sábado, 19 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 25 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 25 YA MWAKA-B
20/9/2015
Somo I: Hek 2:12, 17-20
Zab: 53:3-6, 8
Somo II: Yak 3:16-4:3
Injili: Mk 9:30-37
Nukuu:
“Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake,” Hek 2:17

“Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa,” Hek 2:19

Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya,” Yak 3:16

Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki,” Yak 3:17

Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani,” Yak 3:18

Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata,” Yak 4:2a

Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yah 4:3

Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35

Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma,” Mk 9:37

TAFAKARI: “Mwisho wa ubaya ni aibu; ila tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”

Wapendwa wana wa Mungu, karibuni na tutafakari pamoja na Mama Kanisa Dominika hii ya 25 ya Mwaka “B” wa Kanisa. Ni kweli kwamba mwisho wa ubaya ni aibu; ila tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani. Ndugu zangu, wapo wanaoshikilia maumivu (machungu) bila kuyaacha. Badala ya kutoka katika maumivu kwa kusamehe, wanaendelea kuyakumbuka katika mawazo yao tena na tena. Baadhi ya watu wanaongozwa na chuki kutunza ndani uchungu wao, na wengine huwalipukia watu wengine. Hali zote hizi si nzuri na hazisaidii maishani. Chuki mara nyingi huleta maumivu kwako kuliko yule unayemchukia. Mtu aliyekukosea anaweza kuwa amesahau lile kosa na anaendelea na maisha yake vizuri, wewe unaendelea kuumia na kuhangaika na yaliyopita.

Sikiliza ndugu yangu: Wale waliokuumiza wakati uliopita hawawezi kuendelea kufanya hivyo sasa "isipokuwa" kama utaendelea kutunza uchungu. Yaliyopita yamepita! Hakuna kitakachoyabadilisha. Unajiumiza tu na uchungu wako. Kwa ajili yako, jifunze kutokana na hilo na kisha achana nalo. Maandiko matakatifu yanatukumbusha kuwa, "kwani hasira humwua mtu mpumbavu, nao wivu humwua mjinga." Ayu 5:2.  Kuwa na hofu kiasi cha kufa kwa sababu ya uchungu ni upumbavu, ni kitu kipumbavu kukifanya. Wenye chuki na wivu hufurahia katika haya, “Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake,” Hek 2:17. Wenye wivu na majingu faida yao ni kupoteza muda na kuwa vivuli vya wengine. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya,” Yak 3:16. Je, wapata faida gani kwa haya yote?

Wapendwa wana wa Mungu, kuongozwa na msukumo huo katika maisha ni sawa na kuhangaika kuibomoa nyumba ya jirani yake ilhali wewe mwenyewe hauna nyumba ya kuishi huku ukitegemea hifadhi kwa jirani yako huyo. Ni kuishi katika falsafa ya “sote tukose!” “Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa,” Hek 2:19. Wapo wengi miongoni mwetu hujisikia furaha wakati wenzao wanateseka. Hii siyo hekima ya Mungu hata kidogo. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki,” Yak 3:17. Mimi ninayeishi leo na kesho yanipasa kujua ukweli huu kwamba dunia hii si mahali pangu kwa kudumu. Nipo katika ulimwengu huu kama sehemu ya maandalizi yangu ya maisha ya umilele. Kwa hiyo hatma yangu ya umilele inategemea sana ninavyoishi leo, yaani, mahusiano yangu na Mungu, wenzangu, na mazingira ninayoyaishi. Ni kuishi katika ukweli huu nikijua kwamba, tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani,” Yak 3:18.

Wapendwa wana wa Mungu, tusipoitafuta Amani katika haki hata yale tuyaombayo Mungu hawezi akatupa kwa sababu hayatatufaidia sisi na wenzetu. Tutakuwa tunaomba kwa ajili ya faida yetu binafsi kwa gharama za wengine. Mungu aliye Haki, Upendo, Msamaha, na Amani hawezi kuruhusu jambo hilo hata kidogo. Mungu atakacho kupa wewe hakiwezi kuwa madhara kwa mwingine kwa sababu kila mmoja wetu yupo hapa duniani kwa sababu yake mwenyewe Mungu, na amemuumba kwa sura na mfano wake. Hivyo tunapomwendea Mungu katika hali hii hawezi tutupatia kile tumwombacho. Kwa sababu hiyo, hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yah 4:3.

Ndugu yangu uliyefika jumapili hii ya leo elewa kwamba nafasi yako na hadhi yako mbele ya Mungu haijengwi kwa wingi wa ufahamu wa ulimwengu huu aliouumba Mungu, bali kwa kujinyenyekesha mbele zake ili yeye Mungu abaki kuwa mwalimu wako maisha yako yote. Tendo hili la kujishusha halimaanishi tusijifunze na kutoka kwenye wimbi la ujinga, bali kujifunza kwetu siyo mwisho wa ukweli ule tunaoufahamu na ambao Mungu angependa kutufunulia kadiri ya mapenzi yake. Kwa maana, “kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, wote wafanyao hayo wana akili njema, sifa zake zakaa milele.” Zab 111:10. Hivyo hakuna namna yo yote kwa mwanadamu kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu kusiko kujisalimisha kwake kwa Mungu. Kujisalimisha kwa Mungu ndiyo njia pekee ya kufunuliwa neema na baraka za Mungu. Hivyo Yesu anawaambia Tenashara wake, akisema, “mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35

 Wale wote wenye kumcha Bwana katika uelewa huu, Yesu anawafananisha na watoto wachanga. Kumcha Bwana huku ni kuwa tayari kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu pasipo shaka yoyote. Mtoto humwamini mzazi wake kupita vitu vyote. Hivyo Yesu anawaambia wanafunzi wake, mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma,” Mk 9:37. Ndugu yangu, ukuu wetu upo katika unyenyekevu wetu na kuwa tayari kutumika kwa ajili ya manufaa ya wengi.

Andrea na Yosefu walikuwa marafiki na wafanya biashara. Hata hivyo hawakufanikiwa sana katika biashara zao licha ya kwamba walionekana kufanya bidii sana katika biashara zao. Ndugu hawa walikuwa ni watu wa sala na hivyo kila siku walipenda kusali misa ya asubuhi na baadaye kuwahi kwenye biashara zao.

Andrea na Yosefu walikuwa na maduka  ya kuuza bidhaa mbalimbali, yaliyokuwa yakiongozana katika mtaa wa changamkeni katika mji wao. Mungu baada ya kuona taabu zao na maombi yao kila siku ya misa za asubuhi, alimtuma malaika Gabrieli kwenda kwa Andrea na kumuuliza swali hili: “Omba cho chote kile utakacho Mungu atakupa kitu hicho, ila mwanzako, yaani, Josefu Mungu atampa mara mbili zaidi.”

Baada ya kupata ujumbe huu mzito, Andrea alimjibu Malaika Gabrieli na kumwambia, “nipe siku tatu za kufikiri nami nitakupa jibu.” Siku tatu zilikwenda, na malaika akamjia Andrea na kumwambia, “Je, umepata jibu?” Andrea akamjibu, “naomba niwe chongo.”

Wapendwa wana wa Mungu, Andrea alitafakari sana na kujiuliza kiasi cho chote cha pesa angalikiomba mwenzake Josefu angepata mara mbili zaidi. Hivyo kwa kuongozwa na chuki, aliamua kuomba awe chongo ili mwenzake awe kipofu, na kushindwa kuona kabisa.

Hivi ndivyo maombi yetu yalivyo. Mungu hawezi kamwe kutufungulia baraka na neema kwa mtindo huu.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NIJALIE MOYO SAFI. AMINA

No hay comentarios:

Publicar un comentario