JUMAPILI
YA 24 YA MWAKA-B
13/9/2015
Somo
I: Isa 50:5-9a
Zab:
114:1-9
Somo
II: Yak 2:14-18
Injili:
Mk 8:27-35
Nukuu:
“Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu
yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate,” Isa 50:6
“Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari,
kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona
haya,” Isa 50:7
“Lakini mtu atasema,
Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo,
nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu,” Yak 2:18
“Naye akawauliza, Na
ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe
Kristo,” Mk 8:29
“Akawaita mkutano
pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane
mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate,” Mk 8:34
“Kwa kuwa mtu atakaye
kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili
yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha,” Mk 8:25
TAFAKARI:
“Ni mtu yule tu atakayeiangamiza nafsi yake kwa
ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha dominika ya 24 ya mwaka ‘B’wa
Kanisa. Dominika ya leo tunaalika tumtafakari kwa undani ‘mtu wa ndani’, hasa
NAFSI ili kuisalimisha katika mema na yaliyo makusudi ya Mungu. Mtu kamili anakuwa katika sehemu kuu
tatu:- Nafsi, Roho, na Mwili. “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi Nafsi
zenu na Roho zenu na Miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila
lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” I The 5:23
Katika hili Roho na Nafsi huwa pamoja na ndizo wewe
mwenyewe. Mwili ni nyumba ya roho na nafsi. Katika uumbaji Mungu aliumba mwili
kwa udongo halafu akapulizia pumzi puani ambayo ni roho yake ndipo mtu huyo
akawa nafsi iliyo hai. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi,
akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa. 2:7. Miili
tuliyonayo ni nyumba ya Nafsi na Roho. Kwa hali hii sisi binadamu ni wawili.
Kuna mtu wa ndani na mtu wa nje. Mtu wa ndani ni Nafsi na Roho, na mtu wa nje
ni Mwili lakini watu hawa wapo pamoja hatuwezi kuwatenganisha wala kumwona kwa
macho ya nyama huyu mtu wa ndani, ila yupo.
Katika hili twaona haya yafuatayo:- Huyu mtu wa nje hukua,
kuzeeka na kufa. Mtu wa ndani hakui, hazeeki, wala hafi. Mtu wa ndani
hubadilika kwa kuchakaa kunakotokana na kujeruhiwa na kuumizwa kunakosababishwa
na dhambi na matukio mbalimbali yanayomsibu binadamu. Mtu wa ndani alianza
tangu pale kutungwa mimba siku ya kwanza wakati yai na mbegu na pumzi ya Mungu
alipoweka roho yake. Mtu huyu wa ndani hakui wala haongezeki ila hufanywa upya.
“Kwa hiyo hatulegei, bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu
wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Kwa hiyo huyu mtu wa nje
akifa mtu wa ndani huenda mahali atakapokuwa amejiandalia ama Mbinguni au
motoni.
Wapendwa wana wa Mungu, kwenye Nafsi ndipo penye tatizo
lenyewe kwani ni katikati ya Roho na Mwili. Nafsi hutawaliwa na Hisia, mfano:-
Hofu, Chuki, Hasira, Kujihukumu, Kujikataa, Kukosa furaha, Kukosa upendo,
Kukosa amani, n.k. Ni muhimu sana mtu atawale hisia zake. Nafsi ikiegemea
rohoni huleta matunda mzuri. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani,
uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo
hakuna sheria.” Gal. 5:22-23. Ila nafsi inapoingia katika Mwili mambo huwa
mabaya kwani ufanya matendo ya mwili kama tusomavyo katika maandiko matakatifu,
“basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi,
ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi
husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia
mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi
hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Gal.5:19-21. Ni vizuri kujua nafsi yako
imeegemea wapi. Ikiegemea rohoni utaenda Mbinguni, ikiegemea mwilini utaenda
motoni.
Ndugu yangu unayesafari nami katika tafakari hii hatutaweza
kumfuata Kristo katika mwelekeo ule ule alioufuata, yaani wokovu kupitia
msalaba na kuufikia utukufu kama hatujui Nafsi yetu imeegemea wapi. Kuhusu
jambo hili Yesu analiweka wazi kabisa na kusema, “Kwa kuwa mtu atakaye
kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili
yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha,” Kuiponya Nafsi ni kuiridhia
nafsi kwa kuyapenda na kuyaegemea matendo ya mwili. Kwa mantiki hii ni
kuingamiza nafsi kwa kujua kabisa. Na kuiangamiza nafsi kwa ajili ya Kristo na
Injili-habari njema, ni kuyapenda na kuyaegemea matendo ya Rohoni. Huku ndiko
kuisalimisha Nafsi kuliko kwema na mpango wa Mungu.
Nafsi
husalimika kwa kuyapenda na kuyaegemea matendo ya Rohoni pale tu tunapokuwa
tayari kumfuata Kristo, kujikana nafsi, na kujitwika msalaba wetu daima na kwa
hiari bila shuruti. Yesu “akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye
yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake,
anifuate,” Mk 8:34. Tukijua aliyekamkamilifu ni Mungu tu, basi kila mwanadamu
ili aufikie ukamilifu na kumwona Mungu kama alivyo itampasa kujisafisha kwa
kile ambacho kwa tafsiri ya ndani ni ‘msalaba wa kila mmoja wetu.’ Msalaba
katika tafsiri hii twaweza kusema ni mapungufu aliyokuwa nayo kila mmoja wetu
karidi ya maisha na wito wake. Madhaifu na mapungufu yetu huponywa pale tu
tunapoyapokea ndani na katika Kristo. Hivyo, “tukimtazama Yesu, mwenye
kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa
mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume
wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana
mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao
dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr 12:2-3
Ukweli wa
maisha na tafsiri ya ‘Msalaba,’ katika mwono wa Injili ya leo unatupeleka ndani
zaidi kuijua Imani yetu na yule tunayemwamini na kumfuata. Kumjua ni nani
tunayemfuata, Yesu anauliza swali la uchokozi kwa wanafunzi wake na Petro
anatoa jibu, tena jibu lililo sahihi kabisa. “Naye akawauliza, Na
ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe
Kristo,” Mk 8:29. Kristo yaani, aliyewekwa kwa sababu hiyo, yaani wokovu wa mwanadamu.
Huyu ndiye Masiha kwa ajili ya wokovu wetu.
Imani ya
kweli huwezi itofautisha na matendo ya kweli yanayoambatana na kile mtu
anachoamini. Na wakati mwingine matendo (ya upendo na huruma) husema zaidi ya
kila kilicho ndani ya mtu yaani Imani (yanayoonekana na yasiyoonekana). “Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo.
Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya
matendo yangu,” Yak 2:18. Nabii Isaya yupo tayari kupokea kadhia zote kwa
sababu anayo Imani na Mungu anayemwamini kuwa ndiye msaada na kweli katika
yote. “Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao
ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate,” Isa
50:6. Nabii Isaya yupo tayari kupokea fedheha
zote akijua mwisho wa siku mateso yake si bure kwani anaye mtetezi wa kweli
yaani, Mungu. “Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari,
kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona
haya,” Isa 50:7. Je, mateso uliyonayo yanakupa mwanga zaidi kuhusu Imani yako? Tunapozungukwa na mateso na hali ya kukata
tamaa tujifunze kutoka kwa Mtume Paulo na kusema, “Lakini mimi, hasha,
nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14.
Kijana
Humphrey mcha Mungu na mwenye akili sana darasani hakuwahi kumjua Baba yake
mzazi licha ya kwamba anamjua mama yake mzazi ambaye ni kichaa. Humphery ambaye
kwa sasa ni Mwalimu katika Chuo Kikuu Kimoja Nchini, anampenda sana Mama yake
licha ya hali aliyokuwa nayo.
Jambo la
ajabu na muujiza kwake ni pale anapotafakari ilikuwaje Mama yake kumzaa na
kumtunza hasa katika uchanga wake bila kupata matatizo yoyote yale. Hakika kwa tendo
hili Humphrey umwona Mungu katika mpango mzima wa maisha yake. Licha ya ukali
alikuwanao Mama yake huku akibeba vitu vya hatari kama visu na misumari, makopo
na chupa, hakuweza kumdhuru katika
uchanga wake.
Kwa
upande mwingine Humphrey amekuwa faraja kubwa sana na ulinzi wa kutosha kwa
mama yake mzazi licha ya usumbufu mkubwa anaoupata kwa kupotea mara kwa mara
nyumbani anapoishi na mwanaye huyu. Watu wengi na hasa marafiki zake Humphrey
humshawishi na kumwambia, ni wakati mwafaka angeoa ili apate msaada zaidi
katika kumtunza Mama yake. “Nitao siku ambayo Mungu atamchukua Mama yangu
kutoka dunia hii. Kama aliweza kunizaa na kunitunza katika uchanga wangu bila
kunidhuru, kamwe sintoshindwa kumtunza kwa hali hii aliyonayo sasa,” mara zote
hili ndilo jibu la Humphrey wa marafiki zake. Bila shaka Humphrey angependa
kuleta maneno na manung’uniko kwa yule ambaye angemwoa na kuwa mke wake.
Humphrey
hata mara moja haoni aibu juu ya hali ya Mama yake mzazi. Angeweza kufanya
anachoweza kuikwepa aibu hii kwa sababu elimu anayo na maisha mazuri Mungu
kamjalia. Humphrey yupo tayari kuubeba msalaba huu hadi mwisho, tena kwa fuhara
bila shuruti.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU TUJALIE NEEMA NA UJASIRI WA KUIBEBA MISALABA YETU NAWE HADI MWISHO. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario