ALHAMISI WIKI YA 22 YA MWAKA-B
3/9/2015
Somo: Kol 1:9-14
Zab: 97
Injili: Lk 5:1-11
Nukuu:
“mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa;
mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu,” Kol
1:10
“Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza
katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol
1:13-14
“Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka
kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4
“Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya
kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,”
Lk 5:5
“Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu,
akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8
“Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa
ukivua watu,” Lk 5:10b
TAFAKARI: “Kama ushakutana na Kristo katika Maisha yako lazima akubadili
mwenendo wako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
yawezekana hadi leo licha ya kuingizwa katika urika wa wana wa Mungu na warithi
wa ufalme wake kwa sakramenti ya ubatizo, bado haujawahi kukutana na Kristo
katika maana ya kuguswa kuliko ndani kabisa ya maisha yako. Tunakutana na
Kristo pale tu tunapoanza kuyachukulia maisha yetu na ufuasi wetu kwake kwa
namna iliyo hai na ya kuguswa kwa yale yote tuyafanyayo ndani na katika Kristo
Yesu. Mara tuifikiapo hatua na hali hii, tendo hili haliwi tena tendo au swala
la kihisia, hadithi au simulizi fulani la kufikirika, bali maisha halisi.
Ndugu yangu, maisha halisi
ndani na katika Kristo yanatuwajibisha kwa kila namna, tunapendezwa nayo,
maisha hayo huzaa matunda mema, na mwisho maisha hayo utuongezea ufahamu juu ya
Mungu. Ni kwa mantiki hii Mtume Paulo anawasihi Wakolosai nasi pia kwamba, “tuenende kama ulivyo
wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema,
na kuzidi katika maarifa ya Mungu,” Kol 1:10. Tunawajibika kuuona ukweli huu
tunapopima uzito wa dhambi na wokovu aliotupatia Kristo kwa sadaka ya Kifo
chake pale msalabani. Hakika ni upendo mkubwa sana kwetu wanadamu. Kristo ndiye
pekee anayetuweka huru kutoka nguvu za giza na kutuingiza katika ufalme wa
Mungu kwa pendo lake, kwa sababu ni kwake tu kwenye ukombozi na msamaha wa
dhambi zetu. Hivyo Kristo, “alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza
katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol
1:13-14. Je, ndugu yangu una sababu yoyote ya kuacha kumsamehe mwenzako kwa
vigezo vyovyote vile ulivyo navyo? Ukristo
na ufuasi wangu kwake una maana gani ninapotazama tendo hili la msamaha?
Nisipobadilika katika tendo hili hakika bado sijakutana na Kristo Yesu.
Ndugu
zangu, mahangaiko katika maisha yetu ya kila siku yasiwe ukuta wa kutokuona
uwepo na nguvu ya Kristo Yesu ndani ya yale tuyafanyayo hata kama tunauzoefu
nayo. Kama kweli wasadiki Kristo ndiye Mwokozi, basi ni kwa namna hiyo hiyo
huyaweza yote yaliyo chini ya miguu yake kwa sababu, “amevitia vitu vyote chini
ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa;
ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,”
Efe 1:22-23. Yesu Kristo analiweka jambo hili hadharani anapowakuta Simon Petro
na wenzake waliokuwa mahodari wa kuvua samaki usiku kucha bila kupata chochote.
Naye Yesu anamwambia Simoni, “Tweka mpaka
kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4. Kwa maana nyingine Yesu anamwambia Simoni Petro
kwamba “jaribu tena pasipo kuwa na shaka na urushe kete yako ya mwisho katika
ukamilifu wote.” Maneno haya ya Yesu yanamtia shaka kidogo Simoni Petro
kutokana na uzoefu aliokuwa nao katika kuvua samaki. Hata hivyo Simoni
anamwamini Yesu pasipo shaka na kufanya alivyoagizwa. Hivyo, “Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa,
tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako
nitazishusha nyavu,” Lk 5:5. Ndugu zangu, “ni kwa neno lake Yesu, Simoni Petro
anazishusha nyavu.” Ni kwa njia ya neno Mungu aliumba ulimwengu kutoka utupu.
Hivyo ni kwa neno hili: “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho
chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa
nuru ya watu,” Yoh 1:3-4. Je, bado unamashaka na Neno wa Mungu, yaani Yesu
Kristo?
Muujiza
wa wingi wa samaki uliotokana na hali isiyoyakawaida kadiri ya ufahamu aliokuwa
nao Simoni juu ya uvuvi unamfanya akutane na Kristo katika maisha halisi na
kujiona alivyo kiroho. Hapa ndipo pale tunaposema kwamba unapokutana na Kristo
ndani na katika yeye lazima akubadilishe. Kubadilishwa kwa Simoni kunajionyesha
katika hali ya dhambi iliyoisuta nafsi yake. Hivyo katika mguso huu, “Simoni Petro alipoona hayo, alianguka
magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi,
Bwana,” Lk 5:8. Je, ninapokutana na matendo makuu ya Mungu katika maisha yangu
nauona udhaifu wangu? Je, matendo hayo makuu ya Mungu ni mastahili yangu
yanayotokana na mafanikio yangu na juhudi zangu bila mkono wa Mungu?
Wapendwa wana wa Mungu, tunapokutana na Kristo katika
uhalisia wa maisha yetu ya kila siku, hali hiyo hughubikwa na hofu kubwa kwa
sababu tunajiona kama tulivyo kwani Kristo huwa kioo cha kujitazamia nafsi na
roho yetu. Tupatapo hali hiyo, tusisahau kuwa Yesu anatuambia kama alivyo
mwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b. Maana
yake yake, “usihofu kwani ninakuandaa kwa makubwa zaidi ya hayo
niliyokutendea.” Mungu wetu mara zote utuwazia mambo makubwa zaidi ya yale
tuyafanyayo kila siku, na neema na baraka anazotujalia pasipo mastahili yetu.
Tumsifu Yesu Kristo!
EE YESU MATENDO YAKO KWANGU NI YA AJABU SANA! UTUKUZWE NA
KUHESHIMIWA MILELE. AMINA.
No hay comentarios:
Publicar un comentario