JUMAMOSI WIKI YA 24 YA MWAKA-B
18/9/2015
Somo: 1Tim 6:13-16
Zab: 99:1-5
Injili: Lk 8:4-15
Nukuu:
“Bwana
wetu Yesu Kristo; ambako yeye kwa
majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme
wa wafalme, Bwana wa mabwana,” 1Tim 6:14-15
“ambaye yeye peke yake
hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna
mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata
milele,” 1Tim 6:16
“Na zile penye udongo
mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na
kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia,” Lk 8:15
TAFAKARI: “Yesu Kristo neno la
uzima wetu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, ni ukweli kwamba kuishi maisha
yanayoongozwa na malengo, ni kutawaliwa, na kuelekezwa na makusudi ya Mungu.
Hakuna kitu cha muhimu zaidi kama kujua malengo ya Mungu kwa maisha yako, na
hakuna mbadala kwa hilo-siyo mafanikio, utajiri, kujulikana, au anasa. Vyote
hivyo vinaukomo wake kwa sababu asili yake ni hapa hapa duniani. Yesu Kristo ni
neno la uzima wetu. Asili yake si dunia hii, na ufalme wake si wa ulimwengu
huu. Yesu analithibitisha jambo hili mbele ya Plato, na kusema, “ufalme wangu
sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi
wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme
wangu sio wa hapa,” Yoh 18:36. Yesu Kristo ni neno aliyemwilishwa ambaye hapo
mwanzo alilkuwa na Mungu na vyote vilifanyika kupitia yeye. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa
Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,”
Yoh 1:1-3. Asili hii ya Yesu ndiyo inayompa mamlaka na milki yote ya
vinavyoonekana na visivyo onekana. Kwa mantiki hii, ndani na katika Yesu Kristo
ndiko kwenye uzima wa kweli na umilele.
Wapendwa
wana wa Mungu, hatuna Mfalme wa Wafalme kumzidi Bwana wetu Yesu Kristo. Wafalme
wote waliokwisha tokea katika ulimwengu huu na waliopo ni wakupita tu. Kwa wao
wenyewe hawana uzima huo wa milele kama hawakupewa na Kristo mwenyewe ambaye ni
Mungu. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa
Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1. Ukweli huu Yesu anauthibitisha vile
vile mbele ya Plato ambaye anajinadi kuwa na mamlaka hayo na hivyo kuwa na
uwezo wa kumfungua au kumsulubisha. “Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka
yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia
mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi,” Yoh 19:11. Maana yake nini jambo
hili?
Kwanza
kabisa, Yesu anatufunulia Ukuu na Mamlaka yake aliyo nayo juu uzima na umauti.
Pili, Yesu anatufunulia uhusiano uliopo kati yake na Baba wa mbinguni. Kwa
maana hii, mateso ya Mwana ni mateso pia ya Baba yetu wa Mbinguni.
Alichokifanya Baba ndicho anachokifanya Mwana kwa mapenzi ya Baba wa Mbinguni.
Kwa hiyo linalomsibu Yesu kwa sasa, yaani, mateso na kifo chake, si kwa nguvu
ya Plato, bali ni mapenzi ya Mungu Baba. Hivyo ana dhambi kubwa zaidi
anayepingana na mpango wa Mungu katika safari hii ya ukombozi.
Wapendwa
wana wa Mungu, ni katika mazingira haya tunaweza kutafakari kwa kina masomo
yetu ya leo. Hivyo asili ya Bwana wetu Yesu Kristo na kusudio lake hapa duniani
ndiyo sababu ya kweli kwamba “Yesu Kristo ndiye neno la uzima na umilele wetu.”
Hivyo, “Bwana wetu Yesu Kristo; ambako
yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke
yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana,” 1Tim 6:14-15. Je, ukweli huu
unasema cho chote katika maisha yako na imani yako?
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, licha ya ukweli kwamba Yesu Kristo ni uzima na umilele
wetu, hatuwezi kuficha ukweli kwamba Kristo ndiye hukumu yetu ya mwisho. Kristo
ni uhai wetu katika maana ya kwamba amekibatilisha kifo, hivyo umauti hauna
nguvu tena. “Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya
yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki,
watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo,” Rum 5:17. Ni Kristo “peke
yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna
mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata
milele,” 1Tim 6:16. Hivyo kwa kuishi ndani na katika Kristo sote twaishi katika
nuru hii isiyoharibika.
Injili ya
leo Yesu ametoa mfano wa mbegu kama uzima tunaoupata tukiwa ndani na katika
yeye ikiwa ndilo neno la uzima. Pia katika njili hii Yesu ametoa
maelezo mazuri kwa kile kilichokuwa kimejificha katika fumbo la mfano wake.
Pamoja na kutupa angalisho mwa mifano ya mbegu ilidondoka barabarani, mwenye mwamba, na kwenye mwiba, Yesu
anatusihi tuwe udongo mzuri ili uzima huo usitawi na kuzaa matunda mema. “Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema
wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia,”
Lk 8:15. Neno hilo ndiye Kristo mwenyewe, uzima, na umilele wetu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
EE
BWANA YESU KRISTO TUFANYE UDONGO WENYE RUTUBA. AMINA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario