miércoles, 9 de marzo de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 4 YA KWARESMA

ALHAMISI WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Kut 32:7-14
Zab: 106:19-20, 21-22, 23
Injili: Yoh 5: 31-47
Nukuu:
“Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14

“Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?” Yoh 5:40-41,44

TAFAKARI: “Huruma ya Mungu, Uzima, na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, “Huruma ya Mungu, Uzima na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.” Somo la kwanza Mungu anaonyesha huruma kwa watu wake kupitia Mtumishi wake Musa. Musa akiwa mlimani kupokea amri za Mungu, waliobaki chini wakisubiri maelekezo hayo ya Mungu, walijifanyia mambo yao kwa kujichongea sanamu zoa kama utambulisho wa Mungu wao wa kutengeneza. Hili lilikuwa ni chukizo kubwa kwa Mungu. Kwa hasiri hii Mungu anataka kuliangamiza taifa lote la Israeli kwa kutokuwa na subira. Bwana akamwambia Musa, “Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu. Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize,” Kut 32:9-10.

Musa analiombea taifa lake, kwa kumkumbusha Mungu ahadi zake alizozitoa na kuzifanya na Ibrahimu, Isaka na Israeli. Kwa huruma yake Mungu, anaghairi hasira yake, na kusema, “Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14. Mungu wetu ni Huruma na mara zote yupo tayari kuhurumia na kutusamehe tunapoyakiri makosa yetu na kumrudia. Huruma hii ya Mungu iwe pia ndani yetu hasa pale ninapotakiwa kutoa huruma hiyo bila masharti katika kusamehe. Huu ndiyo mwito wetu pia sisi sote tunaomwamini Mungu, na Mwanaye Yesu Kristo.

Injili yetu ya leo inatupa msingi wa kile tuaminicho na malengo yetu kama wafuasi wake Kristo. Ndugu yangu, uzima wako na utukufu wako hauwezekani pasipo kuwa ndani ya Kristo na katika Kristo. Wayahudi hawaukubali ukweli huu, na badala yake wanamdhihaki Yesu Kristo kwa kutokuamini kwao. Hawatambui pia yale yote yaliyofunuliwa juu ya Kristo katika safari nzima ya historia hii ya wokovu. Yesu anasema mshitaki wao mkuu ni kazi zake, na yale yote yasemwayo katika maandiko Matakatifu. “Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu,” Yoh 5:45-46.

Uzima na utukufu wetu wapatikana katika Kristo kwani Yeye yupo kwa ajili ya hayo na ameyafia hayo. Yatupasa kuyaamini atufundishayo. Na kama hatuyaamini atufundishayo tuziamini kazi zake. “Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?” Yoh 5:40-41,44. Utukufu wa kweli ni ule utokao kwa Mungu, ambao kwa namna ya pekee ndiyo Yesu Kristo anatujalia sisi kutipitia mateso, kifo na ufufuko wake. Hakuna utukufu kwa Mkristo bila msalaba. Uzima huu twaupata kwa kula na kunywa damu yake katika mastahili 1Kor 11:27, ikiwa ndiyo njia ya pekee ya kushiriki mateso, kifo, na utukufu wa Kristo. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54.

Ndugu yangu, wakati ndiyo sasa wa kujipanga sawa sawa na kujua uzima na utukufu wako unatoka wapi. Ishi imani yako ipasavyo na “msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.” Ebr 13:9.

Tumsifu Yesu Kristo

Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma,” Yoh 5:36


Ee Yesu Kristo, nakiri na kuamini kwamba Uzima na Utukufu vya toka kwako tu Wewe uliye yote katika yote. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario