ALHAMISI YA WIKI YA 25 YA MWAKA-B
24/9/2015
Somo: Hag
1:1-8
Zab:
149:1-6, 9
Injili:
Lk 9:7-9
Nukuu:
“Ndipo
neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye
mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?” Hag 1:3-4
“Basi
sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu,” Hag 1:5
“Mmepanda
mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini
hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye
apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka,” Hag
1:6
“Pandeni
milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa,
asema Bwana,” Hag 1:8
“Lakini Herode
akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya
juu yake? Akataka kumwona,” Lk 9:9
TAFAKARI: “Natuzitafakari njia zenu asema Bwana wa Majeshi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, mafanikio ya mtu katika nyanja zote zile hayatofautiani sana na utaratibu mzima wa
maisha ya mtu. Mfano; afya njema ya mwili wa mtu hutegemea sana chakula
anachokula. Ukitaka kujua ufahamu wa mtu kiakili na kitaalumu, tazama mambo
anayoyasoma. Ukitaka kujua hofu ya Mungu ya mtu, tazama uhusiano wake na Mungu,
uhusiano wake na watu, na uhusiano wake na mazingira yanayomzunguka. Ni ukweli
usiotia shaka kwamba hatuwezi kutoa kile tusichokuwa nacho. Hivyo basi, kitu
cho chote afanyacho mwanadamu ni msukumo wa kitu fulani kilichokwishwa kuwepo
kutokana na mpangilio mzima wa maisha yake. Binadamu aweza kuwa cho chote kile
kwa sababu kaumbwa na kuwezeshwa “kuwa-potential” na mwenyezi Mungu. Hivyo
basi, tunapokuwa nje ya ukweli huu niliouelezea kwa kifupi, yatupasa kuzifakari
vyema njia zetu ikiwa ndilo agizo la Bwana wetu wa Majeshi.
Jamii
yoyote ile na hasa inayoongozwa na mambo ya kiroho, mafanikio yao na kudondoka
kwao hutokana na kutokuzingatia kwa undani mahusiano yao kimwili na kiroho.
Kujua mahusiano haya bayana ni kuweka vipaumbele vyako wazi katika maisha
unayoishi. Wengi wetu kutambua jambo hili tunasaidiwa sana na mafungo ya mara
kwa mara. Vipauambele vyetu ndiyo dira inayoongoza maisha yetu. Kwa mantiki
hii, Wayahudi walikuwa na vipauambele vitatu, ambavyo kwayo vilileta karibu
uhusiano wao na Mungu. Kipauambele namba moja ni uwepo wa Hekalu ambapo
waliweza kumsifu Mungu, kumwabudu Mungu, na kumtolea sadaka na shukruni. Hivyo
popote pale walipokuwa, iwe huru au utumwani, uwepo wa Hekalu uliwaunganisha na
Muumba wao.
Kipauambele
namba mbili ni ardhi. Hapa waliweza kupata mahitaji yao ya mwili, na mwisho wa
siku kumtolea Mungu sadaka zao za kuteketeza kama shukrani kubwa kwa Mungu.
Uwepo wa ardhi na umuhimu wake tunaweza kuuona hata leo katika migogoro mingi
kati ya Taifa hili la kiyahudi-Isreaeli, na majirani zake.
Kipauambele
namba tatu ni uongozi imara utakao simamia haki na kweli kwa kila raia wake
wote. Tunaona jambo hili pale wayahudi walipomwomba Mungu kupitia Nabii Samweli
wawe na Mfalme kama yalivyokuwa mataifa mengine yaliyowazunguka. Hivyo Mungu
anawapa angalisho na mwisho anawapatia Mfalme Sauli. “Bwana akamwambia Samweli,
Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana
hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. Basi
sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya
mfalme atakayewamiliki. Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na
desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa
wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.” ISam 8:7, 9, 11.
Mfululizo wa mstari wa 12 hadi ule wa 18 unaelezea desturi ya mfalme huyo na
ukatili wake. Ila sikio la kufa halisikii dawa. Wana wa Israeli kwa kiburi chao
wakamjibu Nabii Samweli na kusema, “sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme
juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue,
tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu.” 1 Sam 8:19-20.
Wapendwa
wana wa Mungu, mambo hayo matatu yalikuwa muhimu sana kwa wana wa Israeli.
Ukweli huu, na hasa kipaumbele cha kwanza kinajionyesha katika somo letu la leo
kutoka kitabu cha Nabii Haggai 1:1-8. “Ndipo
neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye
mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?” Hag 1:3-4. Ni
kweli kabisa mara baada ya kutoka utumwani au uhamisho wa Babeli mwaka 520
Kabla ya Kristo, wana wa Israeli walijisahau katika wajibu wao huu mkubwa wa
kulijenga Hekalu la Mungu. Haggai Nabii anaanzisha kipindi cha mwisho cha
unabii katika Israeli. Wana wa Israeli wanajikuta kutokusonga mbele
kimaendeleo, mwili na roho kwa kutokulitenda jambo hili muhimu. Nabii Haggai
anawapa sababu ya mkwamo wao na kusema, “Mmepanda
mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini
hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye
apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka,” Hag
1:6. Ndugu yangu unaye safiri nami katika tafakari hii ulishawahi kuzitafakari
njia zako katika mikwamo yako kimaisha? Wengi wetu tusipokaa na pesa ingawa
tunafanya kazi na kulipwa mishahara hufikiria tumewekewa kitu kinachoitwa
“kichuma pesa.” Wengine hata kila tunapolima hatupati mazao yenye tija kabisa.
Je, umejiuliza vyema utoaji wako wa zaka? Wengi wetu tunachofanya ni kumwibia
Mungu kila wakati.
Wapendwa wana wa Mungu, Zaka yako ni kama ifuatavyo: Zaka ya fungu la kumi ni mujibu wa mwenye ardhi na mashamba,
na hata waajiriwa katika mtazamo wa kileo. “Usiache kutoa zaka ya
fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya
mwaka,” kumb,
14:22. Ni lazima kumtolea Mungu zaka hiyo, kwa sababu yeye ni Bwana wa ardhi yote
ya Nchi Takatifu. Ni wajibu kutoa zaka
hiyo kwa mazao yote ya ardhi na kuyapeleka patakatifu. Huko ndiko kumcha Mungu
kuliko kwa kweli na haki. “Nawe utakula mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua
apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na
wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng'ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza
kumcha Bwana, Mungu wako, daima,” Kumb 14:23.
Kila mwaka wa tatu zaka hiyo inachukuliwa na fukara. Hiyo ni
sheria ya kitabu cha tano cha Musa. (Hes 18:21-32) inatazama fungu la kumi kama
kodi ya kuwalipia Walawi. Nao
Walawi walilazimishwa kutoa fungu la
kumi la kodi hiyo kwa makuhani kama sadaka ya kuinuliwa kwao kwa Bwana.
Iliwapasa pia kulipa fungu la kumi la mifugo. Tena zaka yote ya
nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni
takatifu kwa Bwana. “Na kama mtu akitaka
kukomboa cho chote cha zaka yake, ataongeza sehemu yake ya tano juu yake. Tena zaka yote ya ng'ombe, au ya
kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa
Bwana,” Law 27:30-32. Fedha nazo
zinaruhusiwa kutolewa badala ya sadaka yenyewe. “Ndipo uzibadili ziwe fedha, na kufunga zile fedha uende nazo
mkononi mwako, hata mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako. Na kama mtu akitaka
kukomboa cho chote cha zaka yake, ataongeza sehemu yake ya tano juu yake,” Kumb
14:25, Law 27:31
Mwisho kabisa, katika kutafakari njia zetu yatupasa kuhoji
ukaribu wetu na Mwana wa Mungu. Herode anaingiwa na hofu baada ya kusikia
habari za Yesu kwa sababu alifikiri baada ya kumwangamiza Yohane Mbatizaji kwa
kumkata kichwa siku ya sherehe ya kuzaliwa kwake-Herode, angeendelea
kuisalimisha dhamiri yake mbaya katika uovu. Herode anataka kumwona Yesu si kwa
sababu anataka kuanzisha uhusiano mzuri naye, bali bila shaka kutafuta namna ya
kumwangamiza ili asiwe tishio kwake. Hivyo anawajibu wale waliomletea habari
juu ya Yesu na kusema, “Yohana nilimkata kichwa;
basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona,” Lk
9:9. Tukitaka kuwa na amani ya kweli ndani yetu lazima tupatanishwe na Kristo.
“Huyu manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata
ondoleo la dhambi,” Mdo 10:43.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Pandeni milimani,
mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema
Bwana,” Hag 1:8
No hay comentarios:
Publicar un comentario