IJUMAA WIKI YA 24 YA MWAKA-B
18/9/2015
Somo: 1Tim 6:2-12
Zab: 48:6-10, 17-20
Injili: Lk 8:1-3
Nukuu:
“Mtu awaye yote
akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu
Yesu Kristo, wala mafundisho yapatanayo na utauwa, amejivuna,” ITim 6:3-4b
“Kwa maana hatukuja na
kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu,” 1Tim 6:7
“Lakini
hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi
zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na
uharibifu,” 1Tim 6:9
“Maana shina moja la
mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo
wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10
“Bali wewe, mtu wa
Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole,”
1Tim 6:11
“na wanawake kadha wa
kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; na wengine wengi,
waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao,” Lk 8:2a, 3b
TAFAKARI: “Wewe mtu wa Mungu,
ukafuate haki, utauwa, Imani, upendo, saburi, na upole; ndiyo uzima wa milele
ulioitiwa.”
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, ni ukweli usiyotia shaka kwamba maisha
ya kila mtu yanaongozwa na kitu fulani. Kwa mtazamo huu haijalishi wewe ni
Mkleri, Mtawa au Mlei. Kila mmoja kadri ya wito wake atafakari haya kwa undani.
Ndugu msafiri mwenzangu, tukirejea kidogo na hasa katika kamusi nyingi
hufafanua neno "ongoza" (drive) kama "kuongoza, kutawala,
kuelekeza." Kwa hiyo, unapokuwa kwa mfano unaongoza gari, unachokifanya ni
kuongoza, kutawala na kuelekeza kwa wakati huo. Je, ni nguvu gani inayoongoza
maisha yako? Sasa hivi unaweza kuongozwa na tatizo, msukumo fulani, au tarehe
ya mwisho kwa kitu fulani. Unaweza kuongozwa na kumbukumbu ya jambo fulani
linaloumiza, hofu mbaya, au imani ya ndani. Kuna mamia ya hali mbalimbali, mambo
muhimu, na hisia ambavyo vyaweza kukuongoza. Hata hivyo, kuna mambo matano
ambayo ni ya kawaida kwa wengi.
1. Watu tulio wengi huongozwa na hatia.
Watu hawa hutumia muda wa maisha yao yote wakiepuka lawama
na kuficha aibu. Watu wanaoongozwa na hatia wanaonewa sana na kumbukumbu.
Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya usoni.Wanajiadhibu bila kujua
kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda dhambi, hatia yake ilimtenga na
Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa
mtoro na mtu asiye na kikao duniani," Mwa 4:12. Hali hii inawaeleza jinsi
watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga katika maisha bila lengo. Mfano
mzuri angalia katika vyama vyetu vya kitume. Wapo walio wengi huama chama
kimoja cha kitume kwenda kingine na mwisho huishia katika nyumba za sala.
Nyumba za sala hapa ninamaanisha vijikanisa vinavyojiibua na kujiinua kwa
wachungaji wao kuwa manabii.
Ndugu yangu, sisi ni matokeo ya muda wetu uliopita lakini
hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo. Kusudi la Mungu halifungwi na muda wako
uliopita. Ona! Alimbadilisha muuaji Musa na kuwa kiongozi mzuri; akambadilisha
Gidioni aliyekuwa mwoga akawa shujaa na hodari; anaweza kufanya mambo ya ajabu
na maisha yako yaliyobaki. Tazama pia maisha ya Mt. Augustino
wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake.
Mungu ni mtaalam wa
kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa
yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha
kubwa wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na
Mungu amefuta mashtaka yao."
2. Watu tulio wengi wanaongozwa na chuki na hasira.
Ndugu zangu, wapo wanaoshikilia maumivu (machungu)
bila kuyaacha. Badala ya kutoka katika maumivu kwa kusamehe, wanaendelea
kuyakumbuka katika mawazo yao tena na tena. Baadhi ya watu wanaongozwa na chuki
kutunza ndani uchungu wao, na wengine huwalipukia watu wengine. Hali zote hizi
si nzuri na hazisaidii maishani. Chuki mara nyingi huleta maumivu kwako kuliko
yule unayemchukia. Mtu aliyekukosea anaweza kuwa amesahau lile kosa na
anaendelea na maisha yake vizuri, wewe unaendelea kuumia na kuhangaika na
yaliyopita.
Sikiliza ndugu yangu: Wale waliokuumiza wakati
uliopita hawawezi kuendelea kufanya hivyo sasa "isipokuwa" kama
utaendelea kutunza uchungu. Yaliyopita yamepita! Hakuna kitakachoyabadilisha.
Unajiumiza tu na uchungu wako. Kwa ajili yako, jifunze kutokana na hilo na
kisha achana nalo. Maandiko matakatifu yanatukumbusha kuwa, "kwani hasira
humwua mtu mpumbavu, nao wivu humwua mjinga." Ayu 5:2. Kuwa na hofu kiasi cha kufa kwa sababu ya
uchungu ni upumbavu, ni kitu kipumbavu kukifanya. Ndugu, kwa nini wajifungia
katika tanuru hili?
3. Watu walio wengi wanaongozwa na woga.
Ndugu, woga hapa unaweza kutokana na jambo baya sana
lililokupata au lililowapata, matarajio yasiyotekelezeka, kukulia katika jamaa
isiyo na uhuru, au hata maumbile ya asili. Bila kujua sababu, watu wanaongozwa
na woga mara nyingi hupitwa na nafasi kubwa kwa sababu wanaogopa kuchukua
hatua. Badala yake wanajitahidi kuwa salama, wakiepuka hasara na hivyo hujaribu
kulinda hadhi yao. Woga ni kifungo ambacho mtu hujifunga mwenyewe na chaweza
kukuzuia kuwa mtu yule ambaye Mungu anapenda uwe.
Unatakiwa kutoka humo
kwa silaha ya IMANI na UPENDO. "Katika pendo hamna hofu; lakini pendo
lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu, na mwenye hofu
hakukamilishwa katika pendo." 1Yoh 4:18. Kwa maneno mengine, upendo halisi
huiondoa hofu kwa kuwa hofu hulemaza, maisha ya hofu-hofu ni ya kifo, hofu ya
hukumu- ni maisha ambayo hayajakamilika katika upendo.
4.
Watu wengi wanaongozwa na mali
Wapendwa tupo pamoja?
Tamaa yao ya kupata vitu linakuwa ndilo lengo la maisha yao yote. Jambo hili haijalishi
upo utawani au kwenye maisha ya ndoa. Msukumo huu wa kutaka zaidi kila siku una
misingi yake katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha
zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo yote matatu
si ya kweli. “Lakini hao watakao kuwa na mali
huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye
kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu,” 1Tim 6:9. Mali
huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na sababu kubwa ndugu yangu, vitu
havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka vipya, vikubwa, na bora zaidi.
Kuna imani pia kwamba
nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na umuhimu unaotegemea
ulivyo navyo ndugu yangu ni vitu viwili tofauti. “Maana
shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali
wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim
6:10. Thamani yako haitegemei
mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu maishani mwako si vitu! Imani ya watu
wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo nyingi kutanipa usalama. Huwezi! Tulio
utawani hatuchoki kuwa na tumiradi binafsi twa siri twingiiii. Usicheke ndiyo
ukweli kwa baadhi yetu. Mambo yanapokwenda vibaya kwenye huto tumiradi tupresha
twa kupanda na kushuka hatukomi.
Ndugu yangu, utajiri
unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza
kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na
Mungu. “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka
na kitu,” 1Tim 6:7. Mt.
Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na
vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo
uchache na huo wingi.
5. Watu wengi wanaongozwa na kutaka sifa
Ndugu yangu, wakati mwingine watu hawa wanaruhusu matarajio
ya wazazi, waume, au wake, watoto, waalimu au rafiki zao kutawala maisha yao.
Watu wazima bado wanajaribu kupata sifa kwa wazazi wao ambao hawajafurahi
kamwe. Wengine wanasukumwa na vikundi vya marafiki, wanahofu wenzao
watawafikiriaje. Kwa bahati mbaya, wale wafuatao kundi au maoni ya mtu binafsi
hupotea ndani yake. Ndugu yangu, kwa nini kujifungia katika gereza hili la
fikra na maoni? “Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala
hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo, wala mafundisho
yapatanayo na utauwa, amejivuna,”
ITim 6:3-4b. Sifa yetu kubwa ni kulitenda lile alilofundisha Bwana wetu Yesu
Kristo kwani ndilo lenye uzima wa milele.
Ndugu yangu, sijui funguo zote za mafanikio, lakini
ufunguo mmoja wa kushindwa ni kujaribu kumpendeza kila mtu. Kutawaliwa na maoni
ya watu wengine ni njia wazi ya kukosa makusudi ya Mungu katika maisha yako.
Bwana wetu Yesu Kristo anatupa angalisho kwa jambo hili, "hakuna mtu
awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu,
ama atashindana na huyu na kumdharau huyu: hamwezi kumtumikia Mungu na
mali." Mt 6:24.
Kuna nguvu nyingi zinazoweza kuongoza maisha yako
lakini zote mwisho wake ni mfu: kutotumia vipawa ulivyo navyo, mahangaiko ya
moyo, na maisha yasiyo ya utoshelevu. “Bali
wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo,
saburi, upole,” 1Tim 6:11. Kuishi katika mfumo huu ndiko kutakako kupa amani ya
kweli na utulivu wa ndani.
Ndugu yangu, kuishi maisha yanayoongozwa na malengo, ni
kutawaliwa, na kuelekezwa na makusudi ya Mungu. Hakuna kitu cha muhimu zaidi
kama kujua malengo ya Mungu kwa maisha yako, na hakuna mbadala kwa hilo-siyo
mafanikio, utajiri, kujulikana, au anasa. Bila malengo, maisha ni
mwendo usio na maana, shughuli bila mwelekeo, na matukio bila sababu. Bila
malengo, maisha ni kitu duni, kidogo sana, kisicho na umuhimu wowote.
Wapendwa wana wa Mungu,
Injili ya leo inatufundisha jambo la muhimu sana kuhusu maisha yetu ya kiroho
na mali tulizonazo. Ukweli ni kwamba, waliokwisha kupata neema, baraka na
uponyaji ni wale tu walijinyenyekesha kwa Kristo mwanakondoo wa Mungu, na
kumtumikia kwa mali zao. “Na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya
na magonjwa wakaponywa; na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao,”
Lk 8:2a, 3b. Je, kuna uhusiano wa namna gani kati ya maisha yako ya kiroho na
mali ulizokuwa nazo?
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU KWETU WATOSHA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario