miércoles, 9 de marzo de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 4 YA KWARESMA

IJUMAA WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Hek 2:1a, 12-22
Zab: 34:17-18, 19-20, 21, 23
Injili: Yoh 7:1-2, 10, 25-30
Nukuu:
“Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa, kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu, wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia,” Hek 2:21-22

“Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado,” Yoh 7:30

TAFAKARI: “Mpango wa Mungu kwa mwanadamu; na njia ovu za mwanadamu”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa namna ya pekee tutafakari neno hili, “Mpango wa Mungu kwa mwanadamu, na njia ovu za mwanadamu.” Mpendwa, somo la leo ikiwa ni pamoja na injili ya leo, yote kwa ujumla wake yanaongelea Mpango wa Mungu kwa sisi wanadamu, na matendo maovu tuyafanyayo kwa kujua au kutokujua ili mradi tu kwenda kinyume na matakwa yake Mungu. Tunaona jinsi ya  mtu wenye haki anavyodhulumiwa na kutendwa vibaya bila hatia yo yote. Tuona katika somo hilo la kwanza binadamu anavyokaa vikao vya kutenda maovu na kushauriana kufanya hivyo kwa utaratibu na kufanikisha jambo hilo.

Mwisho Mungu analiona jambo hilo na analiweka wazi. “Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa, kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu, wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia,” Hek 2:21-22. Jambo lo lote ovu lifanyikalo gizani ipo siku litawekwa hadharani. Mungu kwa uwezo na mamlaka aliyokuwa nayo aweza kuruhusu uovu kwa lengo la kutoa fundisho. Na katika mantiki hii, lililo ovu haliwezi kushinda kamwe! Na kamwe Mungu hawezi kuwa sehemu ya uovu ule kwa sababu Mungu ni Mkamilifu katika ukamifu wote. Kwa hiyo, ye yote yule ajivuniaye kwa uovu anapoteza muda wake bure na mwisho wa siku anajichumia mzingo wa dhambi.

Tunapoitazama jamii yetu leo kama Watanzania, ni wakati wa kulitazama kwa ukaribu Taifa letu na kuliombea sana. Wale wote wafanyao ovu kinyumbe na mpango wa Mungu hasa kwa wale wasiokuwa na sauti, si kwamba hawana chembe ya umungu ndani yao, ila wameamua kufanya hivyo kwa ajili ya nafsi zao na ubinafsi wao. Wamekubali kupatwa na upofu wa kutokuona mema kwa faida ya wengi. Mtu huyu mwenye haki, yaani mwananchi asiye na sauti, akitegemea wenye hekima na busara wamtete, anajikuta anasalitiwa. Mtu huyu ni Kristo anayeteseka leo na sasa. Wategemewa hawa, wamekuwa vipofu kutumia hekima yao kwa kung’ang’ania madaraka na kusahau cheo chao halisi, yaani Utakatifu wao. Hakika adhabu yao mbele ya Mungu ni kubwa.

Injili yetu pia yatuonyesha mtu mwenye haki anavyowindwa na hata kufikia kuutoa uhai wake. Yesu Kristo usalama wake unaingia matatani kwa vile tu anasimamia kweli, haki, huruma, msamaha na upendo. Hii ndiyo asili ya Kristo, na ndiyo asili ya Mungu. Ndiyo kusema kwamba kweli ya Kristo ni kweli ya Mungu. Kristo akiwa neno aliyefanywa Mwili, Yoh 1:14, ni Mungu yule yule tunayetaka kumwangamiza. Je, ikiwa binadamu kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27, vita hii binadamu ataiweza? “Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado,” Yoh 7:30. Hii ni ishara wazi kwamba nguvu za binadamu katika uovu wake dhidi ya Mungu na hasa kwa wanyonge hazitafanikiwa kamwe!

Mambo yote tuyaonayo leo yaliyo kinyume na mpango wa Mungu yana mwisho wake. Hakuna uovu wowote duniani, au tawala zozote duniani zilizodumu kwa muda wote. Uovu ni kinyume kabisa na uwepo wa Mungu. Yote haya tuyaonayo yanasubiri saa yake. Je, tufanye nini katika nyakati hizi za sintofahamu?

Katika nyakati hizi za sintofahamu, kamwe tusipoteze matumaini ndani na katika Kristo. Ni Kristo tu aliyeshinda uovu kwa wema atakayetupitisha katika mkwamo huu. Kristo anateseka sana na wale wanyonge na wasio na hatia katika jamii yetu leo. Kuwa na matumaini ni wito wa kuwa na Imani na Kristo. Imani ya kwamba yote yana mwisho wake, ni swala la Muda tu. Tutaweza kudumu katika matumaini na imani ndani na katika Kristo, kama tuna upendo wa kweli ndani yetu na Kristo. Upendo ni msingi mkubwa wa Matumaini na Imani. Ni katika kupenda twaweza kufanya yote ikiwa ni pamoja na kudumu katika sala hasa kwa kipindi hiki kigumu.

Ndugu yangu, tuwe macho kwa kila kitu tunachokumbana nacho leo, na kukitafakari kwa undani na kumwomba Roho Mtakatifu atusaidie kuona yale yote yaliyojifisha sirini.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi,” Yoh 7:28


Ee Yesu, uliyekubali kuzichukua dhambi zetu pasipo Wewe kutenda dhambi, tufungulie hekima yako hii ili nasi tuwajibike kikamilifu katika kuliondoa giza nene hili la uovu katika jamii yetu leo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario