domingo, 28 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 3 YA KWARESMA

JUMATANO WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo: Kumb 4:1, 5-9
Zab: 148:12.13, 15-16, 19-20
Injili: Mt 5:17-19
Nukuu:
“Na sasa, ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende, mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu,” Kumb 4:1

“Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17

TAFAKARI: “Sheria ya Bwana ni kamilifu, nayo ni uhai wetu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo na tutafakari “sheria ya Bwana na ukamilifu wake.” Sheria ya Bwana ni utaratibu wa kuyaishi yale yampendezayo Mungu, na kuwa na mahusiano mazuri naye kwani Yeye ndiye uhai na uzima wetu. Wana wa Israeli walipewa sheria kama mwongozo wa kutenda na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. “Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe,” Kut 24:12. Sheria hizi zilipaswa kufuatwa kiaminifu na bila kuzichakachua. “Mioyo yenu na iwe kamili kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.” 1Fal 8:61.

Ukamilifu na uaminifu wa mtu ulipatikana katika kuzishika sheria za Bwana. Kwa sababu, “sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.” Zab 19:7. Hivi ndivyo ilivyopaswa kuzishika sheria za Bwana. Na hilo ndilo lililokuwa kusudi la sheria. Jambo la kushangaza wakati wa Yesu, Wayahudi hawakuwa wanafuata Torati kama iliyokuwa mwanzo, yaani, nyakati za Musa. Wayahudi walikuwa wanafuata tafsiri ya Torati ambayo iliendana na matamanio yao na siyo ya Mungu. Huu ndio ugomvi uliokuwepo kati ya Yesu na Waandishi na Mafarisayo.

Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu, Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi), iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati, (Mt 15:2-3, 6; Mk 7:3, 5, 8, 9, 13). Naye Yesu anawaambia, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:8. Mapokea haya ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Mtume Paulo baada ya kuongoka na kuujua ukweli kuhusu sheria ya Bwana anawaambia Wakolosai, Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Ukweli ni kwamba, Mtume Paulo kama Mfarisayo kabla ya kuongoka kwake aliyafuata mapokea haya ya wazee ambayo yalikuwa ni ‘ukweli wa Mungu uliopotoshwa.’ Paulo anakiri jambo hili na kusema, Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal 1:14.

Kwenye jambo hili, yaani kweli ya Sheria ya Bwana, Yesu anawakemea Mafarisayo na Waandishi na kusema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17. Hapa Yesu akubaliani nao kwa swala la kuichakachua Torati kama walivyokwisha kufanya. Yesu anarudisha mpango mzima wa Mungu katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Yesu anatoa zaidi maana ya sheria na ushikaji wa sheria hiyo. Yesu anawakosoa Mafarisayo kwa unafiki wao katika sheria na kusema, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache,” Mt 23:23

Utimilifu wa sheria kadiri ya mpango mzima na mtazamo wa Yesu umebebwa katika upendo. Hii ndiyo amri mpya. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Mtakatifu Agustino anatuambia kwamba, “ukipenda utafanya yote.” Ni katika mantiki hii kwamba, “mkipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Ndugu yangu, ukiona viongozi wetu serikalini au kwenye taasisi yoyote ile wanang’ang’ana kubadili katiba kwa matamanio yao na vyama vyao bila kujali maslahi ya wengi, ni wazi kabisa mwisho wake ni upotoshaji wa kweli na kwenda kinyume na mpango wa Mungu kupitia watu wake.

Katika kweli hili niliyosema kuhusu ung’ang’anizi wa kubadili mambo kadiri ya matamanio ya wachache, bado tunao Mafarisayo na Waandishi katika jamii yetu kama ilivyokuwa nyakati za Yesu. Leo tuna mkwamo mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar kwa sababu tu ya wachache wenye kutanguliza matamanio yao ya kuenzi umilele katika ‘utawala’ bila hofu ya Mungu. Hiki ni kitu kisichowezekana hata kidogo. Katiba haitafsiriwi kama ilivyo, bali inapewa tafsiri kadiri ya matamanio ya wachache ili kukidhi tamaa na makusudi yao huku wengi wakiteseka pasipo sababu za msingi. Yatupasa kila mmoja wetu kadiri ya Imani na itikadi zake aone hili ni tatizo kubwa na linahitaji kutatuliwa haraka. Katiba ndio msahafu wetu sote bila kujali Dini, Imani, na itikadi zetu. Katiba haipaswi kuhodhiwa na Chama chochote kile cha siasa. Tukifanya hivyo tu, tujiandae kwa machafuko makubwa.

Ndugu yangu, nawe uliye Mkristo, Ukristo wetu bila UPENDO wa kweli ni Ukristo MFU. Kwa Mkristo kuwa na upendo wa dhati ni kuzishika amri za Mungu katika ukamilifu wake. “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Na kukaa katika pendo la Mungu ni kuzishika amri zake. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10

Ndugu yangu, ni wakati wa kijitazama, na hasa tukianzia kwenye familia zetu, Jumuiya zetu ndogondogo za Kikristo, na za kitawa, na dhamana tuliyopewa na umma kama viongozi kuishi katika kweli na haki. Huwezi kutenda kweli na haki kama huwapendi wale unao waongoza. Mwenye nafasi hii ya uongozi bila upendo kwa watu wake, ni rahisi sana kusukumwa na ubinafsi wake, na matamanio ya wachache wasio na uchungu na mateso ya wengi. Je, kama kiongozi waishi upendo wa kweli na haki? Mt. Yohane wa Msalaba anasema hivi, “When evening comes, you will be examined in love. Learn to love, as God desires to be loved and abandon your own ways of acting.” Kunapokuwa na upendo wa kweli, sheria ufanya kazi dogo sana, na wakati mwingine sheria hiyo hutoweka kabisa.

Upendo wa kweli utusukuma kufanya zaidi ya yale yanayohainishwa na sheria husika. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Huu ndio mfano wa kuigwa kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tupendane! “The soul that walks in love neither tires others nor grows tired,” Mt. Yohane wa Msalaba.

Tumsifu Yesu Kristo

“Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17


Ee Yesu, nijalie Upendo wa kweli na kukuona kwa kila mmoja ninayekutana naye katika maisha yangu. Amina

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 3 YA KWARESMA

JUMANNE WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo: Dan 3:25, 34-43
Zab: 25:4abc-5ab, 6-7bc, 8-9
Injili: Mt 18:21-35

Nukuu:
“Na sasa tunakufuata kwa moyo wote, tunakucha, na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawasawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.” Dan 3:40-43

“Yesu akamwambia, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22

TAFAKARI: “Msamaha wa Mungu na kweli; ni kuvivaa viatu vya wale waliotusamehe na kujirudi ndani ya nafsi yako kwa wale uliowakosea.”

Wapendwa katika Kristo, leo tujikite katika tafakari yetu kwenye, “Msamaha wa Mungu na kweli; ni kuvivaa viatu vya wale waliokusamehe na waliokukosea.” Masomo yetu leo yanafunua na kufafanua kwa undani hatua za kufikia msamaha, na ulazima wa kutoa Msamaha. Ndugu yangu, Msamaha wa Mungu na kweli huridhiwa naye pale tu tunapokiri makosa yetu kwa dhati. Kukiri makosa ni kujiona kwa ndani, kuukubali ubinadamu wako katika mapungufu, kuwa tayari kuanza upya na vizuri zaidi, kuwa na matumaini na mwelekeo sahihi wa kule tuendako na kupatamani; furaha ya kweli. Somo la kwanza linaelezea hali hiyo.

Azaria anasimama na kukiri mbele ya Mungu kwa niaba ya Jamii yake kule kuishi kusikompendeza Mungu. “Na sasa tunakufuata kwa moyo wote, tunakucha, na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawasawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.” Dan 3:40-43. Hii ni hatua muhimu sana kuelekea msamaha. Je, Mungu anaitaji jambo hili ili kutusamehe? Jibu ni hapana! Kwa kufanya hivyo hatumbembelezi Mungu kwa sababu haitaji kubembelezwa. Yeye ni mkamilifu katika ukamilifu wote na haitaji cho chote kutoka kwa viumbe vyake ili vimuongozee ukamilifu wake. Ila, tunapokiri makosa yetu, tunajitambulisha kwake kwa kukubali ubinadamu wetu na kuwa sisi ni viumbe tu kwake. Tunapokaa katika nafasi yetu kadiri ya uumbaji wake, ndiyo furaha ya Mungu na uzuri wake. Kwa kufanya hivyo, tunapokea lile umbo alilotupa katika uumbaji wetu, yaani sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni katika hatua hii tunatambua kwamba, “rehema na msamaha ni kwa Bwana wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii,” Dan 9:9

Ndugu yangu, haya ndiyo makusudi ya kukiri makosa yetu kabla ya kwenda kuyaungama kupitia Sakramenti ya Upatanisho. Wengi wetu huwa tunakurupuka tu bila kufanya tathimini ya kina kwa yale tuliyokosea. Anayekwenda kuungama bila kufanya zoezi hili la dhamiri, ni kutokuheshimu na kuichezea sakramenti hii ya upatanisho. Hapa tunakumbushwa pia zile hatua za kupitia kabla ya kupata maondolea ya dhambi (rejea mfundisho yako kuhusu sakramenti ya kitubio/upatanishi).

Ni ukweli usiotia shaka kwamba kama Mungu angechukua hatua ya hapo kwa hapo tunapomkosea, sijua kama kuna ambaye angesalimika katika adhabu hiyo. Na ndiyo maana mzaburi anasema, “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna MSAMAHA, ili Wewe uogopwe.” Zab 130:3-4. Kuogopwa kwa Mungu hapa hakumaanishi Mungu wetu ni katili na mwenye kutuburuza katika kufanya jambo. La hasha! Kuogopwa kwake Mungu ni pamoja na ukweli kwamba pamoja na makosa yetu kuwa mengi na yakutisha, bado anatupa nafasi ya kuyakiri na kupatanishwa naye. Kwa mantiki hii, huyu Mungu wetu niwakuogopwa kwa sisi kuwa na hofu naye.

Injili yetu leo inafafanua ulazima wa kutoa msamaha. Kipimo cha kusamehe ni kusamehe bila kipimo. “Yesu akamwambia, ‘Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.’” Mt 18:22. Ndugu yangu, lazima tufahamu msingi wa swali la Petro. Petro anamwambia Yesu, “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?” Mt 18:21. La kujiuliza ni kwamba, kwa nini Petro ajikite kwenye mara saba? Wapendwa, kadiri ya Maandiko Matakatifu, namba saba inamaanisha UKAMILIFU, YAKUTOSHA. Kwa Petro mara hizo saba za tosha na za pendeza machoni mwa Mungu.

Yesu katika hili hatengui ukamilifu na utoshelevu wa mtazamo huo alio kuwa nao Petro, bali anaupa maana zaidi na kuutimiliza, kwani Yeye mwenyewe anasema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17. Tunapotoa msamaha yatupasa kuzama ndani katika tendo la kusamehe na kusamehewa. Ni kuvivaa viatu vya yule aliyekusamehe na wakati huo huo kujirudi ndani kwa yule  uliyemkosea. Unaposamehe kumbuka pia nawe umesamehewa mara nyingi tu.

Ni mangapi unafanya kinyume na mapenzi ya Mungu, lakini yeye amekupa muda wa kujirudi? Je, angetoa adhabu za hapo kwa hapo umengebaki salama kweli? Kwa nini wasubiri kupigiwa chetezo ndio utoe msamaha? Kwa nini tunawazungusha watu kwa kutowasamehe wanapokiri makosa yao na katika unyonge wao? Kwa nini tunaweka vikwazo na sababu nyingi ili tuwasemehe watu waliotukosea hata kama weshakiri makosa yao? Jumuiya ya wakristo, na Kanisa kwa ujumla lisilotoa msamaha ni wazi jumuiya hiyo na Kanisa hilo halimwakilishi Yesu Kristo. Mkusanyiko huo utakakuwa mkusanyiko usio na mwelekeo na mbele yake kuna giza kubwa sana!

Katika Injili ya leo Yesu anatoa simulizi la kuvivaa viatu vya wale waliotusamehe na kujirudi ndani ya nafsi zetu kwa wale tuliowakosea. Hii ndiyo namna ya uzito na ulazima wa kusamehe. Mara nyingi Yesu ameonyesha hali hiyo, na hata umauti wake kwa ajili ya dhambi zetu. Yesu alipoletewa mbele yake mwanamke yule mzizi, aliyasema haya, baada ya kulitafakari tukio hile undani akiwa anaandika chini, “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe,” Yoh 8:7. Wote tunajua kilichofuata baada ya maneno haya ya Yesu.

Bwana wetu Yesu Kristo ni kielelezo sahihi cha Msamaha wa Mungu. Ndugu yangu, “Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Na nikatika “yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:14-15.

Ndugu yangu, msamaha ni Ukristo wetu na maisha yetu kama wafuasi wake Kristo. Msamaha ni tendo la Mungu mwenyewe na sababu ya wokovu wetu. Hakuna anayeishi kwa sababu yake mwenyewe, wala hakuna afaye kwa nafsi yake, Rum 14:7

Ndugu yangu, nani wewe usiye samehe?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yesu akamwambia, ‘Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini,’” Mt 18:22

Ee Yesu, nijalie Roho ya Msamaha na nifanye hivyo bila kujibakiza. Amina

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 3 YA KWARESMA

JUMATATU YA WIKI YA 3 YA KWARESMA

Somo: 2 Fal 5:1-15a
Zab:42:2, 3; 42:3, 4
Injili: Lk 4:24-30
Nukuu:

“Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa nyamba ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14

“Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,” Lk 4:24.

TAFAKARI: Unyenyekevu ni msingi wa Fadhila zote; Tujinyenyekeshe na Mungu atatenda.

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa pamoja tutafakari, “unyenyekevu ni msingi wa Fadhila zote; tujinyenyekeshe na Mungu atatenda.” Masomo yote mawili leo yanatuwasa kutafakari sana tendo hili la unyenyekevu na kujinyenyekesha. Bila shaka wote twafahamu vizuri habari za Jemadari Naamani, na uponyaji wake kupitia Nabii Elisha. Safari ya uponyaji wake haikuwa rahisi, kutokana na njia, na namna ya uponyaji ule ulivyokuwa uwe kwa namna Mungu alivyopenda.

Mara nyingi hatuyapati yale tuombayo, na hata uponyaji wa yale yatusumbuayo kutokana na mitazamo yetu kimaisha, na namna tutakavyo Mungu kufanya huruma na upendo wake. Mtume Yakobo anasema hivi, “hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Tunapokuwa mbele ya Mungu, ni jambo la msingi kujishusha na kujinyekesha kwani sote ni wahitaji na waja wa Mungu. Mungu utukweza tu pale tunapojinyenyekesha kwake na kuukubali ubinadamu wetu. Mungu daima anabaki kuwa Mungu. “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, na ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11. Mtoza ushuru katika sala lake hekaluni, kinyume cha Mfarisayo, sala yake ilisikika mbele ya Mungu kwa sababu alijishusha na kusema kwa unyenyekevu na kwa uchache wa maneno kabisa, “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13. Kwa tendo hili la unyenyekevu la mtoza  ushuru, Yesu anasema, “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; (Mfarisayo) kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:14

Jemadari Naamani anapata uponyaji wa ukoma wake baada tu ya kujishusha na kufanya kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ndugu yangu, Mungu ana njia mbalimbali za kufikishia ujumbe wake kwetu kadiri ya hitaji letu, na kwa kupitia jambo hilo la uponya huo liwe somo la maisha. Naamani anashindwa kupokea njia ya uponyaji ule, yaani, kujichovya mara saba katika mto Jordani, kwa kujitazama historia yake, na ufahamu wake. Mpendwa, “Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mipaka,” Zab 147:5. Hatuwezi kumpangia Mungu namna ya kufanya hata kama tukiwa na nia njema afanye yale tumwombayo na tunayotamani. Hata Yesu mwenyewe, alimwachia Baba yake-Mungu atende kadiri ya mapenzi yake. “Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe,” Mt 26:39.

Naamani Jemadari, anapojinyenyekeza na kumwachia Mungu atende kadiri ya neno lake kupitia mtu wa Mungu Nabii Elisha, Mungu anatenda mara moja. “Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi,” 2Fal 5:14. Kujinyenyekesha ni kukiri makuu ya Mungu kabla na baada anapotenda mema yake kwako. Uponyaji wa Naamani Jemadari unaibua hisia za uchaji na utambuzi wa Mungu huyu wa Ajabu, na kusema, "Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli,” 2Fal 5:15.

Ndugu yangu, tunachojifunza katika maisha yetu ya sala na unyenyekevu ni kwamba tunapokuwa mbele ya Mungu yatupasa kujua kwamba sisi ni viumbe tu, na wahitaji na waja wake Mungu. Mungu haitaji kujua mazuri yetu kwa sababu hayatampunguzia wema, upendo na uzuri wake. Mungu pia haitaji historia ya yale tuyafanyayo kama alivyofanya Mfarisayo, bali tusiache kutenda mema kwani Yeye aliye mema yote na uzuri wote ataonekana katika matendo hayo mema, hasa tunapoyatenda kwa wale aliowaumba kwa sura na mfano wake.

Utendaji wetu uwe kama wa watoto wachanga. Watoto wachanga ndiyo hufunuliwa mambo ya Mungu kutokana na kujiaminisha pasipo shaka kwa wazazi wao. Katika hili Yesu anasema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga,” Mt 11:25. Utendaji huu kama watoto ndio unaoturithisha ufalme wa Mungu.  “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 19:14.

Mwisho wa siku ndugu yangu, tutahukumiwa kwa upendo wetu. Kwa hiyo kwa yale yote tufanyayo na tujihesabie tu kuwa tumefanya yale yampendezayo Mungu. Ndugu yangu, Bwana wetu Yesu Krito anasema, “vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Hatuna chochote za kujivunia mbele ya Mungu zaidi ya kujinyeyekesha. Mafanikio yetu ni moja ya uzuri wake Mungu. Mapungufu yetu ni sababu ya ubinadamu wetu. Mtume Paulo anasema, “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14.

Katika jambo hili ndugu yangu, yatupasa kujua kwa uhakika kwamba Yesu Kristo ni kielelezo cha UNYENYEKEVU. Kifo cha msalaba na cha aibu ni kwa sababu yangu na wewe. Basi, tujivunie tu Msalaba kwani kwayo kuna utukufu. Vingine vyote ni vya kupita tu. Mtume Paulo anatuambia makusudi ya Yesu kufanya hayo yote ni kwamba, “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8. Je, ndugu yangu, una cho chote cha kujivunia na kutojinyenyekesha kwa Mungu?

Injili yetu ya leo tunaona jinsi Yesu anavyohukumiwa kwa kujinyenyekeza. Mara nyingi tunawahukumu watu ndivyo sivyo kutokana na kujua historia zao, maeneo ya kijeografia walikotoka, historia za wazazi wao, mazingira ya makuzi yao, marafiki walioishi nao, na hata mtazamo wao kimaisha. Hili ni kosa kubwa sana kufanya. Hakuna aliyeko hapa duniani kwa bahati mbaya, au kuzaliwa kwa bahati mbaya. Sisi tu malengo na makusudi ya Mungu. Mungu anampango na kila mmoja wetu.

Baada ya Yesu kuwaambia ukweli Waandishi na Mafarisayo kwa kutokuamini kwao, hawapokei ujumbe ule wa ukweli na kubadilika, bali wanatafuta njia ya kumwangamiza. Katika hili Yesu anatujaza ujari kwa kusema, “Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,” Lk 4:24. Maana yake nini? Ukweli ni kwamba, tunaposimama katika kweli, na kuishi kweli hiyo, ni vita twatangaza kwa wale wasioipenda kweli hiyo. Kwa upande wa Imani ni vita, si tu ya nafsi, bali roho pia. Roho ambazo hazimwelekei muumba wake zitakuwa kinyume na yote tusemayo na kuyaishi. Kuishi Ukristo na kumkiri Kristo leo ni vita kubwa ya kiroho. Tulizoea kusikia hadithi za Mashahidi wa Imani karne na nyakati za nyuma, lakini leo ni nafasi na wakati wetu kuwa mashahidi wa Kristo. Kuna kila dalili na sababu za kuutoa ushuhuda huo.

Tunachopaswa kuishi si maisha ya ushindani wa hoja katika majukwaa, bali zaidi ni kuishi na kutoa ushuhuda wa ukimya wa maisha ya kweli ya ukristo wetu. Jambo hili ni muhimu sana, kwani katika utulivu Mungu yupo na kuonekana. “Na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu,” 1Fal 19:12. Huu ni wakati wa mitetemo ya Imani. Nasi tusienende kadiri ya mitetemo hiyo. Tuitafsiri hiyo mitetemo nako tutakutana na Mungu katika utulivu.

Ndugu yangu, Mungu wetu hutenda makuu katika unyenyekevu wetu. Kujinyenyekeza kwetu huku na kwa tendo hilo, kuna faida kubwa. Faida hii siyo kuponywa tu kwa yale yanayotusumbua, bali pia kuwa karibu naye na kujenga mahusiano mazuri na Mungu. Tujinyenyekeshe daima!

Tumsifu Yesu Kristo!

Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu,” Mit 15:33
Ee Yesu tujalie fadhila ya unyenyekevu.

viernes, 26 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 3 YA KWARESMA MWAKA-C

JUMAPILI YA 3 YA KWARESMA YA MWAKA-C
Somo I: Kut 3:1-8, 13-15
Zab: 103:1-4, 3-4, 6-7, 8, 11
Somo II: 1Kor 10:1-6, 10-12
Injili: Lk 13:1-9
Nukuu:
Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea,” Kut 3:2

Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut 3:5 

Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu,” Kut 3:6

Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao,” Kut 3:7

Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; MIMI NIKO amenituma kwenu,” Kut 3:14

wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo,” 1Kor 10:4

Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani,” 1Kor 10:5

Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani,” 1Kor 10:6 

Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke,” 1Kor 10:12 

Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao,” Lk 13:1 

Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?” Lk 13:2 

Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?” Lk 13:4

Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:5

Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate,” Lk 13:8-9 

TAFAKARI: “Vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tatu ya Kwaresma ya Mwaka ‘C’ wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee tutafakari kwa undani maneno haya ya Mungu, “vua viatu vyako miguuni mwake; maana mahali hapo unaposimama ni Nchi Takatifu.” 

Kwanza kabisa, maneno haya ya Mungu ni wito maalum anaopewa Musa kwa kazi maalumu, yaani kuwatoa wana wa Israeli utumwani Misri. Ni kieleleza cha namna ya kuwajibika na kuheshimu wajibu huo kama tendo Takatifu. Hivyo uwepo wa Mungu unajidhihirisha kwa kijinga cha moto chenye kuwaka bila kuteketea. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea,” Kut 3:2

Katika historia ya wokovu wa mwanadamu, na kwa mapenzi yake Mungu mwenyewe, aliliteua Taifa la wana wa Israeli kuwa kielelezo cha kusudi lake, uwepo wake, na ushirika wake. Safari hiyo haikuwa rahisi kwani pamoja na maridhiano kati ya Mungu na Taifa hili kwa njia ya maagano mbalimbali, wakati mwingine kulikuwa na hali ya uasi kwa upande wa mwanadamu na kupelekea kwenda kinyume cha mpango mzima wa Mungu kuelekea ukombozi wa kweli. Hata hivyo Mungu alibaki kuwa mwaminifu nyakati zote, na hakuacha kuwa Huruma, Upendo, na Msamaha wa watu wake. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima,” Isa 49:15-16.  Haki, Huruma, Upendo, na Msamaha ndiyo asili ya Mungu na ndiye Mungu ambaye kwavyo, yaani asili yake haina kipimo. Ni kwa huruma yake Mungu anaona mateso ya watu wake huko Misri. Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao,” Kut 3:7. Wewe na mimi tuliopewa dhamana ya uongozi na Mungu kwa kupitia watu wake, yatupasa kuutazama wajibu huo wa pekee tukitumika kwa Sifa na utukufu wa Mungu kwa ajili hiyo tu.

Pili, maneno haya mazito ya Mungu yanatuingiza katika badiliko la ndani yenye kumpa mtu mtazamo mpya kwa kile atarajiacho kukifanya. Mtazamo huu mpya wa kutenda si ule tena wa mazoea, bali enenda yako iwe katika mtazamo wa Mungu, yaani mtazamo wenye kusukumwa na HOFU ya Mungu mwenyewe. Mtu asiye na hofu ya Mungu, na hasa aliye na madaraka ni hatari sana katika matendo yake. Hivyo katika maana hii kama kiongozi aliye kwa ajili ya watu na Mungu, kuvivua viatu ni kuyashinda matendo ya mwili na kushikamana na tunda la roho. Na  “…tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria” Gal 5:22-23. Matendo ya mwili yasiyomtia mtu hofu ya Mungu ni haya; “…uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Yeyote mwenye kupokea dhamana ya uongozi na aliyetayari kutumika kwa ajili ya watu na kwa sababu ya Mungu ni vyema akajipima vizuri katika tendo hilo la kujivua viatu vyake miguuni mwake. 

Mtazamo huu wa kujipima unatuingiza katika tendo la kiroho na la mabadiliko, yaani, toba ya kweli. Haya ndiyo ayasemayo Yesu katika Injili, yaani TOBA ya kweli na kwa kutokufanya hivyo, basi yale tuyashangaayo kutokea kwa wengine basi nasi yapo mbioni. Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:5. Toba ya kweli ikulenge wewe binafsi katika tenda yako. Usipoteze muda mwingi kuyatazama makosa au mabaya ya wengine au yaliyowatokea kwa wengine na kujisahau kufanya mabadililiko hilo ndani mwako. Hivyo Yesu anatoa angalizo kwa kusema, “Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?” Lk 13:2, 4. Mimi na wewe yatupasa kuwa na utayari wa kupokea huruma ya Mungu kama alivyofanya Mtoza Ushuru. Na tazama, Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi,” Lk 18:13.  Hali na utayari wa Mtoza Ushuru wa kufanya toba ya kweli na kuipokea huruma ya Mungu ni kinyume kabisa na yule Mfarisayo aliyejihesabia haki. Naye (Mfarisayo) alijiinua na kusali hivi, Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru,” Lk 18:11. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, Mungu haitaji orodha ya wema na uzuri wako. Mimi na wewe tunapaswa wema na hiyo ndiyo sifa ya  wana wa Mungu. Na katika wema na uzuri huu hatuongezi au kupunguza wema na uzuri wa Mungu. Ila kwa kutenda mema na kuwa wema tunaudhihirisha Utukufu wa Mungu pale tulipo. Na hii ndiyo maana ya Maneno haya ya Yesu, Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:37, 48. Hivyo yale yote uyafanyayo kwa ajili ya watu na Mungu, yalenge katika utakatifu wako. Bila utakatifu kumwona Mungu ni ndoto isiyowezekana.

Tatu, maneno haya mazito ya Mungu, “Vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni Nchi Takatifu,” yanatukumbusha dhana na dhamana ya uongozi ambao kwa hakika ni mpango wa Mungu kupitia watu wake, na kwa ajili Mungu. Uongozi ni DHAMANA. Dhamana hii ya uongozi inatukumbusha Utakatifu wa kile uwajibikacho kama Kiongozi na Utakatifu wa wale unaowahudumia au kuwaongoza. Viongozi wengi leo wamesahau wajibu na kweli hii mara wapatapo madaraka. Viongozi hawa ni wale wenye hujigeuza na kuwa miungu watu kwa yale wayasemayo na kuyaamuru kwa umma uliowaweka madarakani. Mtume Paulo anatoa angalizo la viongozi wa mtindo huo na kusema, anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke,” 1Kor 10:12. Kiongozi yeyote aliye katika ngazi yoyote ile na taasisi yoyote ile, elewa kwamba pale ulipo katika kutenda kwenye maana ya kutumika, ni sawa na kusimama katika Nchi TAKATIFU kama alivyoambiwa Musa.

Historia ni mwalimu mzuri sana. Vitabu Vitakatifu na hata historia ya mataifa mbalimbali katika ulimwengu huu, vimeonyesha dhairi na pasipo shaka miisho ya viongozi wale ambao hawakuwa na hofu ya Mungu, na kujijeuza wao kuwa miungu watu. Mungu anasema hivi juu ya viongozi wenye kujifanya miungu watu, “nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali,” Isa 13:11b. Mungu kamwe hapendezwa na viongozi wenye kiburi na majivuno kwa sababu hawamwakilishi Mungu zaidi ya nafsi zao. Hivyo Mtume Paulo anatoa angalizo, na kusema, …wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani,” 1Kor 10:5. Wapendwa wana wa Mungu, pona yako na yangu ni kusimama katika kweli na haki, na ninapodondoka nifanya toba ya kweli kwa kuitazama neema na huruma yangu kwangu ilivyo kubwa kuliko dhambi zangu.

Mpendwa wana wa Mungu, tamani kila siku kutenda mema na lililo haki na kweli. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani,” 1Kor 10:6. Kila siku Mungu anakupa nafasi ya kuwa mwema kwa sababu amekuchagua yeye ili uzae matuma mema na yenye kudumu, Yoh 15:16. Yawezekana kwa makusudi kabisa hujayazaa matunda hayo mema licha ya fursa nzuri uliyonayo. Kipindi hiki cha Kwarema kiwe changamoto kubwa kujirudi na kumrudia Mungu. Na ushauri wa mwisho ni huu: Bwana, uuache (mtu huo, mimi, wewe) mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate,” Lk 13:8-9. Amina. 

Wapendwa katika Kristo, bila shaka sote tunamfahamu Jogoo. Jogoo hufikiri bila kuwika mapema asubuhi hakuna mapambazuko. Hivyo bila kuwika kwake siku haiwezi kuanza. Hii ndiyo falsafa ya Jogoo.

Siku moja mapema asubuhi kukiwa bado na mawingu mengi angani, Jogoo alitoka na kujilaza chali chini ya mti akiwa na lengo la kuyazuia mawingu yasidongoke. Akiwa katika mkao huo huku miguu yake akiielekeza juu na akiwa amezikunjua mbawa zake, katawi kidogo cha ule mti kilikwanyuka na kushuka kwa kasi. Jogoo yule kuona vile aliruka huku akiwika kwa hofu.

Baada ya dakika chache Jogoo yule alijiuliza, “hili tawi limetoka ubali wa mita chache sana na limekuwa tishio kubwa la uhai wangu. Je, nitaweza kweli kuyastahimili mawingu yale yaonekanayo kuwa mbali? Kwa mtazamo huu, ni mimi kweli ninayeyaamza mapambazuko?”

Wapendwa wana wa Mungu Jogoo yupo kwenye mchakato wa toba ya kweli. Je wewe na mimi tuliokirimiwa utashi na Mungu tunasubiri nini?

Tumsifu Yesu Kristo!

Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo,” Lk 13:5


Ee Yesu, nikumbushe mara zote kuwa uongozi ni dhamana na kielelezo chake ni kutumia kwa wote kwa hofu yako, nikitambua Utakatifu wa nafasi hiyo na Utakatifu wa wale ninaowaongoza. Amina

jueves, 25 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 2 YA KWARESMA

JUMAMOSI WIKI YA 2 YA KWARESMA

Somo: Mik 7:14-15; 18-20
Zab: 103:1-2, 3-4, 9-10, 11-12
Injili: Lk 15:1-3; 11-32
Nukuu:
“Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18

“Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19

TAFAKARI: “Toba ya kweli; Upendo na Msamaha wa Mungu”

Wapendwa wana wana Mungu, kwa pamoja tutafakari kwa undani “toba ya kweli; Upendo na Msamaha wa Mungu.” Somo la kwanza linatuelezea uhalisia wa Mungu. Mungu kwa asili ni Upendo, Huruma, na Msamaha. Ni Mungu anayetutakia mema muda wote sisi viumbe na wana wake. Ni Mungu anayejifunua kwetu kwa njia mbali mbali, ikiwa ni kwa njia ya  historia na vile alivyoviumba. Ni Mungu ambaye yupo na alikuwepo nyakati zote hata kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu. Tulikuwa daima ndani ya mawazo yake.

 Kwa upande wetu,  tuna kazi moja tu, yaani kumtafuta kwa maana anapatika. Nabii Isaya anatuambia hivi, “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu baribu; Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.” Isa 55:6-7.

Ndugu yangu, kumwasi Mungu ni tendo ambalo lipo chini ya uwezo wetu. Kumrudia Mungu ni tendo la toba na kufanya maamuzi sahihi na ya msingi. Tunapofanya maamuzi haya ni wazi kabisa kwamba yatupasa kuachilia mengi ambayo kwayo yalitupa furaha na hata kujulikana na kujikweza. Ila tukitambua umuhimu wa umilele wa maisha yetu, hatuna budi kuachilia yote haya ambayo ni ya kupita na ya muda mfupi.

Tunapofanya toba ya kweli na kumrudia Mungu, hutupokea kama tulivyo. Mungu katika mapokezi haya hatazamani historia yetu. Mungu huanza mradi mpya nasi na kutufanya wapya tena katika yale mazuri anayotufikiria. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11. Ndugu yangu, kwa nini hubadiliki? Waitaji malaika washuke na kukuambia jambo hili? Kwa nini unakuwa kero kwa ndugu na jirani zako? Kwa nini unakuwa kero kwa wanajumuiya zako na viongozi wako? Je, unapenda kuishi hivyo hadi lini?

Injili yetu ya leo inatupa kisa na simulizi la mwana mpotevu. Wahusika wakuu katika kisa hiki ni Baba mzazi, Mwana mpotevu, na Kaka ya mwana mpotevu. Wengine ni watumishi au watumwa wa Baba mzazi wa Mwana mpotevu, na marafiki wa mwana mpotevu. Mwana mpotevu, tena aliye mdogo katika familia hii, anafanya kitu ambacho si cha kawaida katika jamii na hasa mila na desturi kama zilivyokuwa. Kitendo cha kuomba urithi au sehemu ya mali yake kabla ya kifo cha baba yake, kulimaanisha kumtakia baba yake mabaya. Ni kutokumtambua baba yake. Ni kumchukulia baba yake kama marehemu.

Kwa upande wa baba yake, na kutokana na upendo aliokuwa nao kwa wana wake na familia, anakubali aibu hiyo, na kufanya kadiri ya matakwa ya mwanaye. Baba anampa sehemu ya urithi wake. Yaliyompata kijana huyu wote tunafahamu simulizi hili. Ndugu yangu, kutenda makosa ni hali yetu sote wanadamu. Ila tofauti ipo hapa; unapotambua umefanya kosa na kuchukua hatua kwa uliyoyafanya ndiko kunapoturejeshea hadhi na heshima yetu tena. Mwana mpotevu analiona kosa lake na anakiri kwa matendo na maneno, “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19. Ndugu yangu, haya ndiyo majuto ya kweli. Tunachoangalia si aibu tutakayopata, bali huruma, neema,  na stahili tunayoyapata kwa kufanya toba ya kweli.

Ndugu yangu, unapodondoka kwa sababu ya dhambi, usione aibu kuamka na kuomba msamaha kwa muumba wetu. Yeye Mungu anasema, “mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.” Ufu 1:8. Je, kuna mwingine wa  kumkimbilia zaidi ya Mungu wetu? Mungu aliye Upendo hana mipaka wala masharti ya pekee tunapomrudia. Mungu anasema, “nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,” Mit 8:17.

Upendo wa Baba hauna mfano. Katika simulizi hili la mwana mpotevu, Baba huyu anapomwona mtoto wake, hapendi na wala haitaji kujua historia ya yale maovu aliyofanya. Furaha yake ni kumwona mwanaye kama alivyo, na anajua kurudi kwake ni toba ya kweli. Anachofanya Baba ni kumrudishia stahili yake kama mwana na mmoja wa familia. Ni mumwesabia haki tena kama mwana familia. Lakini jambo la kushangaza ni kwamba tendo hili la Baba, linakuwa sononeko la Kaka ya mwana mpotevu. Haoni maana ya furaha hii na sababu ya kuwa hai mdogo wake. Ndugu yangu, katika safari ya wokovu, tusipende kujitazama wenyewe. Wokovu ni kwa wote na nifuraha ya Mungu. Katika mfano huu, Yesu anawakemea Waisraeli na hasa Mafarisayo ambao wanahuzunika kwa yale anayofanya Yesu ambao ndio upendo wa Mungu Baba.

Yatupasa mimi na wewe kutiana moyo na kufurahia pale wenzetu wanapomwongokea Mungu na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Mara nyingi hatuachi kuwasema vibaya wale wanaojitahidi kuishi njia impendezayo Mungu. Tunawapachika majina mengi, na kuwakatisha tamaa kabisa. Kwa upande wetu, mwenzetu anapojitahidi kuishi vizuri, basi iwe changamoto ya sisi kufanya vizuri.

Ndugu yangu, wakati ndiyo sasa! Kaa na tafakari namna utendavyo. Je, unafanya kadiri ya mapenzi ya Mungu? Urithi wako ni fursa uliyonayo sasa katika utendaji. Je, unatumia fursa hiyo vizuri kwa Sifa na Utukufu wa Mungu? Je, baada ya kuishi ovyo kwa muda wote huo, upo tayari kufanya toba ya kweli na kuacha njia hiyo mbaya? Basi nielewe nafasi niliyo nayo ni leo na sasa tu. Ni vyema nikachukua hatua sasa na kuutafuta uso wa Bwana. “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3

Tumsifu Yesu Kristu!

“Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako,” Lk 15:18-19


Ee Yesu, niongoze katika kweli yako. Amina