JUMAMOSI
WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo:
Hos 6:1-6
Zab:
51:3-4, 18-19, 20-21
Injili:
Lk 18:9-14
Nukuu:
“Maana nataka fadhila
wala si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa,” Hos 6:6
“Lakini yule mtoza
ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali
alijipigapiga kifua akisema, ‘Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk
18:13
TAFAKARI:
“Majuto
ya dhambi ya kweli, na Msamaha dhambi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
na tutafakari leo, “Majuto ya dhambi ya kweli, na Msamaha wa dhambi.” Toba na
majuto ya kweli ni kumrudia Mungu bila kujibakiza. Mungu hujua yote katika
maisha yetu na hata yale ambayo yapo mbele yetu. “Je! Mashomoro watano hawauzwi
kwa sentí mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata
nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko
mashomoro wengi,” Lk 12:6-7.
Somo la kwanza linatupa
picha hiyo na mwono huo wa Mungu. Anachoitaji kwako, ni wewe wenyewe na siyo
yale uyafanyayo. Yakupasa kumjua Mungu, na hii ndiyo fadhila mbele za macho
yake. “Maana nataka fadhila wala si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka za
kuteketezwa,” Hos 6:6.
Ndugu yangu, huyafuti
makosa yako mbele za Mungu kwa wingi wa sadaka za kuteketezwa uzifanyazo au
uzitoazo. Leo hii katika jamii na makabila yetu, bado tupo na tunaendelea kutoa
sadaka za kuteketezwa. Mitambiko isiyokoma, na kwa mitindo mbalimbali. Sadaka
za mbuzi, na kuvishwa ngozi na mabangili ya shaba kwa kushikamanishwa na sadaka
hizo. Wingi wa matendo na sadaka hizi, hauondoi kosa letu mbele za Mungu. Tunachofanya
ni kujiongezea hofu pasipo hofu.
Kukiri na kufanya toba
ya kweli ndiyo salama ya maisha yetu. Sadaka hizi hazimpendezi Mungu. Ni
chukizo mbele ya Mungu. “Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za
dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati),
ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili
kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:8-9. La pili limeshasimamishwa na sadaka
ya mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Kasadaka kako na matambiko yako yananafasi gani
mbele ya Kristo? Acha maigizo hayo!
Habari Njema-Injili yetu
ya leo yatufundisha namna ya kufanya toba ya kweli na mkao wetu mbele ya Mungu
kwenye kiti chake cha Huruma na Msamaha. Ndugu yangu, tuwapo mbele ya Kiti cha
huruma na Msamaha wa Mungu, Yeye haitaji historia ya mema yetu tufanyayo kwa
sababu wema na uzuri ni asili na ni tabia ya Mungu. Haitaji kusikia ubaya wa
wengine, ila makosa yako. Mfarisayo anatoa historia ya mazuri yake na namna
afanyavyo mfungo wake. “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu
wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi
nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote,” Lk 18:11-12.
Ndugu yangu, mbele za
Mungu hatujihesabii haki, bali tunapewa haki hiyo baada ya kufanya yampendezayo
Mungu. Tunachohitaji mbele ya Mungu ni Huruma na Msamaha wake. Tukiwa mbele ya kiti hiki cha Huruma ya Mungu,
hatufanyi malinganisho ya dhambi wala uhalalishaji wa dhambi, ila makosa yetu
tuliyoyafanya kwa kujua au kutokujua. Labda nitoe mfano: Huwezi kwenda kuungama
na kusema hivi; “nimechukua pesa ya mume wangu na kulipa zaka kwa sababu yeye
hapendi kulipa zaka.” Kosa la wizi lipo pale pale, licha ya kwamba nia yako
ilikuwa nzuri, yaani kulipa zaka kwa niaba ya mume wako. Njia mbovu na ovu,
haziwezi kamwe kuhalalisha tendo lolote lile hata kama malengo yake ni mazuri.
Mfano wa kuigwa ni wa
Mtoza ushuru. Mtoza ushuru anajiachia kwenye kiti hiki cha Huruma na Msamaha wa
Mungu kama alivyo na kama alivyoyatenda makosa yake. “Ee Mungu, uniwie radhi
mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa maneno haya yanatosha kupewa dhawabu na kuinuliwa
katika hali yake ya unyonge iliyotokana na dhambi zake. Mtoza ushuru alikuwa
amejawa na hofu ya Mungu kiasi kwamba hakuthubutu hata kuinua macho yake
mbinguni, bali alijipiga-piga kifuani mwake. Hii ndiyo toba ya kweli na aibu
juu ya dhambi. Ndugu yangu, uwapo kwenye kiti cha Huruma na Msamaha wa Mungu, unachoitaji
ni uponyaji wa mwili na roho. Mponyaji wetu ni Mungu anayejua makandokando yetu
yote. Kamwe usione aibu kuziungama dhambi zako, na tena kwa uwazi kabisa.
Ndugu yangu, mara
nyingine waona baadhi ya dhambi zako ni kubwa sana, na mbele ya kiti hiki cha
Huruma na Msamaha, unaishia kusema na “nyingine nilizosahau,” ili hali unajua
hujazisahau. Huku ni kuchezea Kiti hiki cha Huruma ya Mungu na Msamaha, na
zaidi, kumkufuru Roho Mtakatifu. “Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa
Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa,” Lk 12:10. Hakuna
dhambi kubwa mbele ya Mungu ambayo atashindwa kukusamehe, na hakuna dhambi
ndogo mbele ya Mungu ambayo hata ichukulia maanani. Neema na huruma ya Mungu ni
KUBWA kuliko dhambi zako. Ikiwa dhambi ni ukosefu wa kutenda mema na kwenda
kinyume cha upendo wa Mungu, basi hakuna uzito wa dhambi kubwa wala ndogo mbele
ya Mungu kwa kusamehe. Tuziungame zote bila aibu.
Kwa kuziungama dhambi
hizo kama alivyofanya Mtoza ushuru, unahesabiwa haki, na kukwezwa mbele za
Mungu. “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko
yule (Mfarisayo); kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye
atakwezwa,” Lk 18:14.
Ndugu yangu, mali yako
halali mbele ya Mungu ni dhambi zako. Vingine vyote ni mali na uzuri wa Mungu.
Kuviishi kwa amani na uhuru alivyokupa Mungu kama sehemu ya uzuri wake, yakupasa
kusalimisha mali zako kwake, yaani dhambi zako. Hivyo, twende muda na wakati wo
wote kupatanishwa naye kwenye kiti chake hiki cha Huruma, Msamaha, na Upendo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye
dhambi,” Lk 18:13b
Ee Yesu, nijalie neema ya kuziona
na kuziungama dhambi zangu zote bila aibu mbele ya kiti chako cha Huruma,
Msamaha, na Upendo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario