ijumaa wiki ya 25 ya
mwaka-b
25/9/2015
Somo: Hag 1:15-2:9
Zab: 42:1-4
Injili: Lk 9:18-22
Nukuu:
“Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa
majeshi, Hag 2:8
“Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu
wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani,
asema Bwana wa majeshi,” Hag 2:9
“Akawaambia, Nanyi
mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,”
Lk 9:20
“akisema, Imempasa
Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani
na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka,” Lk 9:22
TAFAKARI: Utajiri wa kweli ni kuwa na Kristo aliyekubali kuwa maskini
ili uwe tajiri.”
Wapendwa wana wa Mungu, wengi wetu tunafikiri furaha ya kweli
na amani ndani mwetu ni kuwa na mali au vitu au utajiri fulani. Ukweli ni
kwamba ni vyema kuwa na yule anayeutoa utajiri huo na amani ya kweli ndani ya
mioyo yetu, kuliko kuridhika na haya ya leo na kesho tu. Yesu Kristo amejitoa
sadaka na kufa pale msalabani ili mimi na wewe tuwe matajiri wa kudumu. “Maana
mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili
yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini
wake,” 2Kor 8:9
Wapendwa tupo
pamoja? Kwa hiyo si vyema hata kidogo
tukasukumwa na tamaa ya kupata vitu na jambo hili kuwa ndilo lengo la maisha
yetu hapa duniani. Tamaa ya kuwa na kitu haijalishi upo utawani au kwenye
maisha ya ndoa. Msukumo huu wa kutaka zaidi kila siku una misingi yake katika
udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa wa
muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo yote matatu si ya kweli. “Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu
na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu
katika upotevu na uharibifu,” 1Tim 6:9. Mali huleta furaha ya "muda
mfupi tu." Na sababu kubwa ndugu yangu, vitu havibadiliki, hivyo
vinatuchosha na tunataka vipya, vikubwa, na bora zaidi. Ukweli ni kwamba
tunasahau kuwa, “fedha
ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi, Hag 2:8. Ukiwa
na vitu hivi elewa kwamba wewe ni mtunzaji tu kwa muda fulani, na ipo siku
utaviacha vyote hapa hapa duniani na mwingine atapewa kuvitunza kama wewe
ulivyopewa leo na kesho.
Kuna imani pia kwamba
nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na umuhimu unaotegemea
ulivyo navyo ndugu yangu ni vitu viwili tofauti. “Maana
shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali
wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim
6:10. Thamani yako haitegemei
mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu maishani mwako si vitu! Imani ya watu
wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo nyingi kutanipa usalama. Huwezi! Tulio
utawani hatuchoki kuwa na tumiradi binafsi twa siri twingiiii. Usicheke ndiyo
ukweli kwa baadhi yetu. Mambo yanapokwenda vibaya kwenye huto tumiradi tupresha
twa kupanda na kushuka hatukomi.
Ndugu yangu, utajiri
unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza
kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na
Mungu. “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka
na kitu,” 1Tim 6:7. Mt.
Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na
vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo
uchache na huo wingi. Mungu anaufunua ukweli halisi wa sisi kushikamana nao
kupitia kinywa cha Nabii Haggai, na kusema, “Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa
mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali
hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi,” Hag 2:9. Utukufu huu na amani hii
ya kweli tunaipata kwa Kristo mwenyewe.
Hata hivyo yatupasa kumjua huyu Yesu ni nani kwetu. Yesu
alitaka kujua kutoka kwa watu na hata kwa wanafunzi wake wa karibu kabisa
wanamtazamo gani juu yake. Mtume Petro anatoa jibu sahihi kuhusu Yesu, na lile
lililo mpasa Kristo katika ulimwengu huu. “Akawaambia, Nanyi
mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu,”
Lk 9:20.
Mpendwa unayesafiri nami katika tafakari hii nikuulize swali
la msingi; pamoja na majibu ya wengine, na hasa jibu alilolitoa Petro kuhusu
swali alilouliza Yesu, wewe binafsi Yesu kwako ni nani? Jibu la Petro kwa
tafsi, Kristo yaani Masiha wa Mungu, ndiye yeye tu aliyewekwa katika mpango
mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Hivyo tutaiona mbingu na kuufurahia uhuru wa
kweli endapo tu tutakuwa tayari kushikamana na mwana huyu wa Mungu. “Yeye ndiye
jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la
pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina
lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,”
Mdo 4:11-12. Hivyo kufikia hatua hii la kuokolewa kwetu kupitia jina hili
hatunabudi kushiriki njia ile aliyopitia Bwana wetu Yesu Kristo kama
anavyowanong’onozea wanafunzi wake siri hii na kusema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee
na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka,” Lk
9:22. Ndugu yangu hakuna PASAKA PASIPO IJUMAA KUU. Ndivyo hivyo kwetu kama
wafuasi wake Kristo tulio hai kwamba hakuna UTUKUFU PASIPO MSALABA.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE YESU
WEWE NDIYE FURAHA YETU YA KWELI. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario