JUMANNE WIKI YA 25 YA MWAKA-B
22/9/2015
Somo: Ezr 6:7-8, 12,
14-20
Zab: 121:1-5
Injili: Lk 8:19-21
Nukuu:
“Iacheni kazi hii ya nyumba ya Mungu, msiizuie; waacheni
liwali wa Wayahudi, na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu mahali
pake,” Ezr 6:7
“Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na
aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno
hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu,” Ezr 6:12
“Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa msaada wa
kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga, wakaimaliza kazi
yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta
mfalme wa Uajemi,” Ezr 6:14
“Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi
katika zamu zao, kwa ajili ya huduma ya Mungu, iliyokuwako Yerusalemu; vile
vile kama vilivyoandikwa katika chuo cha Musa,” Ezr 6:18
“Kwa maana makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote
pamoja; wote walikuwa hali ya tohara; wakachinja Pasaka kwa ajili ya wana wote
wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao,”
Ezr 6:20
“Akawajibu akasema,
Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya,” Lk
8:21
TAFAKARI: “Wale wote wenye hofu ya
Mungu hubarikiwa katika mambo yao.”
Wapendwa wana wa Mungu,
mwanadamu ye yote asiyekuwa na hofu ya Mungu ni hatari sana kwake yeye
mwenyewe, kwa wenzake, na mazingira yake. Mwenye hofu ya Mungu hutambua
mafanikio yake na madhaifu yake. Mizania hii umwongoza katika kweli na haki.
Ukweli utakuwa maisha yake kwa sababu anajijua udhaifu wake na mazuri yake.
Haki itakuwa kielelezo chake cha kutenda akiongozwa na upendo usiobagua kwa wale
wote wanaomzunguka.
Wapendwa wana wa Mungu,
faida ya kuwa na hofu ya Mungu ni kuyawaza na kuyatenda yale ya Mungu. Hofu hii
hutuinua na kuyatafuta yale yaliyo juu
kule Kristo na Mungu walipo. Hatuwezi kamwe kuridhika na haya ya leo na kesho
tu. Hofu ya Mungu hutusukuma kuelekea umilele. Mtume Paulo anatuwasa na kusema,
“basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko,
ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Hofu hii ya Mungu utufanya kutafuta
zaidi yale yaliyo ya Mungu.
Wapendwa katika Kristo,
tunaona hofu hii ya Mungu ikimsukuma Mfalme Dario katika uhamasishaji wa
kujenga nyumba ya Mungu. Naye anawaambia watu wake, “iacheni kazi hii ya nyumba ya Mungu, msiizuie;
waacheni liwali wa Wayahudi, na wazee wa Wayahudi, waijenge nyumba hii ya Mungu
mahali pake,” Ezr 6:7. Uwepo wa Hekalu kwa kumwabudu Mungu na kumtolea
shukrani, uwepo wa ardhi kwa kujipatia mahitaji yao ya mwili, na uwepo wa
uongozi imara, vilikuwa vithibitisho vya uwepo wa Mungu katika maisha ya
Wayahudi. Hivyo kulikuwa na hitaji kubwa sana ya kuiisimamisha nyumba ya
Mungu-Hekalu. Ilikuwa ni kosa kubwa na laana kwa Mungu kwa ye yote atakaye zuia
mpango huu Mtakatifu. Hivyo Mfalme Dario anatoa angalisho kwa ye yote
atakayezuia mpango huu. “Na Mungu huyu, aliyelifanya jina lake likae pale, na
aangamize wafalme wote, na watu wote, watakaonyosha mikono yao kulibadili neno
hili, na kuiharibu nyumba hii ya Mungu, iliyoko Yerusalemu,” Ezr 6:12. Hofu ya
Mungu utupeleka pale alipo Mungu.
Ni ukweli kwamba tunapoliona tatizo kwa pamoja ni kwa njia
hiyo hiyo tatizo hilo hutatuliwa kwa wepesi zaidi. Kiongozi Imara kama Dario
alikuwa kielelezo cha umoja ule Mungu aliokuwa anautaka kwa watu wake. Hivyo
tamko la Mfalme Dario linapokelewa na wote na kazi ya Mungu inafanyika. “Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa,
kwa msaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga,
wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi,
na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi,” Ezr 6:14. Hapa tunaona mafanikio
tuyapatayo tunapoongozwa na hofu ya Mungu. Wale wote wenye hofu ya Mungu
hubarikiwa katika mambo yao.
Ndugu zangu, hofu ya Mungu utujengea utaratibu wa namna ya
kufanya. Hapa ukweli na haki katika kuona na kutenda ujidhihirisha. Dhamiri zetu
ndani utusukuma kwa lile la kweli na haki. Kila mmoja kadiri ya nafasi, uwezo,
na wito wake atafanya kwa ajili ya wengine. Matokeo ya tendo hili uzaa hali ya
kufaidiana kuliko kweli na haki. Hivyo, “wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi
katika zamu zao, kwa ajili ya huduma ya Mungu, iliyokuwako Yerusalemu; vile
vile kama vilivyoandikwa katika chuo cha Musa,” Ezr 6:18. Huku pia ndiko
kuongozwa kwa ufunuo wa Roho na mapendo ya kweli. Ni kwa namna hii, “kila mmoja
hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la
hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yule yule,” 1Kor 12:7-8.
Kwa maana nyingine kila mmoja wetu atakuwa kile alicho na makusudi na Mungu
katika kuumbwa kwake, yaani, kumjua Mungu, kumpenda Mungu, kumtumikia Mungu, na
mwisho turudi kwake mbinguni kwenye umilele.
Wapendwa wana wa Mungu, tunapokuwa kweli kile tulicho,
kikiambatana na makusudi ya Mungu katika uumbaji wetu, maisha huwa tendo la
shukrani kwa Mungu kila tuivutapo pumzi yake. Shukrani azitoazo mwanadamu kwa
muumba wake ni tendo la kusadifu yale yote ayapatayo kuwa si kwa nguvu na uweza
wake mwanadamu, bali ni Mungu mwenyewe. Ni kujua kwamba yote tuyapatayo ni kwa
neema zake Mungu. Kwa kutambua ukweli huu, “makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote
walikuwa hali ya tohara; wakachinja Pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho,
na kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao,” Ezr 6:20. Sifa
na shukrani ni kwa Mungu peke yake kwani matendo yake kwetu ni makubwa sana.
Wapendwa katika Kristo, hofu hii ya Mungu licha ya kutuongoza
katika kweli, haki na upendo wa dhati, utuunganisha kuwa kitu kimoja katika
Kristo. Sote huwa ndugu katika Kristo si kwa njia hii ya kibailojia, bali
ufanywa ndugu kiroho na kutuvusha katika mitizamo ya kibinadamu isiyo beba
umilele ule tunaoutamani. Hivyo Yesu analisema jambo hii akifafanua maana ya
ndugu pale alipoletewa taarifa ya uwepo
wa Mama yake na ndugu zake wakimsubiri nje ya Hekali. Naye anasema, “Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na
kulifanya,” Lk 8:21. Ni kwa hofu ya Mungu tu twaweza lisikia neno la Mungu na
kulifanya. Na tunapolisikia na kulifanya neno hili la Mungu bila mawaa, baraka
na neema huwa matunda yake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye;
kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala
kupokea zawadi,” 2Nya 19:7
No hay comentarios:
Publicar un comentario