JUMATATU
WIKI YA 24 YA MWAKA-B
Sikukuu
ya Kutukuka kwa Msalaba
14/9/2015
Somo I: Hes 21:4b-9
Zab: 77:1-2, 34-38
Somo II: Flp 2:6-11
Injili: Yoh 3:13-17
Nukuu:
“Bwana akamwambia
Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu
aliyeumwa, aitazamapo ataishi,” Hes 21:8
“tena, alipoonekana
ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya
msalaba,” Flp 2:8
“Na kama vile Musa
alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi
kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,”
Yoh 3:14-15
“Maana Mungu hakumtuma
Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye,”
Yoh 3:17
TAFAKARI: “Penye Msalaba pana
uzima na uponyaji.”
Wapendwa
wana wa Mungu, ni kweli usiyotia shaka kwamba penye msalaba pana uzima na
uponyaji. Tumekombolewa kupitia Msalaba: mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu
Yesu Kristo. Kwa mantiki hii tunajichukulia misalaba yetu kwa upendo na bila shuruti tukiwa na Kristo aliyeushinda
msalaba kwa utii na uvumilivu wote, tunauhakika wa uzima wa milele na uponyaji
kadiri ya muda na wakati inavyompendeza Mungu.
Kivuli
cha msalaba halisi wa Kristo kinaonekana kwa Waisraeli kwa njia ya njoka
aliyeinuliwa na Musa baada ya kutubu na kuiacha njia yao mbaya. Kupitia ishara
hii, wana wa Israeli wana ponjwa na kuishi. “Bwana akamwambia
Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu
aliyeumwa, aitazamapo ataishi,” Hes 21:8. Nyoka huyu wa shaba ni kivuli halisi
cha msalaba halisi wa Kristo. “Na kama vile Musa
alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi
kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,”
Yoh 3:14-15. Mpango wa Mungu katika historia ya wokovu wetu hauwezi kusitishwa wala
kupingwa kwa nguvu yeyote ile.
Leo
tunapofanya sherehe ya kutukuka kwa msalaba Mtakatifu wa Yesu, tunatambua kwa
kina kabisa kuinuliwa kwa fumbo zima la msalaba kama kielelezo cha wokovu,
tukijua fika ni mti ambao wokovu wetu umetundikwa juu yake. Ukweli huu ndio
unaotufanya sisi sote twende na kuabudu Msalaba Mtakatifu.
Ndugu
yangu Msalaba kutukuka ni kielelezo cha unyenyekevu wetu kama wafuasi wa Kristo
aliyeushinda msalaba kwa kujinyenyekeza hadi mwisho. Mtume Paulo anasema hivi; “tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza
akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:8. Unyenyekevu ni msingi imara wa Imani yetu kote
kwa matendo na kinadharia.
Ujio wa Bwana wetu Yesu
Kristo haukuwa na lengo la kutoa hukumu, bali tuwe na imani ya kweli na kuishi
maisha ya umilele ikiwa ndiyo mpango mzima wa historia ya wokovu wetu. “Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu,
bali ulimwengu uokolewe katika yeye,” Yoh 3:17
Wapendwa wana wa Mungu,
hukumu ya Mungu itamfika kila mmoja wetu kwa kadiri ya kazi na wito wake. Basi
yanipasa kuwa makini na mwaminifu katika kazi na wito wangu.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU MSALABA WAKO
UNIKUMBUSHE WAJIBU WANGU HAPA DUNIANI DAIMA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario