh 18:5

“Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” Yoh 18:8

“Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” Yoh 18:11

“Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.” Yoh 18:20-21

“Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?” Yoh 18:23

“Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?” Yoh 18:34

“Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Yoh 18:36

“Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.” Yoh 18:37

“Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.”  Yoh 19:11

“Mama, tazama, mwanao.” Yoh 19:26

“Tazama, mama yako.” Yoh 19:27

“Naona kiu.” Yoh 19:28

“Imekwisha.” Yoh 19:30

TAFAKARI: “Mateso na kifo cha aibu cha Bwana yetu Yesu Kristo, ni ushindi wa wema dhidi ya uovu, kuinuliwa kwa wanyonge na wanyofu wa moyo, uponyaji wa maumivu ya ndani, na ni njia pekee ya kujipatia Utukufu.”

Wapendwa wana wa Mungu leo tunatafakari fumbo zima la mateso, na kifo cha msalaba cha Bwana wetu Yesu Kristo. Hapa ndipo kwenye hitimisho zima la safari yetu ya Ukombozi. Hapa ndipo kwenye ushindi dhidi ya umauti na mwelekeo wa umilele. Hapa ndipo sote kwa utofauti wetu twafanywa upya na kuwa wana pekee na wapendwa wa Mungu. Hapa ndipo mimi na wewe kama wafuasi wa Kristo twajivunia Ukristo wetu kwa sababu kuna maisha tena ya umilele baada ya kifo kilichopigwa mwereka na ushindi wa Yesu Kristu dhidi ya dhambi.

Ndugu yangu mpendwa unayesafiri nami katika tafakari hii, naona ni vyema tuzame katika neno hili, “Mateso na kifo cha aibu cha Bwana yetu Yesu Kristo, ni ushindi wa wema dhidi ya uovu, kuinuliwa kwa wanyonge na wanyofu wa moyo, uponyaji wa maumivu ya ndani, na ni njia pekee ya kujipatia Utukufu.” Yesu Kristo anayeyakubali mateso haya na aibu hii kubwa dhidi ya dhambi zangu na zako, anakubali kuyabeba yote kwa unyenyekevu na ustahimilivu uliotukuka. Nabii Isaya anatoa wasifu wa huyu abebaye kadhia hii, yaani kwa unabii huo, Yesu  ndiyo mtazamo na kwelekeo wake wa kuyapokea mateso na karaha hizi. Alidharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.” Isa 53:3.

Pamoja na karaha na kadhia hizi, na hasa kukataliwa na watu waliomfahamu, Yesu Kristo bado anajinyenyekesha na kuwa tayari kutaabika kwa faida yako na yangu, na tendo hili linakunifanya mimi na wewe tuwe huru mwili na roho. Kukombolewa huku na kufanywa huru mwili na roho kumemgharimu sana Mwokozi wetu. Mtume Petro anasema, “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikiavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Hakika mateso ya Yesu ni huzuni kubwa hasa tunapotenda dhambi tukilinganisha na majitoleo yake ya kutupatanisha na Mungu Baba. “Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake,” Isa 53:7

Wapendwa katika Kristo, kwa mwono huu wa Yesu Kristo mbele ya watesi wake, ni vyema tuyatafakari maneno yale aliyoyatamka Yesu Kristo tangu kukamatwa kwake alfajiri na mapema hadi pale alipoitwa roho yake. Kila alilolitamka Kristo ni fundisho la kina kwetu. Alfajiri na mapema siku ya Ijumaa, kundi kubwa la askari wa kirumu wakiongozwa na Msaliti Yuda Iskariote, hawakumjua Yesu mpaka pale alipojitambulisha mwenyewe. “Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, “Ni nani mnayemtafuta?” Yoh 18:4. Kwa swali hili laonyesha wazi Yesu anafanyiwa hujuma iliyo wazi. Kama angekuwa mwovu kwa matendo yake, basi kusingalikuwa na ulazima wa kujitambulisha. Mara nyingi na walio wengi wamejikuta magerezani kama ndoto vile na wakati mwingine wakijikuta wanasomewa mashitaka wasiyo yajua na hata kuhukumiwa kifo. Jambo kama hili mara nyingi linakuwa ni agizo kutoka kwa wakubwa na wenye pesa hasa kwenye utawala dhalimu. Pamoja na dhulima hii, Yesu hakimbii wala kujificha. Badala yake anajisalimisha mwenyewe pasipo hofu. Anawaambia, “Ni mimi.” Yoh 18:5. Tendo hili la kujitambulisha Kristo kuwa ni yeye, mara unatokea muujiza wa kwanza, ‘wote wanadondoka chini.’

Hata katika muujiza huu, bado wanashindwa kugundua usafi na wema wa Yesu. Wakiwa katika hali ya sintofahamu, Yesu anawasaidia kwa kujitambulisha tena, na hapa akiwakingia kifua wanafunzi wake. “Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.” Yoh 18:8. Yesu akiwa Baba wa Familia mwenye kujali na kuwajibika, anajitoa muhanga mwenyewe ili wamtende yeye tu, na familia yake iwe salama. Huyu ni mzazi anayejali familia yake hata nyakati za kiza kinene. Leo wazazi wengi wamezitelekeza familia zao kwa ulevi, ukahaba, kuwa na nyumba ndogo, na wakati mwingine kupenda anasa na tafrija kulikopindukia.

Wapendwa, ule msemo wetu kwamba damu nzito kuliko maji, anautumia Mtume Petro kwa kujaribu kumnusuru Yesu Kristo, kwa kumkata sikio mmoja wa vibaraka aliyetambulika kwa jina la Malko. Mara Yesu anazuia damu kumwagika, na kutoa onyo kwa Petro. “Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?” Yoh 18:11. Kristo anatufundisha tusiwe wepesi wa kulipa baya kwa baya. Hayo siyo malengo na mtazamo wa Mungu na hata wa Ukristo wetu. Ingalikuwa hivyo, basi hata yeye Kristo angeweza hata kuwashushia moto kutoka mbinguni wakaungua wote waliotumwa kumkamata. Je, ni mara ngapi nimekuwa mtu wa visasi hata kuishi kwa visasi muda wote? Kuonyesha kuwa Yeye, yaani, Yesu Kristo hayupo katika lolote lililo ovu, anafanya muuza mwingine kwa kulirudisha sikio pale lilipoondolewa kwa upanga. Kristo bado anatenda wema hata pale ambapo mazingira yangemshawishi kutokufanya hivyo. Kwa upande wa watesi wake hata hili hawalioni. Hakika sikio la kufa alisikii dawa!

Ndugu yangu, kukamatwa kwa Yesu Kristo hakukua kwa haki na uhalali wowote, na hata mashitaka yake yalikuwa ya kuokoteza okoteza tu. Kitu cha ajabu ni kwamba waliomkamata hawakujua sawa sawa kisa cha kufanya hivyo. Na badala yake wanataka Yesu Mwenyewe ayaseme makosa yake. Huu ni uonevu uliokithiri. Hata katika hali hii Yesu hajitetei kwa yale mema aliyoyafanya badala yake anashauri waulizwe wale alioishi nao na kuwafundisha kweli. Yesu anawaambia, “Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.” Yoh 18:20-21. Ni mara ngapi tunasikia watu wamebambikiziwa kesi za mauaji? Wapo wengi hata leo hii wanateseka kama Kristo magerezani bila kujua hatma yao. Ni mara ngapi nimetoa ushahidi wa uongo, na hata kushuhudia uongo? Leo mtu kuporwa haki yake umekuwa utamaduni na wenye kuhalalishwa katika jamii yetu. Mfano; si ajabu kuona na kusikia aliyeshinda ndiye kashindwa, na aliye shindwa ndiye kashinda. Mbaya zaidi jamii yetu leo imeanza kujijengea utamaduni huu mwovu.

Ndugu yangu, hata kwa ukweli aliousema Yesu, bado anaonekana mkosefu, na hivyo anachapwa vibao. Wapo watu wengi kati yetu wanaoteseka katika mateso ya kimfumo. Mateso ya kimfumo ni pale wachache na wenye uwezo wanapokandamiza haki za wanyonge na hasa wale wanoonekana kuwa mwiba katika maslahi yao. Leo tunashuhudi baadhi ya watu wakiuwawa kwa vile tu wamesimama katika kweli. Wapo wengine wanauwawa kwa vifo nyamavu kwa kulishwa sumu ya muda mrefu. Wapo wengi wanaofukuzwa kazi na hata kufunguliwa kesi lukuki kwa vile tu hakubaliani na uovu wa kimfumo. Haya yote Yesu anakabiliana nayo. Katika hali hii Yesu jibu lake ni hili, “Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?” Yoh 18:23. Kwa kweli Kristo hakufanyiwa haki hata kidogo. Wapo pia wengine wanateswa na kunyanyaswa kama Kristo kwa kutosikilizwa na hata kujitetea. Leo polisi si mahali salama tena ambapo unaweza kupakimbilia ili upate msaada.

Yesu Kristo ni Mfalme wa amani, upendo, haki, upole, unyenyekevu, na hivi ndivyo vinavyompa nguvu ya maadili kusema na kusimama katika kweli. Anapoulizwa kama yeye ni mfalme, Yesu Kristo anashangazwa na swali hili kutokana na kutokufahamu kwao. “Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?” Yoh 18:34. Maisha ya Yesu ni somo tosha la kile asemacho na akiishicho. Kwa kuulizwa kama yeye ni mfalme, Yesu anaandaliwa kesi ya kubambikiziwa. Leo pia wapo watu wengi wanasota maabusi na wengi magerezani kwa kubambikiziwa kesi za uongo. Katika hali hii, Yesu anawafundisha na kutufundisha tena, ili waelewe na tuelewe sababu ya maisha yake hapa duniani. “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Yoh 18:36. Yesu Kristo ni mfalme wa Amani. Na utimilifu wa ufalme huu ni maisha ya umilele.

Ndugu yangu, sababu kubwa ya Yesu kuwa kile alicho ni kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi, na kuokoa kile kilichoumbwa na Mungu na kwa njia ya Mwanaye, yaani Yesu Kristo, Yoh 1:3. Yesu Kristo hasiti kusema yeye ni mfalme kwa maana ya ufalme wa haki, amani, upendo, unyenyekevu na upole. “Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.” Yoh 18:37. Ni katika kuishi kweli na kutafuta kweli tunakuwa huru ndani na katika Kristo. Kwa mantiki hii hakuna mwenye mamlaka ya mwisho kuhusu uhai wa mtu, isipokuwa Mungu mwenyewe, ambaye kwa namna ya pekee ameyafunua hayo kwa mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Katika jambo hili Yesu anatoa onyo kwa Pilato na tawala zote zile kandamizi. “Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.”  Yoh 19:11. Ndugu yangu uliyejaliwa kuwa na mamlaka na dhamana pale ulipo, je, wayatumiaje madaraka hayo?

Kanisa leo yaani; Moja, Takatifu, Katoliki, na la Mitume, ni taswira ya Yesu Kristo mwenyewe ambao ni  mwili wake, na sisi waamini ni viungo vya mwili huo. Katika mantiki hii, mafundisho na matendo ya Kanisa lazima yawe na mwono na ufanyisi wa Kristo mwenyewe. Jambo hili Yesu Kristo akiwa katika hatua zake za mwisho kabla ya kutwaa roho yake, analikabidhi Kanisa kwa Mama yake Mzazi, katika maana ya uangalizi na ulezi, na lenye mamlaka fundishi. “Mama, tazama, mwanao.” Yoh 19:26. Na ni kwa namna hiyo pia Kanisa linajikabidhi katika mikono ya Mama Maria. Mwana “Tazama, mama yako.” Yoh 19:27.

Ndugu yangu, Yesu anasema, “Naona kiu.” Yoh 19:28. Kiu ya Yesu kwangu na kwako, ni kuwa na upendo wa kweli kwako binafsi, sisi kwa sisi, na Mungu. Kiu yake ni kuona tunakuwa jumuiya inayoongozwa na upendo, yenye kuhurumiana na kutaabikiana. Kwa maana hiyo, tunapoutazama msalaba tuone upendo huo ambao kwa sauti ya ukimya inasikika kutoka kwenye mikono yake licha ya kufungwa kwa misumari ikisema “embu ona nilivyokupenda na ninavyokupenda, njoo kwangu na nitakupokea kama ulivyo. Nimeutoa uhai wangu kwa sababu nakupenda upeo. Na kwa sababu hiyo nakupenda kama ulivyo.”

Ndugu yangu, neno la mwisho la Yesu, ni hili, “Imekwisha.” Yoh 19:30. Safari ya kukukomboa na kunikomboa imefikia kilele chake hapa msalabani. Hapa ndiyo mwisho wa yote pale tunapokuwa ndani na katika Kristo. Kwa maneno haya, ninaona mambo haya niutazamapo msalaba mtakafifu; Ninaona kiti chake cha hukumu yaani boriti lile alilowambwa mwokozi wangu. Kiti hiki mahudhui yake ni UPENDO NA HURUMA YA MUNGU. Hapa ndipo sehemu salama na ndipo penye uponyaji wa ndani wa maumivu yetu kila mmoja kadiri ya historia yake na makuzi yake. Kwenye huu msalaba ninaona kofia yake ya kifalme iliyosukwa kwa taji la miba. Ufalme na utawala wake niwakufikika na kila mmoja wetu. Ni ufalme wa amani. Ni hapa tu ninapoweza kuyatafakari makuu ya Mungu na mapito ya maisha yangu na kupata faraja ya moyo wangu kwa sababu najua ninaye jemedari aliyeshinda uovu kwa wema, bila fujo wala vita.

Ndugu yangu, ni ukweli usiotia shaka kwamba uponyaji kutoka kwa Mungu tunaupata hasa katika sehemu kubwa mbili:-

Msalabani alipowabwa Yesu. Hapa Yesu alichukuwa magonjwa yetu, taabu, maumivu, hofu, dhambi na hata umaskini wetu. Yesu aliteseka kiroho kwa kubeba dhambi tulizotenda na kuhukumiwa pasipo kosa lolote. Pia aliteseka kihisia kwa aibu aliyopata kwa kuwambwa uchi msalabani.  “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.  Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa,” Isa 53:3-4. Mateso ya Yesu ni kama ifuatavyo:-Alikuja kwa wale aliowapenda sana lakini walimkataa, pale msalabani alipoteza kila kitu, Mitume, Heshima yake, na Utu wake. Kutokana na Yesu kubeba huzuni, fadhaa na masikitiko yetu ndiyo maana sisi tunapona kwa kupigwa kwake na tunapona mwili, nafsi, na roho. “Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” Ebr 4:15

Uponyaji wa Roho Mtakatifu. Uponyaji huu tunaupata kupitia Roho Mtakatifu katika wakati huu wetu na tangu wakati wa Yesu alipoanza huduma yake. “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao,” Isa 61:1. Ili tupate uponyaji ni lazima tumruhusu Roho Mtakatifu atuponye. Tujiachie kwake naye atatenda.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.” Yoh 18:20-21


Ee Yesu na Bwana wangu, mimi ni nani basi nisiyesamehe?

No hay comentarios:

Publicar un comentario