jueves, 31 de marzo de 2016

TAFAKARI: IJUMAA YA OKTAVA YA PASAKA

IJUMAA YA OKTAVA YA PASAKA
Somo: Mdo 4:1-12
Zab: 118:1-2, 4, 22-24, 25-27a
Injili: Yoh 21:1-14 
Nukuu:
Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni,” Mdo 4:3

Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya,” Mdo 4:7

 “Jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu,” Mdo 4:10

Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 12 

Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu,” Yoh 21:3

Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La,” Yoh 21:5

Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki,” Yoh 21:6

Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana,” Yoh 21:7

“Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini,” Yoh 21:7b

Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka,” Yoh 21:11

TAFAKARI: “Litupeni jarife  upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata.”

Wapendwa wa Mungu, Tumsifuni Yesu Kristo kwa wingi wa neema na baraka zake anazotujalia kila siku tunapo tafakari neno lake. Wapendwa leo kwa namna ya pekee tuyatafakari naneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo, “Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata.” Neno hili Yesu anawaambia wanafunzi wake ambao wameshinda usiku kucha wakivua samaki, na kutoka wakavu kabisa. Neno hili la Yesu Kristo limejaa neema na maarifa, limejaa upyaisho na mwelekeo mpya, limejaa nguvu na matumaini, limejaa uthaminishwaji katika kutenda vyema tena. Sababu kubwa na neno hili ni UPANDE WA KUUME liliko elekezwa lile JARIFE. Ni upande walioheri na salama. Ni upande wenye baraka.

Neno hili ndiyo siri kubwa ya uinjilishaji wa kina, chini ya msukumo wa Roho Mtakatifu wa Kanisa la jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Roho huyu Mtakatifu, ndiye kichocheo kikubwa cha ushupafu waliokuwa nao Mitume, licha ya kuhujumiwa mara kwa mara kwa sababu la JINA LlLE KUU LA BWANA WETU YESU KRISTO MNAZARETI. Mitume baada ya ufufuko wa Kristo, walisongwa sana, kwa sababu tu walishuhudia ufufuko wa Kristo. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni,” Mdo 4:3. Misukosuko hii tunayoiona leo katika zama zetu, inakishindo kikuu sana. Leo, Wakristo wengi uharabuni, Iran, na baadhi ya nchi za Afrika kama Nigeria, Somalia, Sudani ya Kaskazini, Tanzania Visiwani yetu ya leo; wanateswa na hata kuuwawa kwa sababu tu wao ni Wakristo.

Pamoja na hali hiyo, Mtume Petro kama kiongozi hakusita kusema iliyo kweli mbele ya macho ya hawa wahujumu wa Kanisa la Kristo. Wanapohojiwa ni kwa mamlaka gani wanafundisha kuhusu JINA LILE-YESU KRISTO, na Imani hiyo, Mitume hawasiti kusimama kwa lililo kweli. Petro bila kupepesa macho anasema,Jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu,” Mdo 4:10. Kiongozi wa dini leo ambaye anapenda kupata sifa na kupendwa na wote, na hasa wanasiasa ambao kwao rushwa ni sifa ya utumishi bora, hakika mbele ya JINA HILI, kiongozi huyu atakuwa na swali kubwa la kujibu.

Petro kama walivyokuwa Mitume wengine hawakuwa na elimu ya ajabu sana zaidi ya stadi za kupambana na maisha ya kila siku. Petro Mtume kama walivyo wengine katika kundi hili la Mitume, walikuwa wavuvi. Watu hawa kwa mang’amuzi yao ya maisha, ilikuwa ni jambo la ajabu kutoa elimu hii ya wokovu juu ya siri ile kubwa ya Ufalme wa Mungu na Uzima wa milele kwa wale waliokuwa wamebobea kwenye uwanja huo kama Waandishi, Mafarisayo na Masadukayo. Jambo hili linatupa ukweli wa nguvu na mwongozo wa Roho Mtakatifu kwa Kanisa hili la Mwanzo. Leo, tunamwitaji sana huyu Roho Mtakatifu katika Kanisa, na siyo majina na vyeo visivyokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maisha yetu ya Imani na ya Kiroho. Wapendwa huu ndio ukweli kwamba, Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 12.

Tunapojaribu kuchenga ukweli huu, tunakuwa nje ya kweli mzima ya mafundisho ya Kristo na lengo zima la umilele wa maisha haya tunayoyaishi. Mara kwa mara kunakuwa na vishawisha vya kurudi nyuma na kufanya yale tuliyoyazoea. Hata Mitume hawakuweza kukwepa hali hiyo, kwani maisha yao na ukuuaji wao wa Imani ulilandana sana na maisha na mazingira yao. Hivyo Mtume Simon Petro anawaambia wenzake, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu,” Yoh 21:3.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapokuwa nje ya mpango mzima wa Mungu, na hasa kwa wale tuliopewa thamana hiyo, mafanikio ya yale tuyatamaniyo huwa hewa na kutoweka kabisa. Kumhubiri Kristo na kumshuhudia kwa maneno na matendo ni kazi ya kila  aliyebatizwa na kuimarishwa. Hivyo basi, yatupasa kulifanya tendo hilo pasipo shaka. Kristo hachoki tukumbusha tunapokengeuka kuhusu ukweli huu. Kristo aweza kutumia njia mbalimbali kuwakilisha ujumbe wa kweli hii. Kwa upendo wake, Kristo mara zote anapenda kujua mahangaiko yetu, na kuturudisha katika mstari. Katika hali ya kuchoka na uchovu mwingi kwa kupigika usiku kucha bila kupata samaki, anawaambia wanafunzi wake, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La,” Yoh 21:5. Kwa maana nyingine Yesu anataka kutuambia, Je, mnapozifuata njia zenu na kuacha maagizo yangu mnapata mafanikio?

Kuonyesha ukweli wa jambo hili, Yesu Kristo, anawafundisha njia na maagizo yake yaliyo kweli na sahihi kwa uzima wa mwili na roho. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki,” Yoh 21:6.

Wapendwa katika Kristo, yawezekana ushapigana sana na maisha kiasi kwamba kila siku ni aheri ya jana. Jambo la kwanza usitafuta mchawi wala kwenda kwa waganga, au kusafisha nyota kama tunavyosikia wengi wakidanganywa. Jambo la kwanza chunguza uhusiano wako na Mungu. Je, umelitupa jarife hilo upande wa kuume wa chombo chako yaani, maisha yake? Je, unaisha kadiri ya matakwa ya Mungu? Kama hapana, Je, unaridhika na hali hiyo? Kama siyo, Je, ni kitu gani kinachokukwamisha kurejesha uhusiano huo? Kama uhusiano wako na Mungu ni mzuri na bado unapigika sana na maisha, jambo hilo unalichukuliaje? Je, walichukulia kama kusahauliwa na Mungu, au kutokutendewa haki na Mungu? Je, unaelewaje subura ya Mungu kwa yale uyaombayo na kuyatamani?

Ndugu yangu, hakuna jambo lolote tuombalo Mungu aache kutupatia. Kama itatokea kwa hapa duniani hatukulipata basi jua umeandaliwa jambo hilo kwa umilele wake, mara baada ya maisha haya ya hapa duniani. Kamwe Mungu hamtupi mja wake. Kwa wale ambao Mungu ametukirimia zaidi na hata kupita mahitaji yetu, tunachukuliaje jambo hilo? Je, tunamtambua Mungu katika mali na utajiri wetu? Ukweli ni kwamba kamwe hatutaweza mtambua Mungu kwa yale tuliyonayo, kama hatuna upendo na Mungu. Yohane Mtume anamtambua Kristo kwa sababu alikuwa na upendo wa dhati kwa Kristo na Kristo alikuwa anampenda kwa namna ya pekee. Na hivi ndiyo Injili inavyotuambia, Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana,” Yoh 21:7.

Kumtambua huku Kristo, Yohani habaki na hali hiyo mwenyewe. Anamwambia na Petro pia. Je, tunapoguswa na upendo wa Kristo na Mungu tupo tayari kuushirikisha kwa wenzetu nao wapate wokovu huo? Tunaona baada ya Petro Mtume, kusikia habari hiyo, anajitosa kwenye maji maana alikuwa uchi. “Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini,” Yoh 21:7b. Mpendwa tunayesafari wote katika tafakari hii, Petro kuwa uchi hapa kunamaanisha kwa upande mwingine kwamba anatambua kujikwaa kwake kunakotokana na kutokuyafanya yale aliyopaswa kufanywa kama kiongozi, kama niliyoeleza hapo mwanzo.

Mara baada ya Petro kujitambua, anaingia chomboni na hapa tunaona maajabu haya. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka,” Yoh 21:11. Ndugu yangu, jarife hili halina tofauti na Kanisa kama chombo cha wokovu ambacho kazi yake kubwa ni kuwavuta watu kwa Kristo na kuwapeleka kwake wakiwa salama. Usalamu huu ni idadi inayotolewa ya samaki hawa. Tutajulikana kwa idadi yetu mbele za Mwanakondoo. Nasi tukifika mbele ya uso wa Mungu tutajulikana kwa idadi, na wale tuliopewa kazi hiyo yatupasa tutoe hesaba ya idadi tulioifikisha mbele ya Mungu na Mwanakondo.

Hata hivyo tunasikia jarife hili-Mtego huu, haukupasuka licha ya wingi wa samaki wale. Jibu ni kwamba mtego haukupasuka kwa sababu u imara. Mtego, yaani Jarife kama Kanisa, na Sakramenti ya wokovu wetu, uimara wake unatokana na uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu, ambaye uyaratibisha yote kadiri ya mahitaji ya Kanisa lake kwa nyakati zote. Tumruhusu Roho Mtakatifu huyu afanye kazi yake, na siyo Roho Mtakavitu. Roho Mtakavitu atalipasua JARIFE-KANISA. Roho Mtakavitu huyu ni: SIFA, CHEO, KUJULIKANA KULIKO BINAFSI, MAMLAKA MBELE ZA WATU, NA MBAYA ZAIDI KWA VIONGOZI WALA RUSHWA. Tusichoke kuhubiri na kuishi kwa vitendo Huruma ya Mungu kwa sababu hata hawa viongozi wala rushwa,  wote wasio na hofu ya Mungu ndani yao, na sisi sote kwa ujumla wetu kama Kanisa na wabatizwa tunahitaji huruma hiyo na wokovu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 12


Ee Yesu na Mwokozi wetu, tujalie mara zote kuutafuta uso wako wa Huruma ili tuufikie uzima ule wa milele uliyotuhaidia. Amina

miércoles, 30 de marzo de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI YA OKTAVA YA PASAKA

ALHAMISI YA OKTAVA YA PASAKA
Somo: Mdo 3:11-26
Zab: 8: 2ab, 5, 6-7, 8-9
Injili: Lk 24:35-48 
Nukuu:
Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu,” Mdo 3:19-21

Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi,” Mdo 3:13-15

Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Lk 24:36 

Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo,” Lk 24:39

Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:46-48 

TAFAKARI: “Amani iwe kwenu; ni Salamu, Zawadi na Mtazamo mapya wa maisha ya Ufufuo na Uzima.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, maisha ya ufufuko ni maisha ya amani ya kweli ndani ya kila mmoja wetu anayeamini ufufuko wa Kristo. Ni kwa maana hii leo tunaalikwa kutafakari neno hili, “amani iwe kwenu; ni Salamu, Zawadi, na Mtazamo mpya wa maisha ya Ufufuo na Uzima. Amani kama maisha ya ufufuo na uzima yanajionyesha na kutendeka wazi katika jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Mtume Petro haogopi kulisema hili mbele ya Wayahudi wenye itikadi kali za kidini na hasa juu ya Yesu Kristo waliyeutoa uhai wake bila huruma. Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi,” Mdo 3:13-15

Wapendwa kwa kosa hili la kumwua Mkuu wa uzima, kurejesha huruma na msamaha wa Mungu, yatupasa kufanya toba ya kweli. Neema na baraka huja kwa kukiri pale tulipojikwaa kwa kujua na hata kwa kutokujua, kunakotokana hasa na kutotimiza wajibu wetu wa kila siku. Toba ya kweli ndicho kielelezo cha kujenga tena urafiki na uhusiano na Mungu ambao ulibomolewa kwa dhambi zetu, na tunazidi kuubomoa kwa dhambi zetu hata sasa. Daraja la kuelekea upatanisho huo na Mungu, limekwisha jengwa tayari kwa sadaka ya Kristo pale msalabani. Naye Petro anasema, Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu,” Mdo 3:19-21

Wapendwa wana wa Mungu, kwa sasa twaweza kuuona uso wa Mungu kwa kupitia kwanaye Yesu Kristo. Hivyo kupatanishwa na Mungu kunawezekana tu kwa kupitia mwanaye Yesu Kristo ambaye hata sasa Kanisa linamshuhudia. Kanisa kama chombo katika safari ya kuelekea uzima wa milele, na Sakramenti ya Wokovu, kinatuwezesha kwa kupitia maadhimisho ya Masakramenti yake kuuona uso wa Mungu baada ya kushiriki Masakramenti haya kwa uaminifu wa kweli. Ndugu yangu, leo tunapatanishwa na Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo, kwa Sakramenti ya kitubio. Na hapa kwa namna ya pekee tunaonja upya huruma na neema ya Mungu. Je, lini ilikuwa mara yako ya mwisho kupokea sakramenti hii?

Injili ya leo inatuelekeza kuyaona maisha ya Uzima na Ufufuo kupitia Amani ya kweli ndani mwetu. Zawadi ya Yesu Mfufuka kwa wanafunzi wake na wale wote waliomridhia ni Amani. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Lk 24:36. Baada ya tukio hili, amani inakuwa ndicho kielelezo cha maisha ya Uzima na Ufufuo. Hakika Mungu hapatikani katika fujo na machafuko yanayosababishwa na tamaa na ubinafsi wetu. Uhakikisho huu, yaani, Amani ndani ya mioyo ya Wakristo wa kwanza unaondoa woga na mashaka yote. Kristo yu hai kweli kweli na siyo hadithi za kufikirika. Yesu Kristo anawaambia wanafunzi wake walikuwa wamejificha wa hofu, “Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo,” Lk 24:39

Hili ni hakikisho la wazi kwamba Yesu Kristo hakuwa mzimu fulani katika hali yake ya kufufuka kwake. Hivyo kuthibitisha kwamba yeye si mzimu, alikula pia kipande cha samaki wa kuoka kuwahakikishia alikuwa mtu kweli baada ya ufufuko wake. Mtazamo huu, ndio matazamo wa Kanisa leo, licha ya changamoto nyingi tunazozipata nje ya Imani yetu ya Kikristo ambao kwao wanataka kutulazimisha na kutufanya tuamini kwamba kilichotokea kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kilikuwa ni mchezo wa kuingiza. Kwa mantiki hiii, Kristo Mfufuka anasisitiza kwa kusema, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:46-48. Ndugu yangu uliyeimarishwa, wewe ni shahidi kweli wa Kristo?

Wapendwa katika Kristo, hapana shaka kabisa kwa sasa wengi wetu tunaishi kwa hofu kubwa sana tunapoona Wakristo wenzetu wanauwawa kwa ukatili uliokithiri kwa sababu tu wao ni Wakristo. Hata hivyo tusisahau ukweli kwamba hata Kanisa hili tunaloishi leo na kushuhudia imani, limekuwa Imara kama lilivyo kutokana na Damu za wafia dini waliotutangulia kwa nyakati tofauti katika historia ya Kanisa letu. Bila shaka ni wakati wetu pia kutoa ushuhuda huo kwa kufa kifo Dini na Imani ya kweli.

Tumsifu Yesu Kristo!

Yesu Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:46-48

Ee Yesu Kristo, katika hali hii ya sintofahamu juu ya Imani na Ukristo wetu leo, tujalie neema ya kufa kifo dini katika Imani ya kweli. Amina


martes, 29 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMATANO YA OKTAVA YA PASAKA

JUMATANO YA OKTAVA YA PASAKA
Somo: Mdo 3:1-10
Zab: 105:1-2, 3-4, 6-7, 8-9
Injili: Lk 24:13-35
Nukuu:                           
Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:4-6

“Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu,” Mdo 3:7

Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao,” Lk 24:15

Macho yao yakafumbwa wasimtambue,” Lk 24:16

“Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli,” Lk 24:19-21

Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?” Lk 24:25-26

Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha,” Lk 24:29

TAFAKARI: “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha; Ndiyo mkao wa Kipasaka, yaani, Ufufuo na Uzima”

Wapendwa wana wa Mungu, ni wakati mwingine tena tunapa fursa ya kuyatafakari Makuu ya Mungu. Kwa namna ya pekee na tulitafakari neno hili, “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha; ndiyo mkao wetu wa Kipasaka, yaani, Ufufuo na Uzima.” Mkao wa Kipasaka-Ufufuo na Uzima tunauona katika somo letu la leo, ikiwa ndiyo shabaha kubwa ya jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Hamu na uhitaji wa kukaa na Kristo Mfufuka, unajitokeza katika Injili yetu ya leo, pale wanafunzi wa Yesu waliokuwa wakielekea Kijiji cha Emau kumtaka akae nao kwani kumekwisha kuchwa, na mchana unakwisha.

Mkao huu wa Kipasaka-Ufufuo na Uzima ndiyo nguvu la Kanisa la Kristo. Mitume hawana cha kutoa zaidi NEEMA na BARAKA za Kristo Mfufuka. Mkao huu unabadilisha tabia na mazoea yetu katika maisha. Kristo anapokuwa kila kitu katika maisha yetu, hubadili maisha yetu na kuwa maisha ya uhai na uzima. Ni katika hali hii tunaopolewa kutoka kwenye kiza na kuingizwa katika mwanga. Tunatolewa katika makaburi yetu na kupelekwa kwenye mwanga na uzima. Tunatolewa katika kufa kufa kwetu kunakotokana na magonjwa na mahangaiko ya maisha na kupelekwa kwenye uzima na faraja.

Ni kwa sababu hii Mtume Petro na Yohana wanamtoa Bwana yule ombaomba katika mlangoni katika kuchoka kwake, na kumwingiza katika uzima na furaha ya kweli. Jambo hili linafanyika ndani na katika jina la Yesu. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:4-6

Yesu anapokuwa maisha yako ya kila siku unatiwa nguvu na kuondolewa kupooza kwako. Jambo hili hufanyika na uwezekana tu pale unapokubali kuongozwa na kushikwa mkono na Yesu. “Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu,” Mdo 3:7. Hapa ndipo tunapoanza maisha mapya tunapokubali kuongozwa na Kristo Mfufuka.

Injili yetu ya leo inatupa umuhimu wa kukaa muda wote na Kristo Mfufuka. Maisha yetu yanapita kwa kasi sana kama moshi, na wakati mwingine tunaishi tukiwa wakavu sana kiroho. Yesu Kristo kwa walio wengi ni Yesu wa Historia. Kwa walio wengi Yesu huyu hana nguvu tena. Tatizo kubwa tunalokutana nalo katika maisha ni kuyaweka matamanio yetu mbele zaidi ya mafundisho na kweli anayotufundisha Kristo. Sintofahamu hii inawakuta wanafunzi wale ambao wanaona Kifo cha Kristo kama tukio la kudanganywa hivi, na hakuna maana kabisa kwa yule ambaye walimtegemea sana na leo anawaangusha. Kifo hiki cha aibu cha msalaba kwa wanafunzi hawa kimewatoa matumaini yote.

Yesu Kristo hata katika sintofahamu hizi, bado yupo tayari kutusikiliza na kuzidi kutufundisha, licha ya kwamba hatumuoni kwa kuificha taswira yake, ili mradi tu tumpe nafasi. “Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli,” Lk 24:19-21.

Yesu hachoki kutukumbusha yaliyompasa kufanya na yaliyotabiriwa juu yake. Haya yote yapo katika Maandiko Matakatifu. Mt. Jerome anasema hivi kuhusu Yesu Kristo, “tunapokuwa wajinga wa maandiko matakatifu, ni kwa namna hiyo hiyo tu wajinga kuhusu Yesu Kristo.” Kuhusu jambo hili Yesu anatupa sababu ya yale yote yaliyojiri kuhusu Kifo na Ufufuko wake. Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?” Lk 24:25-26. Ndugu yangu hapa tunakumbushwa pia, kwamba hakuna Utukufu pasipo Msalaba. Penye Msalaba pana Utukufu, na sasa ni rahisi kuupata Utukufu kwa sababa Kristo kesha ushinda Msalaba.

Wapendwa, Kristo anajifunua kwetu leo katika kuumega mkate. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao,” Lk 24:30-31. Kuumega mkate kunatanguliwa na kulishwa neno lake na kulielewa. Tukio la wanafunzi wa Yesu kukutana naye njiani kuelekea Kijiji cha Emau, ni mtiririko mzima wa adhimisho la Misa Takatifu. Adhimisho hili lina sehemu kuu mbili; Liturjia ya neno na liturjia ya Ekaristi Takatifu. Kwa mantiki hii, uwezekano wa Kristo kujifunua kwetu wakati wa Ekaristi Takatifu, unabebwa kwanza na ufahamu wetu wa kulisikiliza neno lake, kulipokea, kulitafakari, kulishirikisha, na kuliishi. Wanafunzi hawa wa Yesu wanakuwa na hamu ya kukaa naye zaidi baada ya kulishwa neno na Kristo ingawa hawakumfahamu.

Ndugu zangu, wale ambao wamezoea kuchelewa na mara nyingine kushiriki tu liturjia ya Ekaristi Takatifu, ni wavamizi wa Mlo Mtakatifu wasioujua vizuri. Ni sawa na kukishambulia chakula kitamu na kizuri wakati ukiwa na mikono michafu. Ni vizuri kuhudhuria sehemu zote mbili za kiliturjia na ndivyo inavyotakiwa kwa Mkristo na hasa kwetu, ambao Ekaristi Takatifu kicho kiini cha yote. Wapo kati yetu ambao huingia Kanisani na moja kwa moja kujongea Meza ya Bwana. Huu ni uhuni wa hali ya juu kufanywa na Mkristo. Mwisho na muhimu tusichoke kuudhuria mara kwa mara maadhimisho ya Maabudu ya Yesu wa Ekaristo-Sakramenti Kuu. Hapa anakaa kwetu na kujifunua kwetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:6


Ee Yesu, Bwana wangu na Mungu wangu, kaa nasi Bwana nyakati zote za maisha yetu hapa nduniani ili tuweze pia kufika kwako mbinguni. Amina

lunes, 28 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMANNE YA OKTAVA YA PASAKA

JUMANNE YA OKTAVA YA PASAKA
Somo: Mdo 2:36-41
Zab: 33:4-5, 18-19, 20, 22
Njili: Yoh 20:11-18
Nukuu:
Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38

Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie,”  Mdo 2: 39 

Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi,” Mdo 2:40

Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa,” Yoh 20:15

Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu),” Yoh 20:16

Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu,” Yoh 20:17 

TAFAKARI: “Kwa Ufufuko wa Yesu Kristo sote twahesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli; Naam, sote kwa upendo wa Mungu twaitwa wana wake na yeye ni Mungu wetu.”

Wapendwa wana Mungu, tendo la ufufufuko wa Bwana Wetu Yesut Kristo, linatuwezesha na linakuwa neema na baraka kwetu, hasa ule uwezo wa kupokea vipawa vya Roho Mtakatifu pale tu tunapofanya toba ya kweli. Ni kwa dhambi zetu imekua sababu ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, na ni kwa kupitia toba ya kweli kwa dhambi zetu twapokea neema na baraka, na kuhesabiwa tena haki kuwa warithi na wana wa Mungu. Ni kwa sababu hii, leo kwa namna ya pekee tutafakari juu ya neno hili, “Kwa Ufufuko wa Yesu Kristo sote twahesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli; Naam, sote kwa upendo wa Mungu twaitwa wana wake na yeye ni Mungu wetu.”

Mtume Petro, kwa kujaliwa ujasiri na nguvu ya Kristo Mfufuka, haoni haya kuwaambia Wayahudi ukweli kuhusu wokovu wao baada ya kufanya kosa la kumwua mwenye haki-Yesu Kristo. Hata sasa Mtume Petro ananiambia mimi na wewe ambao twahitaji huruma na neema ya Mungu. Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38. Ndugu yangu, ni kwa jina la Yesu Kristo tu twaweza kupata msamaha wa dhambi, na kupatanishwa tena na Mungu Baba. Na ni kwa njia ya ubatizo tunafia dhambi na kuzaliwa wapya kama ishara halisi ya Ufufuko wa Yesu Kristo. “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu alisiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:13-15. Ili tufaidi neema za Ufufuko wa Bwana Yesu Kristo, ikiwa pamoja na vipawa vya Roho Mtakatifu, yatupasa kufanya toba ya kweli, ikiambatana na kuzaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Toba ya kweli ni kutambua kule kujikwaa kwetu, na kuyaacha maanguko hayo, huku tukifuata njia iliyo sahihi. Yesu Kristo pasipo shaka yeyote, ndiye njia sahihi ya kufuata, kwani kwa Ufufuko wake, yaliyo ya kale, na yasasa, na yajayo yamekwisha eleweka. Tuendako sasa twakujua. Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu,” Yoh 20:17. Ili tupate mastahili ya kumshika Kristo Mfufuka, yatupasa kufanya toba ya kweli kama nilivyokwisha kusema. Yesu anamwambia Mariamu na kumbumbusha toba ya kweli. Huu ni wito wa kujitakasa kwa yale mambo yanayotukwamisha kuiona sura ya Mungu. Mastahili yetu baada ya kuhesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli, ni maisha ya utakatifu.

Maisha mapya baada ya Ufufuko, ni maisha ya Utakatifu kwa wote wanaoridhia njia ya Kristo. Kuridhia njia hii ni kufanya toba ya kweli. Tendo hili la toba ya kweli ndani na katika Kristo, linatupa mastahili sawa bila kujali historia zetu mbaya, makabila yetu, na hata utaifa wetu. Tendo hili linatupa uhalali wa kuwa wana wa Mungu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie,”  Mdo 2: 39. Tendo hili ni upendeleo mkubwa sana kwetu, na upendo wa Mungu wa ajabu. Je, watambua jambo hilo? Je, wayajua mapungufu yako? Je, waona umuhimu wa kupatanishwa na Mungu Baba kupitia ushindi wa Mwanae dhidi ya uovu na dhambi?

Njia na namna yetu ya kuishi baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo inatusukuma kuishi upya katika kutenda na kunena. Ni maisha ya ushuhuda wa kweli. Kwa maana hii, Mtume Petro anasema, “Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi,” Mdo 2:40. Leo tunaisha katika kizazi chenye ukaidi uliokithiri. Leo walio wengi siyo kwamba tu hawaamini, ila pia hawaoni umaana wa maisha yenye uhusiano na Mungu. Wengi wamefiki hatua ya kuona historia nzima ya wokovu wetu kama hadithi za kufikirika tu. Tupo kwenye wakati wa “ponda mali kifo chaja.” Kwa mtu yeyote na hasa kiongozi akikosa hofu ya Mungu ndani yake, maisha na utu wa binadamu hauna tofauti na bidhaa rahisi na isiyodumu kuwahi kutokea. Leo tunashuhudia mauaji ya wazi na kikatili kuwahi kutokea.

Jambo muhumu la kujiuliza katika maisha yako, “unatafuta nini, na kwa sababu gani?” Mariamu anamtafuta Yesu Kristo kaburini akiwa analia, ili hali Yesu Kristo keshafufuka. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa,” Yoh 20:15. Mariamu bado yupo kwenye fikra za umauti wa Yesu.

Ndugu yangu, Mariamu mara baada ya kumtambua Kristo, anaanza maisha mapya. Yesu anakuwa mwalimu wa maisha mapya. Mariamu analisema jambo hili toka ndani ya moyo wake. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu),” Yoh 20:16. Mwalimu ndiye ajuaye yale tunayotaka kujifunza. Mwalimu ndiye ajuaye siri ya kile tunachotaka kukijua. Mwalimu hutuongoza, kutuelekeza, na kutuonyesha kuona kile anachokiona yeye ambacho ndiyo makusudia ya yale tunayojifunza.

Ndugu yangu, hatuwezi kuona na kujua siri ya maisha ya umilele, bila kuwa na Mwalimu wetu Yesu Kristo. Tutaona yale ayaonayo Kristo endapo tu tanamwamini. Yesu anasema, “mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35. Kupata neema na baraka yatupasa kumwamini Kristo. Naye anasema, “aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji hai itatoka ndani yake,” Yoh 7:38. Kuishi maisha ya ufufuo na uzima yatupasa kumwamini Kristo. Naye anatupa hakikisho hilo kwa kusema, “mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi,” Yoh 11:25. Kumwamini Yesu Kristo ni kumwamini Mungu Baba aliyempeleka na kumwamuru kuyafanya yote. “Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka,” Yoh 12:44. Tunapomwamini Kristo, tunafunuliwa makusudi yake hapa duniani na kufanywa kila mara kuishi katika nuru yake. “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46. Na mwisho tunaweza kujua na kuzifanya kazi alizozifanya Kristo endapo tunamwamini. “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12. Ndugu yangu, Yesu ni nani kwako? Je, unayoimani thabiti kwa hayo unayoishi ndani na katika Kristo?

Tumsifu Yesu Kristo!

Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38


Ee Yesu, tuwezeshe kufanya toba ya kweli. Amina

domingo, 27 de marzo de 2016

TAFAKARI: JUMATATU YA OKTAVA YA PASAKA

JUMATATU YA OKTAVA YA PASAKA
Somo: Mdo 2:14, 22-32
Zab: 16:1-2a, 5, 7-8, 9-10, 11
Injili: Mt 28:8-15
Nukuu:
“Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,” Mdo 2:32

“Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt 28:10

“Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala,” Mt 28:12-13 

TAFAKARI: “Kuishi imani ya kweli”

Wapendwa wana wa Mungu, tukiwa katika oktava ya pasaka, yaani siku nane za Pasaka, kwa leo tutafakari neno hili, “kuishi imani ya kweli.” Moja ya kweli kwamba Kristo amefufuka na yu hai, ni ujasiri wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo kuishi kwa matendo na kumuhubiri Kristo mfufuka bila shaka na wasiwasi wowote. Jumuiya hii ya kwanza wapo tayari kwa lolote limuhusuyo Kristo Mfufuka. “Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,” Mdo 2:32. Ushupavu huu ni kutokana na kuguswa na kuishi uhasilia wa Ufufuko wa Kristo. Hapana shaka kwamba Kristo amefufuka na yu hai katika maisha yetu na hali zetu kila siku.

Uthibitisho huu wa imani huondoa hofu yote kwani tegemeo kubwa lishajionyesha katika maisha ya kila siku. Kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu analiweka jambo hili wazi kwa wale waliomfia na kumtumainia, “Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt 28:10.

Ndugu yangu, galilaya yako ni pale unapoishi maisha ya kila siku. Kama mtu wa ndoa, uaminifu wako katika Sakramenti hiyo ni makutano ya Kristo mfufuka na ndiyo Galilaya yako. Kama wewe ni mtawa kama mimi, maisha haya ndiyo ninapokutana na Kristo mfufuka pale ninapoisha nadhiri zangu kwa uaminifu kadiri ya mwongozo wa mwanzilishi wetu na mtazamo wa Kanisa. Nje ya hapo ni kupoteza muda tu. Ni katika hali hii naweza kukutana na Yesu Mfufuka. Hakuna mbadala wake. Ndugu yangu tuheshimu na kuzijali ndoa na maagano yetu na nadhiri zetu katika maisha. Mateso na mahangaiko katika wito wako ni ishara ya wazi kwamba unachokitaka na kukitafuta kina gharama, thamani, na baraka mbele ya uso  wa Mungu. Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kinatufundisha kwamba hakuna UTUKUFU PASIPO MSALABA.

Ukweli huu kuhusu ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo walijaribu kuupotosha lakini hawakuweza. “Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala,” Mt 28:12-13. Ndugu yangu, huwezi kuzuiya upepe kwa mikono yako. Nguvu na kweli ya Mungu hii juu ya maarifa yetu yote. Hivyo usipo jikabidhi kwa Kristo utajikabidhi kwa shetani. Uchaguzi huu upo chini ya uwezo wako. Njia sahihi na ya kweli ni kujisalimisha mikoni mwa Kristo ambaye ameyashinda yote.

Ndugu yangu, hakuna maisha ya usalama kama hujikabidhi kila siku mikoni mwa KRISTO. Huyu ndiye ajuaye yaliyo kabla na mwisho wa nyakati zetu. Kujikabidhi mikoni mwake kunaitaji utayari wetu tu. Utayari huu ni kufanya mapenzi yake kila siku ya maisha yetu. Ukaribu wetu na Kristo ni kuyafanya mapenzi ya Baba yake aliye Mbinguni. Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu,” Mt 12:50.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,” Mdo 2:32


Ee Yesu Mwema, niongoze katika kuyafanya mapenzi yako na Baba aliye Mbinguni. Amina