viernes, 25 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 25 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 25 YA MWAKA-B
26/9/2015
Somo: Zek 2:1-5, 10-11a
Zab: Yer 31:10-12, 13
Injili: Lk 9:43-45
Nukuu:
Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana,” Zek 2:10

Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu,” Lk 9:44 

Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile,” Lk 9:45

TAFAKARI: “Mungu hujifunua katika hali zetu za mahangaiko na mateso; usipoteze Imani yako hata kama huelewi sababu ya hali hiyo.”

 Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka katika maisha yako ushafikwa na hali ambayo huwezi ona mbele tena kutokana na kusongwa na kila aina ya misukosuko. Wakati mwingine unapojaribu kutatua jambo fulani mara linaibuka lingine kubwa au baya zaidi. Tukiwa katika sintofahamu hizi ni rahisi sana kuyumba katika Imani. Ni wakati huu tunapoona na kupata shauri mbalimbali na tusiposimama imara katika imani tunaanguka. Mungu anawaambia wana wa Israeli na sisi pia leo hii  kupitia Nabii Zakaria kwamba, Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana,” Zek 2:10. Hakuna kitu kibaya katika maisha kama kukata tamaa. Maneno haya ya Mungu yanatuhamasisha tusikate tamaa. Hata katika shida na mahangaiko yetu Mungu yupo nasi. Kukata tamaa ni kumkufuru Roho Mtakatifu anayefanya kazi ndani yetu. Dhambi hii ya kumkufuru Roho Mtakatifu haisamehewi hata kidogo. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasemehewa.” Mt 12:31. Je, walifahamu jambo hilo ndugu yangu?

Bila shaka kupitia mahangaiko haya na mateso hayo tunaandaliwa kwa lililo kubwa zaidi mbeleni na kuwa walimu wazuri zaidi kwa kwenye shida kama hiyo huko mbele ya safari. Kila kitu kinamakusudio yake katika maisha. Kama tuliumbwa wa sababu na makusudi ya Mungu, basi kila jambo ndani yetu linasababu yake na ujumbe wake hasa kuhusu imani yetu.

Bwana wetu Yesu Kristo anatujengea ujasiri wa kustahimili mahangaiko na mateso kama anavyowaambia wanafunzi wake nyakati zile, kwamba, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu,” Lk 9:44. Ni kweli na haki kabisa kwamba ujumbe huu kibinadamu hausikiki vizuri masikioni mwa wanafunzi wake kwa mtazamo walikuwa nao juu ya Yesu Kristo. Maneno haya yanasikika kama jambo la kufikirika vile. Bila shaka swali la msingi mioyoni mwa wanafunzi wake Yesu lilikuwa hivi: maneno haya yana ukweli gani ikiwa Yesu huyu tunayemjua anaonekana kuweza vyote na mkono wa Mungu ukifanya kazi juu yake atiwe nguvuni mikononi mwa watu? Maandiko matakatifu yanatuambia kwamba, “hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile,” Lk 9:45. Kwa makusudi na nia njema kabisa ya Mungu anaweza kuuficha ukweli fulani kwa lengo la kipimo cha Imani yetu.

Katika maisha yetu ya kila siku yapo mazingira fulani na hata nyakati fulani kwayo ukweli juu ya Mungu hujificha. Mara nyingi na tulio wengi nyakati za furaha na amani huwa hatuoni uwepo wa Mungu. Hali hii hututia kiburi cha kujinyanyua na kumweka Mungu kama hitaji la pili au la tatu katika maisha. Ni wakati wa “ponda mali kifo chaja.” Kumbe wakati kama huu wa furaha ndiyo wakati mzuri zaidi kumpa Mungu sifa na shukrani. Ni wakati nzuri zaidi wa kuzama katika mafumbo na makuu ya Mungu tukijua kwamba utulivu husadifu uwepo wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


KAA NASI BWANA DAIMA. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario