ALHAMISI WIKI YA 23 YA MWAKA-B
10/9/2015
Somo: Kol 3:12-17
Zab: 150:1-5
Injili: Lk 6:27-38
Nukuu:
“Basi, kwa kuwa
mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu
wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana,
na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana
alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi,” Kol 3:12-13
“Zaidi ya hayo yote
jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:13
“Na kila mfanyalo, kwa
neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu
Baba kwa yeye,” Kol 3:17
“Lakini nawaambia
ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia
ninyi, wabarikieni
wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi,” Lk 6:27-28
“Maana mkiwapenda wale
wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda
wale wawapendao,” Lk 6:32
“Bali wapendeni adui
zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu
itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa
wasiomshukuru, na waovu,” Lk 6:35
“Basi, iweni na
huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma,” Lk 6:36
“Kwa kuwa
kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38b
TAFAKARI: “Tunakutana na Yesu mara
zote tunapopenda kweli na kusamehe kweli bila kipimo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Ukristo wetu siyo ule wa kwenda Makanisani kila siku hata kama tendo hili
lenyewe sio baya, siyo ule wa kuwa wanachama wa vikundi mbalimbali vya kitume
hata kama kwa kuwafanya hivyo si vibaya, siyo ule wa kuyanena tu matakatifu
bila kuyaishi, na siyo ule wa kujitoa katika Kanisa bila kuonja upendo wa
sadaka zile tuzitoazo. Hakika kama ninayafanya haya kwa kuwapendezesha watu,
bado sijakutana na Yesu, na inawezekana kabisa kutokukutana naye. Ukristo wetu
ni pale tu tunapopenda kweli na kuishi ukweli huo, na tunaposamehe kweli na
kuishi ukweli huo bila kipimo kila siku na nyakati zote.
Wapendwa, sisi sote
tuliobatizwa tu wateule wa Mungu na warithi wake. Kwa upendeleo huu wa Mungu
kila mmoja wetu anahesabiwa haki ya kuwa mtakatifu pale anapoishi upendo huo wa
Mungu na msamaha wake. Hivyo taswira yetu kama wafuasi wake Kristo yatudai kuwa
watu wa rehema, utu wema, wanyenyekevu, wapole, wavumilivu, wasamehevu, na
wenye kuchukuliana kwa upendo mapungufu yetu katika kurekebishana. Mtume Paulo
anatuwasa, “basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao,
jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu
akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na
ninyi,” Kol 3:12-13. Je, ndugu yangu, una sababu yeyote ya kutokupenda na
kusamehe?
Upendo
kwa Mkristo ndiyo mizania ya yote hayanenayo na kuyatenda. Hivyo, “zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,”
Kol 3:13. Tunakamilishwa na upendo wa Mungu, na ni kwa namna hiyo hiyo
tunakamilishana tunapoishi upendo huu katika kweli yake kwa wenzetu. “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika
jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye,” Kol 3:17. Tendo hili la
kuyatazama yote katika upendo wa kweli linatusukuma pasipo shaka kumtolea Mungu
shukrani ya kweli. Shukrani hiyo hujeuka kuwa kielelezo cha neema na baraka za
Mungu zisizo na kikomo. Ndugu yangu, moyo usiokuwa na shukrani ukausha mema
yote.
Upendo wa
kweli huvunja mipaka yote na kuta zote zinazotuzuia kuuona upendo wa Kristo na
sadaka yake pale msalabani. Upendo huu utusukuma kupenda hata pale tunapoumia
kama binadamu kwa kufanya tendo hilo kutokana na yaliyotusibu na yaliyopita na
kutufanya kile tulicho. Upendo huu ujenga tena daraja Imara la kuwapenda hata
wale maadui wetu. Tendo hili la upendo linatukutanisha na Yesu aliyependa hata
kuutoa uhai wake kwa ajili yetu. Kwa tafsiri hii, upendo unakuwa AMRI. Hivyo
Yesu anatuambia leo neno hili la uzima sisi tusiosikia, “wapendeni adui zenu,
watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni
wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi,” Lk 6:27-28.
Tendo hili ndilo linalotofautisha kati ya anayemjua Kristo na aliye mfuasi wake
Kristo, Mpagani na anayeongozwa na hofu ya Mungu, na Mkristo wa kubatizwa na
anayeishi ahadi za ubatizo.
Upendo wa
kweli unatupa mtazamo mpya wa vitu na hasa watu wale wote unaokutakana nao na
kuishi nao. Huruma huwa msukumo wetu wa ndani katika kuuona ukweli,
kuutafakari, na kuutenda hata kama mazingira utuwiya vigumu kufanya hivyo.
Tendo hili kimtizamo kwa yale yote tunayokutana nayo, utuweka karibu sana na
Mungu. “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma,” Lk
6:36. Huruma hii ufunua undani wetu ambao huwa kielelezo sahihi cha kuona
upendo wa Mungu kwa wenzetu hasa pale tunapotoa hukumu kwa wenzetu. Mzaburi anatufikirisha
ukweli huu kwa kusema, “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani
angesimama?” Zab 130:3. Ndugu yangu, hapa tunaalikwa kuwa na huruma kama Mungu
alivyo na huruma nasi. Mara tulifanyapo tendo hili ndani na katika Kristo
ambaye ndiye ufunuo ulio kamili wa Mungu, tendo hili huwa baraka na mizania ya
kuhesabiwa haki mbele za Mungu. “Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho
mtakachopimiwa,” Lk 6:38b. Je, walifahamu jambo hili? Mwisho wa maisha yetu
hapa duniani tuwe tayari kwa maswali haya matatu mbele ya Mungu:
1.
Ulipenda vipi katika
maisha yako niliyokupa hapa duniani?
2.
Umetumiaje vipaji
nilivyokupa?
3.
Je, maisha ya Mwanangu
mpendwa Yesu Kristo yalikuwa na maana yoyote kwako?
Tumsifu
Yesu Kristo.
EE
YESU NIFANYE KUWA CHOMBO CHA UPENDO NA HURUMA YAKO POPOTE PALE NINAPOISHI.
AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario