JUMANNE WIKI YA 24 YA MWAKA-B
15/9/2015
Somo: 1Tim 3:1-13
Zab: 100:1-3, 5, 6
Injili: Lk 7:11-17
Nukuu:
“Na alipolikaribia
lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye
ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye,” Lk 7:12
“Bwana alipomwona
alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13
“Akakaribia, akaligusa
jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia,
Inuka. Yule maiti akainuka,
akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:14-15
“Hofu ikawashika wote,
wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia
watu wake,” Lk 7:16
“Ni neno la kuaminiwa;
mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema,” 1Tim 3:1
“Basi imempasa askofu
awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu,
mkaribishaji, ajuaye kufundisha,” 1Tim 3:2
“Vivyo hivyo mashemasi
na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana, si
watu wanaotamani fedha ya aibu,” 1Tim 3:8
“Kwa maana watendao
vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani
iliyo katika Kristo Yesu,” 1Tim 3:13
TAFAKARI: “Huwezi kuwatumikia watu
kama huwapendi.”
Wapendwa wana wa Taifa la
Mungu, ni ukweli usioshaka kwamba huwezi kuwatumikia watu kama huwapendi. Hata
hivyo, katika hali ya kawaidi inawezekana ukatoa bila kupenda, ila huwezi
kupenda bila kutoa. Kwa kusumbuliwa, mfano, mtu anayekuomba kila siku unaweza
kumpa anachokuomba kuepukana na usumbufu. Ila kama unapenda kweli utajikuta
unatoa hata kama hujaombwa. Ukweli huu ndio anatufundisha Mtume Paulo kwamba,
yote yatafika wisho yaani, MATUMAINI, NA IMANI, ila UPENDO utadumu daima. “Basi,
sasa inadumu Imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni
upendo,” IKor 13:13.
Upendo aliokuwa nao Bwana
Yetu Yesu Kristo ni kama kikohozi, kwamba huwezi kuzuiya kinapokujia. Hivyo
Yesu akiwa safarini kuelekea mipaka ya Naini, anakutana na tukio la
kuhuzunisha, yaani kifo. Akiwa Bwana wa wazima na wafu, Yesu anashindwa kujizui
katika PENDO la kweli. “Na alipolikaribia
lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye
ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye,” Lk 7:12. Yesu
anapokutana na hali hii anakuwa mfariji wa kwanza kabisa kwa wale wote
wanaoomboleza. Kwanza kabisa anatutoa hofu. “Bwana alipomwona
alimwonea huruma, akamwambia, Usilie,” Lk 7:13. Huyu ndiye Yesu, mwalimu na
kiongozi. Yupo tayari kufanya yote kwa sababu anatupenda kama tulivyo na
mapungufu yetu. Yupo tayari kuyafuta machozi yetu na kuwa tumaini jipya na
lenye heri. Yesu anatufundisha kwamba bado tumaini lipo ndani yake
tunapomwamini licha ya matatizo tunayokabiliana nayo kwa sasa. Matatizo siyo
mwisho wa tumaini jipya ndani na katika Kristo.
Wapendwa
katika Kristo, tunaye Jemedari wa kweli na hai kila siku ya maisha yetu. Je,
bado unamashaka ya kuambatana na Jemedari huyu? Yesu ndiye kimbilio yetu na
yetu yote matumaini. Kamwe ndani ya uongozi wake hatuwezi kuwa mateka tena. Kwa
Yesu kuna uhuru wa kweli na tunaona upendo wa kweli. Yesu hutenda makuu kwetu
siyo kwamba ni mastahili yetu, bali hawezi kuacha kufanya hivyo kwa sababu
anatupenda upeo. Kwa upendo huo, Yesu “akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua
wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza
kusema. Akampa mama yake,” Lk 7:14-15. Kwa upendo wa Kristo sote unainuliwa
kutoka hali yetu ya kufa na kukata tamaa. Ndugu yangu elewa kila unapokosa
mwelekeo wa maisha Yesu anakuambia INUKA!
Wapendwa
wana wa Mungu, upendo huu wa Yesu unapokuwa sehemu ya maisha yetu kila siku,
kamwe hatubaki kama tulivyokuwa mwanzo. Upendo huu hujenga hofu ya Mungu ndani
mwetu na kuzidi kuyaona yote katika Kristo Mfufuka na hali. Upendo huu
unatuwajibisha kuwa kama Kristo mwenyewe, yaani, kuwa habari njema kwa watu
wote. Hivyo wakazi wa Naini “hofu ikawashika wote,
wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia
watu wake,” Lk 7:16. Huyu ndiye Kristo Kiongozi mwenye upendo wa kweli, na
anatutaka mara zote tuwe kielelezo cha upendo huo, kila mmoja kadiri ya hali na
ngazi yoyote ya uongozi aliyopewa kama dhamana, ikiendana na wito wake.
Katika
hali ya wito, Mtume Paulo anawazungumzia watu wawili, yaani mwenye hadhi ya
Askofu na Shemasi. Mtume Paulo anawazungumzia watu hawa kutokana na nafasi zao
katika utume na jamii wanayoishi, ikiambatana na mapasa yao. Sifa kuu ya watu
hawa ni kutumika ipasavyo na bila kujibakiza kwa wote, ili Kristo aonekane kwa
wote aliowafia kwa UPENDO. Hivyo basi, Askofu ili ambebe Kristo katika
ukamilifu wote yampasa “awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi
na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha,” 1Tim 3:2. Kadiri
ya mapokea ya Kanisa la zamani Askofu aliruhusiwa kuoa. Ila kadiri ya mahitaji
ya nyakati mbali mbali katika Kanisa lililokuwa na kuongezeka, ilionekana ni
vyema kwa makleri kutokuoa ili wasijigawe katika upendo wa Kristo kwenye huduma
zao Kikanisa. Mashemasi pia iliwapasa “wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si
watu wa kutumia mvinyo sana, si watu wanaotamani fedha ya aibu,” 1Tim 3:8.
Kadiri ya mang’amuzi ya uongozi na maisha ya wito, kupenda fedha ni
“shina moja la mabaya ya kila namna; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo
wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10. Ila “watendao vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri
mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu,” 1Tim 3:13. Yote huwa sawa katika
upendo, na ndiyo dira ya kila kitu tukifanyacho. Kwani “ukipenda utafanya yote,”
Mt. Augustino wa Hippo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU TUJALIE UPENDO WAKO, NA TUYAFANYE YOTE KWA UPENDO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario