miércoles, 30 de septiembre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 26 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 26 YA MWAKA-B
1/10/2015
Somo: Neh 8:1-12
Zab: 18:8-11
Injili: Lk 10:1-12
Nukuu:
“Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati,” Neh 8:9

“Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu,” Neh 8:10 

Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Lk 10:2

Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii,” Lk 10:7

Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia,” Lk 10:8-9

TAFAKARI: “Furaha na Amani ya kweli tunapojitoa bila kujibakiza ndani na katika Kristo Yesu kuuishi na kuuhubiri Ufalme wa Mungu.”

Wapendwa katika Kristo, neno furaha au amani la weza kuwa na maana tofauti tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine. Ni kweli pia kati yetu tunamwelekeo wa kuona furaha yetu au amani yetu hutokana na “vitu.” Tulivyonavyo. Hivyo vitu fulani katika maisha vinakuwa vigezo vya furaha na amani ya mtu. Kabla ya kuzama katika tafakari hii ni vyema tuyatafakari maswali matatu ya Mhubiri.
Swali la kwanza la muhubiri kuhusu “faida” anauliza kama ifuatavyo, “Mtu ana faida gani ya kazi yake yote aifanyayo chini ya jua?” Ndugu yangu yawezekana kabisa kazi yako ikawa sababu ya furaha na amani yako. Ni kweli kwamba sana unafanya kazi na una nguvu za kufanya hivyo. Je, nguvu hizo zikikuishia na uzee ukakunyemelea, kazi yako itaendelea kuwa sababu ya furaha na amani yako? Tafakari sana jambo hili ndugu yangu.

Mhubiri anaendelea kuuliza swali yake la pili na kusema, Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo?” Mhu 3:9. Yawezekana furaha na amani yako imejikita katika shughuli zako za kila siku kama vile biashara, maswala ya siasa, ufundishaji, uimbaji, na tume mbalimbali kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake. Je, hiyo tu ndiyo sababu ya furaha na amani yako? Je, utadumu katika shughuli hiyo kwa muda gani? Umejaribu kujiuliza mwisho wa shughuli hiyo utakuwaje? Je, utahimili ushindani wa shughuli hiyo daima? Bila shaka furaha na amani katika swali hili la Mhubiri ipo hatiani.

Mhubiri anatuuliza swali la tatu kuhusu faida na kusema, Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au Maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai?” Mhu 6:8. Wapendwa, mwenye hekima ni yule mwenye uwezo wa kuona ukweli na uhalisia wa jambo kama ulivyo. Pili ni yule ambaye kwa kupitia mang’amuzi ya maisha yake anakuwa tayari kuyatafutia suluhisho matatizo anayokumbana nayo na hasa jamii ile anamoishi. Katika mwono huu, mtu mwenye hekima huweza kuzisoma alama za nyakati za wakati wake na kuona mbali zaidi kule anapoelekea licha ya kwamba bado hajaishi hali hiyo. Je, mtu mwenye hekima kwa kuyajua hayo yote ndiyo msingi wa furaha na amani yake?

Mtu mpumbavu ni yule ajifanyaye mwelewa kumbe si mwelewa katika uhasilia wa mambo kama yalivyo. Ni mtu yule anayeshupalia ujinga kwa kiwango cha juu. Je, msimamo huu kimaisha ndiyo sababu ya furaha yako? Na siku basi utakapotambua ukweli kama ulivyo ndiyo itakuwa mwisho wa furaha na amani yako? Masikini ni ye yote yule mwenye uhitaji. Kama sote ni wahitaji, basi sote ni maskini wa viwango tofauti. Mbele ya walio hai ni wale wote wanaoishi katika umilele. Hawa ni watakatifu wa Mungu. Bila shaka hawa wana furaha na amani ya kweli kwa sababu wanamwona Mungu kama alivyo na wanaishi si tena katika imani na matumaini, bali katika umilele wa upendo wa Mungu. “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13.

Wapendwa wana wa Mungu, Mhubiri natupatia jibu la maswali hayo matatu na kusema, Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua,” Mhu 2:11. Je, kama hakuna faida yo yote chini ya jua, furaha na amani yangu ya kweli naipata wapi? Yesu anatuambia jambo hili wazi, “kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Ndugu yangu unayesafiri nami kati tafakari hii, furaha ya kweli tunaipata pale tunapokuwa watu wa kiasi, yaani kuishi kwa uchache. Jambo hili tunaliona katika mfano ule wa talanta. “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako,” Mt 25:23. Furaha ya kweli tunaipata pale tunaposhiriki mateso yetu kikamilifu na Kristo. Ni pale tunapoisha kweli na haki bila kumwonea aibu Kristo. Ni pale tunapotesaka kwa ajili ya Kristo na hasa kuwa sauti za wasiokuwa na sauti katika jamii dhalimu na ovu. Yesu anasema hivi, “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22.

Wapendwa wana wa Mungu, amani ya kweli ni ile tuipewayo na Kristo mwenyewe, yaani tunapokuwa ndani na katika yeye. Amani hiyo siyo ile tuipewayo na ulimwengu huu. Tukiwa ndani na katika Kristo hatuwezi kuishi katika mifadhaiko wala woga. Yesu anatuambia, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,” Yoh 14:27. Na tunaipata amani hii tunapotenda kadiri anavyotufundisha Kristo. Kuyatenda yale yampendezayo Mungu siyo yale yafaidishayo nafsi na mwili tu. “Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17. Kuna faida kubwa kuteswa kwa kutenda mapenzi ya Mungu kuliko kutenda mabaya. “Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya,” 1Pet 3:17.

Hivyo wapendwa wana wa Mungu furaha yetu na amani yetu ya kweli ni kutenda kadiri ya Mungu apendavyo, na kufanya hivyo bila kujibakiza. Tunapoikubali hali hii tuwe tayari kupokea mateso na kadhia zote ndani na katika Kristo. Hatuna sababu ya kuendelea kuomboleza na kusikitika kama tunaye Mungu ndani yetu. Wana wa Israeli walipoipokea torati haikuwapasa tena kuendelea kuomboleza na kufia masikitiko yao. Nabii Nehemia anawaambia Waisraeli, “Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati,” Neh 8:9. Kama kweli ninayo imani na neno la Mungu, na Kristo aliyekufa kwa ajili yangu, sina sababu ya kuwa na mashaka wala hofu juu ya maisha yangu na Kristo.

Wapendwa katika Kristo, furaha ya Bwana ni nguvu yetu. Tunapojazwa amani na furaha ya Bwana ndani yetu hakuna cho chote tutakachofanya bila kufanikiwa. Maisha yetu yatakuwa yanaongozwa kwa malengo ya Mungu mwenyewe. Hivyo Nabii Nehemia anawaambia watu wake kwamba, “Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu,” Neh 8:10. Je, ni nani atakaye kuwa na nguvu juu yetu kama Mungu yu upande wetu? Hivyo mimi na wewe ni sababu tosha ya kuuleta ujumbe wa amani na furaha ya Mungu kwa watu. Na pale ambapo haipo furaha na amani hiyo, yatupasa kuiomba kwa Mungu, naye atatoa kadiri ya mahitaji yetu. Kama jumuiya ya wenye hofu ya Mungu, Yesu anatualika kuliomba hili kadiri ya maitaji ya kanisa lake, na kusema, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Lk 10:2. Hili ni jukumu la kila mbatizwa.

Kufikia lengo la kuutangaza ufalme wa Mbinguni kwa wengine, sisi tuliopata habari hii ya wokovu yatupasa kulisimamia jambo hilo kwa weledi mkubwa, kwa kuwa waaminifu kwalo, na kuushikila ukweli huu bila kutetereka. Yesu anatutaka kuwa makini sana huko tuendako kuupeleka ujumbe wa wokovu. Naye anasema, Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii,” Lk 10:7. Na lifanyike jambo moja kwa wakati. Hii ni pamoja na kuwa makini kwa jambo lile lile tu. Tusibebe ajenda nyingi katika safari hii ya uinjilishaji. Mambo hayo {mfuko, mkoba, viatu na wala kuwaamkie mtu njiani} tukiambatana nayo yatatuchanganya na kutufanya tupoteze mwelekeo. Tuambatane na kubeba yale tu tunayohitaji kwa utume huo. Tusipokuwa na uchache wa vitu furaha na amani ya kweli hutoweka. Tusiuzunike pale ambapo tunaona mambo hayakwenda kama tulivyotarajia. Kufanya hivyo ni kupoteza muda bure kwani muda hautungoji hata kidogo.

Katika jambo hili Yesu anasema, “Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia,” Lk 10:10-11. Jambo la msingi la kuzingatia ni kufanya yale tu tuliyotarajia kuyafanya na kuwa na mahusiano mazuri na wale tuliokusudia kuwainjilisha neno la Mungu. Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia,” Lk 10:8-9. Tuyafanyapo haya kwa unyenyekevu bila kujibakiza huwa msingi wa furaha na Amani yetu.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUFANYE VYOMBO VYA FURAHA NA AMANI YAKO. AMINA

martes, 29 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 26 YA MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 26 YA MWAKA-B
30/9/2015
Somo: Neh 2:1-8
Zab: 136:1-6
Injili: Lk 9:57-62
Nukuu:
Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga,” Neh 2:5 

Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58

Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu,” Lk 9:60  

Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62

TAFAKARI: “Ni heri ukawa baridi au joto kuliko kuwa vuguvugu katika Imani.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, Imani ya mtu husema yote kuhusu maisha ya mtu. Imani siyo kitu tunwezacho kukiona kwa macho yetu ya nyama, na kukipima ukubwa na upana wake, bali Imani huonekana katika maisha mazima ya mtu ikiwa ni pamoja na changamoto zinazobeba maisha hayo ya kila siku. Nathubutu kusema kwamba sisi tulio wengi kama Wakristo na Wakatoliki kwa kiasi kikubwa tu wakristo wa majina tu, na wakati mwingine wakristo wa jumapili. Tunafika mahali na kumfanya Mungu wetu kama kituo cha msalaba mwekundu. Tunamwitaji Mungu pale tu tunapobanwa na matatizo. Hata katika hali ya matatizo tunajitoa kwake kwa masharti fulani.

Wapendwa katika Kristo, masomo yetu ya leo yanagusia kwa kiasi kikubwa nini maana ya imani na kuishi imani hiyo. Yapo mambo makuu manne tunayoweza kujifunza kuhusu Imani kutoka kwenye masomo yetu ya leo. Kwanza kabisa Imani ya kweli siyo kuwa waaminifu kwa tamaduni zetu kwa vile tu zilishikiliwa vizuri na wazee wetu kiupofu. Wakati mwingine mila zetu na desturi ni mkusanyiko wa viaminika kimazoea ambavyo mwisho wa siku havina uhalisia na uhusiano wo wote na hali halisi ya ukweli huo. Mazingira kama haya wakati mwingine yanakufanya kuwajibika kulipopita kiasi pasipo kujielewa. Mwisho wa siku tunakuwa watumwa na siyo huru tena. Hali hii tunaiona katika somo la kwanza. Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga,” Neh 2:5. Tunaona jinsi gani mtu huyu anavyokuwa na shauku ya kuujenga mji wa makaburi.

Lakini tukumbuke kwamba mara baada ya kufufuka Yesu, malaika wanawapa ujumbe muhimu wanawake wale waliokwenda kaburini na kumkosa Yesu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia,” Mt 28:5-7. Hivyo ndugu zangu Imani yetu leo inatuelekeza kuwa, Yesu huyu aliye shauku yetu tunakutana naye Galilaya na siyo kaburini. Galilaya yako ni hapo ulipo kadiri ya wito na utume wake. Ishi vyema hapo ulipo na timiza yote na hasa yale madogo madogo kwa upendo na unyenyekevu mkubwa. Hapo utakutana na Yesu. 

Jambo la pili tunalofundishwa leo kuhusu Imani, ni namna tunavyochukulia ufuasi wetu. Je, ninakiri kumfuata Yesu popote atakapo kuwa kama upepo na bendera? Je, katika ufuasi huo natambua mapaswa yake? Je, nipo imara na nitakuwa imara katika nyakati zote na hasa zile nyakati za sintofahamu? Yesu anampa angalisho mtu yule aliyekutana naye njiani na kusema yupo tayari kufuatana naye ko kote atakapokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58. Kwa maneno mengine Yesu anatuambia hakuna maslahi yo yote kibinadamu zaidi ya maisha ya umilele kutoka kwake. Kama ni swala la utajiri na kuwa na maisha mazuri siyo kipaumbele katika ufuasi wetu kwake. “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:9. Kazi yetu ya kwanza ni kuutafuta kwanza ufalme wa mbinguni na mengine yote tutapewa kwa ziada.

Jambo la tatu tunalofundishwa leo kuhusu Imani ya kweli ni utambuzi wa kweli na kujua nafasi ya Mungu katika maisha yako. Bila shaka hakuna asiyekuwa na hofu ya kifo. Ila kifo kipo tupende au tusipende. Na kama umezaliwa basi ipo siku utakufa. Kwa hiyo katika uhalisia wa kifo hatupaswi kukiogopa. Yatupasa kuishinda hofu ili tuwe tayari kukipokea kifo kama njia pekee ya kuishi umilele tunaojiandaa leo hapa duniani. Hakutakuwa na maisha baada ya umilele baadaye bila kupita katika fumbo hili la kifo. Hivyo Yesu anamtoa hofu ndugu yule aliyetoa hoja ya kwenda kwanza kumzika Baba yake ndipo amfuate. Naye Yesu anamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu,” Lk 9:60. Je, Yesu anatukataza kuwazika wazazi wetu? La hasha! Kufanya hivyo atakuwa anaenda kinyumbe na ile amri ya nne ya Mungu, “waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12. Yesu anachotaka kutuambia ni kwamba kifo ni ukweli usiopingika na hivyo shughuli zake zisiwe sababu ya kutokupokea ujumbe wake wa uzima wa milele.

Na jambo la nne na la mwisho tunalofundishwa leo kuhusu Imani ni kule kuwa na msimamo thabiti wa wito tulio nao na kile tulichoitiwa. Hii ni pamoja na kutokuwa na kigeugeu na kutazama nyumba tulipotoka kwa malengo ya kujaribu tena. Wengi wetu baada ya kubatizwa tumerudi kuishi maisha ya kipagani kabida. Wengi wamekuwa washirikina wa kupindukia na kuongozwa na nguvu za giza ili hali tumejivika visakramenti mwili mzima. Katika hili Yesu anatupa angalisho, na kusema, “Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62. Kwa maneno mengine ni heri kuwa baridi au joto, kuliko kuwa vuguvugu katika Imani.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUPE NGUVU YA KUINUKA PALE TUNAPODONDOKA. AMINA

lunes, 28 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-B: Sikukuu ya Malaika Wakuu

JUMANNE WIKI YA 26 YA MWAKA-B
Sikukuu ya Malaika Wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli
29/9/2015
Somo: Dan 7:9-10, 13-14
Zab: 137:1-8
Injili: Yoh 1:47-51
Nukuu:
Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14

Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya,” Yoh 1:50

Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu,” Yoh 1:51

TAFAKARI: “Naye atayatenda yote kadiri ya mahitaji yetu. Tumwamini daima.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anasheherekea sikukuu ya Malaika wa Kuu; Mikaeli, Gabrieli, na Rafaeli. Hawa malaika wakuu wanatambulika hivyo kutokana na kazi zao na jumbe zao walizokuwa wakiziwakilisha kwa watu mbalimbali kutoka kwa Mungu. Tafsiri ya majina yao imebeba ujumbe na maana ya kile walicho. Malaika Mkuu Mikaeli, kutoka Kiebrania inamaanisha “Nani ni sawa na Mungu?” Ni malaika alikingaye Taifa la Mungu. Jina hili linamaanisha pia “zawadi kutoka kwa Mungu.” Kazi yake na namna alivyotumika tunaweza rejea sehemu hizi katika Maandika Matakatifu {Dan 10:21; 12:1, Kut 23:20, Yud 9, Ufu 7:12}.

Malaika Mkuu Gabrieli kwa Kiebrania inamaanisha “Bingwa au Mshindi wa Mungu.” Ni mpeleka ujumbe maalum kwa watu kutoka kwa Mungu. Tunaona Malaika huyu Mkuu akimsaidia Nabii Danieli kutafsiri ndoto {Dan 8:16; 9:21}. Gabrieli anapeleka pia ujumbe kwa Zakaria kuhusu kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji {Lk 1:19}. Tunaona vile vile Malaika huyu Gabrieli akimfikishia ujumbe Bikira Maria kuzaliwa kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo {Lk 1:26}. Malaika Mkuu Rafaeli, kwa Kiebrania, “Aliyeponywa na Mungu. Vile vie ilimaanisha mlinzi wa geti la hekalu kwenye agano la kale.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapotazama kazi za malaika hawa tunaona ni kwa namna gani Mungu amewatumia katika historia nzima wa wokovu wetu. Kanisa pasipo shaka leo linasheherekea kwa kutambua nafasi na kazi zao kwa wokovu wa Mwanadamu. Ni kweli kwamba malaika humzunguka Mungu pale alipo na kuwa tayari kufanya yale atakayo Mungu. Lakini leo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Padre ambaye ni Kristo mwingine, amepewa mamlaka na uwezo wa kumshusha Mungu kwa watu anaowahudumia kupitia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hivyo kwa kupitia Mwanaye Yesu Kristo, Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14.

Ndugu zangu katika Kristo, tunapomwamini Kristo na kukaa katika njia, kweli na uzima wake, tunashirikishwa makubwa zaidi ambayo hatukuwahi kuyaona. Yesu anamwambia Nathanaeli ukweli huu, “Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya,” Yoh 1:50. Kristo akiwa ndiyo Jana yetu, Leo yetu, na Umilele wetu, anayafahamu yote kwa sababu kwa kupita yeye yote yalifanyika, Yoh 1:3. Kwa uwezo huu aliokuwanao Yesu, anawaambia wanafunzi wake na sisi pia kwamba, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu,” Yoh 1:51. Yatupasa kusadiki yote haya naye Mungu kupitia mwanaye Mpendwa Yesu Kristo atayatenda maishani mwetu kadiri ya mahitaji yetu.

Tumsifu Yesu Kristo!


MALAIKA WAKUU WA MUNGU MTUOMBEE. AMINA

domingo, 27 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 26 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 26 YA MWAKA-B
28/9/2015
Somo: Zek 1:1-8
Zab: 101:16-23, 29
Injili: Lk 9:46-50
Nukuu:
Bwana amewakasirikia sana baba zenu,” Zek 1:2

Basi, uwaambie, Bwana wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema Bwana wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi,” Zek 1:3

akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa,” Lk 9:48 

Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu,” Lk 9:50

TAFAKARI: “Wakati ndiyo sasa.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna mtihani mgumu kwa mwanadamu kama kufanya maamuzi ya kina kuhusu mwelekeo mzima wa maisha yake. Mara zote binadamu amekuwa na uhakika wa jana kuliko kesho ambayo bado kufikika. Ila ukweli ni kwamba hatuwezi kuwa na kesho nzuri kama hatuna leo nzuri. Hivyo kama jana haikuwa nzuri basi itakulazimu ufanye maamuzi mazuri na ya kina leo ili kesho yako iwe nzuri. Wakati ndio sasa! Kama sijui cho chote kuhusu uhai wangu dakika chache kuanzia sasa, hivyo muda ninaoishi sasa ni muhimu sana kufanya maamuzi ya kina kwa kile ambacho kipo chini ya uwezi wangu kwa maisha yangu na vizazi vijavyo.

Mungu aliye UPENDO na kwenye kututakia MEMA daima, anakuwa sababu ya kuwafanya Waisraeli wafanye maamuzi ya kina kuhusu maisha yao na vizazi vijavyo anapowaambia kupitia Nabii Zekaria akisema, Bwana amewakasirikia sana baba zenu,” Zek 1:2. Ndugu yangu, sababu ya kufanya maamuzi hayo ni pale tunapokuwa nje ya mpango mzima wa maisha yetu na mahusiano yetu na Mungu. Hivyo wito wa Mungu kwetu ni kumrudia na kuwa na hofu hiyo ya Kimungu. Zekaria Nabii anawaambia ujumbe huu wa Mungu kwa wana wa Israeli, “Bwana wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema Bwana wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi,” Zek 1:3. Hakuna njia nyingine ya kuwa karibu na Mungu kama hautajisalimisha kwake. Kujisalimisha kuliko kweli ni tendo la Ibada. Tendo hili la Ibada linajulikana kama ‘kuabudu.’ Tunapofanya maabudu tunajisalimisha kwa Mungu, na kwa namna hiyo tunamrudia Mungu naye anaturudia kwa kutuneemesha upendo wake.

Wapendwa wana wa Mungu, tendo zima la kujisalimisha na kutupeleka katika maabudu kama Ibada, linatualika kwa namna ya pekee kujishusha na kujinyenyekeza mbele ya kile kilicho kikuu zaidi na chenye kusema yote kuhusu uhai wetu. Tunajinyenyekesha chini ya Mamlaka ya Mungu si kwa unyonge, bali ndiyo njia pekee ya kuwa kile tulicho na mpango wa Mungu. Kujishusha na kujinyenyekeza ndiko tunapokufanya kuwa binadamu halisi kadiri ya mpango wa Mungu na lengo la uumbaji wako. Huku ndiko kujipokea kama ulivyo. Kujipokea kama ulivyo ndiyo njia pekee ya kuanza kufanya mabadiliko ya kina kuhusu maisha yako. Mabadiliko yote yale lazima yaanze sehemu fulani. Hivyo mabadiliko ya kimwili na kiroho kumwelekea Mungu wetu, huanza pale tu tunapojipokea kama tulivyo, yaani, kujishusha, na kujinyenyekeza mbele yake aliye uhai, uzima, na umilele wetu.

Bila kufahamu ukweli huu, tunaona katika somo la injili njinsi ambavyo wanafunzi wa Yesu wakibishana njiani kuhusu ‘nani aliyemkubwa kati yao.’ Kutafuta ukubwa na ukuu bila kujua mapaswa na matakwa yake, ni chanzo kikubwa sana cha kwenda kinyume na mpango wa Mungu na watu wake. Yesu baada ya kutambua ukweli huu ndani ya mioyo ya wanafunzi wake, anawapa angalisho ya kile wanachokitamani. Naye Yesu anawaambia wanafunzi wake kwa mfano, “Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa,” Lk 9:48. Udogo anauongelea Yesu ni ule utayari wa kujifunza, kumtegemea Mungu pasipo shaka kama afanyavyo mtoto kwa mzazi wake, kujishusha na kujinyenyekeza hasa tutoapo huduma kwa wengine pasipo kujiinua binafsi zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, ye yote atakaye fanya tendo lo lote la upendo, matumaini, na imani hata kama si mmoja katika mtazamo wa kundi unaloishi na jumuiya unayoshirikiana nayo, mtu huyo hayupo kinyume cha matamanio ya Mungu kwetu. Jambo hili Yesu analiweka sawa anapopata taarifa ya wanafunzi wake walipomkataza mtu mmoja kutenda lililojema eti kwa vile tu hakuwa mmoja wao. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu,” Lk 9:50. Kuwa kinyume na mpango wa Mungu ni pamoja na kule kutojisalimisha kwa mtu huyo katika mpango mzima wa wokovu wa Mungu. Ni pale pia tunajiinua nafsi zetu na kusahau hatma ya maisha yetu. Ni pale pia kwa uhakika tunapojitanguliza mbele zaidi na kusahau usalama wetu upo chini na jemedari wetu Mkuu Yesu Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU NASI TUNAKUBALI KUWA WAKATI NDIYO SASA. AMINA

sábado, 26 de septiembre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 26 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 26 YA MWAKA-B
27/9/2015
Somo I: Hes 11:25-29
Zab: 18:8, 10, 12-14
Somo II: Yak 5:1-6
Injili: Mk 9:38-43, 45, 47-48
Nukuu:
Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze,” Hes 11:28

Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake,” Hes 11:29 

Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi,” Mk 9:38

Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu,” Mk 9:39-40

Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini,” Mk 9:42

Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika,” Mk 9:43

Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum,” Mk 9:45

Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum,” Mk 9:47

Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho,” Yak 5:3

Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo,” Yak 5:5

TAFAKARI:Na tuwe wafadhili sisi kwa sisi, tuone mazuri kwa wenzetu na vipaji vyao, tuwe wenye huruma, tukisameheana kama na Mungu katika Kristo alivyotusamehe sisi.”

Wapendwa wana wa Mungu, karibuni katika tafakari yetu ya leo. Leo Mama Kanisa katika dominika hii ya 26 ya mwaka “B,” anatualika tutafakari kwa undani mahusiano yetu na wenzetu hasa akitutaka tuyaone mazuri kwa wenzetu ikiwa ni pamoja na vipaji na karama zao, tuwe wafadhili sisi kwa sisi, tuwe wenye huruma, na tusameheane kama na Mungu katika Kristo alivyotusamehe sisi.

Mara nyingi kwa wasioongozwa na hofu ya Mungu ni vigumu kuona mazuri kutoka kwa wengine. Ni katika mazingira haya tunapozungumzia swala zima la mtu kuwa na wivu. Wivu kama wivu siyo kitu kibaya. Wivu ikiwa ni tokeo la nafsi kutawaliwa na hisia, ni kama kioo cha kujitazama na kujiona vizuri mara baada ya kuona utofauti wa kweli kati yako na wenzako na mazingira yanayokuzunguka. Hivyo tendo hilo huweza kukuongoza kuliko kwema na haki, kujipima uwezo wako, na fursa zote zinazokuzunguka ikiwa ni kiashirio cha kufanya vizuri zaidi endapo nafsi hivyo itaegemea roho. Wivu katika maana hii utuelekeza katika maendeleo. Na huu ndio wivu wa maendeleo. Wivu huwa shahuku ya kufanya vizuri zaidi bila kumdhuru mwenzako kwa hali yoyote ile, na mazingira yanayokuzunguka unapoyachukulia kama fursa ya kufika pale mazuri na pema zaidi.

Ni hatari sana wivu unapotupeleka katika hali ya chuki na hasira kwa wengine na mazingira yanayotuzunguka. Wivu huu ni tokea la nafsi inapoegemea mwili na matendo yake. Tatizo kubwa hapa ni pale tunaposhindwa kujipokea kama tulivyo na kuanza hapo tulipo kuzonga mbele. Hata kama chumba hakina mwanga haitoshi kulalamika tu kwa ukweli huo bila kufanya cho chote kadiri ya mazingira uliyonayo kama fursa pekee. Kama hakuna umeme basi uwashe angalao mshumaa. Na kama hakuna mshumaa washa basi hata kijinga cha moto. Na kama hakuna mshumaa na kijinga cha moto, fungua basi hata madirisha uweze kunufaika na mwanga wa mbalamwezi kutoka nje.

Wivu wa kubomoa, yaani unaoongozwa na chuki na hasiri kwa vile tu mwenzangu anafanya vizuri kuliko mimi, ni hatari sana kwani hali hiyo itakudumaza mwili, akili, na roho. Somo letu la kwanza kutoka kitabu cha hesabu, na Injili yanaongelea vizuri sana kuhusu wivu na athari zake. Kila mmoja wetu amejaliwa kwa namna ya pekee vipawa mbalimbali. Tatizo letu kubwa ni pale tunapopoteza muda mwingi kunakili vipaji vya wengine na kuacha kuendeleza vile alivyotupatia Mungu. Tunapenda sana kuwa vivuli vya wengine. Hakika kwa hali hii lazima uwe tayari kudumaa mwili, akili, na roho. Tunaona katika somo la kwanza kwamba Mungu mwenye uwezo wote, na mwenye kumpa kila mmoja wetu kadiri apendavyo, anashuka na kutoa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa na kuwapa watu wengine kwa muda fulani tu kadiri alivyoona inampendeza. Hata baada ya muda huo kwisha, walionekana watu wawili hemani, Eldadi na Medadi wakiwa bado wana upako wa kutabiri. Jambo hili linakuwa chukizo kwa Yoshua, na anamkaripia Musa kwa kusema, “Ee bwana wangu Musa, uwakataze,” Hes 11:28. Musa kwa kuelewa sisi sote katika umoja na  utofauti wetu ndio uzuri wa Mungu, anamjibu Yoshua na kumwambia, “Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake,” Hes 11:29. Ndugu yangu kwa nini basi mara kwa mara unajisikia vibaya mwenzako anavyofanya vizuri?

Wapendwa wana wa Mungu, tunaona tukio kama hili kwenye somo la injili. Tunaona Yohana anamkataza mtu mmoja aliyekemea pepo kwa kutumia jina la Yesu. Wakati mwingine tunapoongozwa na roho ya wivu hujikuta tunajihesabia haki pasipo haki yo yote. Naye anamwambia Yesu, “Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi,” Mk 9:38. Yohana anapotoa taarifa hii mbele ya Yesu, anakutana na karipio zito kutoka kwa Yesu. Yesu anajibu na kuwaambia, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu,” Mk 9:39-40. Hapa Yesu anatufundisha uzuri wa umoja wetu katika utofauti wetu kama wana wa Mungu. Hivyo yatupasa kutakiana mema na hasa kutambua vipaji vya wenzetu kwa ajili ya manufaa ya wote. Huu ndio utendaji wa Mungu. Hivyo tunawaswa kujihadhari sana na ile dhambi ya kuwakwaza wengine wafanyapo mema. Hivyo Yesu anasema, Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini,” Mk 9:42. Kufungiwa jiwa shingoni na kutupwa haharini kulimaanisha kwamba kwa kosa hilo la kukwaza ilitosha kutokuonekana katika sura ya dunia na hata masalia ya mwili wako. Tunajua wazi kwamba mtu akifa maji huzama na mwisho wa siku mwili wake uelea juu. Kwa kufungiwa jiwe shingoni kusinge ufanya mwili uelee juu ya maji.

Wapendwa wana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo anaenda mbali zaidi akigusia dhambi zile ambazo huwa vichocheo vya kuwa na wivu na kuzama zaidi katika dhambi. Hivyo ili tuwe mikono salama yatupasa kuachana na mizizi hiyo ya dhambi. Hivyo kama mkono wako ndio sababu ya kuikosa mbingi afadhali usiwe na mkono huo. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika,” Mk 9:43. Mkono hapa unaweza kutafsiriwa kama ukarimu wetu kwa wenzetu. Hivyo uchoyo ukiwa ndio sababu ya kukosa mbingu ni fadhali kuachana na tabia hiyo. Tuwe wakarimu kwa watu wote bila kubaguana.

Na endapo mguu wako unakuwa sababu yakutokuiona mbingu ni aheri kutokuwa na mguu huu. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum,” Mk 9:45. Kwa kutumia miguu yetu twaweza kuwafikia watu na kuhubiri habari njema kwao. Hivyo tendo hili twaweza kuwa wawakilishi wazuri wa Kristo kama wamisionari. Vile vile kwa miguu yetu twaweza kuwa waenezaji wabaya sana wa habari mbaya kama umbea na hivyo kule machafuko na kutokuelewana katika jamii. Kama hili linajitokeza twatupasa kuwa makini sana. Yatupasa kuwa chombo cha amani ya Bwana kama asemavyo Mt. Franscisko wa Assis.

Ndugu yangu, na endapo jicho lako litakuwa sababu ya kutokuurithi ufalme wa mbinguni, ni aheri ukawa chongo. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum,” Mk 9:47. Kupitia jito tunaona na kutamani. Kupitia jicho tunaona na kuongoka. Kupitia jicho tunaona na kumtukuza Mungu kwa uzuri wa uumbaji wake. Lakini jicho lako likiwa sababu ya wivu na chuku kwa wengine, basi jicho hilo halikufai. Jicho hili litusaidie kuona mahangaiko na shida za watu wengine pia. Hatupaswi kufumba macho tunapoona haki za watu zinakanyagwa.

Mtume Yakoba katika somo letu la pili anaongelea sana kuhusu kutokutaabikiana sisi kwa sisi. Ni vyema kuona uhalisia wa maisha ya watu na kuwapa kadiri ya mapato yao alisi na staha zao za kazi. Matajiri wengi na watu wenye uwezo hawachoki kuwanyonya wanyonge. Wanyonge hutumikishwa kazi ngumu na kwa muda mrefu na mwisho wa siku wanalipwa kidogo sana na kisichoweza kukidhi mahitaji yao halisi. Hivyo Yakobo anawapa onyo matajiri na makabaila, Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho,” Yak 5:3. Utajiri wo wote ule unaotokana na dhuluma hakika ni laana kubwa sana kwa Mungu. Katika mazingira ya kawaida, watetezi wa wanyonge ni viongozi wale tuliowapa dhamana katika uongozi. Lakini kitu cha kushangaza ni pale tunapoona viongozi wakijinufaisha wenyewe na kuwadhulumu wanyonge wakiungana na matajiri na makabaila ndani na nje ya nchi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo,” Yak 5:5. Je, leo katika Taifa letu wanyonge wana heri yo yote? Je, nina mchango gani katika ukweli huu? Yatupasa tufika mahali na kuona ukweli kama ulivyo na daima tutende kwa haki bila kubaguana. Ili kutoka kwenye ombwe hili la uongozi na mfumo mbaya wa kuwanyonya wanyonge yatupasa kila mmoja wetu kutambua ukweli wa tatizo kama jamii moja, na pia kutambua uwezo, vipaji na karama za wengine. Hivyo kwa umoja wetu tunaweza kuurekebisha na kuutoa kabisa mfumo kandamizi katika jamii yetu. Uovu hauwezi kudumu milele. Na mwisho wa uovu ni aibu.

Devotha ni binti mwenye akili na  karama nyingi. Kutokana na karama zake hizo aliona inafaa na kumpendeza Mungu kama angejiunga na maisha ya kitawa ili awe na nafasi nzuri zaidi kuvitoa vipaji vyake kwa wengi. Hakika aliona kwa njia hii anaweza kufikika kwa wengi na ni kwa namna hiyo Kristo angejulikana kwa wengi.

Baada ya kumaliza kidato cha sita akiwa amefaulu vizuri masomo yake ya sayansi (PCB), alishauriana na wazazi wake kuhusu nia yake hiyo na kupata baraka zote kwa kile alichopenda kuwa katika maisha yake. Kwa upande wa Devotha alifarijika sana na uelewa wa wazazi wake. Hivyo Devotha alijiunga na shirika moja la kitawa ambalo karama na huduma zao huwa mashuleni na mahospitalini.

Dada Devotha alipita vizuri katika hatua za mwanzo, yaani, ukandidati na upostulanti, hivyo akachaguliwa kuendelea na unovisi. Unovisi ni hatua muhimu sana kwa maisha ya kitawa, na baada ya hatua hii ilimpasa kuweka nadhiri za mwanzo kwa muda wa mwaka mmoja. Hatua hii ilikuwa na changamoto sana kwa Devotha. Devotha hakukata tamaa licha ya kutoelewana vizuri na Mlezi wake.

Hofu ya Mlezi wake ilikuwa kwamba kwa uwezo wa akili na karama alizokuwa nazo Devotha vingeweza kumtia kiburi na baadaye kutokuendelea na maisha ya kitawa. Kilichompoza Devotha ni kule kuwa wazi na kusema alichoona ni kweli na haki bila kumkwaza ye yote. Hivyo hali hii ilimletea shida sana Devotha. Wiki moja kabla ya kufunga nadhiri wakiwa jumla ya wanovisi saba, Devotha alitwa na kupewa ujumbe huu na mlezi wake: “Devotha, baada ya mashauriano na wengine katika nyumba hii yetu ya unovisi, nimeonelea kwa dhamiri yangu safi kwamba huwezi kuendelea na maisha haya ya kitawa. Hivyo, unaweza kuwa mama mzuri tu katika Taifa la wana wa Mungu. Kwa maana hiyo, hutakuwa mmoja ya wale wenzako sita watakao funga nadhiri wiki ijayo. Mungu anguangazie zaidi katika maisha yako. Kwaheri na wasalimie wazazi wako.”

Devotha alipokea kwa masikitiko makubwa sana habari ile. Hata hivyo alijipa moyo sana na kusema, “Ee Bwana wafahamu nia yangu tangu nikiwa mdogo. Hata sasa sijabadili nia yangu na ninaona maisha haya ndiyo ninayoweza kutimiza ndoto yangu. Ee Mama Bikira Maria na Mwanao Yesu Kristo msiniache.” Sala hii ilimpa ujasiri sana Devotha. Hivyo siku iliyofuata Devotha aliondoka utawani.

Miaka kumi na nane baadaye, Devotha alikwisha maliza masomo yake ya udaktari na kuwa Dactari bingwa wa upasuaji na magonjwa ya watoto na akina mama. Akiwa anajiandaa kuelekea uwanja wa ndege majira ya saa saba mchana kwa ajili ya safari ya saa kumi na moja jioni kuelekea Marekani kwa semina ya wiki moja, Devotha alipigiwa simu na kuitajika haraka sana katika chumba cha upasuaji.

Basi Dr. Devotha alikimbia haraka na kuingia moja kwa moja katika chumba cha upasuaji alipokuwa ameandaliwa mgonjwa yule. Basi baada ya upasuaji ule uliochukua takribani masaa mawili na kufanikiwa, ndipo Devotha alipopewa yaliyojiri kuhusua mgonjwa yule. Kwa ufupi hapakuwa na dactari mwingine wa kufanya upasuaji wa ugonjwa ule isipokuwa Dr. Devotha. Ni yeye tu aliyekuwa na uwezo wa kufanya upasuaji ule, na kama isingekuwa hivyo mgonjwa yule angefariki masaa machache baadaye.

Baada ya maelezo yale kutoka kwa madaktari wasaidizi,  Dr. Devotha alipenda kumjua mgonjwa yule. Jambo la furaha na kusikitisha mgonjwa yule alikuwa Mlezi wake wa unovisi miaka 18 iliyopita. Mkuu wa shirika lile akiwa na masista wengine alitoa shukrani zake kwa niaba ya Sista aliyepata upasuaji ule, kwa kusema, “tunajisikia furaha sana kwa uwepo wako na vipaji vyako Mungu alivyokujalia. Kwa upande wetu kama shirika tunachoweza kusema leo labda lilikuwa kosa lenye bahati kukuondoa utawani. Tunaomba utusamehe kwa yaliyokwisha tokea na Mungu akutumie vizuri zaidi kwa wengine wenye shida kama hii iliyompata sista wetu.” “Nami najisikia furaha kubwa sana kutoa huduma kwa Mlezi wangu. Haya yote nayaona kama mpango wa Mungu kunikutanisha na Mlezi wangu ambaye hakuweza kunifahamu vizuri. Nami nilishayasamehe yote miaka 18 iliyopita. Nimeweka nadhiri mbele ya Mungu kuwa mlei mmisionari maisha yangu yote. Asanteni masista yanipasa kusafiri hapo saa kumi na moja jioni hii kuelekea Marekani. Tutaonana tena Mungu akipenda. Kwa herini,” Dr. Devotha aliwaaga masista wale kwa furaha na tabasamu la afya.

Wapendwa wana wa Mungu, mwisho wa chuki, wivu, ubaya na uovu ni AIBU. Usiacha kutenda mema daima.

Tumsifu Yesu Kristo!


EE YESU TUFANYE VYOMBO VYA AMANI YAKO DAIMA. AMINA