JUMATANO
WIKI YA 23 YA MWAKA-B
9/9/2015
Somo:
Kol 3:1-11
Zab:
144:2-3, 10-13
Injili:
Lk 6:20-26
Nukuu:
“Basi mkiwa
mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono
wa kuume wa Mungu. Yafikirini
yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi,” Kol 3:1-2
“Basi, vifisheni
viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo
mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa
ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu,” Kol 3:5-6
“Mkivaa utu mpya,
unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba,” Kol 3:10
“Hapo hapana Myunani
wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala
mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11
“Heri ninyi watu
watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama
neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani
siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni,
maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo,” Lk 6:22-23
TAFAKARI:
“Furaha ya kweli ni kuyapata yote ndani na katika Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu,
licha ya kubatizwa kwetu na kuwa warithi halali wa ufalme wa Mungu, tunaishi
katika changamoto nyingi kutekeleza kwa uaminifu mkubwa ahadi zetu za ubatizo.
Changamoto hizi zinapotuzidi zinatuondolea ndoto ile ya furaha ya kweli ndani
na katika Kristo. Hivyo kufikia lengo na makusudio ya furaha hii ya kweli ndani
na katika Kristo, Mtume Paulo anatupa leo msingi wa kukabiliana na changamoto
hizo za Imani pale tunapotaka kuishi vyema ahadi zetu za ubatizo. Naye anasema
hivi, “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo
katika nchi,” Kol 3:1-2. Ndugu yangu unayesafiri na mimi katika tafakari hii,
yatupasa kwanza kabisa kuyatafuta yaliyo juu Kristo aliko.
Ndugu
yangu, mambo yaliyo juu aliko Kristo ni yale yote yanayotuongoza huko aliko,
yaani ufalme wa mbinguni na umilele wake. Kwa
maneno mengine ni “kuvaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano
wake yeye aliyeuumba,” Kol 3:10. Utu huu upya
ni tendo la kupiga vita aina zote za dhambi kwa sababu dhambi ufifisha na
kuzorotesha utu wetu wa ndani ambao ni nafsi na roho.
Jambo la pili na lenye
maana kabisa katika maisha ya kiroho ni kufikiri muda wote yale yaliyo juu na
siyo yaliyo katika nchi. Hapa Mtume Paulo anaongelea sana swala la nafsi ya
mtu. Nafsi inapoegemea zaidi katika mwili matokea yake ni anguko kuu na mwisho
wa matumaini yote ya kuurithi ufalme wa Mungu. Hapa ndipo binadamu anapoonekana
mara zote kufikiri yaliyo katika nchi na yasiyo na umilele. Kuepukana na kadhia
hii, Mtume Paulo anatoa angalisho kwa kusema,
“Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati,
uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu
ya Mungu,” Kol 3:5-6. Ghadhabu ya Mungu hapa ni kuukosa ufalme wake na
kuangamia milele pasipo kuwa na nuru yake.
Ndugu yangu, pale nafsi inapoegemea roho,
ndipo tunapojazwa tumaini jipya na kufanywa upya siku kwa siku. “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa,
lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Kuishi ukweli huu ndani na katika Kristo ni
kuchuchumilia cheo chetu halisi, yaani UTAKATIFU WAKO! Cheo hiki kila mmoja
wetu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ndiyo stahili yake, na anaipata kwa
kuishi kweli kwa mafundisho ya Kristo, na kutimiza ukweli huo kwa uaminifu.
Hivyo hasili zetu katika maana ya mila na desturi zetu, familia zetu, koo zetu,
makabila yetu, na utaifa wetu hazina uhalalisho wowote katika cheo hiki kama
hatunaye Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Ni kwa sababu hii Mtume Paulo
anawapa angalisho watu wa nyakati zake, na sisi pia kwa kusema, “hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala
kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote,
na katika yote,” Kol 3:11.
Wapendwa
katika Kristo, angalisho la mtindo huo alilotoa Mtume Paulo na lenye kutuweka
katika mstari sahihi kuelekea urithi tulioandaliwa na wenye hadhi ya cheo
chetu, ndilo alilolikazia Yesu Krito katika injili ya leo anapozungumzia heri
zile nne na ole zile nne. Maisha yetu ya leo na mahangaiko yake yamo katika
haya anayoyakazia Bwana wetu Yesu Kristo katika injili ya leo. Kila heri moja
huenenda na ole yake. Heri yao masikini kwa ajili ya Kristo, humpatia maskini
huyo ufalme wa Mungu. Umaskini hapa ni uhitaji wa Kristo kila siku ya maisha
yako. Hakuna anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. “Kwa maana kama
tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama
tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8. Kinyume chake ole
matajiri na walio na mali kwa walivyo kuwa navyo bila Kristo ni faraja ya leo
na kesho tu, na mwisho wake ni kiama. Wote walio na njaa na kiu ya haki katika
Kristo kamwe hawataona njaa, kwani Kristo atawashibisha daima kwa tendo hilo
licha ya upinzani wake. Kinyume chake, ole walioshiba sasa kwa kuzikanyaka haki
za wengine na wanyonge kwani wataona njaa ya milele.
Katika
jamii yetu leo wapo watu wengi wanaolia kwa shida mbalimbali ili hali wapo
wanaosheherekea na kutapanya vitu ovyo bila kuwajali wahitaji na wanyonge.
Kristo anatuambia wanaotaabika sasa katika ulimwengu huu watacheka na kufurahi
milele. Kwa upande wa pili, wote wanaocheka sasa na kuyafumba macho yao kwa
kutokuona shida za wengine hao wataomboleza daima. Je, ndugu yangu kwa nini
waandaa maombolezo ya kudumu katika umilele wote unaposhindwa kunyoosha mkono
wa heri kwa mwitaji unayeishi naye katika familia yako, jumuiya yako ya kitawa,
jumuiya yako ndogo ya Kikristo, ofisi moja ya kazi, kigango chako, na hata
parokia yako?
Vile vile
katika jamii yetu leo wapo wengi wanaochukiwa bila sababu ya msingi,
wanaotengwa kutokana na misimamo yao katika kweli, wanaoshutumiwa na kunenewa
uovu kwa sababu tu wanapenda kumuishi Kristo na kuwa pembeni ya kundi ovu
linalopendwa na wengi. Hawa Kristo anasema thawabu yao ni kubwa mbinguni. “Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu,
na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani
siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni,
maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo,” Lk 6:22-23. Kinyume chake ni
wake wanaopenda kuonwa wema na kusifiwa hata kama hawajafanya chochote. Hawa
taji lao ni unabii wa uongo ambalo halina thamani yoyote mbele ya Mungu. Hawa
ndio wale wanaopoteza muda na maisha yao kila siku. Ni sawa na parachuti
lililojaa hewa na kuelea juu kabisa angani na mara hufikwa na kikomo
linapokutana na ncha ndogo sana ya mwiba. Hewa yote hutoweka na kusinyaa.
Tumsifu Yesu
Kristo!
EE
YESU NITUMIE VYEMA KADIRI YA MPANGO WAKO KWANGU. AMINA
No hay comentarios:
Publicar un comentario