miércoles, 16 de marzo de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MT. JOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA

JUMAMOSI WIKI YA 5 YA KWARESMA
19/3/2015
Mt. Yosefu, Mume wa Bikira Maria

Somo I: 2 Sam 7:4-5, 12-14, 16
Zab: 89:2-3, 4-5, 29, 29
Somo II: Rum 4:13, 16-18, 22
Injili: Mt 1:16, 18-21, 24
Nukuu:
“Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu,” 2 Sam 7:13-14

“Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheri bali kwa haki aliohesabiwa kwa imani. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi wote,” Rum 4:13, 16

“Naye Yusufu mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:19

TAFAKARI: “Utabiri juu ya Yesu Kristo, na kuhesabiwa haki kwa Yusufu/Yosefu Baba Mlezi wa Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, karibu katika tafakari yetu ya leo, ambapo Mama Kanisa anafanya Sikukuu ya Mtakatifu Yusufu/Yosefu Baba Mlezi wa Yesu Kristo, na kuadhimisha pia miaka mitatu ya Uongozi wa Baba Mtakatifu wetu Fransisco. Tafakari yetu ya leo imejikita katika wazo kuu hili, “utabiri juu ya Yesu Kristo, na kuhesabiwa haki kwa Yusufu/Yosefu Baba Mlezi wa Yesu Kristo.”

Somo letu la kwanza na la pili katika siku hii maalumu, yanatupatia utabiri wa Yesu Kristo na kazi yake katika utimilifu ulio wazi wa historia ya wokovu wetu. Somo la kwanza limetupa kwa ufupi utabiri huo wa Yesu Kristo kwa maneno haya, “Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu,” 2 Sam 7:13-14. Kazi kubwa atakayokuwa nayo Kristo ni kuijenga nyumba ya Mungu kwa jina la Mungu, na kiti cha ufalme wake kitafanywa kuwa imara Milele. Je, nyumba ya Mungu ni nini? Na, kiti chake cha ufalme ni kipi?

Ndugu yangu, nyumba ya Mungu ni Kanisa lake kama jengo, na wafuasi wa Kristo, yaani wale wote waliobatizwa kwa jina lake, na kuyaishi yale yote aliyoyafundisha kama mwendelezo wa ufunuo wa aliye yote katika yote na utimilifu wote. Kanisa hili la wabatizwa ni hili linalotembea, yaani Kanisa la hija, Kanisa la Watakatifu Mbinguni, na Kanisa linaloteseka Toharani ambalo kwalo, lahitaji sala na maombi ya Kanisa la hija na Kanisa la Watakatifu Mbinguni.

Kanisa hili la hija ni mchanganyiko wa Watakatifu na wadhambi. Ni Kanisa linaloendelea kutakatifuzwa kwa neema zipatikanazo katika Kanisa kwa njia ya Masakramenti yake. Mimi na wewe tupo katika Kanisa hili la hija. Tunaitaji maelekezi na mwongozo wa Kristo na Kanisa la Watakatifu katika wongofu wetu wa kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Ni Kanisa lililojaa Huruma ya Mungu, na kuongozwa kwa unyenyekevu katika kujiachia katika Kristo na ndani ya Kristo, kama asemavyo Mtume Paulo, “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.” Flp 3:12,14. Wito wetu mkuu tulio wafuasi wa Kristo ni kuwa WATAKATIFU.

Kiti cha Ufalme wake Kristo ni Mamlaka “Authority” yake. Mamlaka ya Kristo si Nguvu “Power” katika mtazamo wa kiutawala wa leo na kisiasa, bali ni mamlaka katika Maadili “Moral.” Kwa hiyo ni kiti cha nguvu ya Mamlaka ya kimaadili “Moral Authority,” ambayo kiundani inanguvu kuliko nguvu ya siasa katika utawala “Political Authority.” Nguvu hii ya kiutawala kwa mtazamo wa Kanisa na Kristo imelindwa na kuachwa katika mambo makuu matatu;  Maandiko Matakatifu “Scriptures”; Mapokea ya Mitume kuanzia Kristo mwenyewe hadi leo katika umoja wa Maaskofu “Tradition; na Mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium.” Mambo haya matatu kwa mtazamo wa leo Kikanisa ndiyo kiti cha ufalme wa Kristo. Ni mwendelezo wa yale aliyokuwa akiyafanya na anaendelea kuyafanya hadi mwisho wa nyakati. Hapa ndipo tunapouona umoja wa waamini ndani na katika Kristo. Misingi hii na miimili hii mitatu yapaswa kuwa Imara muda wote na kutosigana. Yote hufanywa kwa unyenyekevu mkubwa, kwa kila mmoja watu kujua nafasi yake katika safari hii ya wokovu.

Mpendwa wana wa Mungu, somo letu la pili, laufunua utabiri huo wa Kristo na mwendelezo wake katika kuyaishi, kwa maneno haya, “Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheri bali kwa haki aliohesabiwa kwa imani. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi wote,” Rum 4:13, 16.

Hapana shaka ye yote ndugu yangu, kwamba, mpango wa Mungu katika wokovu licha kwamba ulianza kwa mtu mmoja kama Ibrahimu, na tena kwa kundi la watu yaani Waisraeli (Torati), utimilifu wake ni kwa watu wote kwa sababu, Ibrahimu alihesabiwa haki ya kuwa Baba wa sisi sote. Yesu Kristo katika mateso, kifo na ufufuko wake kaliweka jambo hili wazi na kwa uelewa mkubwa sana. Kwa sababu hiyo, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Katika kifo chake sisi sote kama wafuasi wa Kristo tumehesabiwa haki kwa damu yake Msalabani kwa upendo wake huu mkuu. Sisi si watumwa tena, bali ni rafiki zake na ndugu zake Kristo. Kwa maana hiyo, “Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.” Yoh 15:15. Litendwalo ndani na katika Kristo ni lile tu liufunualo; upendo wake, unyenyekevu wake, uaminifu wake, upole wake, utii wake, amani yake, na utakatifu wake.

Injili yetu ya leo, na hasa siku hii kuu ya Mtakatifu Yusufu/Yosefu, imelenga katika kuhesabiwa haki Yosefu kama Baba Mlezi wa Yesu Kristo. Kibinadamu ni vigumu sana kupokea hali iliyomkuta Yosefu. Ni ukweli ulio wazi kwamba kwa vile Yosefu alimpenda sana Mama Bikira Maria, hakutaka kumwaibisha. Unyenyekevu wake huu unamfanya Yosefu achukue hatua ya busara kwa kufanya hivi: “Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:18b-19. Je, ni aibu gani ingempata Mama Bikira Maria kama Yosefu angeamua kuliweka wazi?

Ndugu yangu, kadiri ya Sheria za kiyahudu na utaratibu wao kuhusu mahusiano, Bikira Maria ilimpasa adhabu ya Kifo. Kuwa na ujauzito kabla ya ndoa halisi ya Kiyahudi lilikuwa kosa kubwa sana. Si aibu kwa Bikira Maria tu, bali hata kwa familia yake kwa kukosa malezi mazuri ya Binti yao. Kwa kosa hili adhabu yake ilikuwa hivi. “Lakini ikiwa ni kweli neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira; na wamtoe nje yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.” Kumb 22:20-21.

Kwa mantiki hii, Yosefu alijua wazi kitakacho mpata Bikira Maria hivyo anaamua kumwacha kwa siri. Na kwa vile kadiri ya uchumba na maandalizi ndoa ya kiyahudi huchukua si chini ya miezi sita, bila shaka Yosefu alijua uaminifu wa Bikira Maria, kuwa ni binti aliyekuwa na malezi mazuri. Ujauzito huu ulimchanganya sana Yosefu. Hivyo kutohusika na jambo hili ambalo kwake lilikuwa ni fumbo, anaamua kutoshiriki kumwaka damu yake. Hapa ndipo anapohesabiwa haki Mtakatifu Yosefu kwa uthibitisho wa maneno haya ya Malaika, “Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu,” Mt 1:20. Malaika wa Mungu anafunua ukweli wa kitakachozaliza kuwa kina mkono wa Mungu na ni kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima. “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao,” Mt 1:21. Je, akina baba katika ndoa zenu mna kifua kizito kama cha Mt.Yosefu?

Ndugu yangu, yakujifunza kutoka kwa Mt.Yosefu yapo mengi sana kwa Kanisa katika ujumla wake na kwa kila mmoja wetu. Kwa upande wa Kanisa na hasa wale waliopewa dhamana katika utumishi wa Kristo, yatupasa kuwa na subira na unyenyekevu kama wa Mt. Yosefu katika kuona, kufikiri, kuamua, na kutenda. Msingi wa haya yote ni unyenyekevu. Kwa kila mmoja wetu, na hasa wana familia ya Mungu, yatupasa kusikiliza sana sauti iliyopo  ndani mwetu na kuamua lililo jema zaidi, na sio ushindi wa haraka usio na tija. Pili, hatujihesabii haki hata kama tunayomastahili katika yale yatuhusuyo kisheria, kimtazamo, na hata  kimila na desturi zetu. Tumpe kwanza nafasi Roho Mtakatifu atuelekeze namna ya kufanya pale tunapokabiliwa na giza nene katika maamuzi.

Mwisho wapendwa, tuliombee Kanisa lote kiulimwengu, na hasa maeneo yale ambayo Wakristo wenzetu wanateseka na kuuwawa kikatili kwa sababu ya Imani yao juu ya Kristo na Mungu aliye hai. Tuliombee Kanisa na hasa leo ambapo Baba Mtakatifu anapoadhimisha miaka mitatu ya uzinduzi wa ofisi yake ya Kipapa kama Baba Mtakatifu. Tuliombee pia Kanisa letu mahalia la Tanzania hasa katika kipindi hiki cha sintofahamu nyingi za kiimani.

Tumsifu Yesu Kristo

“Naye Yusufu mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:19


Ee Yesu, tuhesabie haki kwa kile tulicho kila mmoja kadiri ya wito wake.

No hay comentarios:

Publicar un comentario