jumatano wiki ya 25 ya
mwaka-b
23/9/2015
Somo: Ezr 9:5-9
Zab: Tob 13:2-4, 6-8
Injili: Lk 9:1-6
Nukuu:
“Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata
leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu,
tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga,
tumechukuliwa mateka, tumenyang'anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama
hivi leo,” Ezr 9:7
“Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu,
hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu.
Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu,”
Ezr 9:8
“Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika
utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili
kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka,
atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu,” Ezr 9:9
“Akawatuma wautangaze
ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa,” Lk 9:2
“Akawaambia, Msichukue
kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja
wenu asiwe na kanzu mbili,” Lk 9:3
“Na nyumba yo yote
mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke mjini,” Lk 9:4
“Na wale
wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo, yakung'uteni hata mavumbi ya miguuni
mwenu, kuwa ushuhuda juu yao,” Lk 9:5
TAFAKARI: “Yote yanamwisho ndani na katika Kristo Yesu. AMINI pasipo
SHAKA.”
Wapendwa wana wa Mungu, napolitazama Taifa letu leo
linanifikirisha sana na Taifa la wana wa Israeli katika nyakati mbalimbali
wakionja mateso ya utumwani na kabla na baada ya kuwa huru katika inchi ile ya
ahadi waliyopewa na Mungu. Furaha ya wana wa Israeli haijawa ya kudumu hata
hivi leo. Vita na machafuko havijafikia ukomo wake. Tofauti iliyopo leo na zama
zile ipo kwenye ukweli wa tafsiri na maana nzima iliyobeba historia ya wokovu
wetu.
Kama ilivyo kwa upande wa kifo kabla na baada ya Kristo,
ndivyo hivyo ilivyokuwa hata sasa, ila kifo hiki cha sasa kina uelewa mpana
kuliko ilivyokuwa kabla ya Kristo. Ndani na katika Kristo kifo hakina nguvu
tena, kwani kwa mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo hukumu ya kifo
imebatilishwa. Sote tu huru na warithi wa ufalme wa Mungu kwa sadaka yake pale
msalabani. Yatupasa kufa na kufufuka nale kila siku tunapoishi kweli ahadi zetu
za ubatizo.
Taifa letu leo linapita kipindi kigumu zaidi kuliko
ilivyokuwa siku zile za mwanzo wa uhuru wetu. Ni kweli yapo mambo mengi mazuri
tuliyoyaonja mara baada ya uhuru wetu kama Taifa kutoka mikononi mwa Waingereza
na yapo mabaya zaidi ambayo kama Taifa hatukujali kuyapa msisitizo na sasa
yamekuwa shumiri kwetu. Je, Mungu wetu yule mwenye huruma amebadilika? La
hasha! Mungu anasema hivi; “Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto
waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda
mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa,” Yer 4:22. Wapendwa wana wa
Mungu, yatupasa kuyatafakari maneno haya mazito ya Mungu kama Taifa. Yawezekana
chanzo cha mahangaiko yetu kama Taifa kipo juu ya upumbavu wetu. Wana wa
Israeli wanakiri upumbavu wao kwa kusema, “tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata
leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu,
tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga,
tumechukuliwa mateka, tumenyang'anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama
hivi leo,” Ezr 9:7. Hivi kweli Taifa letu pamoja na utajiri wake ni laana
kwetu? Kwa nini basi kila kukichwa hatuishi kulalama kama mayatima!
Wapendwa wana wa Mungu lazima tukiri kwa dhati kwamba wakati
fulani na watu fulani katika Taifa hili wametufikisha hapa tulipo. Je,
tuendelee kulalama ilihali Mungu anakuonyesha neema yake kupitia matukio
mbalimbali ya sasa? Je, tunayo nafasi ya kujinasua kutoka katika mtego huu wa
uovu? Hatima ya wana wa Israeli ilikuwa chini ya mikono yao ama kusuka au
kunyoa. Vile vile hatima ya Taifa letu ipo chini ya mikono yetu. Kila mmoja
wetu itampasa kuona, kutathimini na kuchukua hatua. Kila Taifa lina utaratibu
wake wa kujinusuru kutoka mikono ya waovu na uovu. Bila shaka kwa upande wetu
wa Tanzania huu ndio wakati wa kuona, kutathimini na kuchukua hatua. Wana wa Israeli walipo ona nuru ya Mungu
katika mahangaiko yao walisema kwa pamoja, “Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu,
hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu.
Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu,”
Ezr 9:8. Je, twahitaji Mungu kushuka na kutuambia haya ili hali tumefunuliwa
ukweli na kupewa nuru ya Mungu? Kama hata upande ule wa uovu unalalamika kuhusu
uovu, Je, hiyo haitoshi kuona kwamba mimi na wewe yatupasa kuchukuwa hatua
sahihi tusije angamia katika uovu moja kwa moja? Kwa upande wangu binafsi
naliamini sana neno hili, na ninaona huu ndio wakati wakujinasua kutoka mzimu
huu wa uovu na maovu.
Wapendwa wana wa Mungu, maisha haya tunayoishi leo kama Taifa
siyo makusudi ya Mungu na uumbaji wake. Tuelewa kwamba tumeumbwa na Mungu ili
tumjua, tumpende, tumtumikie na mwisho turudi kwake mbinguni. Je, twawezaji
kuyafanya hayo yote katika hali hii ya dhiki na machafuko? Yatupasa kufanya
kitu. Wana wa Israeli walivyojitambua walisema
haya ya moyoni, “hijapokuwa sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu
hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya
wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na
kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu,” Ezr 9:9.
Tanzania kama Taifa letu na nyumba, imebomoka. Taifa linahitaji wajenzi wapya
na wenye moyo na uchungu na siyo wababaishaji wenye kutumia wimbo ule ule wenye
kulevya, na baada ya ulevi huo mateso na mahangaiko yapo pale pale.
Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu ni sababu ya uzuri wa
Taifa letu. Uzuri huo upo ndani yetu tangu kuumbwa kwetu. Tunaye chapa ya Mungu
ambaye ndiye ukamilisho wa uzuri wote kwa yale yanayoonekana na yasiyoonekana.
Hivyo Yesu anamtuma kila mmoja wetu kupambana na yaliyomaovu. Naye “akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa,” Lk
9:2. Ufalme wa Mungu ni ufalme wa amani,
upendo, umoja, haki na kweli. Tunapoona hakuna amani, upendo, umoja, haki na
kweli, Mungu hayupo nasi. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha mambo hayo
yapo na yanadumu. Katika vita hii, Yesu anawaasa wanafunzi wake na sisi pia kwa
kusema, “msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate,
wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili,” Lk 9:3. Maana yake nini? Kwa hali ilivyo sasa yatupasa
kupigania hili ambalo halipo na ni nadra kupatikana katika ufalme wa Mungu,
yaani, amani, upendo, umoja, haki na kweli katika Taifa letu. Mada na mahitaji
mengine ya ziada nje ya ukweli huu hayana umuhimu hata kama yanahitajika.
Wapendwa wana wa Mungu,
katika safari hii tuelewe kwamba mambo siyo rahisi. Kurudisha ufalme wa amani,
upendo, umoja, haki na kweli pale ambapo hayo mambo yalisahaulika na kuwa faida
kwa wachache waliojineemesha na kuhodhi mamlaka, haitakuwa jambo rahisi kwao
kukubali ukweli huu licha ya kwamba hakuna njia nyingine. Siri ya ushindi ni
hii anayotuambia Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba, “na nyumba yo yote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke mjini,”
Lk 9:4. Kukaa ndani ya nyumba ile ile ni kusimama katika kweli hata kama
itatulazimu kufa kwa ajili ya kweli. “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli
itawaweka huru.” Yoh 8:32. Asiye pokea kweli hii na akapenda kung’ang’ana na
uongo na upotoshaji, hakuna muda wa kupoteza katika vita juu ya uovu. Naye Yesu
anasema, “na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo, yakung'uteni
hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao,” Lk 9:5. Ni swala la
wakati tu kwamba historia ndiyo itakayo kuwa hukumu kwa wale wote walioukataa
ukweli, na ukweli ule ule walioukataa utasimama daima.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
YESU TUSIMAMA NASI KATIKA VITA HIVI DHIDI YA UOVU KATIKA TAIFA LETU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario