JUMATANO WIKI YA 24 YA MWAKA-B
16/9/2015
Somo: 1Tim 3:14-16
Zab: 110:1-6
Injili: Lk 7:31-35
Nukuu:
“Lakini nikikawia,
upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo kanisa
la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli,” 1Tim 3:15
“Mungu
alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na
malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa
juu katika utukufu,” 1Tim 3:16b
“Wamefanana na watoto
walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza;
tuliomboleza, wala hamkulia,” Lk 7:32
“Mwana wa Adamu
amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa
divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi,” Lk 7:34
TAFAKARI: “Usiache kutenda
Mema kwani ndicho tulichoitiwa kama wana wa Mungu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa njia ya tafakari iliyo hai twaweza kukutana na Mungu aliye
hai kadiri ya mazingira yetu, kazi zetu, na mtindo wa maisha tulioamua kuishi
kwa mapenzi ya Mungu mwenyewe. Twauona upendo wa Mungu katika uumbaji wake
ambayo ndiyo mazingira tunayoyaishi. Kila tuonacho kinafunua uzuri, upendo,
wema, na malengo la Mungu kwa mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake.
Hapana shaka yoyote kwamba Mungu kayafanya kama yalivyo kwa upendo kwa sababu
YEYE NI UPENDO.
Ndugu
yangu unayeambatana nami katika tafakari hii, ni kweli kabisa tunakutana na
upendo wa Mungu katika kazi zetu, uwe umeajiriwa au kujiajiri mwenyewe. Mahusiano
yetu na kile tufanyacho, wale tunaowahudumia, na matokea ya huduma yetu kwa
watu, ni tendo la upendo wa Mungu hasa pale lengo zima ya kuyafanya hayo yote
halina msukumo au uhusiano wa moja kwa
moja na ubinafsi wetu. Je, ni dhambi kupata faida kwa kile tufanyacho? La,
hasha! Faida yetu katika hili mara zote iwe kuwapata watu na siyo kuwapoteza.
Kuwapata watu liwe lengo msingi la kile tukifanyacho. Mtaji wetu mkubwa hasa
katika uinjilishaji ni watu. Mmisionari bila watu ni sawa na kupiga mashuti
pasipo goli. Je, nitawapataje watu? Nawapata watu kwanza kabisa kwa kuwajali
watu hao, kwa kuwahudumia ipasavyo, na mwisho kwa kuwasikiliza kuliko kweli,
upendo na haki. Msukumo wa tendo hili usijengwa katika dhana ya “kudhaniana
vibaya.” Ni vyema katika hili kuwe na vyombo rasmi vya mazungumzano. Vyombo
hivi viwe na fursa ya kutuleta pamoja na kujadiliana katika pendo, kweli, na
haki. Jambo hili likifanyika katika ukweli na uwazi huu hata kama nitapata
faida haitakuwa dhambi kwani ni matokea ya furaha ya wote.
Wapendwa
wana wa Mungu, uhai wa Kanisa leo lazima ujengwe katika mtazamo huo na misingi
hiyo niliyoieleza hapo juu. Huku ndiko kuenenda katika nyumba ya Mungu kuliko
hai, nguzo na msingi wa kweli wa Kanisa. Mtume Paulo hasiti kulisema jambo hili
kwa Timotheo, kwamba, “inawapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo kanisa
la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli,” 1Tim 3:15. Biashara kubwa
Kanisani ni kuuishi upendo wa Mungu aliye hai. Kama kuna mengine zaidi ya haya
basi ni mbwembwe tu. Upendo wa Mungu aliye hai unajidhihirisha katika mwili
wake, yaani Yesu Kristo, unajidhihirisha katika haki na roho, ulioonekana na
malaika zake, upasao kuhubiriwa kwa watu na ulimwengu wote, na mwisho ndio
utakao tupeleka katika utukufu wake mbinguni. Hii ndiyo kazi ya Kanisa kama
sakramenti ya wokovu wetu. Hivyo, “Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika
kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa,
Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu,” 1Tim 3:16b.
Kanisa kama wabatizwa na sakramenti ya wokovu, linachangamoto zake nyingi ili
kufikia malengo haya tajwa hapo juu. Changamoto kubwa ni ubinafsi wa wana
Kanisa wenyewe. Ni hatari sana tunapotanguliza nafsi zetu na matakwa yetu na kumwacha
Kristo aliye dira ya maisha yetu na Imani yetu.
Ubinafsi
huu unampa mshtuko mkubwa Bwana wetu Yesu Kristo na kujiuliza, afananishe na kitu gani kizazi hiki? Yesu
anatufananisa na kizazi kilichokufa gazi na chenye upofu wa kutokuona yaliyo
makuu ya Mungu kwa wengine, na badala yake kujiona chenyewe na mahitaji yake
binafsi. Na Yesu anasema, “wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema,
Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia,” Lk 7:32.
Ndugu yangu, usipotoka nje ya matamanio yako kimwili na kiroho, bado hujauonja pendo,
kweli, na haki ya Mungu. Badala yake utakuwa mtu wa majungu tu pasipo sababu ya
msingi kwa sababu mizania yako ya kweli itakuwa mwono wako mwenyewe. Ni vigumu
kwa hali hii kuona mema ya wenzako. Vile vile itakuwia vigumu kujirekebisha.
Ndiyo maana katika hili yote yale aliyoyafanya Yohane Mbatizaji walimwona kama
ana pepo hivi. Jicho la ubinafsi kamwe haliwezi kuona na kusadifu mema ya
mwingine. Sana sana ni kuyabomoya na kuyaharibu ya wengine ili wewe uonekana
hata kama ni chukizo kwa wale unaowafanyia hayo.
Yesu pia
anapatwa na changamoto hiyo aliyoipata Yohane Mbatizaji. Wayahudi waliojawa jicho
la ubinafsi hawayaoni mema na mazuri ya Yesu. Badala yake ni shutuma na
upotoshaji wa wema na upendo wa Mungu. Yesu analitambua hili na kusema, “Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema,
Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye
dhambi,” Lk 7:34. Je, hali hii inasema nini juu ya maisha na wito wako?
Kadiri ya
mang’amuzi ya maisha ni kweli isiyopingika kwamba ukitenda wema lazima utasemwa
vibaya, ukitenda vibaya na kuwa mbaya kwa kwetu vile vile utasemwa vibaya,
usipotenda chochote utasema vibaya. Hivyo katika hali hii Kristo anatuambia
tusiache kutenda mema kwa sababu ndicho tulichoitiwa na Mungu. “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji
Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika
kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu
lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele.
Amina,” Ebr 13:20-21.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU TUFANYE MWANGA NA NURU PALE TULIPO KWA MATENDO YETU MEMA. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario