viernes, 4 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA KWARESMA MWAKA-C

JUMAPILI YA 4 YA KWARESMA YA MWAKA-C
Somo I: Yos 5:9a, 10-12
Zab: 34: 1-6, (k) 8
Somo II: 2Kor 5:17-21
Injili: Lk 15:1-3, 11-32
Nukuu:
Bwana akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu,” Yos 5:9

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17

Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor 5:21

Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,” Lk 15:2

Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati,” Lk 15:13

Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa,” Lk 15:17 

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19

Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni,” Lk 15:22 

mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia,” Lk 15:23-24 

Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi,” Lk 15:28

Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona,” Lk 15:29-30 

Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako,” Lk 15:31 

TAFAKARI: “Majuto ya dhambi, na Toba ya kweli; Huruma, Msamaha, na Upendo wa Mungu Baba.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya nne ya Kwaresma ya mwaka “C” wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee, Mama Kanisa anatutaka tutafakari ‘Majuto ya dhambi, na toba ya kweli; Huruma, Msamaha, na Upendo wa Mungu Baba.’ Masomo yote matatu ya leo yanauthihirisha ukweli huo uliobebwa kwenye historia nzima ya wokovu wetu. Mungu aliye Huruma, Msamaha, Haki, Kweli, na Upendo ambayo ndiyo asili yake, yupo tayari kuanza upya na kila mmoja wetu licha ya uhusiano huo kuvunjika kutokana na dhambi.

Utayari wa Mungu Baba wa kuanza upya na mwanzo mpya na kila mmoja wetu upo nyakati na muda wote. Naye Mungu anasema, Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi,” Ufu 1:8. Ila njia sahihi ya kumrudia Mungu na kuanza upya naye kulikovunjika kutokana na dhambi zetu, ni kwa njia ya majuto ya dhambi zako, na kufanya toba ya kweli. Ukweli huu tunauona katika Injili ya leo iliyobeba simulizi la ‘Mwana Mpotevu.’

Wapendwa wana wa Mungu, hata pamoja na kiburi chetu kama wanadamu, na wakati mwingine kutokuona uhitaji wa huruma, msamaha, na upendo wa Mungu, Mungu mara zote amekuwa msababishi katika kurudisha uhusiano huo na viumbe vyake licha ya kuasi kwao. Hivyo Bwana akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu,” Yos 5:9. Tendo hili linadhihirisha asili ya Mungu, yaani, Huruma, Msamaha, Haki, Ukweli, na Upendo. Hivyo ili Mungu atimize hazma yake hii, hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5.  Na huu ndio ukaribu wa Mungu kwa mwanadamu, yaani, kuujenga upya tena uhusiano na wanawe kwa lengo la kuwaweka huru kutoka utumwa wa dhambi.

Wapendwa katika Kristo, leo huruma na msamaha huo tunaupata kupitia Kristo mwenyewe ambaye ndiye  Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Leo pia kwa namna ya pekee huruma na msamaha huo wa dhambi tunaupata kupitia Kanisa kama Sakramenti ya wokovu wetu. Mamlaka hayo kayatoa Kristo mwenyewe katika Kanisa, na kwa watumishi wake waliohesabiwa haki hiyo na Mama Kanisa kabla ya kupaa kwake Mbinguni. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Hivyo ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, Mungu Baba kupitia Mwanaye Mpenzi na Kanisa lake, anakualika kupatanishwa naye kila upumuapo pumzi yake.

Je, ni kwa nini yatupasa kupita kwa Kristo ili tuupate huo upatanisho na Mungu? Wapendwa wana wa Mungu, somo la pili limetupatia jibu halisi na kamili ‘kwa nini lazima Kristo.’ Ni kwa kupitia Kristo na ndani ya Kristo tunakuwa viumbe vipya na kuanza upya katika safari ya uzima wa milele. Ni kwa sababu hiyo, hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya,” 2Kor 5:17. Na nikupitia Kristo tu ambaye, Yeye asiyejua dhambi (Mungu) alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor 5:21. Hivyo kwa mantiki hii, hakuna miongoni mwetu awezaye kujihesabia haki pasipo Kristo. Haitawezekana ndungu yangu!

Ni kwa ukweli huu kwamba, hatuwezi kujihesabia haki pasipo Kristo ukweli ambao wanaupinga Mafarisayo na Waandishi. Watu hawa walijihesabia haki pasipo haki ya kweli ambayo yatoka kwa Mungu mwenyewe. Yesu anawakemea wazi wazi na kutoa angalizo kwetu kwa kusema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3. Kwa mtazamo huu wa Mafarisayo na Waandishi, hawakuona haja ya majuto ya dhambi zao, na hata kufanya toba ya kweli. Walijiona safi na kamili, na hivyo hawakuhitaji huruma na msamaha wa Mungu. Ukaribu wa Yesu na ushiriki wake na wokosefu kwa lengo la kuwatoa katika hali zao duni na udhaifu ulio tokana na dhambi, tendo hili linaonekana kikwazo kwa Mafarisayo na Waandishi. Na hii ndiyo sababu ya manung’uniko yao kwa Yesu, “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,” Lk 15:2. Mfano wa Mwana Mpotevu katika Injili ya leo unajibu manung’uniko hayo ya Mafarisayo na Waandishi. Mfano huu unaweka wazi ukweli huu kwamba, ‘Neema na Huruma ya Mungu ni KUBWA kuliko dhambi za mwanadamu pale mwanadamu huyo afanyapo majuto na toba ya kweli.’

Kwa kujibu manung’uniko waliyokuwa nayo Mfafarisayo na Waandishi juu wa ukaribu aliokuwa nao Yesu kwa wadhambi, Injili inahainisha wahusika wakuu watatu; Baba mzazi, Mwana mpotevu, na Kaka ya mwana mpotevu. Wengine ni watumishi au watumwa wa Baba mzazi wa Mwana mpotevu, na marafiki wa mwana mpotevu. Mwana mpotevu, tena aliye mdogo katika familia hii, anafanya kitu ambacho si cha kawaida katika jamii. Kitendo cha kuomba urithi au sehemu ya mali yake kabla ya kifo cha baba yake, kulimaanisha kumtakia mabaya Baba yake. Ni kutokumtambua Baba yake. Ni kumchukulia Baba yake kama marehemu.

Kwa upande wa Baba yake, na kutokana na upendo aliokuwa nao kwa wana wake na familia, anakubali aibu hiyo, na kufanya kadiri ya matakwa ya mwanaye. Baba anampa sehemu ya urithi wake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati,” Lk 15:13.Yaliyompata kijana huyu wote tunafahamu vizuri simulizi hili.

Ndugu yangu, kutenda makosa ni hali yetu sote wanadamu. Ila tofauti ipo hapa; unapotambua umefanya kosa na kuchukua hatua kwa uliyoyafanya ndiko kunapoturejeshea hadhi na heshima yetu tena. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa,” Lk 15:17. Baada ya kutindikiwa na mambo kwenda ndivyo sivyo, Mwana mpotevu analiona kosa lake na anakiri kwa matendo na maneno, “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19. Ndugu yangu, haya ndiyo majuto ya kweli. Tunachoangalia si aibu tutakayopata, bali huruma, masamaha, na mastahili tunayotarajia kuyapata kwa upendo wake Mungu kwa kufanya toba ya kweli.

Ndugu yangu, tunapodondoka kwa sababu ya dhambi, tusione aibu kuamka na kuomba msamaha kwa muumba wetu. Yeye Mungu anasema, “mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” Ufu 1:8. Je, kuna mwingine wa  kumkimbilia zaidi ya Mungu wetu? Mungu aliye Upendo hana mipaka wala masharti ya pekee tunapomrudia. Mungu anasema, “nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,” Mit 8:17.

Upendo wa Baba hauna mfano. Baba huyu anapomwona mtoto wake, hapendi na wala haitaji kujua historia ya yale maovu aliyofanya. Furaha yake ni kumwona kama alivyo na anajua kurudi kwake ni toba ya kweli. Na hivi ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu wa Huruma na Neema. Anachofanya Baba katika simulizi hili la Mwana Mpotevu ni kumrudishia mastahili na hadhi yake kama mwana na mmoja wa familia yake. Alipomwona tu mwanaye,  baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni,” Lk 15:22. Mwana Mpotevu anarudishiwa hadhi na mastahili yake kama mwana familia kama ilivyo na itakavyo kuwa mbele ya Mungu tunapofanya majuto na toba ya kweli. 

Tendo hili la Baba, wapendwa wana wa Mungu, linakuwa sononeko la Kaka ya mwana mpotevu. Haoni maana ya furaha hii na sababu ya kuwa hai mdogo wake. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi,” Lk 15:28. Ndugu yangu, katika safari ya wokovu, tusipende kujitazama wenyewe. Wokovu ni kwa wote na nifuraha ya Mungu na kwa wote wenye mapenzi mema, yaani watakatifu wa Mungu. Tendo la wokovu ni furaha na sherehe kwa wote kwa sababu tunairudia sura yetu halisi, yaani, sura ile na mfano ule wa Mungu tulioumbwa nayo, mwa 1:27. Mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia,” Lk 15:23-24. Katika mfano huu, Yesu anawakemea Waisraeli na hasa Mafarisayo na Waandishi ambao wanahuzunika kwa yale anayofanya Yesu kuufunua Upendo wa Mungu Baba.

Wapendwa katika Kristo, yatupasa kutiana moyo na kufurahi mwenzetu anapomwongokea Mungu na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Mara nyingi hatuachi kuwasema vibaya wale wanaojitahidi kuishi njia impendezayo Mungu. Tunawapachika majina mengi, na kuwakatisha tamaa kabisa. Kwa upande wetu, mwenzetu anapojitahidi kuishi vizuri, basi iwe changamoto ya sisi kufanya vizuri. Hivyo basi tulio karibu na mwanga wa Mungu, na kuenenda kadiri ya upendo wa Mungu, tuwe na huruma kwa wote wanaomrudia muumba wao tukijua kwamba, tu pamoja na Baba na Upendo wake sikuzote, na vyote alivyo navyo ni vyetu sote, Lk 15:31. Hivyo tuuvue ubinafsi wetu na tuwe na huruma ili tuyaone mahitaji ya wengine na hasa ya kiroho.

Ndugu yangu, wakati ndiyo sasa! Kaa na tafakari namna utendavyo. Je, unafanya kadiri ya mapenzi ya Mungu au wajitazama mwenyewe? Urithi wako ni fursa uliyonayo sasa katika utendaji. Tuepuke sononeko la Mwana yule Mkubwa, “Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona,” Lk 15:29-30. Je, kwa kuwa karibu na Baba unatumia fursa hiyo vizuri kuonja huruma na upendo wake Mungu? Na kama Mwana Mpotevu, Je, baada ya kuishi ovyo kwa muda wote huo, upo tayari kufanya toba ya kweli na kuacha njia hiyo?

Basi yanipasa nielewa kwamba nafasi niliyo nayo ni leo na sasa tu. Ni vyema nikachukua hatua sasa na kuutafuta uso wa Bwana. “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3. Amina

Baba Mazoea alihabatika kuoa na kupata watoto wanne. Maisha ya familia hii yalikuwa ya dhiki kubwa sana. Umoja na mshikamano wao kama familia ndiyo ilikuwa sababu ya kuwa na matumaini kwamba ipo siku yote yatakuwa vizuri. Mama Mazoea hakuacha kamwe kumwombea Mumewe kwa Mungu ili apata kazi.

Basi baada ya miezi kama minne hivi, zilitangazwa kazi za ulinzi katika shirika moja la wanyama pori. Baba Mazoea alichaguliwa baada ya kufaulu vizuri mtihani ule wa usahili. Baba Mazoea alianza kazi kwa bidii sana na kuijali familia yake vizuri sana. Kwa mwaka mmoja mambo mengi yalibadilika kwenye familia hii. Walikula vizuri, walivaa vizuri, waliboresha nyumba yao, na watoto walisoma vizuri.

Mwisho wa mwaka ule, Baba Mazoea alipandishwa cheo na kuwa mlinzi Mkuu ikiwa ni pamoja na kupata tunzo la mfanyakazi bora wa shirika lile la wanyama pori. Tunzo ile iliambatana na kitita cha milioni tano. Familia ilikuwa na furaha sana. Wakiwa katika furaha ile kama familia, Baba Mazoea alitoweka nyumbani ghafla. Wiki, mwezi, na miaka ilipita bila mafanikio. Nyumbani na hata kazini kwake hawakujua alikotowekea.

Maisha yalibadilika na kuwa mabaya sana katika familia ya Baba na Mama Mazoea. Watoto halisoma kwa shida, na Mama Mazoea aliishi kwa huzuni sana. Baada ya miaka tisha hivi, walipata taarifa ya Baba yao kuwa alitoroka na msichana mmoja na kuishi naye migodini. Taarifa hii ilichochea chuki na hasira kwa watoto dhidi ya Baba yao.

Siku mmoja jioni baada ya miaka 14 kupita, alionekana nje ya nyumba mtu mmoja akiwa amechoka sana huku akibeba mfuko wa kigunia wenye vijinguo vichache vilivyochakaa. Huyu alikuwa Baba Mazoea aliyejisalimisha katika familia yake akiwa amechoka vibaya. Watoto hawakutaka kabisa Baba yao kuingia ndani ya nyumba ile. Ila mkewe aliwasihi watoto wake na kusema, “eleweni huyu ni Baba yenu na ataendelea kuwa Baba yenu. Hamna Baba mwingine, na wala hakuna duka lolote dunia wanamouza wazazi. Msameheni, na kwa hali yake hii anahitaji huruma na upendo mkubwa kutoka kwenu.” Baada ya maneno haya ya Mama Mazoea, kwa taratibu na mwendo wa kujiburuza, Baba Mazoea aliingia ndani.

Ukimya mkubwa ulitanda sebuleni pale. Mama alikwenda jikoni na aliandaa uji haraka na kuuleta mezani. Kabla ya kunywa uji ule, Baba Mazoea aliyasema maneno haya, “wanangu wapendwa na mke wangu mpenzi, niwieni radhi kwa yote yaliyotokea na niliyoyatenda kwenu kama Baba wa familia hii. Mnayo haki na sababu ya kutosha kuchukia na kunichukia kwa yote yaliyotokea. Binafsi najiona kutostahili kuwa nanyi tena, ila sina mji mwingine na ndugu wengine zaidi yenu ninyi kama familia yangu. Kwenu nawaomba huruma na msamaha. Nipokeeni kama nilivyo. Asanteni.” Baba Mazoea alibubujika machozi ya utu uzima!

Huku machozi yakimbubujika, Baba Mazoea aliufungua mfuko wake na kutoa cheti chenye rangi ya kijani hivi. Cheti kile alimkabidhi mkewe na kusema, “kwa sana ninaishi kwa matumaini. Mimi ni mwathirika wa gonjwa hili la ukimwi. Bado nawapenda wanangu na mke wangu. Naomba mnipende hata katika hali hii.” Familia yote bila kuambizana waliamka na kumkumbatia Baba yao huku machozi yakiwatoka.

Wapendwa wana wa Mungu, kuna ushindi mkubwa sana ufanyapo majuto na toba ya kweli, na pale unaposamehe kutoka ndani ya moyo wako na kuanza upya. Amina.

Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi, Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe. Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako, Hata misiba hii itakapopita,” Zab 57:1


No hay comentarios:

Publicar un comentario