viernes, 11 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 23 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 23 YA MWAKA-B
12/9/2015
Somo: I Tim 1:15-17
Zab: 112:1-7
Injili: Lk 6:43-49
Nukuu:
Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele,” I Tim 1:16

kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk 6:44

Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake,” Lk 6:45

Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake,” Lk 6:47

TAFAKARI: “Je, wewe ni Muhenga au Lihoka?”

Wapendwa wana wa Mungu, uwepo wetu hapa duniani si wa bahati mbaya. Kila mmoja wetu ni upendo na kusudio la Mungu kuwa hapa duniani na kwa namna inayompendeza Mungu huyo aliyetuumba kwa sura na mfano wake. Hata pamoja na makusudio hayo ya Mungu, mwanadamu kapewa heshima kubwa zaidi ya viumbe vyote kwa kuwa kiumbe shirikishi katika uumbaji na Mungu. Hivyo basi kuwa kwetu wazuri na wenye kumpendeza Mungu kunatokana na ushiriki wetu huo katika uumbaji. Mt. Augustino anatufundisha kwamba ‘aliyekuumba wewe pasipo wewe hawezi kukuokoa wewe pasipo wewe.’ Hii ina maana ya kwamba uzuri wetu na ubaya wetu unamchango kutoka kwetu. Mungu ambaye ni ukamilifu wote hatuwezi kumfananisha na ubaya wowote. Je, Mungu aweza kuruhusu ubaya? Jibu ndiyo! Ila katika ubaya huo siyo kukupoteza, bali kukupata katika ukamilifu kama Yeye alivyo mkamilifu.

Hivyo wapendwa wana wa Mungu, lengo la maisha yetu hapa duniani ni maandalizi ya uzima wa milele, na tunapotoka katika ulimwengu huu tubakie kuwa Wahenga. Mhenga ni mtu yule aliacha mambo mazuri ya kuigwa baada ya maisha yake hapa duniani. Mtume Paulo anatujengea taswira hiyo katika waraka wake wa kwanza kwa Timotheo. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele,” I Tim 1:16. Ndugu yangu, hapo ulipo kadiri ya wito wako na vipawa alivyokupa Mungu ni kielelezo kwa wale watakaomwamini Yesu baada ya maisha yakeo hapa duniani? Kama huna jibu la swali hili elewa kabisa unaelekea kuwa Lihoka, yaani, hutakuwa na kitu cha kuigwa baada ya maisha yako hapa duniani.

Katika Injili yetu ya leo, Yesu anatujengea kwa upana taswira ya kuwa Wahenga, yaani kutambulika kwa matendo yetu mema. Yesu anasema, tu wahenga kwa sababu, kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk 6:44. Ndugu yangu tenda mema na kuwa mwema kila siku. Hiyo ndiyo njia salama kwa mwili na roho yako katika umilele. Matokea yake ni kwamba, mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake,” Lk 6:45. Mtu mwema ndiye Mhenga, na mtu mwovu ndiye Lihoka.

Ndugu yangu, ni lipi ungependa kuwa au kuacha nyumba baada ya maisha yako hapa duniani? Yesu anatupa uhakika wa kile tutakachokuwa pale tunapoamua kufuata mafundisho yake. Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake,” Lk 6:47. Ni kwa kusikia neno lake na kulitenda huwa wahenga mara baada ya maisha yetu hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NASI TWATAMANI SANA KUWA WAHENGA. LITENDE JAMBO HILO KADIRI YA MASTAHILI YETU. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario