IJUMAA WIKI YA 23 YA MWAKA-B
11/9/2015
Somo: 1Tim 1:1-2, 12-14
Zab: 15:1-2, 5-8, 11
Injili: Lk 6:39-42
Nukuu:
“Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa
sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo
kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata
rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani,” 1 Tim
1:12-13
“Mnafiki
wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema
kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako,” Lk 6:42b
TAFAKARI: “Bado unayo nafasi
ya kujirudi kutoka ukengeufu wa Imana. Huko ndiko kuongoka kuliko kwa kweli.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kama wewe umebatizwa elewa kuwa unaishi ndani ya wokovu
aliotupatia Bwana wetu Yesu Kristo kwa kifo chake pale msalabani. Ni jambo la
kusikitisha sana kwamba tulio wengi hatuoni thamani ya wokovu huu tuliopewa
bure kwa upendo wa Mungu Baba kupitia mwanaye Yesu Kristo. Tendo hili kwetu ni
heshima kubwa sana, kwani tumenyanyuliwa katika udogo wetu na kuinuliwa palipo
juu kabisa alipo Kristo na Mungu wetu.
Ndugu
yangu, licha ya mastahili haya aliyopewa wanadamu, Mungu hakumuondolea
mwanadamu huyu uhuru wake wa kuamua kutenda yaliyo mazuri au mabaya. Uhuru tuliopewa
na mwenyezi Mungu ni changamoto kubwa sana katika kuiishi Imani yetu. Uhuru huu
mara nyingi unatutoa katika mstari wa kuyaishi yale yampendezayo Mungu. Ni kwa
kupitia uhuru huu pia tunaweza kuziacha njia zetu mbaya na kumrudia Mungu kwa
toba na majuto. Hivyo basi, kila siku ya maisha yetu tunaitwa katika wongofu wa
roho zetu. Siyo kuokoka, bali kuongoka kwani wokovu kesha tupatia Kristo.
Wokovu ambao ni uwezekano wa kufanywa wana wa Mungu kesha tupatia Kristo
mwenyewe kwa sadaka ya mateso na kifo chake pale msalabani. Hivyo yatupasa
kuziishi ahadi zetu za ubatizo muda wote wa maisha yetu hapa duniani.
Kukengeuka
kwetu na kunakotufanya kuwa nje ya Imani yetu kunatokana kwanza kabisa na
ujinga wetu, yaani kutokujua dhamani ya Imani yetu, na lengo lake katika safari
ile ielekeayo katika uzima wa milele. Mtume Paulo ni mmoja ya watu walioishi
vibaya na baada ya kujitambua, hasa pale alipojeuzwa na Kristo anayasema haya
kinabaugaba. “Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa
sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo
kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata
rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani,” 1 Tim
1:12-13. Tendo hili ndilo lijulikanalo kama KUONGOKA. Mt. Augustino ni mfano
mwingine wa wale walioacha njia zao mbaya na kuongoka. Tusomapo kitabu chake
cha Maungamo tunaona wazi tendo hili la kuongoka. Mt. Augustino ana fafanua kwa
undani alivyoutafuta ukweli sehemu mbalimbali na kusahau kuwa ukweli huo
alikuwa nao ndani yake. Alipoigusa neema ile ya wokovu wa Kristo ndani yake
yote yalifunuliwa na akawa mpya ndani na katika Kristo.
Pili,
kukengeuka kwetu katika Imani kunatokana na unafiki wetu. Kwa ufupi unafiki ni
kuujua ukweli ulivyo lakini kutokana na mazingira au mtazamo wa watu, mhusika
anaukwepa ukweli ule na kuishi kadiri na mazingira yale na mitazamo ya watu
wale ili kuwapendezesha au kuwafurahisha. Kwa upande mwingine ni kuishi kile
usicho na kukubali kuwa kivuli cha kitu ambacho sicho ulicho. Ili urudi katika
mstari ulioukwepa, yaani Imani ya kweli, itakupasa kuurudia ukweli kama ulivyo
na kwa kufanya hivyo utaweza kusonga mbele na kuwa nuru na mwanga kwa wengine.
Jambo hili Yesu Kristo analikemea kwa nguvu zote na bila kupepesa macho. Wenye
tabia kama hizi Yesu Kristo hana haya kutuambia hivi; “Mnafiki wewe, itoe
kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa
kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako,” Lk 6:42b. Yesu amewafananisha
watu wa mtindo huu kwa nyakati mbalimbali kama vipofu na makaburi yaliyopakwa
chokaa. Ole kwa waandishi na mafarisayo tunasoma vizuri habari hii kutoka
mwinjili Mathayo hasa ile sura ya 23 yote.
Ndugu
yangu, kama wewe leo una taaluma yoyote ile na ukashindwa kutoa huduma kadiri
ya taaluma yako kwa wale wanaohitaji huduma hiyo, jua kwamba tendo hilo ni
mwelekeo wa ukengeufu wa kile ulichosomea, na mwisho wa siku tendo hilo
litahathiri Imani yako kwa kiwango hicho hicho. Jambo hili likikutokea huwezi
kukwapa tuhuma na lawama za kuwa mnafiki, na huna tofauti na waandishi na
mafarisayo wa nyakati zile za Yesu. Basi kama mimi ni mwalimu wa dini,
mwanasheria, Bwana afya, mwalimu, Mwanasiasa, nk, ni wakati wa kujichunguza
vizuri.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE YESU aliyeTUtia nguvu kwa sababu ULITUona kuwa waAminifu,
UkaTUweka katika utumishi wakO USITUACHE TUKENGEUKE. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario