ALHAMISI WIKI YA 24 YA MWAKA-B
17/9/2015
Somo: 1Tim 4:12-16
Zab: 110:7-10
Injili: Lk 7:36-50
Nukuu:
“Mtu awaye yote asiudharau
ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na
katika upendo na imani na usafi,” 1Tim 4:12
“Basi, yule Farisayo
aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii,
angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba
ni mwenye dhambi,” Lk 7:39
“Kwa ajili ya hayo
nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana;
lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo,” Lk 7:47
“Akamwambia yule
mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani,” Lk 7:50
TAFAKARI: “Sote twahitaji
upendo, huruma, na msamaha wa Mungu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. Kama
jambo hili lina ukweli katika maisha na asili yetu, basi yupo aliye mkuu kuliko
sisi na mweza wa yote. Huyu ndiye hakimu wa haki kwa sababu kutoka kweka
twauonja upendo, huruma na msamaha. Tumeuonja na tunauonja upendo huo, huruma
hiyo, na msamaha huo kwa kupitia neno aliyemwilishwa yaani mwanaye Yesu Kristo.
Hivyo, “hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa
ajili ya rafiki zake.” Yoh 15:13. Kuuthamini ukweli huu na kuuishi
kunatupelekea kuyatafakari mawaidha na wosia wa Mtume Paulo: “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao
waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi,” 1Tim
4:12. Haya yanawezekana pale tu tunapofundisha kweli hiyo, tunapoishi vipaji
vyetu ipasavyo, na mwisho tunapodumu katika hayo mawili daima. Ukweli wa haya yote
ni kwamba, “hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye
kwa nafsi yake,” Rum 14:7. Hivyo fundisho hili na tendo hili linatufunza
unyenyekevu.
Injili ya
leo tunamuona Yesu anaalikwa nyumbani kwa Mfarisayo mmoja ale chakula. Katika
tukio hilo; upendo, huruma, na msamaha wa Mungu unajidhihirisha. Upendo,
huruma, na msamaha wa Mungu hautokani na mila na desturi zetu wanadamu, bali ni
kweli iliyo ndani ya Mungu mwenyewe ambayo ina uhusiano wa karibu kabisa na wa
moja kwa moja na namna tulivyoumbwa, yaani, ‘kwa sura na mfano wake,’ Mwa 1:27.
Sheria zetu licha ya ukweli unaoufunua kadiri ya mazingira yetu na wakati
mwingine katika mapungufu yake, siyo sababu ya upendo, huruma, na msamaha wa
Mungu kwetu, “kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake
kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria,” Rum
3:20.
Yesu
anautambua udhaifu huu wa sheria za wanadamu, na hasa katika jamii yake ambayo
waliachana na torati na kufuata tafsiri ya torati na masimulizi yake, yaani,
TALMUD. “Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni
mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni
nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi,” Lk 7:39.
Jambo
la kushangaza zaidi wakati wa Yesu, Torati ile ambayo ndiyo ilikuwa mstakabali
wa Taifa la wana wa Mungu-Waisraeli, ilikwisha chakachuliwa vya kutosha na
hivyo Taifa hili lilikuwa linafuata Tafsiri yake tu kwa sehemu kubwa. Jambo
muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu Wayahudi na hasa mafarisayo na
waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha
ya dini na matendo yake kupitia masimulizi) iliyojulikana kwa ujumla kama
TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka
Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)
Kwa mantiki hiyo hapo
juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa
350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed)
katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na
waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga
jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati. Ni ukweli wa
Mungu uliopotoshwa.
Wapendwa wana wa Mungu,
Mungu wetu hana macho tuliyo nayo sisi ambayo yana kikomo na umbali fulani wa
kuona. Macho ya Mungu, au kwa namna nyingine muono wa Mungu uvuka hata uwezo
wetu wa kuona na matokeo yetu ya kufikiri. Hivyo Yesu anaurejesha uhai wa Mungu
kwa maisha ya kweli na sababu ya kuumbwa huyu mwanadamu. Hivyo kwa tukio hili
la mwanamke huyu mwenye dhambi nyumbani mwa Mfarisayo, Yesu anasema bila
kupepesa macho yake, “kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake
ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo
hupenda kidogo,” Lk 7:47. Licha ya udhaifu wake kama mwanadamu, mwanamke huyu
akuacha kuonja upendo wa Mungu na kurudisha upendo huo kwa Yesu kadiri ya uwezo
wake. Anafanya tendo hili kwa kumdondoshea
machozi miguu ya Yesu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, hakuacha
kumbusu sana miguu ya Yesu, na kumpaka miguu ya Yesu marhamu. Ni ukweli kwamba,
“hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipenda, Mungu hukaa ndani yetu,
na pendo lake limekamilika ndani yetu,” 1Yoh 4:12. Msukumo huu wa upendo
haumzuii Yesu kumwambia mwanamke huyu kuwa, “Imani yako imekuokoa, enenda zako
kwa amani,” Lk 7:50. Kila mmoja wetu anahesabiwa haki mbele za Mungu si kwa
kile alicho, bali ni upendo, huruma, na msamaha wake Mungu mwenyewe. “Maana ni nani
katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya roho ya binadamu iliyo
ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa
Mungu,” IKor 2:11.
Je, ndugu
yangu unalo la kumficha Mungu? Basi kama kweli tunataka kuponywa kama mwanamke
huyu yatupasa kujisalimisha kila siku mbele za Mungu. Tunafanya hivyo tukijua
kwamba, “wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi
utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu,” Ebr 4:13. Hapo vipi
ndugu yangu?
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU HATUNA CHA KUKUFICHA. TUNAOMBA HURUMA NA MSAMAHA WAKO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario